Kiburi ni nini?
Kulingana na biblia kiburi “ni hali ya mtu kujiinua kifikra, na kuamini kuwa hahitaji msaada wowote kutoka kwingine”. Hali hii inaambatana na kudhihirisha tabia nyingine ndogo ndogo kama majivuno, matukano, au kuwadharau wengine, au kuwa na ujasiri kupitiliza na hata kukufuru.
Viburi vimegawanyika katika sehemu mbili (2);KIBURI BINAFSI, na KIBURI CHA UZIMA.
KIBURI BINAFSI:
Kiburi binafsi ni kile kinachomfanya mtu aamini kuwa Mawazo yake, au maamuzi yake, au msimamo wake ni thabiti na hauwezi kubadilishwa na yeyote. Mtu mwenye kiburi binafsi hata aambiwe ukweli kiasi gani, au athibitishiwe jambo kiasi gani bado huwa habadiliki. Tayari anachokiamini, au alichokiamua amekiamua!. Mtu mwenye aina hii ya kiburi anakuwa pia ni mbishi na mtu wa mashindano, na anakuwa anajiona yeye ni bora kuliko wengine wote..
Mithali 13:10 “Kiburi huleta mashindano tu; Bali hekima hukaa nao wanaoshauriana”.
Kiburi binafsi kipo kwa Wakristo na kwa wasio waKristo..
Kwa wakristo ni pale ambapo mtu hataki kuambiwa jambo wala kuelekezwa ndani ya kanisa…yeye mawazo yake ndio bora siku zote, au njia zake ndio bora, na zaidi ya yote anakuwa anapenda kuwa juu ya wote, na anawadharau wengine wote…
WaKristo wenye kiburi cha namna hii Bwana amesema anapingana nao…
1Petro 5: 5 “..ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa SABABU MUNGU HUWAPINGA WENYE KIBURI, lakini huwapa wanyenyekevu neema”.
Mithali 29:23 “Kiburi cha mtu kitamshusha; Bali mwenye roho ya unyenyekevu ataheshimiwa”.
Kwa wasio wakristo ni pale ambapo mtu hashauriwi na yeyote, juu ya jambo lolote, hata aambiwe vipi anakuwa yupo vile vile, yeye ni wa kuelekeza tu na sio wa kuelekezwa.
KIBURI CHA UZIMA:
Kiburi cha uzima ni kile kinachozungumziwa katika.. 1 Yohana 2:16
“Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na KIBURI CHA UZIMA, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.”
Kiburi cha Uzima ni kiburi kinachompata mtu kutokana na Vitu alivyonavyo, au anavyotegemea kuwa navyo..
Watu wengi wenye mali wanakuwa na hiki kiburi(japokuwa si wote, bali asilimia kubwa).. Wanaona mtu asiyekuwa na mali kama wao hawezi kuwaambia chochote,..kiburi hiki cha mali kinamfanya mtu aone hata Mungu hana maana, Neno la Mungu kwake ni kama habari zilizopitwa na wakati.
Kulifanyia mizaha Neno la Mungu, ni habari ya kawaida kwao…hata wasikie maonyo ya Mungu kiasi gani, kwao ni habari tu upuuzi.. Mioyo yao imeinuka kutokana na Mali au vitu walivyonavyo, wanaona wanaweza kula hata pasipo kumwomba Mungu, wanaweza kuendeleza maisha yao hata pasipo kupiga magoti.. hivyo hawamhitaji Mungu tena..
Kiburi hiki ndio kibaya kuliko vyote, na ndicho kilichozungumziwa sehemu nyingi katika biblia.. naa watu wote wenye hiki kiburi, biblia imeandika hatima yao..
Isaya 2:12 “Kwa maana kutakuwa siku ya Bwana wa majeshi juu ya watu wote WENYE KIBURI NA MAJIVUNO, na juu ya yote yaliyoinuka; nayo yatashushwa chini.”
Mithali 16:5 “Kila mwenye moyo wa kiburi ni chukizo kwa Bwana; Hakika, hatakosa adhabu”.
Mithali 8:13 “Kumcha Bwana ni kuchukia uovu; Kiburi na majivuno, na njia mbovu, Na kinywa cha ukaidi pia nakichukia.”’
Ayubu 40:12 “Mtazame kila mtu mwenye kiburi ukamshushe, Ukawakanyage waovu hapo wasimamapo”.
Zaburi 119:21 “Umewakemea wenye kiburi, Wamelaaniwa waendao mbali na maagizo yako”.
Soma pia Mithali 21:4, Mithali 16:18, Zaburi 31:18, Zaburi 119:51, Mithali 11:2, na Malaki 4:1 biblia imeelezea zaidi juu ya kiburi na madhara yake..
Tujiepushe na kiburi, tunyenyekee chini ya mkono wa Mungu ulio hodari
Bwana akubariki.
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
MADHARA YA KUKOSA MAJI YA UZIMA BAADA YA KIFO.
About the author