Uovu unapoongezeka sana na kufikia kiwango ambacho watu hawataki tena kubadilika..biblia inatuambia Mungu huwa anaachilia nguvu ya upotevu ili waendelee kuuamini UONGO. Ile nguvu ya kumfanya mtu aone njia anayoiendea sio sawa inaondoka ndani yake na inakuja nguvu nyingine mpya ya kumfanya aone na kuamini asilimia mia kwamba yupo katika njia sahihi.
Mstari huo tunausoma katika kitabu cha..
2Wathesalonike 2:10 “na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa.
11 Kwa hiyo Mungu awaletea nguvu ya upotevu, wauamini uongo;
12 ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu”.
Leo tutaangalia mifano baadhi katika biblia ya watu ambao hawakutaka kudumu katika kweli na hivyo Mungu akawatumia nguvu ya kuamini uongo, ili wakaangamia katika huo.
Huyu ni mtu, Bwana alimuonya asiende kuwalaani Israeli lakini akawa hataki kusikiliza sauti ya Mungu, kinyume chake akawa analazimisha kwenda kuwalaani watu wa Mungu ili apate fedha na umaarufu kutoka kwa Mfalme wa Moabu..alionywa lakini hakusikia…matokeo yake Mungu akamwambia aende! Na yeye kudhani kwamba Mungu tayari kampa kibali alienda pasipo kujua kuwa tayari ile nguvu ya upotevu ya kuuamini uongo inampeleka pabaya…kama sio yule punda kumsaidia angeshakufa..(kasome kitabu cha Hesabu 22).
Huyu Mungu alimwonya mara nyingi sana juu ya uovu wake, ageuke atubu lakini hakusikia, mpaka ilipofika siku ambayo Mungu aliiachia nguvu ya upotevu ishuke juu yake, auamini uongo…Siku hiyo alitaka kwenda vitani na Mungu akatuma pepo la uongo liwaingie manabii wake ili wamwambie uongo…Kwani hao manabii wake kila siku walikuwa wanamwambia ukweli lakini siku hiyo waliingiwa na pepo pasipo wao kujua na kujikuta wanaona maono ya uongo, na kumpotosha mfalme..
1Wafalme 22: 20 “Bwana akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili akwee Ramoth-Gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi.
21 Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, MIMI NITAMDANGANYA.
22 Bwana akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka ukafanye hivyo.
23 Basi angalia, Bwana ametia pepo wa uongo kinywani mwa manabii wako hawa wote; naye Bwana amenena mabaya juu yako”.
Mfalme Ahabu akaenda kwenye vita, akiwa amedanganywa na pasipo kujua kuwa amedanganywa…na akafa!
Mfalme huyu naye njia zake hazikumpendeza Mungu..kwani aliwasumbua sana wana wa Israeli , na wakati ule ambao njaa ilipokuwa kubwa Samaria mpaka kufikia kiwango mavi ya njiwa na kichwa cha punda kuuzwa kwa bei kubwa mjini kutokana na njaa iliyosababishwa na mfalme huyu..Na ndiye aliyemdharau Mungu wa Israeli na kusema ni Mungu wa milimani na si wa nchi tambarare. Na japokuwa Mungu aliyanusuru Maisha yake mara nyingi ili atubu…lakini hakuwahi kutubu Zaidi ya yote alizidi kufanya vita na Israeli. Lakini ilifika siku moja akaugua sana, na akatuma watu wamwendee Elisha Nabii ili aulize kwa Mungu kama atapona au la!…Na kilichotokea ni nguvu ya upotevu kuachiliwa juu yake ili auamini Uongo..
Tusome..
2Wafalme 8:7 “Kisha, Elisha akaenda Dameski; na Ben-hadadi, mfalme wa Shamu, alikuwa hawezi; akaambiwa ya kwamba, Yule mtu wa Mungu amefika hapa
8 Mfalme akamwambia Hazaeli, Chukua zawadi mkononi mwako, ukaende ili kumlaki yule mtu wa Mungu, ukamwulize Bwana kwa kinywa chake, kusema, Je! Nitapona ugonjwa huu?
9 Basi Hazaeli akaenda kumlaki, akachukua zawadi mkononi mwake, za kila kitu chema kilichopatikana Dameski, kiasi cha mizigo ya ngamia arobaini, akaenda, akasimama mbele yake akasema, Mwana wako Ben-hadadi, mfalme wa Shamu, amenituma kwako, kusema, Je nitapona ugonjwa huu?
10 Elisha akamwambia, Enenda, ukamwambie, BILA SHAKA UTAPONA; LAKINI BWANA AMENIONYESHA YA KWAMBA BILA SHAKA ATAKUFA.
…………..14 Ndipo akamwacha Elisha, akarudi kwa bwana wake; naye akamwambia, Elisha alikuambiaje? Akajibu, Aliniambia ya kuwa BILA SHAKA UTAPONA.
15 Ikawa siku ya pili yake, akatwaa tandiko la kitanda, akalichovya katika maji, akalitandaza juu ya uso wake, HATA AKAFA. Na Hazaeli akatawala badala yake”.
Umeona hapo?..Bwana alimwonyesha Elisha kuwa huyo mfalme atakufa lakini alimpa maagizo Elisha amdanganye Ben-hadadi kwamba atapona lakini kumbe atakufa!..
Hiyo ni baadhi ya mifano tu!, ndugu mpendwa saa tunazoishi ni za hatari sana….Tujitahidi sana tuupende na kuufuata ukweli ambao upo katika Neno la Mungu, ili Nguvu hii ya upotevu iliyoachiwa duniani sasa ya kuuamini uongo isije ikatumeza, na ghafla tukajikuta kwenye ziwa la Moto.
Hususani katika kipindi hichi cha siku za Mwisho, uongo umezagaa kila mahali…
Nimewahi kuona muhubiri maarufu akihubiri na kutetea dhambi madhabahuni, hali kadhalika nimeona mwingine akitumia maandiko kabisa kusapoti uvaaji wa suruali na vimini, na kama mtu huyajui maandiko vizuri anakuchukua!..kama ni wa kusoma tu mstari mmoja bila kujua mingine unakwenda na maji! Na maelfu tayari wamechukuliwa!. Hiyo ni mifano tu ya nguvu ya upotevu iliyoachiliwa nyakati hizi ili watu waamini uongo.
2Timotheo 3:13 “lakini watu wabaya na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika”.
Tutubu dhambi, na kujitenga na uovu kwa kadiri tuwezavyo..Bwana atusaidie, tukimwamini yeye, tukimtegemea yeye ni mwaminifu, hawezi kutuacha tukadanganyika au kuchukuliwa na hizo nguvu..Hivyo ni wajibu wetu kumpenda Mungu siku zote kwa nguvu zetu zote, kwa roho zetu zote na kwa akili zetu zote.
Bwana atubariki.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
About the author