HADITHI ZA KIZEE.

HADITHI ZA KIZEE.

Mtume Paulo anamwambia Timotheo “Bali hadithi za kizee, ZISIZOKUWA ZA DINI, uzikatae; nawe ujizoeze kupata utauwa.”( 1Timotheo 4.7).

Hizi hadhithi za kizee ni zipi? (kwa kiingereza zinaitwa old wives’ tales). Ni Misemo na hadithi zilizotungwa na watu wa zamani, ambazo kwa kuzitazama kwa nje zinaonekana kama zina ukweli fulani ndani yake, lakini kimsingi hazina uhalisia wowote, ni hadithi za uongo. Karibu kila jamii zipo na naamini hata wewe ulishakutana nazo.

Kwa mfano embu jaribu kutafakari maneno haya ambayo pengine ulishawahi kuyasikia.

* Ukiwa unakojoa hakikisha unatema mate chini, vinginevyo mama yako atavimba matiti.

* Mtoto mchanga akiangalia kioo haoti meno,.

* Mtu akikuruka hutorefuka.

* Mtoto wa kike akikaa katikati ya mlango, hatoolewa

* Ukipita makaburini, ukanyoosha kidole chako kuelekea kule, king’ate mpaka kiume vinginevyo mama/baba yako atakufa.

* Binti akipika huku aimba, ataolewa mbali.

* Mwanaume asilie kwenye sufuria la sivyo siku ya ndoa yake mvua nzito itanyesha.

* Ukimuona albino usipojitemea mate kifuani mwako, basi wewe nawe utazaa albino. n.k N.K. zipo nyingi.

Sasa mambo haya, yameaminika kwa wengi, mpaka imefikia hatua licha tu ya kubakia kwenye jamii ya watu wasiomini (yaani watu wasio wakristo), sasa imefikia mpaka kwa watu wanaomfahamu Mungu, waliookoka . Siku moja nilisikia mtu mmoja anayejiita mtumishi wa Mungu kwenye Whatasapp, anaitwa Apostle Vincent Mkalla(samahani kwa kulitaja jina) akitoa ujumbe ambao umesambaa sana mitandaoni na unajulikana na wengi, katika ujumbe huo, alitoa habari ya mti mmoja ujulikanao kama mti MWAMVULI, akisema mti huu, ukiwa umepandwa nyumbani, basi fahamu kuwa utaleta mabalaa makubwa katika hiyo nyumba, anasema kwanza kabisa ukichunguza utaona kuwa baba ya nyumba hiyo lazima afe, pili, unaleta hali ngumu za kiuchumi katika familia, tatu unaleta magonjwa, na pia unasababisha familia kutawanyika, familia kuwa na madeni, pia watu wa nyumba hiyo wanajikuta wanapitia katika hali ya kulaumiwa pasipo kujua chanzo ni nini n.k.…na mambo mengine aliyoyasema pale kuhusiana na mti..

 

Lakini kilichonisikitisha zaidi wakati huo nilipokuwa ninasikiliza nilikuwa na mama mmoja, ambaye naye alikuwa anausikiliza kwa makini sana, kwa hofu akiamini kinachozungumzwa pengine ni kweli, na siku chache mbeleni nilikwenda nyumbani kwao, ambapo mti huo wenye kivuli ulikuwa umepandwa uwani, nikakutwa umekatwa, hali kadhalika niliporudi nyumbani kwetu kwa mama, nikakutwa umekatwa,maana hata nyumbani upo, na sehemu nyingine nyingi.. Kwa hofu kwamba madhara yatokanayo na mti huo waliosikia kutoka kwa mtumishi huyo wa Mungu yasiwakute.

Kaka/Dada hizi ni nyakati za mwisho na biblia inasema..

1 Timotheo4 : 1-2”Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wenginewatajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;

2 kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe;

Hizi ndizo siku hizo za mwisho, Na hizi ndio HADITHI ZA KIZEE ZISIZO ZA DINI Mtume Paulo anamwonya Timotheo ajiupushe nazo, ni mafundisho ya mashetani, hadithi ambazo zinafanya watu wapoteze shabaha ya kuujua uweza wa Mungu bila wao kujua wakidhani kuwa vitu vya asili vinaweza kuathiri hatma zao na sio mambo ya rohoni. Na hilo ndio linalowafanya wengi mpaka kufikia hatua ya kuabudu sanamu, kwasababu imani yao kidogo kidogo ilianza kuhamishwa kutoka kwa Mungu, na kuanza kuangalia mambo ya mwilini kama suluhisho la mambo yao na matatizo yao. Mwisho wa siku hata mtu akiwambiwa kaoteshe mkaratusi katikati ya shamba lako utapata hela atakwenda na kufanya hivyo kwasababu siku nyingi tayari alishahamishwa Imani yake kutoka katika Neno la Mungu na kuingizwa katika “Maashera” (ibada za masanamu), na pasipo yeye kufahamu hajui kuwa anamwabudu shetani mwenyewe..

Dada yangu tena sikumoja ananiambia ukiona mjusi au mende, kwenye nyumba hiyo ni ishara mbaya, ya kutokufanikiwa kiuchumi.

Siku nyingine nikakuta Ua moja ambalo sikujua maana yake, mpaka siku moja mama yangu mdogo ambaye amesema ameokoka aliponiambia ua lile, ni la Baraka linaeleza hali ya kiuchumi ya nyumba hiyo,likistawi basi uchumi unastawi, likisinyaa basi uchumi ni mdogo..Niliposikia vile nilisikitika sana rohoni.

Kumbukumbu 16:21 “Usipande mti uwao wote kuwa Ashera kwako kando ya madhabahu utakayofanya ya Bwana, Mungu wako”.

Sasa Yapo mambo mengi hatuwezi kuyasema yote hapa, yanafundishwa na baadhi ya watu wanaojiita ni watumishi wa Mungu na yanazidi kukithiri, na kusambaa, naamini hata na wewe ulishakutana yao.

Ndugu nataka nikuambie ukweli wa kibiblia hakuna ubaya wowote katika miti, ikiwa imepandwa kwa nia njema, hakuna ubaya wowote wa vyakula vya aina Fulani, ikiwa navyo vimepokelewa kwa shukrani kama biblia inavyosema, vyote vinatoka kwa Mungu, na vimeumbwa na Mungu..Kusema mti Fulani unasababisha kifo cha baba wa nyumba, jiulize ni nyumba ngapi duniani zimefiwa na wazazi wao,

Unaposema miti inasababisha hali mbaya kiuchumi ni familia ngapi duniani zinapitia matatizo ya kiuchumi?. Ndugu yangu, chanzo cha matatizo yote ni DHAMBI, na kutokumjua Kristo na uweza wake, lakini badala yake, wanafundisha chanzo cha mafarakano na magombano katika familia ni MITI, tangu lini mti ukimfarakanisha mtu na mtu?..Na mtu huyo anajiita ni mtumishi wa Mungu, na bado tena mkristo anamwamini mtu wa namna hiyo kisa tu katumia vipengele fulani vya maandiko kutibitisha uongo wake, na wengi wanamwamini, hujui kuwa hata shetani alitumia maandiko kuuthibitisha uongo wake kwa Yesu kule jangwani.

Hofu zimewakubwa watu wengi mpaka sasa, kila kitu wanachotokea hata kujikwaa kidogo tu anasema kalogwa, akipishana na paka, kuna mtu kamwendea kwa mganga, akipishana na mbwa mweusi usiku basi ni mchawi, sasa mbwa wa kweli atakuwa ni yupi? Kama kila mbwa ni mchawi, bundi wa kweli aliyeumbwa na Mungu atakuwa ni yupi kama wote ni wachawi, paka wa kweli aliye mweusi ambaye aliumbwa na Mungu atakuwa ni yupi kama kila paka mweusi ni mchawi,?…utasikia mwingine anakuambia jicho likicheza kidogo tu anasema kuna mtu anamsema, akipiga chafya kuna watu wanamtakia mabaya, huyo ni mkristo anazungumza maneno hayo. ..HADITHI ZA KIZEE zisizo na dini…

2 Timotheo 4.3 “Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti;

4 nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo.

5 Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia mabaya, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiliza huduma yako.”

Timotheo kama mwalimu alionywa ajiuepushe na injili za namna hiyo, hali kadhalika azikatae, azikemee zisifundishwe katika kanisa la Mungu, na sisi leo tunazikemea na tunazikataa zisifundishwe kwa watu..Leo watu wengi wanafahamu zaidi habari za uchawi na ushirikina kuliko hata kumjua Mungu, shuhuda zilizojaa kwenye kichwa vya watu ni uchawi tu, kana kwamba huo ndio msingi wa kuwa mtu wa rohoni. Na hiyo inapelekea watu kuwa WAOGA kwa shetani, kwasababu mioyo yao imejazwa shuhuda za shetani zaidi kuliko Mungu, Mtu anaogopa hata kusalimia, au kumsaidia mtu asiyemjua kwa hofu tu ya uchawi, lakini haogopi maneno ya Mungu yanayomkataza yeye kwenda kutenda dhambi za makusudi. Na siku zinavyozidi kwenda hofu hii inazidi kuongezeka katikati ya watu..(hususani wanaojiita wakristo).

Hivyo hata ukiwaeleza nguvu zilizokatika Neno la Mungu, haziwasaidii sana, kwasababu mioyo yao haijajazwa na Neno la Mungu bali Neno la Shetani. Kwasababu biblia inasema Hazina yako iliyo ndipo utakapokuwepo na moyo wako. Na hivyo kila elimu inayokuja inawachukua..leo hata wakiambiwa wasipange mchicha kwenye nyumba zao zinawaletea umaskini watafanya hivyo, kesho wakiambiwa wasitumie mafuta ya nazi ya roho za majini watatatii, kesho kutwa wakiambiwa wakate kidole gumba kinawaletea mikosi na wakithibitishiwa na maandiko mawili matatu, watafuata..kwasababu ndani yao kumjua Mungu hakupo..Biblia inasema Tumjue sana Mungu ili tuwe na AMANI sio tumjue sana shetani ndio tuwe na Amani…Elimu ya shetani haileti amani bali hofu.

Mtu akija kukuambia leo, kuna bundi nimemwona batini kwako jana usiku, na ni mchawi…kitakachofuata hapo ni hofu, na wala si kitu kingine, utaanza kuiogopa hata nyumba yako unayoishi…

Lakini leo hii utakaposikia elimu iliyopo katika uweza wa Mungu…Kwamba Kristo alitwaa madhaifu yetu na yeye anatupenda kiasi cha kutuhurumia, na tena anatuambia tuutafute kwanza ufalme wake na haki yake, Hakuna hata unywele wetu mmoja utakaopotea, na zaidi ya yote anatuambia sisi tuliomwamini kuwa Baba yetu wa mbinguni anatujali sisi kuliko baba zetu wa kimwili..Mambo hayo ukiyajua yanakupa amani na furaha katika wokovu…na hayakufanyi kuwa mateka zaidi yanakufanya kuwa huru, elimu ya mashetani ndio inayokufanya kuwa mateka, na matunda ya roho ya shetani ndio haya..uwoga, hofu, mashaka, kukosa raha, uchungu, wasiwasi,visasi, wivu, hasira, chuki n.k mambo haya yote yanazalishwa na roho za mashetani kupitia elimu zake. Na shetani ndio anataka mambo hayo yawepo ndani ya mtu, ili apate nafasi ya kumkandamiza kimawazo na kiakili, Lakini Roho Mtakatifu ndani ya mtu, hayupo hivyo na wala matunda yake hayapo hivyo ….matunda ya Roho wa Mungu ndio haya..

Wagalatia 5: 22 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,

23 upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria”.

Hizi ni nyakati za hatari ndugu yangu, mafundisho kama hayo yatazidi kuongezeka, hayataishia kwenye miti, wanyama, na vyakula, yataendelea mpaka kwenye mwili wako, na maumbile yako..Hivyo usipokuwa makini kwa kutaka kukaa chini na kujifunza zaidi uweza wa Mungu katika Neno lake, KUMJUA SANA MWANA WA MUNGU (Waefeso 4:13)…badala yake unapenda kutafuta njia za mwilini kutatua matatizo yako nataka nikuambie ukweli wote, shetani atakutesa sana, utakosa raha ya kuishi hata kama unajiita umeokoka… na mwisho wa siku utachukuliwa na wimbi hilo na manabii, na waalimu wa uongo, ambao hao Injili ya kweli ya Kristo ipo mbali nao.

Sina muda wa kutosha ningekupa mifano kadha wa kadhaa ya hawa watumishi wa shetani ambao mimi binafsi nimewahi kukutana nao..ambao wengine wanatumia mifupa, na nywele, na biblia kuchukua watu mateka na sana sana wanawake kwasababu wao ndio sana sana wanahangaika huku na kule kutafuta mambo ya rohoni…Watumishi hawa ni ngumu sana kuwagundua kwasababu shetani kawanoa vya kutosha kama hujui maandiko wanakuchukua…na target yao kubwa ni wanawake…

1 Timetho 3:5 “…wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao.

6 Kwa maana katika hao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu, na kuchukua mateka wanawake wajinga wenye mizigo ya dhambi, waliochukuliwa na tamaa za namna nyingi;

7 wakijifunza siku zote, ila wasiweze kabisa kuufikia ujuzi wa kweli.

8 Na kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Musa, vivyo hivyo na hawa wanapingana na ile kweli; ni watu walioharibika akili zao, wamekataliwa kwa mambo ya imani”.

2 Petro 1.16 “Maana hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake; bali tulikuwa tumeuona wenyewe ukuu wake”.

Kristo alipokuwa duniani hakutuelekeza katika miti, wala vyakula, wala wanyama, wala hakutuhubiria habari za washirikina na wachawi, badala yake alitumia muda mwingi kutufundisha jinsi ya kuwa na mahusiano ya karibu na Baba yetu wa mbinguni kama yeye alivyokuwa kwa baba yake..Na hilo ndio jambo la muhimu kwasababu ukishajua nafasi yako kwa Mungu wako basi hayo mambo mengine hayatakusumbua, hutakuwa na hofu, ya kifo, au matatizo, au shida, au chochote kile kwasababu baba yako atakuwa pamoja na wewe wakati wowote kukusaidia…hutakimbilia kwenda kuisingizia miti, na paka, na mbwa, na bundi, na mijusi, na popo, na fisi, kwa hali unayoipitia…Badala yake Mungu ndiye atakayekuwa jibu lako wakati wote.

Hivi unajua kwamba wapagani wasiomjua Mungu, hawakuanza hivi hivi kuabudu miti na mawe?..unalijua hilo?..walianza kidogo kidogo kufikiri tatizo Fulani linasababishwa na miti Fulani au mawe Fulani, na walipoisafisha ile miti na yale mawe waliona kama matatizo yameondoka lakini walipoona kuwa kuna mengine ni sugu..waliona njia pekee ni kwenda kwa unyenyekevu chini ya hiyo miti..kuiomba kwa upole na utaratibu iwaondolee hayo matatizo na endapo hayo matatizo yataondoka basi wanaahidi kuifanyia jambo Fulani labda kuipa heshima Fulani..na kwasababu ni shetani yupo nyuma ya ule mti..anaondoa lile tatizo lao kwa muda na wale wanadhani ni mti umesikia maombi yao, hivyo wanaugeuza ule mti kuwa mungu wao..na shetani anatuma maroho yake kuwaingia wale watu wakati mwingine wanaanza kuota ndoto zinazoutukuza ule mti au wengine wanaona vitu vya ajabu kwenye ule mti n.k..lengo ni kutoa umakini wao kumhusu Mungu wa Mbinguni na kuwaleta kuamini miti na mawe kama miungu…Na haishii hapo akishajua watu wameuamini ule mti kupita kiasi..anawapa mpaka nafasi ya wao kuomba maombi yao au kupeleka mahitaji yao kwenye ule mti na akawafanyia…

Sasa roho hiyo hiyo ndio inayoingia kwa kasi katika kanisa katika siku hizi za mwisho, wengi wanaingizwa kwenye ibada za sanamu pasipo wao kujijua, shetani anahamisha umakini wa watu kumhusu Mungu wa Kweli wa Mbinguni na kuwatengenezea watu miungu ya kuiabudu, miti, mawe, sanamu n.k

Warumi 8: 35 “Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga?……..

38 Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo,

39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu”.

Ni matumaini yangu kuwa umepata kitu na utazidi kuchukua tahadhari juu ya hizi HADITHI ZA KIZEE, na kuanza kumtazama Mungu ili njia zetu ziwe zimenyooka siku zote.Na tuwe na Amani.

Ubarikiwe. Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

MAFUNDISHO YA MASHETANI

SI SHETANI BALI NI WEWE. (CHAGUA MEMA)

CHANZO CHA MAMBO

JINSI WATU WANAVYOZAMA KATIKA USHIRIKINA NA UCHAWI.


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Raymond A. Ndumbalo
Raymond A. Ndumbalo
2 years ago

Amen.Ubarikiwe na Bwana