Biblia inaposema Yesu ameketi mkono wa kuume inamaana gani?

Biblia inaposema Yesu ameketi mkono wa kuume inamaana gani?

Mungu mara nyingi huwa anatumia lugha ya picha au maumbo, ili kutupa sisi uelewa mzuri kuhusiana na mambo ya rohoni. Kama tunavyojua inapotokea mtawala, labda raisi amekualika uketi pamoja naye meza moja ule chakula, ni wazi kuwa kwa tendo hilo litakuwa limekupandisha hadhi sana.

Sasa zamani, za wafalme ilikuwa mtu aliyepewa heshima kubwa aliwekewa kiti chake kidogo pembeni mwa mfalme upande wake wa kuume. Na hiyo ilikuwa inamaana kubwa zaidi ya heshima peke yake, bali pia ilimaanisha kupewa mamlaka.

Hivyo katika biblia unapokutana na “mkono wa kuume” Mungu ametumia picha hiyo kumaanisha aidha mambo haya makuu matatu;

  1. Heshima
  2. Mamlaka
  3. Ulinzi

1. HESHIMA.

Maandiko kutuambia Kristo, ameketi mkono wa kuume wa Mungu, ni kutuonyesha, hadhi na ukuu alionao sasa. Mbinguni wapo malaika wengi wenye nguvu, wapo wenye uhai wanne, wapo maserafi na mamilioni ya malaika, lakini hakuna hata mmoja alipewa hadhi ya kuwa karibu/sawa na Mungu zaidi ya Kristo, Bwana wetu.

Waebrania 1:13  Je! Yuko malaika aliyemwambia wakati wo wote, Uketi mkono wangu wa kuume Hata nitakapoweka adui zako chini ya nyayo zako? 14  Je! Hao wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu?

Kwahiyo, aliyepokea heshima, ya juu zaidi ya viumbe vyote ni Kristo Yesu Bwana wetu. Na ndio maana tunamwabudu na kumtukuza. Na heshima zote na shukrani zinamwelekea yeye tu peke yake. Ndiye Mfalme wa Wafalme, na Bwana wa Mabwana. Hafananishwi na mwanadamu yoyote duniani, au malaika yoyote mbinguni.

2. MAMLAKA.

Lakini pia mkono wa kuume sio tu heshima bali pia huwakilisha mamlaka, Kuketi kwake kule, ni kuonyesha mamlaka ya kumiliki na kutenda jambo lolote na kutiisha vitu vyote chini yake anayo.

Waefeso 1:20  aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; 21  juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; 22  akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo 23  ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote

> Vilevile anayo mamlaka ya kutuombea na kutuondolea dhambi, kama kuhani mkuu,

Warumi 8:34  Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea.

>Mamlaka ya kutumwagia vipawa vya rohoni na nguvu ya kushuhudia habari njema.

Matendo 2:33  Basi yeye, akiisha kupandishwa hata mkono wa kuume wa Mungu, na kupokea kwa Baba ile ahadi ya Roho Mtakatifu, amekimwaga kitu hiki mnachokiona sasa na kukisikia,

Luka 16:19  Basi Bwana Yesu, baada ya kusema nao, akachukuliwa juu mbinguni, akaketi mkono wa kuume wa Mungu. 20  Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo

3. ULINZI.

Uwapo karibu na mfalme, maana yake upo salama, chini ya mfumo wa ulinzi wake. Hivyo Mungu kumweka Kristo kuumeni mwake ni kutuonyesha sisi,ufalme wa Kristo hauhasiki. Na wanaompinga kazi yao ni bure. Na Mungu atawaweka maadui zake chini ya miguu yake.

Zaburi 110:1 Neno la Bwana kwa Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, Hata niwafanyapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako.

Lakini jambo ambalo watu wengi hawajua ni kwamba Bwana anataka na sisi tumweke yeye mkono wetu wa kuume, maana yake tumpe heshima yake, katika mambo yetu, na yeye, atatuheshimisha, atatuinua, na atatulinda.

Matendo 2:25  Maana Daudi ataja habari zake, Nalimwona Bwana mbele yangu siku zote, Kwa kuwa yuko upande wa mkono wangu wa kuume, nisitikisike.

Usiweke Mali kuumeni kwako, usiweke elimu, au mwanadamu kuumeni kwako. Bali Kristo tu peke yake.

Unaweza pia kupitia vifungu hivi Kwa maarifa zaidi; Mathayo 22:44 , Matendo 7:55, Wakolosai 3:1, Waebrania 1:3,13, 10:12, 1Petro 3:22.

Bwana akubariki.

Je! Kristo yupo kuumeni kwako? Fahamu tu ili Kristo awe pembeni yako, na wewe pembeni yake wakati wote, ni sharti uwe umeokoka. Na wokovu unakuja kwanza kwa kutubu (, yaani kukubali kuacha njia mbaya), na hapo hapo unaupokea msamaha wa dhambi, kisha Kristo anaingia moyoni mwako. Na baada ya hapo unaitimiza haki yote kwa kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi, wa maji mengi na kwa jina la Bwana Yesu, na Roho atakuwa tayari ameshakuja ndani yako kuanzia huo wakati na kuendelea. Ikiwa upo tayari kumpokea Yesu leo akusamehe dhambi zako, basi fungua hapa kwa mwongozo mfupi wa sala ya toba>>>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Ubarikiwe.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

Moyo wake mwenye hekima upo upande wa kuume, maana yake nini?

Kwanini Yesu Kristo ni mwana wa Adamu?

Nini maana ya.. “Utoapo sadaka mkono wako wa kuume usijue ufanyalo mkono wako wa kushoto”

KWANINI YESU NI ADAMU WA PILI?

Je! waliokufa kabla ya Bwana Yesu wataokolewaje?

NI KWASABABU YA YESU KRISTO.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments