Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo mwokozi wetu. Karibu tujifunze maneno yake ya uzima.
Ni wazi kuwa kila mmoja wetu anatamani kumzalia Mungu matunda mengi, anatamani kuona karama yake ikifanyika Baraka kwa watu wengi, anatamani kuona watu wakiokoka, watu wakijengeka, watu wakiinuliwa. Lakini anapoona haoni matokeo haya, katika hatua za awali za utumishi, anaishia kuvunjika moyo na kusema nachofanya ni kama sio huduma yangu.
Lakini hajui kanuni za Mungu anazozitumia ili kutufikisha katika viwango vya uzaaji wa matunda. Bwana Yesu alisema, tukikaa ndani yake, na yeye ndani yetu, tutazaa sana,(Yohana 15:1-8) Lakini bado wengi tunadhani kukaa ndani ya Bwana, ni kusema nimeokoka..hilo tu!. Jambo ambalo si kweli, wapo waliokaa kwa muda mrefu lakini hawazai matunda yoyote. Kukaa ndani ya Kristo sio tu kuokoka bali ni kujua kanuni za Kristo za uzaaji wa matunda.
Tusome, maandiko haya, yatusaidie kuona jambo hili kwa undani. Haya ni maagizo ambayo Bwana aliwapa wana wa Israeli kuhusiana na miti yao ya matunda watakayoipanda wafikapo Kaanani.
Walawi 19:23 “Nanyi hapo mtakapoingia nchi ile, mkiwa mmepanda miti ya namna zote kwa ajili ya chakula, ndipo mtayahesabu matunda yake kama ni KUTOTAHIRIWA; muda wa miaka mitatu miti hiyo itakuwa kwenu kama kutotahiriwa; matunda yake hayataliwa.
24 Lakini mwaka wa nne matunda yake yote yatakuwa ni MATAKATIFU, kwa ajili ya kumpa Bwana shukrani.
25 Na katika mwaka wa tano mtakula katika matunda yake, ili ipate kuwapa MAONGEO YAKE; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu”.
Mungu anawaonyesha kanuni ya uzaaji matunda, ambayo imegawanyika katika hatua kuu tatu.
Hatua ya kwanza, ni ile miaka mitatu ya kwanza(Kutokutahiriwa):
Katika hii miaka miti huwa inazaa matunda, lakini matunda yale, huhesabiwa kama ni najisi: Wakulima wanaelewa vema kuwa sikuzote matunda ya kwanza, huwa ni dhaifu, hayana ladha nzuri, hivyo yameapo, hukatwa na kutupwa, ili kupisha ukuaji mwingine, na umeaji mzuri wa matunda mapya kwa msimu ujao.
Kufunua karama zetu, pindi uokokapo, huna budi kuzaa matunda haya ya awali. Ambayo ki-msingi huwa hayana matokeo yoyote makubwa, unaweza ukafanya kazi ya Mungu ambayo ni kama vile haina matunda yoyote, utajiona haustahili, au haujui, lakini ni sharti uendelee kuzaa, kwa kipindi ulichowekewa mbele yako. Ukishavuta hatua hii,ndipo unaingia ya pili. Huwezi pelekwa nyingine kama hii ya kwanza hujapitia.
Hatua ya pili: Kuyafanya matakatifu kwa Bwana.
Wana wa Israeli, bado hawakuruhusiwa, kuyala matunda yao, hata katika mwaka wanne, japo matunda yanakuwa yameshakomaa na kukidhi kuliwa kabisa, lakini hawakuruhusiwa kuyala, bali waliagizwa wayatoe wakfu kwa Bwana. Hii maana yake ni nini, karama au huduma uliyopewa, wapaswa uigharimie wewe, hapa ni kukubali kujitoa kikamilifu katika wito huo uliopewa na Mungu. Nguvu zako, akili zako zote, hata mali zako ziwekeze kwa Bwana. Watu wengi,wafikapo hatua hii,wanasema huku ni kugumu, uzalendo umenishinda, tena nimpe Mungu, badala yeye ndio anipe mimi. Ndivyo hata huyu mkulima anavyowaza, nimesubiria miaka yote hii mitatu ‘matunda yanakuja na kuanguka tu’, halafu mwaka huu wa nne, badala nifaidi, nashangaa, kuambiwa nimtolee tena Bwana. Ndugu hiyo ndiyo kanuni ya Ki-Mungu. Kutoa! Hakuepukiki kwa Bwana.
Hatua ya tatu: Maongeo.
Maongeo ni maongezeko, yaani Baraka. Au kuzaa kupita kiasi.
Katika mwaka wa Tano, ndio mkulima anaanza kuona faida ya kazi yake yote. Miti ya waisraeli ilibarikiwa kipekee tofauti na ile ya mataifa mengine,kwasababu ilifuata kanuni hii ya Mungu. Walikuwa wanavuna kupita kiasi, kila mwaka mizeituni, mizabibu, tini, ilitoa matunda mengi kupita miti yote ya matunda ulimwenguni.
Nasi pia, ili tufikie hatua ya kuona maongeo katika huduma zetu. Hatuna budi, kwanza kutumika kwa uaminifu na kwa uvumilivu kwa kipindi Fulani, bila kuona faida yoyote inayoeleweka katika huduma/karama zetu, hatuna budi kupitia kukosea sana, unamuhubiria mtu, unadhani atasimama, kesho anarudi nyuma, matunda yako ni kama kazi bure. Lakini hilo halina budi lifanyike, kamwe mambo hayaji ndani ya siku moja, fanyia kazi kwanza kile ulichopewa,bila kujali matokeo ya nje.
Vilevile Baada ya kipindi Fulani. Utagharimika, ujitoe, haswaa, katika huduma/karama hiyo. Hapa usizuie chochote ulichonacho, unampa Mungu vyote, kama malimbuko kwake, hii ni kuonyesha upendo wako kwa hicho unachotaka umzalie Mungu matunda.
Na mwisho. Bwana anabariki. Matunda yanakuja, katika utimilifu wote. Maono yako yanatimia, karama yako inakuwa sababu ya wengi kumgeukia Mungu.
.Lakini kumbuka “Kamwe usikae tu na kusema siku moja nitafikia pale” bila kuonyesha bidii sasa. Utamaliza miaka 20 katika wokovu, hujamzalia Mungu tunda lolote. Bwana atusaidie kulitambua hili.
Njia mojawapo ya kutambua hicho ulichopewa ni karama yako, ni kusikia msukumo wa kukifanya kwa Mungu. Huo msukumo utendee kazi sana. Utakuwa msaada mkubwa sana mbeleni.
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
NITAIFAHAMU VIPI KARAMA YANGU?.
Maongeo ni nini?(Wakolosai 2:19)
NENO LA MUNGU NI UFUNUO MKAMILIFU.
NI KWA NAMNA GANI ROHO HUTUTAMANI KIASI CHA KUONA WIVU?
About the author