Swali: Inakuwaje manabii wa uongo wanakuwa na uwezo wa kutoa pepo kwa jina la YESU?, na ilihali hawana mahusiano na Mungu wa kweli? je ni nguvu gani wanazitumia? Za Mungu au shetani?.
Jibu: Zipo aina mbili za manabii wa uongo. Aina ya kwanza ni ile inayotumia nguvu za giza asilimia mia moja (100%), kundi hili halihusishi kabisa jina la YESU katika huduma zake, wala halimhubiri YESU wa kweli bali shetani.
Hawa wanakuwa ni wachawi waliovaa suti na kushika biblia, na Neno la MUNGU linasema tutawatambua kwa matunda yao, na si mwonekano wao wa nje.
Kundi la Pili: la manabii wa Uongo, ni wale ambao sio wachawi lakini halina mahusiano na MUNGU, maana yake aidha wanamtumikia MUNGU kwa faida za matumbo yao, au walishamwacha MUNGU na kufuata akili zao, kundi hili ndio hatari zaidi kwasababu bado linaweza kutumia jina la YESU na miujiza ikatendeka.
Mtu anakuwa kashapoteza mahusiano na MUNGU lakini bado upako anao!.. utauliza hilo linawezekanaje?.. Mkumbuke MUSA!.. Bwana MUNGU alimwambia auambie mwamba utoe maji, lakini yeye pamoja na ndugu yake Haruni, hawakumsikiliza MUNGU wakaenda kufanya kinyume na walivyoagizwa, na jambo la ajabu ni kwamba ijapokuwa walikuwa wameenda kinyume na agizo la MUNGU (wapo nje na mpango wa Mungu) lakini walipouchapa mwamba ulitoa maji, binafsi ningetegemea maji yasitoke mwambani kwasababu walikuwa nje na agizo la MUNGU, lakini haikuwa hivyo.
Hesabu 20:6 “Musa na Haruni wakatoka pale palipokuwa mkutano, wakaenda hata mlangoni pa hema ya kukutania, wakaanguka kifudifudi; utukufu wa Bwana ukawatokea.
7 Bwana akasema na Musa, akinena,
8 Twaa ile fimbo, ukawakusanye mkutano, wewe na Haruni ndugu yako, ukauambie mwamba mbele ya macho yao utoe maji yake, nawe utawatokezea maji katika mwamba, na hivyo utawanywesha maji mkutano na wanyama wao.
9 Musa akaitwaa hiyo fimbo kutoka mbele za Bwana kama alivyomwamuru.
10 Musa na Haruni wakawakusanya kusanyiko mbele ya mwamba, akawaambia, Sikieni sasa, enyi waasi; je! Tuwatokezee maji katika mwamba huu?
11 Musa akainua mkono wake akaupiga ule mwamba kwa fimbo yake mara mbili; maji yakatoka mengi, mkutano wakanywa na wanyama wao pia.
12 Bwana akamwambia Musa na Haruni, Kwa kuwa hamkuniamini mimi, ili kunistahi mbele ya macho ya wana wa Israeli, basi kwa sababu hiyo, hamtawaingiza kusanyiko hili katika ile nchi niliyowapa”.
Umeona hapo?.. ijapokuwa Musa alikuwa anatembea nje ya agizo la MUNGU, lakini bado upako alikuwa nao, na manabii wa uongo ni hivyo hivyo, wanaweza kuwa wanatembea na upako wa MUNGU wa kweli lakini hawana MUNGU maishani mwao, na mwisho wao ni mbaya…na hawa tumeambiwa tutawatambua kwa matunda yao na si upako wao, wala mwonekano wao.
Mfano mwingine ni Yule nabii mzee tunayemsoma katika biblia, aliyemwambia uongo nabii mwenzake, na badala nguvu za MUNGU zimwondoke baada ya kusema kwake uongo, kinyume chake ndio kwanza anapokea unabii mwingine kumhusu mwenzie. Soma habari hiyo katika 1Wafalme 12:11-30.
Ikifunua kuwa unabii, au muujiza au upako mtu/mtumishi alionao sio kipimo cha kwanza cha kumtambua nabii/mtumishi wa Mungu wa kweli, bali ni mtu kuwa na mahusiano mazuri na MUNGU, kwani maandiko yanasema Yohana Mbatizaji hakufanya ishara wala muujiza hata mmoja lakini mbinguni alihesabika kuwa mkuu kuliko manabii wote na watu wote wa agano la kale (Yohana 10:41 na Mathayo 11:11).
Na tena Bwana YESU alisema wengi watakuja siku ile wakisema, hatukutoa pepo na kufanya unabii kwa jina lako?.. na yeye atasema siwajui mtokako! (Mathayo 7:21-22).
Ili kumtambua kuwa huyu ni Nabii wa kweli na si wa uongo, ni matunda anayoyatoa.. Maana yake Matunda ya maisha yake, na matunda ya kazi yake.
Matunda ya maisha yake ni jinsi anavyoishi, je anazaa matunda ya Roho mtakatifu tunayoyasoma katika Wagalatia 5:22?.. au ni mtu wa namna gani?..kama maisha yake si kulingana na Neno la MUNGU bali ni mtenda dhambi, basi huyo hata kama anauwezo wa kusimamisha jua, bado hatupaswi kudanganyika kwake.
Vile vile kama matunda anayoyazaa kutokana na kazi yake (maana yake watu anao wahubiria) hawawi wasafi mwilini na rohoni, hiyo ni ishara nyingine ya kumtambua nabii huyo kuwa si wa MUNGU. Kwani kama watu anaowatengeneza hawana tofauti na wa ulimwengu, maana yake matunda yake si matunda ya kiMungu bali ya adui.
Hiyo ndio namna pekee ya kuwapima manabii au wachungaji au waalimu au mitume wa kweli na wale wa uongo, na tunapowafahamu biblia imetuonya tujihadhari nao.
Mathayo 7:15 “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali.
16 Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? 17 Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya.
18 Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri.
19 Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni.
20 Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua.
21 Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni”.
Bwana atusaidie.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Ni mji gani mtakatifu shetani aliomchukua Bwana YESU? (Mathayo 4:5)
SADAKA INAHARIBU NGUVU ZA MADHABAHU ZA MASHETANI.
SADAKA INAHARIBU NGUVU ZA MADHABAHU ZA MASHETANI.
About the author