TWAENENDA KWA IMANI NA SI KWA KUONA.

TWAENENDA KWA IMANI NA SI KWA KUONA.

Jina la Bwana YESU KRISTO, aliye Mkuu wa mbingu na nchi libarikiwe.

Maandiko yanasema..

2 Wakorintho 5:6 “Basi siku zote tuna moyo mkuu; tena twajua ya kuwa, wakati tuwapo hapa katika mwili, tunakaa mbali na Bwana.

7 (Maana twaenenda kwa imani, si kwa kuona.)

Leo tujifunze nini maana ya “tunaenenda kwa Imani na si kwa kuona”.

Wengi wetu tunadhani kuona kwa macho ndio njia pekee ya kulithibitisha jambo, lakini kiuhalisia kuona sio njia pekee ya kuthibitisha jambo, hata hivyo ni moja ya njia hafifu sana.

Kwa mfano macho hayawezi kupambanua ubwabwa wenye chumvi na ule usio na chumvi, maana yake huwezi kutazama ubwabwa na kujua ule umewekwa chumvi au la!. Macho yatapambanua tu aina ya chakula kilichopo mbele yako, kwamba ule ni ubwabwa na si ugali lakini hayawezi kufanya kitu kingine zaidi ya hicho.

Lakini ulimi unaweza kupambanua vyote, ubwabwa ukiwekwa kinywani ulimi unaweza kupambanua kuwa ule ni ubwabwa na si ugali, vile vile unaweza kupambanua kuwa ubwabwa ule umewekwa chumvi au la!.

Kwahiyo kuona si njia kamilifu ya kuthibitisha jambo.

Na katika mambo ya rohoni ni hivyo hivyo, maandiko yanasema “hatwenendi kwa kuona bali kwa Imani”.

Macho yetu hayana uwezo kamilifu wa kupambanua mambo ya rohoni. Ndio maana leo hii Bwana hajaruhusu tuujue uso wake, au tuwe tunamwona, ndipo tumthibitishe kwamba yupo, au tuweze kumsikia na kumwelewa.

Ni kwasababu hata tukimwona bado hatutamjua, kama vile macho yalivyo na uwezo wa kuona jambo lakini si kuonja jambo. Vivyo hivyo hata leo hii katika maisha haya tukimwona Bwana kwa macho, haitatusaidia sana, zaidi ya kumwona kwa Imani.

Leo hii watu wengi sana wanatafuta kumwona Bwana katika mwili, wengi wanafunga na kuomba Bwana Yesu awatokee kwa namna ya kimwili, wamwone na kuzungumza naye.

(Hata mimi nilishawahi kufanya hivyo, nilifunga na kuomba Bwana anitokee na kusema nami, niliendelea hivyo kwa muda mrefu mpaka Bwana aliponipa ufahamu, na kujua kuwa maombi niombayo sio ya kishujaa bali ni ya kitoto.

Kwamba sio ushujaa kutokewa na Bwana na kuzungumza naye bali ni utoto na uchanga..na wlaa.hakitaniongezea chochote kiroho. Tomaso alitafuta kumwona Bwana kwa namna ya mwili baada ya kufufuka kwake, lakini baada ya kutokewa alidhani atasifiwa na Bwana, lakini hakusifiwa.

Yohana 20:29 “Yesu akamwambia, Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona,wakasadiki”

Nataka nikuambie na wewe usijaribu kufanya hivyo (Ndio unaweza kufanya hivyo, na Bwana akakusikia na kujidhihirisha kwako kwa namna ya kimwili,na ukamwona na mkazungumza), lakini nataka nikuambie Tukio kama hilo kukutokea ni nadra sana kwasababu sio njia kamilifu ya Bwana alitoichagua kwa nyakati hizi.

Ni sawa sawa na mtu aje akuombe wewe mzungumze kwa njia ya barua za posta na si SIMU, kwamba yupo Morogoro halafu akitaka kukujulia hali au kukupa ujumbe fulani basi atumie aandike barua aipeleke posta na kuituma, kisha wewe uipokee na kumjibu kwa njia hiyo hiyo ya posta!.

Umeona? Ni jambo ambalo ni gumu kwako wewe kulifanya kwasababu ni teknolojia ya zamani na inayogharimu fedha na muda.

Kadhalika na njia ya Mungu kuzungumza nasi kimwili kwake ni teknolojia ya Zamani.

Ndio maana ni ngumu leo hii kututokea na kuzungumza nasi.

Bwana Yesu kukaa katika hali hiyo ya kutotutokea tokea kimwili ni yeye ndio kaichagua hiyo njia kwa faida yetu sisi, na si kwasababu sisi ni wenye dhambi ndio maana hatutokei tokei, wala si kwasababu hatuna maombi ya kutosha ndio maana hatutokei..hapana ni kwasababu teknolojia hiyo ni ya zamani kwake na haitufai sana sisi.

Bwana alisema..

Yohana 16:7 “Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu”.

Umeona?.. hapo anasema mimi yanipasa niondoke ili msaidizi aje, na Si yeye aondoke kwasababu hatuombi au kwasababu sisi ni wenye dhambi.

Hakuna maombi yoyote ambayo yangeweza kumbakisha Bwana Yesu katika mwili hapa duniani.

Sasa swali “Tunaenendaje kwa Imani”?

Tunaenenda kwa Imani kwa kumpokea huyo Roho Mtakatifu, ambaye amemwagwa kwetu.

Tukimpata huyu hata Bwana Yesu asipotutokea kwa namna ya mwili katika maisha yetu yote, bado tutakuwa tumeyajua Yesu sana, tutakuwa tumemwelewa kwa undani wote kana kwamba yupo nasi katika mwili.

Yohana 16:13 “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.

14 Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari.

15 Na yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasheni habari”.

Leo hii wengi hawamtaki Roho Mtakatifu lakini wanamtaka Bwana Yesu katika mwili. Pasipo kujua kuwa Roho Mtakatifu ndio ukamilifu wote wa Bwana Yesu.

Na hawamtaki kwa matendo yao na si kwa midomo, ndio maana hawamwoni Yesu katika maisha yao, ndio maana hawamwelewi na ndio maana shetani anawasumbua sana.

Je na wewe umempata Roho Mtakatifu?
Kama bado na unamtamani uwe naye basi usihofu! Kwasababu haihitaji utoe fedha ili umpate, wala haihitaji ufunge kwa maombi, wala haihitaji uende kwenye shule au chuo cha biblia, wala huhitaji mhubiri au mchungaji ndipo akupatie..

Unachokihitaji sasa ni kanuni ya jinsi ya kumpata, na kanuni hiyo ni rahisi, na ipo katika biblia tu! Na hakuna sehemu nyingine unaweza kuipata.

Na kanuni hiyo ni KUTUBU DHAMBI ZAKO KWA KUMAANISHA KUTOZIFANYA TENA, NA KUBATIZWA!!…Basi!!!

Matendo 2:37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?

38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”.

Hapo mstari wa 39 hbiblia inasema… “Ahadi hiyo ni kwaajili YENU na watoto wenu”..
Maana yake ni kwaajili yako na wewe ndugu yangu!.

Sasa kama kanuni ni rahisi hivyo kwanini leo hii usitubu, na kwanini leo hii usibatizwe kwa jina la Yesu?

Bwana akupe kuchagua njia bora!

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

NI KWA NAMNA GANI ROHO HUTUTAMANI KIASI CHA KUONA WIVU?

KUSAMBAA KWA ROHO YA MPINGA-KRISTO.

Dini ni nini, na Imani ya kweli ni ipi?

BIBLIA INAITAJA NJIA KUU YA MFALME, NJIA HII NI IPI?

KUOTA NYOKA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Edward Bavunah
Edward Bavunah
2 years ago

Amina ujume wa baraka sana