Bwana ametupa agizo na wajibu wa kwenda kuihubiri injili ulimwenguni kote, na kuwafanya mataifa kuwa wanafunzi wake.(Mathayo 28:19)
Alisema pia mavuno ni mengi lakini watendakazi ni wachache. Ikiwa na maana lengo lake ni yeye apate mavuno mengi kutoka kwetu. Lakini huwenda tukaona sisi ni shida, kufanya hivyo.
Hata kama itakuwa kwetu ni shida kuvuta watu, bado Yesu anaona ni rahisi kwetu..Kwani mahali pengine alisema mashamba yameshakuwa meupe tayari kwa mavuno, wapo ambao tayari walishayataabikia, sisi ni kumalizia tu. Hivyo ni rahisi sana.
Lakini ili injili yetu itoe matokeo aliyoyakusudia, yatupaswa tujifunze kanuni zote za kiuinjilisti na kuzitumia, kisha miongoni mwa hizo Bwana azitumie kuleta matokeo yake. Kuliko kutegemea kanuni moja tu Fulani na kupuuzia nyingine.
Ni sawa na mvuvi ambaye anashikilia uvuvi wa ndoano tu, lakini hajui kuna wa nyavu, au wa mkuki au wa kutegea, lakini pia kuna wa majira mbalimbali ya kuvua, kuna ya usiku, au ya mchana.
Na sisi katika utumishi wetu wa kuwavuta watu kwa Yesu, tufahamu pia njia zote.
Sasa kibiblia zipo kanuni kuu (8), zinazovuta watu.
Hii ndio njia kuu na ya kwanza, ambayo ndio inasimama kama uti wa mgongo wa uinjilisti. Kwamba ni sharti kila mmoja wetu atumie kinywa chake, ujuzi wake, elimu yake, ufahamu wake, kumuhubiri Kristo kwa watu kwa namna yoyote. Utashuhudia shuleni, nyumba kwa nyumba, masokoni, barabarani, vijiweni, mitandaoni n.k. Ni agizo la Bwana na linapaswa lifanywe na wote.
Mathayo 5:16
[16]Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.
Wapo watu si rahisi kugeuka kwa kusikia unawaelezea habari za Yesu, ni rahisi kugeuka wanapomwona yule anayewahubiria mwenendo wake ni tofauti na wa kwao. Na hilo likamchoma moyo na kumfanya amgeukie Kristo moja kwa moja.
Hivyo angaza mwenendo wako, kwa watu, ikiwa hawataamini kwa lile Neno, basi waamini kwa mwenendo wako mzuri.
1Petro 3:1 Kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno; 2 wakiutazama mwenendo wenu safi, na wa hofu
Ni ile hali ya kujaribu kuchukuliana na mawazo ya wale watu, na wakati mwingine hali zao, kana kwamba ni mmojawao, kisha kutumia fursa hiyo kuwaeleza habari za Yesu. Wengine huvitiwa kwanza na jinsi unavyothamini hali zao, sio kwa jinsi unavyo eleza vema Neno au mwenendo wako. Ni njia ambayo aliitumia Paulo na ikamletea matokeo mengi sana ya waongofu.
1Wakorintho 9:19 Maana, ingawa nimekuwa huru kwa watu wote, nalijifanya mtumwa wa wote, ili nipate watu wengi zaidi.
20 Nalikuwa kama Myahudi kwa Wayahudi, ili niwapate Wayahudi; kwa wale walio chini ya sheria, nalikuwa kama chini ya sheria, (ingawa mimi mwenyewe si chini ya sheria), ili niwapate walio chini ya sheria.
21 Kwa wale wasio na sheria nalikuwa kama sina sheria, (si kwamba sina sheria mbele za Mungu, bali mwenye sheria mbele za Kristo), ili niwapate hao wasio na sheria.
22 Kwa wanyonge nalikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu.
23 Nami nafanya mambo yote kwa ajili ya Injili ili kuishiriki pamoja na wengine.
Zingatia kujichanganya sio kushirikana na dhambi zao, hapana, bali kuwepo katikati yao ili kuwaondoa huko, huku wewe mwenyewe ukijilinda nafsi yako usitekwe na dhambi zao.
Unaweza kudhani kila eneo unaweza kuhubiri na kuleta matokeo unayoyatazamia. sio kweli, Mitume walivua samaki usiku kucha lakini hawakupata kitu, baadaye Yesu akawaambia tupeni jarife upande wa kuume mtapata (Yohana 21), sehemu nyingine aliwaambia waende vilindini. Na walipofanya vile walipata samaki wengi. Paulo mwanzoni aliegemea injili yake kwa wayahudi sana, akapitia ukinzani, lakini kumbe Mungu alimkusudia aende kwa mataifa, na alivyotii agizo lile matokeo yakawa makubwa. (Matendo 22:21)
Hivyo ni muhimu kuomba Bwana akupe dira, lakini pia katika kuhubiri kwako utaona eneo Fulani lina matunda mengi, basi ujue hapo ni dira yako. Au njia Fulani ukiitumia wengi huvutiwa kwa Kristo, basi fanya hivyo. Lakini hili ni kuendelea kuomba na kuhubiri Mungu mwenyewe ataielekeza dira yako, kama ni hapo au kwingine, kama ni njia hiyo au njia nyingine, la kuzingatia ni kuwa mwepesi kutambua upepo wa Roho unakufanikisha wapi. Kisha ongeza nguvu nyingi sana hapo, kuliko kule kwingine.
Yapo makundi ambayo, Mungu anajua yakiona tu muujiza au ishara fulani huvutika kirahisi. Na hili pia ni eneo la kumwomba Bwana, ajalie kunyosha mkono wake kuponya maana lina mvuto mkubwa na wa haraka sana.
Kanisa la kwanza liliomba maombi ya namna hiyo.
Matendo 4:29 Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, 30 ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu
Hivyo popote uendapo pia hakikisha unawaombea na watu, shida zao. Kwasababu kwa njia hiyo Roho Mtakatifu hupata nafasi ya kupenyeza mvuto huo, kwao.
Busara ni namna nzuri kunena, hadi kuushawishi moyo wa mtu. Bwana Yesu anataka na sisi tujae busara ndani yetu aliyoifananisha na kama ile ya nyoka.
Mathayo 10:16 Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa-mwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua.
Nyoka alijua akimwendea Hawa kwa ukali, au kulazimisha isingewezekana, lakini alijishusha na kujifanya kama mtu wa mashauri, afichuaye siri, Jambo ambalo ni uongo. Na sisi hatuna budi kujua kunena kwa hekima, ili wale tuwahubirio tuishawishi mioyo yao, mpaka kumgeukia Kristo ambaye ndiye kweli. Tujifunze kueleza uzuri wa Yesu. Lakini pia tusiwe watu wa kauli mbaya kwa tunaowahubiria hata kama watatupinga.
Kuna la watu hatutaweza kulipata kama hatutaingia gharama kubwa kwa ajili yao. Wakati mwingine hata kuhatarisha maisha. Kwasababu mahali walipofungwa na adui, pana ngome nzito. Mfano wa hawa ni wale waliofungwa katika vifungo vikali sana vya kidini.
Kuwang’oa huko ni kujiandaa na dhiki. Cha kuomba hasaa hapa kwa Mungu ni ujasiri kwa kanisa la kwanza lilivyoomba.
Hichi ndio kilele cha juu kabisa cha kiuinjilisti. Ndio wito Yesu aliowaitia mitume wake utakaowafanya wafikie kona zote. Kuwa tayari kufa kwa ajili ya walio dhambini. Ndio maana si wote waliweza kuambatana nao, Bali walibakia tu kuwaadhimisha.
Matendo 5:12 Na kwa mikono ya mitume zikafanyika ishara na maajabu mengi katika watu; nao wote walikuwako kwa nia moja katika ukumbi wa Sulemani;
13 na katika wote wengine hapana hata mmoja aliyethubutu kuambatana nao; ila watu waliwaadhimisha;
Kuna wengine si rahisi kuokoka ki-uinjilisti tu, bali pia kuwaombea. Hii ni njia inayolegeza nira za mwovu mioyoni mwa watu. Injili yako inaweza isiwe na shida lakini mioyo yao ya jiwe ikawa vile, hata uhubirije hawewezi kukuelewa.
Paulo alikuwa ni mtu wa kuwaombea sana watu wake wayahudi waokolewe. Maandiko yanasema ombeaneni ninyi kwa ninyi mpate kuponywa.
Warumi 10:1 Ndugu zangu, nitakayo sana moyoni mwangu, na dua yangu nimwombayo Mungu, ni kwa ajili yao, ili waokolewe.
2 Kwa maana nawashuhudia kwamba wana juhudi kwa ajili ya Mungu, lakini si katika maarifa.
Usione shida kuwaombea ndugu zako ambao hawajaokoka, wafanyakazi wenzako, majirani zako, jamii yako n.k. Ni maombi yasiyo na ukomo fanya hivyo kila siku, maombi yako ni silaha kubwa sana ya kiuinjilisti. Lakini usiombe tu na kukaa ukasema namwachia Bwana. Hapana unawaombea na huku unawahubiria.
Hivyo kwa hitimisho ni kwamba, tukijifunza njia zote hizi, na kuziachilia katika maisha yetu ya kiutumishi ni hakika kuwa lipo kundi litaokoka tu. Lakini kutegemea njia moja peke yake huubana utendaji kazi wa Roho Mtakatifu ndani yetu, . Ukihubiri changanya na hizo nyingine, kisha yeye aamue ni ipi itamvuta mtu kwa wakati huo.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
KWANINI KILA MWAMINI ANAPASWA AWE MHUBIRI WA INJILI
UFUATILIAJI NI SEHEMU YA HUDUMA MUHIMU KWENYE UINJILISTI
About the author