JIBU: Tusome,
Yeremia 31:22 “Hata lini utatanga-tanga, Ee binti mwenye kuasi? Kwa maana Bwana ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda mwanamume”.
Katika biblia hususani agano la kale utaona sehemu nyingi, Mungu akilifananisha Taifa la Israeli na mwanamke aliyeolewa, na Bwana Mungu mwenyewe akijifananisha kama Mume wa Taifa hilo, Ndio maana mwanzo kabisa katika zile amri kumi alizozitoa Mungu, alianza na kusema yeye ni Mungu mwenye “Wivu”, wivu unaozungumziwa hapo ni wivu wa mwanaume kwa mke wake.
Kwahiyo popote pale Israeli ilipoasi na kumwacha Mungu na kwenda kuabudu miungu mingine, katika roho ilitafsirika kama ni mwanamke aliyemwacha mumewe na kwenda kufanya uzinzi nje ya ndoa. Kwahiyo Taifa la Israeli lilifananishwa na mwanamke aliyeolewa, au binti aliyeposwa.. unaweza kusoma hayo binafsi katika mistari ifuatayo. (Isaya 54:5, Yeremia 3:1-14, Yeremia 13:27, 1Nyakati 5:25, Hosea 3:1-5, Zaburi 106: 33-41, Ezekieli 23:21-29).
Kwa msingi huo, tunaweza kurudi kusoma Yeremia 31:22 “Hata lini utatanga-tanga, Ee binti mwenye kuasi? Kwa maana Bwana ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda mwanamume”.
Hapo mwanamke anayezungumziwa ni Israeli (Yaani Taifa la Mungu), Huyo ndiye binti mwenye kuasi, kwanini ametajwa kama binti mwenye kuasi, ni kwasababu alikuwa amemwacha Mungu ambaye ndiye mume wake na kwenda kutanga-tanga kuabudu miungu mingine.
Sasa hapo anasema Bwana ameumba jambo jipya.. “mwanamke atamlinda mwanamume”..maana yake hapo kale ni “mwanamume ndiye aliyekuwa anamlinda mwanamke”. Sasa kulinda kunapozungumziwa hapo sio ulinzi dhidi ya maadui, La!. Bali ulinzi wa kimapenzi. Maana yake katika jambo hilo jipya, Mwanamke atakuwa na wivu mwingi juu ya mume wake, Maana yake atakapoona mumewe kamwacha, atajisikia vibaya na wala hataruhusu hilo jambo, wakati wote atatamani awe karibu na mume wake kuliko kawaida, hatoruhusu mahusiano yake yaharibike kwa vyovyote vile. Tofauti na hapo kwanza ambapo Mwanamume ndiye aliyekuwa anatia bidii kumlinda mkewe.
Sasa tafsiri yake katika roho ni kwamba wakati utafika ambapo Taifa la Mungu ambalo linafananishwa na mwanamke, litakuwa linampenda Mungu sana, na kumtafuta, na kumwonea Mungu wivu lenyewe..Maana yake Mungu ataweka kitu ndani ya watu wake ambacho kitawafanya wao wenyewe watafute kumpenda Mungu sana na kwa bidii. Ndio maana mbele kidogo katika hiyo hiyo sura ya 31, ya kitabu hicho hicho, utaona Bwana Mungu analiweka hilo sawa, kwamba itakuwaje.
Tusome..
Yeremia 31:31 “Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda. 32 Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa MUME KWAO, asema Bwana. 33 Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. 34 Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue Bwana; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao, asema Bwana; maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena”.
Yeremia 31:31 “Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda.
32 Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa MUME KWAO, asema Bwana.
33 Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
34 Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue Bwana; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao, asema Bwana; maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena”.
Umeona hapo?..Mstari wa 32 anasema “ingawa nalikuwa mume kwao”. Lakini agano lake walilivunja…Lakini katika agano hilo jipya, wao wenyewe watamtafuta Mungu, hawatahitaji tena kusukumwa sukumwa. Kuna kitu kitaingia ndani yao ambacho kitawafanya waulinde upendo kwa Mungu wao.
Na agano hili jipya, au “jambo jipya” lilianza siku ile ya Pentekoste ambapo Roho Mtakatifu alishuka katikati ya watu wake, siku hii, ndipo wakati ambapo Mungu alianza kutia sheria ndani ya mioyo ya watu, kiasi kwamba kwa yeyote ambaye atapokea Roho Mtakatifu, hatahitaji tena kusukumwa sukumwa katika kumtafuta Mungu, kuna kiu Fulani ya kipekee itaingia ndani yake, hiyo itampeleka mwenyewe kumtafuta Mungu, atajikuta tu anatafuta kuulinda uhusiano wake na Mungu usipotee (Hapo anamlinda mwanamume wake yaani Yesu), hatahitaji kuambiwa na Mungu hapaswi kujichubua, hapaswi kuiba, hapaswi kubeti, hapaswi kuvaa nguo nusu utupu, kwani ndani yake tayari ipo sheria, iliyoingia, ambayo inamshuhudia kabisa kwamba anapovaa mavazi yasiyompasa anafukuza uwepo wa Mungu ndani yake.
Kwahiyo kwa mtu aliyepokea Roho Mtakatifu, tayari jambo jipya limeumbika ndani yake. Na biblia inasema wote wasio na Roho Mtakatifu hao sio wake (Warumi 8:9). Na habari nzuri ni kwamba Roho Mtakatifu sio wa watu baadhi tu Fulani. La!.. Bali ni zawadi kwa wote ambao wanamkimbilia Bwana.
Matendo 2:39 “Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”.
Kwahiyo tunaishi katika siku ambazo ili kumpendeza Mungu ni lazima tuwe na Roho Mtakatifu. Swali ni je! Jambo jipya limeumbika moyoni mwako?..Je kuna nguvu inayokusukuma kwa Mungu? Je kuna hofu ya Mungu ndani yako ambayo inakufanya uhakikishe unaulinda wokovu wako?..Kama ndiyo basi usimzimishe huyo Roho aliyeko ndani yako, kwasababu huyo ndio Muhuri wa Mungu kwetu (Waefeso 4:30). Lakini kama hiyo nguvu haipo ndani yako, basi unaihitaji leo kwasababu pasipo Roho kamwe hatuwezi kumkaribia Mungu.
Hivyo kama unataka kumpokea Roho Mtakatifu maishani mwako, ni sharti kwanza umwamini Yesu maishani mwako, kwamba alikuja kufa kwaajili ya dhambi zako, na pia akafufuka, na sasa anaishi. Na baada ya hapo, tubu dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, hakikisha unaziacha kwa vitendo, maana yake kama ulikuwa unaiba unaacha kuiba,kama ulikuwa mzinzi unaacha uzinzi, kama ulikuwa unaufuata ulimwengu huu, unaacha. Na baada ya hapo Roho Mtakatifu ataanza kukupa amani, ambayo itakamilika baada ya wewe kwenda kubatizwa ubatizo sahihi, kama bado hujabatizwa. Ubatizo sahihi ni ule wa kuzama kwenye maji tele na kwa jina la Yesu Kristo (Matendo 2:38, 8:16, 10:48, 19:10).
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali. Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Nini maana ya “wanawake saba watamshika mtu mume mmoja”
KWANINI UNAPASWA UWE BIBI ARUSI NYAKATI HIZI ZA MAJERUHI?
NA ROHO NA BIBI-ARUSI WASEMA, NJOO!
KARAMU YA MWANA-KONDOO.
Rudi nyumbani
Print this post
Umehubiri vizuri mwishoni ukavuruga tupo ambao hatujazama tumebatizwa kwa maji machache lakini tunaye Roho mtakatifu
Umefanya vizuri kupokea Roho Mtakatifu, lakini hata kama umeshashampokea ni lazima kubatizwa kwa maji, kama ilivyokuwa kwa Kornelio, alipokea Roho Mtakatifu lakini bado ilimpasa abatizwe kwa Maji.
Matendo 10:47″Ni nani awezaye kuzuia maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vile vile kama sisi? 10.48 Akaamuru wabatizwe kwa Jina lake Yesu Kristo. Ndipo wakamsihi azidi kukaa siku kadha wa kadha”.
Tafuta ubatizo mwana wa Mungu!!