Je! waliokufa kabla ya Bwana Yesu wataokolewaje?

Je! waliokufa kabla ya Bwana Yesu wataokolewaje?

Swali: Je waliokufa kabla ya Bwana Yesu kuja (yaani watu wa agano la kale)wataokolewaje?.. kwamaana tunajua kupitia damu ya Yesu tu! ndio tunapata ukombozi wa hakika wa dhambi, sasa waliokuwa wanaishi katika agano la kale wataokolewaje na ilihali Kristo alikuwa hajafa bado, na damu iondoayo dhambi haijamwagika?.

Jibu: Ni kweli ukombozi unapatikana kupita damu ya Yesu tu!

Lakini ni vizuri kufahamu kuwa Agano jipya halikuja kulifanya agano la kale liwe uongo, badala yake limekuja kulikamilisha agano la kale, kama Bwana wetu Yesu alivyosema mwenyewe katika Mathayo 5:17..

Mathayo 5:17  “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza”

Sasa Ili tuelewe vizuri hebu tutafakari  mfano ufuatao.

Taasisi moja imedahili wanafunzi wake walioingia kupitia mfumo wa makaratasi, kwamba mwanafunzi ili akubalike kujiunga na chuo hana budi kuwasilisha fomu zake katika ofisi ya taasisi hiyo…. Lakini mwaka mmoja baadaye ikabadili mfumo na kuanza kudahili wanafunzi wapya kupitia mfumo wa kieletroniki kwamba ili mwanafunzi akubalike kujiunga na taasisi hiyo hana budi kutumia mfumo wa kielekroniki hata akiwa nyumbani kupitia internet. Na kwamba hakuna mwanafunzi yeyote atakayeweza kupokelewa bila kutumia mfumo huo, kwani ni mrahisi na mwepesi katika kutunza kumbukumbu.

Sasa swali ni je! mfumo huo mpya ulioanza utawafanya wale wanafunzi wa zamani ambao walitumia mfumo wa zamani kuwa si wanafunzi halali tena wa taasisi hiyo?.. au itawafanya wale waliokwisha kuhitimu zamani, waliotumia mfumo wa zamani vyeti vyao kuwa batili?.

Jibu ni la!.. Wataendelea kuwa wanafunzi, isipokuwa watakaojiunga upya hawana budi kutumia mfumo mpya..kwasababu mfumo wa zamani utakuwa umeshabatilika!.

Kadhalika na Agano la kale ni hivyo hivyo…Ulikuwa ni mfumo wa zamani wa kuwasogeza watu karibu na Mungu, lakini ulikuwa na mapungufu mengi!.. Lakini muda ulipofika, ulikuja mfumo bora Zaidi na mwepesi na wa haraka ambao utamwingiza mtu katika ufalme wa Mungu kirahisi na kihakika zaidi, na huo ndio mfumo wa Agano jipya kupitia agano la damu ya Yesu Kristo, na si tena damu ya mafahali na kondoo..kama maandiko yanavyosema katika Waebrania 10:4.

Waebrania 10:4 “Maana haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi.”

Na hivyo kulifanya Agano la kwanza liwe chakavu na agano la pili liwe jipya sawasawa na Waebrania 8:13.

Waebrani 8:13  “Kwa kule kusema, Agano jipya, amelifanya lile la kwanza kuwa kuukuu. Lakini kitu kianzacho kuwa kikuukuu na kuchakaa ki karibu na kutoweka”

Neno “kuukuu” maana yake ni “kuchakaa”… kwahiyo lilipokuja agano jipya, basi agano la kwanza likafanyika kuwa la kale, lisilotumika tena… hivyo kwasasa halifanyi kazi tena.

Kwahiyo waliokuwepo ndani ya Agano la kwanza kabla ya Bwana Yesu hao watahesabika kuwa watakatifu sawasawa tu waliopo sasa katika agano jipya leo, ndio maana akina Musa, Eliya, Henoko, Ibrahimu, Daudi, Danieli na wengineo wanatajwa kuwa miongoni mwa watakatifu, tena mashujaa wa Imani… ijapokuwa hawakubatizwa! Wala kumwona Masihi..

Lakini baada ya Bwana Yesu kuja na damu yake kumwagika basi wote watakaozaliwa baada ya hapo, hawana budi kulitumia agano jipya, na kuachana na lile la kale…na yeyote atakayejitumainisha kwa agano la kale basi hataweza kuokoka kabisa.

Hiyo ndio sababu kwanini tunapaswa tulijue sana Agano jipya na misingi yake, kwasababu tukianza kuwatanzama watu wa Agano la kale, pasipo kujua misingi ya agano jipya, tutajikuta tunachukua vitu visivyofaa kwa watati wa sasa….kwamfano tukimtazama Daudi na maisha yake na kanuni alizokuwa anatembelea si zote zitatufaa sisi watu wa agano jipya, kwamfano utasoma ijapokuwa Daudi aliupendeza Moyo wa Mungu sana lakini alikuwa na wake wengi na alikuwa na visasi na maadui zake.

Sasa tutachukua na kujifunza Imani ya Daudi, unyenyekevu wa Daudi na mengine mazuri, lakini hilo la kuoa wake wengi, Agano jipya inalikataza, hilo la kulipiza kisasi agano jipya limetuzuia..…hatuna budi kumsikiliza aliye mkuu Zaidi ya Daudi, na Sulemani, na Musa, na Eliya ambaye ni Yesu, anayetajwa kama Mjume wa Agano jipya (katika Waebrania 9:15 na Waebrania 12:24), ambaye anasema kila amwachaye mkewe na kuoa mwingine azini, na ndoa ni mke mmoja, mume mmoja..si Zaidi ya hapo!(Mathayo 19:4), ambaye amesema “tusilipe kisasi” (Mathayo 5:38-39). n.k

Bwana akubariki.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mada Nyinginezo:

MJUMBE WA AGANO.

LITURJIA NI NINI? NA JE IPO KIMAANDIKO?.

Biblia ilimaanisha nini iliposema “Mwanamke atamlinda mwanamume” Yeremia 31:22?

JE! ULEVI NI DHAMBI?.

Nini maana ya “Bwana Yesu ni mzaliwa wa kwanza wa waliokufa?”(Ufunuo 1:5)

NJIA NYINGINE YA KUPATA REHEMA NA KIBALI KUTOKA KWA MUNGU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments