Unajua ni kitu gani kilikuwa kinaendelea siku chache kabla ya Nuhu kuingia Safinani?…Mungu alimwambia Nuhu ingia wewe na mke wako na watoto wako na wanyama wote ndani ya safina..
Sasa kitendo tu cha Nuhu kuingia mule , muda huo huo Mungu aliufunga mlango. Lakini cha kushangaza zaidi ni kuwa tendo la kufunga mlango halikumaanisha kuwa mvua itaanza kunyesha siku hiyo hiyo, hapana tunasoma mvua haikunyesha siku ile ile, bali ilisubiri muda wa siku saba, ndipo baadaye gharika ikashuka.. Mwanzo 7:13-17
Jambo tunaweza kuona hapo ni kuwa mlango wa wokovu ulikuwa umeshafungwa siku kadhaa nyuma kabla ya siku yenyewe ya maangamizi kufika..Pengine baadhi ya watu kuona jinsi mlango ule ulivyofungwa kwa namna isiyokuwa ya kawaida, walighahiri mawazo yao, wakamfuata Nuhu, wakamgongea mlango, wakimwambia Nuhu tufungulie tumegundua ni kweli hii dunia inakwenda kuangamizwa yote hivi karibuni hivyo na sisi tunataka kuzisalimisha roho zetu, tunakusihi utufungulie na sisi tuingie ndani…
Jibu la Nuhu, lilikuwa ni nini?, Mimi sikuufunga mlango, ni Mungu ndiye aliyeufunga na sijui katumia njia gani kuufunga kwasababu sioni hata komeo, wala kufuli pembeni, ni kama vile tumesakafiwa humu ndani, nitawasalidieje ndugu zangu..Ombeni, kwa Mungu labda atawasikia na kuwafungulia huu mlango kwasababu siku yenyewe ya maangamizi naona bado haijafika..
Pengine wale watu wachache waliokuwa pale nje, wakaanza kumlilia Mungu kwa machozi sana ili wafunguliwe mlango lakini hakukuwa na aliyejibu.. wengine walidhihaki na kuona Nuhu ndo kaamua kabisa kujisakafia ndani afie kule,..lakini wale wachache pengine wakaendelea kumsihi Nuhu kutafuta njia ya kuingia safinani.. Siku tano kabla ya gharika, wakaongezeka na wengine tena, nao pia wakawa wanamwambia Nuhu tufungulie ndugu zako, kwa maana kutokana na hali hii tunaoiona inavyoendelea sasa hivi, hii dunia siku chache sana inakwendwa kuangamizwa tufungulie Nuhu, tumetubu na ndio maana tumekuja kabla ya maangamizi yenyewe kufika tunakuomba utufungulie….Lakini Nuhu jibu lake lilikuwa ni lile lile sikuufunga mlango mimi..
Siku tatu kabla gharika, watu bado wanabisha hodi tu, wanatafuta upenyo mdogo lakini hawaoni, siku mbili kabla ya gharika, wanazidi kumsumbua Nuhu labda atafute kiupenyo cha mlango kwa huko ndani uvunje tuingie, lakini biblia inatuambia safina ile ilipigwa lami nje na ndani, hivyo hakukuwa na uwezekano wa kuivunja kiurahisi…
Mpaka ilipotimia siku ile ya gharika yenyewe kushuka,walikuwepo wengi sana pale nje ya safina wakimlilia Mungu, na kubisha hodi kwa bidii sana..lakini walikuwa tayari wameshachelewa..
Ndugu Biblia inatuambia wazi kama ilivyokuwa wote wakaangamia…hakuna aliyesalimika….Sasa biblia inatuambia kama ilivyokuwa katika siku za Nuhu ndivyo itakavyokuja kuwa katika siku za kuja kwake mwana wa Adamu..Bwana Yesu alisema wazi kabisa..
Luka 13:24 “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze.
25 Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana, tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako;
26 ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu.
27 Naye atasema, Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu.
28 Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje”.
Wengi tunadhani mambo hayo yatayokea baada ya kufa, jibu la ni La!, Hayo mambo yatakuwa ni hapa hapa duniani kipindi kifupi kabla ya unyakuo kupita…kuna watu watatamani sana waingizwe katika orodha ya watakaonyakuliwa lakini itakuwa ni ngumu tena..
Fahamu kuwa kitendo cha unyakuo sio kitendo cha kuotea tu, kwamba tunaishi ilimradi tu,halafu siku ile ikifika tutatoweka tu kwa bahati, hapana, Unyakuo unao HATUA zake..Na wale watakaonyakuliwa watajijua kabisa…jambo ambalo hawatajua ni siku yenyewe ya kuondoka, lakini watapewa uhakika huo wa kuondoka wakiwa bado wapo hapa hapa duniani kama vile ilivyokuwa kwa Eliya..
Sasa uhakika huo watautolea wapi?
Ukisoma kitabu cha ufunuo sura ya 10 yote utaona yapo mambo ambayo Yohana alionyeshwa akiwa katika kile kisiwa cha Patmo yahusuyo sauti za zile ngurumo saba, ambapo alipotaka kuziandika aliambiwa asubiri kwanza asiandike….Sasa hizo ni siri ambazo Mungu amezitunza kwa ajili ya bibi-arusi wake anayejiwekwa tayari leo hii kwa unyakuo.. Siri hizo hazijaandikwa mahali popote kwenye biblia..Lakini wakati huo utakapofika, Mungu atazihubiri duniani…Na hizo ndizo zitakazomvuta bibi-arusi ndani ya safina tayari kwa unyakuo siku yoyote..
Sasa wale ambao sio bibi-arusi wa Kristo,watakaposikia hizo jumbe zinahubiriwa, ndipo na wao watakaposhtuka ahaa!! Kwa mambo haya, ndio tunajua sasa unyakuo kweli ni siku yoyote..Hapo ndipo na wao watakapoanza shamra shamra za kumtafuta Mungu kwa kumaanisha, ndipo watakapoanza kubisha na kugonga kwa nguvu, wakitamani nao wahesabiwe..Siku hizo wataitafuta hiyo neema kwa bidii zote lakini hawataipata…
kwasababu mwana wa Adamu ameshasimama na kuufunga mlango…
Hao ndio wale wanawali wapumbavu, waliokwenda kutafuta mafuta na waliporudi wakakuta mlango umeshafunga..Ndivyo itavyokuja kuwa siku za hivi karibuni..(Soma Mathayo 25:1-12)
Nataka nikuambie ukishasikia tu ujumbe mwingine wa tofauti unapita duniani kote kwa nguvu nyingi za Mungu na udhihirisho mwingi, na kusikia mambo mageni masikioni mwako, yahusuyo safari ya kwenda nyumbani kwa Baba, kama bado wewe ni mkristo vuguvugu, basi ujue habari yako imeshakwisha mlango wa neema umekwisha fungwa..Ni heri kama utakuwa umesimama katika utakatifu na imani kwasababu hapo ndipo utakapopata uhakika wa kuondoka kwako hivi karibuni..Lakini kama wewe ni vuguvugu kwasababu hapa hatuzungumzii wale ambao ni baridi kwasababu wao hawataelewa chochote kitakachokuwa kinaendelea, tunamzungumzia wewe ambaye ni vuguvugu, habari yako siku hiyo itakuwa imekwisha..
Wewe ndio itakaoshuhudia wenzako wakienda mbinguni,..Utakuwa umelala na mume wako ambaye kila siku unamwona anajibidiisha kumtafuta Mungu na wewe utajikuta umeachwa, utakuwa unazungumza na mke wako na ghafla ataondoka, mwanao atakuwa amekwenda shule siku hiyo utashangaa harudi…Na ndio maana biblia inatuasa, TUJIWEKE TAYARI, kwa maana hatujui ni siku gani ajapo Bwana ..Hii dunia haina muda mrefu, Unyakuo si jambo la kulichukulia juu juu tu, ukiukosa ule, hali itakayokuwa inaendelea hapa duniani haielezeki, Bwana Yesu anavyosema utalia na kusaga meno alimaanisha kweli hivyo kwamba kusema hivyo kuwa kutakuwa na maombolezo ya ajabu kwa wale ambao watakuokosa unyakuo.
Bwana atutie nguvu katika safari yetu.
Maran Atha.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
USIPOWATAMBUA YANE NA YAMBRE, KATIKA KANISA LA KRISTO, UJUE UMEPOTEA.
About the author