Kama leo hii Mungu akikutoa katika utumwa wa dhambi (Yaani kuokoka), basi weka akilini kuwa unapopelekwa kutakuwa ni nje ya matarajio yako, na pengine pasiwe ni pa kuvutia kabisa katika macho yako. Ni vizuri tukafahamu njia za Mungu, ili pale tunapokutana nazo tusiwe ni watu wa kulaumu laumu, au kuuliza uliza ni kwanini hivi, kwanini vile?
Kipindi kile Mungu alipowatoa wana wa Israeli katika nchi ya Misri, walitazamia kupitishwa katika NJIA kuu ya mataifa yote, iliyojulikana kama njia ya wafilisti. Njia hiyo ilikuwa ni ya haraka na ya chap chap, kiasi kwamba kama wangeipitia hiyo, ingewachukua wiki kadhaa tu wangeshafika Kaanani. Lakini Mungu alikuwa na sababu ya wao kutowapitisha njia ile..Tusome..
Kutoka 13:17 “Ilikuwa hapo Farao alipokwisha kuwaacha watu hao waende zao, Mungu hakuwaongoza kwa njia ya nchi ya Wafilisti, ijapokuwa ilikuwa ni ya karibu; maana Mungu alisema, Wasije wakaghairi watu hawa hapo watakapokutana na vita, na kurudi Misri;
18 lakini Mungu akawazungusha hao watu kwa njia ya bara kando ya Bahari ya Shamu; wana wa Israeli wakakwea kutoka nchi ya Misri hali wamevaa silaha”.
Unaona wana wa Israeli walipitishwa katika njia ngeni kabisa machoni pao, njia yenye ukingo wa mbeleni ya bahari, njia ya vichakani, isiyopitwa na watu, njia ya upweke..Mpaka biblia inatuambia hicho ndicho kilichomvutia Farao, kuwafuatilia tena ili wawateke nyara wawarudishe Misri. Lakini hawakujua kuwa Mungu yupo kule kuwatetea.
Kutoka 14:1 “Bwana akasema na Musa, akamwambia,
2 Waambie wana wa Israeli, kwamba warudi na kupiga kambi yao mbele ya Pi-hahirothi, kati ya Migdoli na bahari, kukabili Baal-sefoni; mtapanga mbele yake karibu na bahari.
3 Naye Farao atasema katika habari za wana wa Israeli, Wametatanishwa katika nchi, ile jangwa imewazuia wasitoke.
4 Nami nitaufanya uwe mgumu moyo wa Farao, naye atafuata nyuma yao; nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote; na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana. Basi wakafanya hivyo.
5 Mfalme wa Misri aliambiwa ya kuwa wale watu wamekwisha kimbia; na moyo wa Farao, na mioyo ya watumishi wake, iligeuzwa iwe kinyume cha hao watu, nao wakasema, Ni nini jambo hili tulilotenda, kwa kuwaacha Waisraeli waende zao wasitutumikie tena?
6 Akaandalia gari lake, akawachukua watu wake pamoja naye;”
Hata sasa, wapo watu wanapookoka, na ghafla kuona mambo yanakwenda kinyume na matazamio yao, wanapolazimika kuishi staili nyingine ya maisha, wanageuka na kurudi nyuma na kuuacha wokovu. Na tena pale wanapoona, kuna ukigo mzito mbele yao na kwamba wakiendelea na njia hiyo ya wokovu watakwama ndio kabisa wanakimbia kwa miguu yote miwili, na kusema huyu si Mungu.
Pengine mwingine atapitia shida kidogo, au dhiki kutoka kwa ndugu, au kupungukiwa, jambo ambalo ni kinyume na matarajio yake, wakati hapo mwanzo yeye alidhani akimpokea Kristo siku hiyo hiyo mambo yataanza kuwa safi, sasa anapoona kumetokea mitikisiko Fulani katika maisha, anamwacha Mungu anasema huyu sio Mungu.
Ndugu ikiwa kweli umetubu dhambi zako, na umejitwika msalaba wako kumfuata Kristo, umesema mimi na ulimwengu ndio kwaheri, kamwe usitazame nyuma, pale unapoona mambo yanakuja kinyume na matarajio yako, wewe songa mbele. Ni Mungu ndiye kakusudia kukupitisha hapo, usianze kulaumu laumu au kunung’unika, na kusema kwanini mimi, maadamu Kristo yupo ndani ya moyo wako, songa mbele. Unapoona njia hiyo imekuwa ndefu sana, kama vile huielewi itaisha lini? Bado usiwe mwepesi wa kutazama nyuma. Wewe endelea mbele maadamu unamwona Kristo kila siku katika maisha yako. Kumbuka iliwachukua miaka 40 wana wa Israeli kuifikia Kaanani yao.
Nawe pia upo wakati Bwana aliouweka atakufikisha katika Kaanani yako ya hapa duniani na mbinguni. Ni wewe tu, kutambua kuwa njia za Mungu sio njia zetu. Jambo ambalo wengi wetu hatulijua pale tunaposema tumemfuata Kristo, na huku tunamtaka Mungu atatupitisha kwa njia ya wengi.
Kamwe tuondoe hayo mawazo. Yeye ana njia zake, na wanadamu wana njia zao. Hilo tulifahamu. Na pia tukumbuke mtoto yoyote wa Mungu, atapitishwa tu kwenye njia hizo, haijalishi ni mjanja, au hodari, au tajiri au maskini kiasi gani, ni lazima atakutana tu na njia hizi zisizoeleweka za Mungu, kwasababu madarasa ya Mungu hayarukwi. Na tabia ya hizi njia ni kuwa zinaambatana ni miujiza mingi ya Mungu, ikiwa na maana mtu anaweza kufikia mahali anaona amekwama, ghafla anashangaa amepitaje pitaje mazingira hayo, huo ndio uthitibisho kuwa yupo katika njia hiyo ya Mungu.
Lakini kama akistahimili, basi ajue, licha tu ya kuupokea uzima lakini mwisho wako atakuwa ni wa mafanikio na wa Baraka sana hapa duniani.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mafundisho mengin
Mada Nyinginezo:
About the author