JINSI YA KUSIMAMA NA KUFUNDISHA/ KUHUBIRI

JINSI YA KUSIMAMA NA KUFUNDISHA/ KUHUBIRI

Ni kanuni gani ya kuzingatia wakati wa kuhubiri/kufundisha ili usimzimishe Roho?.

Kuna vita vikubwa sana vya kiroho vinavyoinuka muda mchache kabla ya kusimama kufundisha/kuhubiri ambavyo ni lazima mkristo avijue na ajue jinsi ya kuvishinda ili injili ya Bwana isizuilike.

Baada ya kuandaa somo kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu, hatua inayofuata ni wewe kwenda kuwasilisha ujumbe ulioupokea mbele ya mtu au watu. Sasa ni muhimu kujua kanuni za kuwasilisha ujumbe ili usije ukamzimisha Roho, kwasababu Roho Mtakatifu pia anaweza kuzimishwa ndani ya mtu na mtu mwenyewe, na shetani ndicho anachokitafuta hicho, lengo lake Injili isiwafikie wengine.

(Kumbuka shetani mwenyewe hawezi kumzimisha Roho Mtakatifu, kwasababu Roho Mtakatifu ana nguvu kuliko yeye), anachokifanya shetani ni kuzikoroga hisia za mtu ili zisiruhusu Roho Mtakatifu kufanya kazi ndani yake. Na neno linatuambia kuwa “tusimzimishe Roho”

1Wathesalonike 5:19  “Msimzimishe Roho”.

Wengi huwa wanamzimisha Roho Mtakatifu wakati wa kusimama kufundisha/kuhubiri pasipo wao kujijua..unakuta wakati wanaandaa somo/mahubiri wanakuwa katika uwepo mkubwa sana lakini wakati wa kufundisha au kuhubiri ule uwepo au ile hali ya kutiririka inapotea, na hivyo kumfanya huyu mtu ajihisi Mungu hayupo naye au kamwacha.

Kiuhalisia huyu mtu hajaachwa na Roho Mtakatifu, isipokuwa hali yake ya ndani imezuia utendaji kazi wa Roho Mtakatifu.

Sasa yafuatayo ni mambo ya kuzingatia ili Roho asizime ndani yako, (kule kutiririka kusikome), na ule ujumbe wa Roho Mtakatifu ulioupokea ufike kwa walengwa kama Roho alivyokufunulia.

1.Usijipange kwa maneno mengi.

Epuka kujipanga kwa maneno mengi;  Maneno mengi yanazuia kutiririka kwa Roho Mtakatifu, wengi wanadhani kuwa na maneno mengi ndiko kueleweka, pasipo kujua kuwa anayewagusa watu na kuwafanya waelewe ni Roho Mtakatifu, hivyo ukifuata kanuni ya Roho Mtakatifu utaeleweka tu na utakuwa na matunda.

Unapojiandaa kwa maneno mengi, utajikuta unategemea yale maneno yako, na hivyo wakati Roho Mtakatifu anataka kuingiza mada nyingine katika akili yako wakati wa kufundisha ule ukuta wa maneno uliojiwekea unazuia kinywa cha Roho Mtakatifu kifanye kazi, na hivyo utajikuta unafundisha kwa akili zako, na yale maneno uliyoyaandaa yanapokwisha unajikuta na wewe umekauka, huna cha kusema Zaidi.

Kwahiyo jiandae kwa maneno machache tu!, hata kama unaona somo litakuwa ni fupi sana, Roho Mtakatifu ndio anataka iwe hivyo, ili hayo maneno mengine ayajazie yeye, ukiweka desturi hiyo siku zote utaona muda hautoshi, utaona daftari lako lina maneno machache uliyoyaandaa, lakini muda uliofundisha ni madakika mengi au masaa mengi, ukiona hiyo hali imekutokea jua sio wewe uliyekuwa unafundisha bali ni Roho Mtakatifu ndani yako.

2. Usifikiri fikiri.

Kufikikri fikiri ni nini utaenda kusema au kuhubiri, kunazima kinywa cha Roho Mtakatifu. Unapofika wakati wa kwenda kufundisha wengi huwa wanapaniki na kuwaza mara nyingi nyingi ni nini wataenda kusema, na hivyo kujikuta kulazimisha kupanga maneno ya kuzungumza kuanzia mwanzo hadi mwisho. Ukiona hiyo hali inakujua ndani yako dakika chache kabla ya kusimama kufundisha au kuhubiri ikatae!. Kwani ni adui anataka kutumia fikra zako kumzimisha Roho ndani yako.

Siku zote usijiangalie hali uliyonayo kifikra wakati wa kwenda kufundisha, hata kama hukumbuki chochote, wewe tulia mpaka wakati utakapofika wa kusimama, funga fikra zako kufikiri ni nini utaenda kufundisha au kuhubiri, ukiona mawazo hayo yanakujia hamisha fikra zako kwa kutafakari mambo mengine ya kiMungu au soma Neno, kwasababu wakati huo ndio wakati wa vita vikali, shetani anatumia nguvu kubwa sana kumshambulia mtu katika hii hatua.

Hivyo funga fikra zako na subiri ule wakati wa kufundisha Roho Mtakatifu atakupa cha kusema wakati ule ule utakaposimama kufundisha.

Kanuni kama hii Bwana Yesu aliwafundisha wanafunzi wake wakati wakipelekwa mbele ya watu wa Mataifa, akawaambia wasifikiri fikiri watakavyojibu kwani watapewa kinywa saa ile ile watakaposimamishwa.

Mathayo 10:19 “ Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema

20  Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu”.

Kwahiyo na wewe usiwe mtu wa kufikiri fikiri utakavyosema, subiri ule muda utakapofika utapewa kinywa cha kusema, ambacho hata wewe mwenyewe utajishangaa.

3. Usijiangalie udhaifu wako na Jiachilie

Usijipime kwa kujiangalia udhaifu wako, kama unajua kuhubiri au la!, kama una kigugumizi au la!, kama una uzoefu au la!..Kwani kinywa chochote kilichovuviwa na Roho Mtakatifu kina nguvu kwasababu kimebeba ujumbe wa Roho Mtakatifu.

Hivyo kabla ya kwenda kufundisha weka kando udhaifu wako, weka kando kumbukumbu za nyuma ambazo unahisi uliwahi kukosea, weka kando hisia kwamba husikilizwi au hueleweki, au unapotezea watu muda.

Zungumza kile kinachokuja kinywani mwako muda ule kwa ujasiri wote, (achilia moyo wako na fikra zako), wala usijilinganishe na yeyote wala usitafute kufundisha kama mtu Fulani unayemjua, hapo utaona Roho Mtakatifua atakavyokutumia na utakavyomhisi akitenda kazi ndani yako kwa viwango vingine.

4. Usiongozwe na  muda.

Ukiona hofu ya kuwahi kumaliza inaingia ndani yako, ikatae hiyo hali!.. Kwasababu ni mbinu nyingine ya shetani kumzimisha Roho Mtakatifu ndani yako (Kumbuka tena shetani mwenyewe hawezi kumzimisha Roho Mtakatifu, kwasababu Roho Mtakatifu ana nguvu kuliko yeye), anachokifanya shetani ni kuzikoroga hisia zako ili zisiruhusu Roho Mtakatifu kufanya kazi ndani yako.

Kwahiyo  hofu ya muda ikatae. Kama umepewa lisaa la kufundisha, usianze kuwaza utasema nini kwenye hilo lisaa lote (hiyo sio kazi yako) ni kazi ya Roho Mtakatifu, ukianza kuwaza utasema nini muda wote huo wakati utakapofika hofu iliyopo ndani yako itamzuia Roho Mtakatifu kusema kupitia wewe. Wewe anza kufundisha kana kwamba utamaliza dakika tano zijazo, na utaona Roho Mtakatifu atakachokifanya!.. Kama atapenda umalize ujumbe kwa dakika hizo hizo tano, wala usiogope!, ndivyo alivyotaka yeye, na kama atakusudia ufundishe kwa kwa lisaa au masaa mawili, atakupa maneno na utashangaa yametoka wapi.. Kwahiyo ondoa hofu ya muda!.

5. Wahusishe watu katika kufundisha kwako

Hii ni njia nyingine ya kuendeleza uwepo uwepo wa Roho Mtakatifu usikatike ndani yako, tumia muda kuwauliza maswali unaowafundisha kama unaweza kufanya hivyo, au kuwapa jukumu la kusoma mistari ya biblia n.k

Hizi ni baadhi ya njia chache utakazoweza kuzitumia ili Kile Roho Mtakatifu alichokufunulia kiweze kuwafikia walengwa.

Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba kabla ya kwenda kusimama kufundisha ZILINDE SANA FIKRA ZAKO!.. Kwasababu hizo ndizo shetani anashughulika nazo kuharibu mambo.

Bwana akubariki.

Ikiwa hukupata somo la “Jinsi ya kuandaa somo basi wasiliana nasi kwa njia ya inbox”

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Jinsi ya kuandaa Somo la kufundisha

Wanikolai ni watu gani? Katika biblia?

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

Roho Mtakatifu ni nani?.

MASOMO MAALUMU KWA WANAWAKE.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
4 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Rebecca Petro
Rebecca Petro
1 year ago

Rebecca

Wycliff
Wycliff
1 year ago

Nimepata funzo nzuri hilo BWANA awabariki sana