Category Archive Mafundisho

MPE MUNGU MAJUTO YAKO.

Kila mwanadamu maadamu amezaliwa na kuishi duniani, ndani yake lazima kuna kiwango tu cha majuto..

Wengine wana majuto makubwa sana, wengine kiasi.

Majuto ni hali ya kuhuzunishwa na matokeo ya machaguzi au maamuzi yaliyofanyika katika maisha.

Kwamfano kijana anaweza kuchagua kukatisha masomo kisha aende mtaani, kuuza peremende, sasa hayo ni maamuzi yake, lakini baadaye anapoona haoni matokeo makubwa, kinyume chake anawaona wenzake waliosoma wamepiga hatua kubwa anaanza kuingiwa na huzuni ya kujishitaki mwenyewe, sasa hayo ndio majuto.

Mwingine amechagua kuishi na mtu bila kufunga naye ndoa, hatimaye akazalishwa, watoto wengi na kuachwa..baadaye umri umeenda anataka kuoelewa, inakuwa shida…anaingiwa na majuto.

Mwingine amepoteza miaka mingi duniani kumtumikia shetani, sasa ameshakuwa mzee anajisikitikiza miaka yake ya ujana aliyoipoteza yenye nguvu alikuwa wapi asimtumikie Mungu…

Majuto yapo ya namna nyingi, na kila mtu kwa sehemu yake anayo majuto fulani, haijalishi unaishi wapi, au umefanikiwa vipi…kuna mahali ulikosea na yakaingia..

Kimsingi majuto sio dhambi, ni hali ya ki-Mungu kabisa ambayo mwanadamu ameumbiwa ndani yake..

Lakini ni vema kujua namna ya kuyaweka mahali pake..kwasababu yasipoweza kutenganishwa ipasavyo hupelekea hasara kubwa mno ndani ya maisha ya mtu.

Katika biblia kulikuwa na watu wawili ambao walihuzunishwa na maamuzi walillyoyafanya …mmoja ni Petro, mwingine ni Yuda.

 Yuda alihuzunishwa lakini huzuni yake ilimpelekea kujinyonga…Petro alihuzunishwa lakini huzuni yake ilipelekea kulilia msaada wa Mungu..(badiliko)

Petro aliruhusu majuto yake yabebwe na Mungu, Yuda aliruhusu yabebwe na shetani.

Lakini majuto yalikuwa yale yale…Yuda hakukosea kujuta hadi kurudisha pesa

2 Wakorintho 7:8-11

[8]Kwa sababu, ijapokuwa naliwahuzunisha kwa waraka ule, sijuti; hata ikiwa nalijuta, naona ya kwamba waraka ule uliwahuzunisha, ingawa ni kwa kitambo tu. 

[9]Sasa nafurahi, si kwa sababu ya ninyi kuhuzunishwa, bali kwa sababu mlihuzunishwa, hata mkatubu. Maana mlihuzunishwa kwa jinsi ya Mungu, ili msipate hasara kwa tendo letu katika neno lo lote. 

[10]Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti. 

[11]Maana, angalieni, kuhuzunishwa kuko huko kwa jinsi ya Mungu kulitenda bidii kama nini ndani yenu; naam, na kujitetea, naam, na kukasirika, naam, na hofu, naam, na shauku, naam, na kujitahidi, naam, na kisasi! Kwa kila njia mmejionyesha wenyewe kuwa safi katika jambo hilo. 

Umeona Majuto ya ki-Mungu huleta toba.. lakini majuto ya shetani hupelekea mauti..

Ukishaanza kujiona kama wewe huwezi tena, Mungu kakuacha, hufai, huna maana, hustahili, ujue shetani yupo nyuma ya juto hilo, ambalo anataka kukusababishia usiinuke tena, ujitenge, ujiue, uache kwenda kanisani, aache maombi, uache kumtafuta Mungu, uache uchungaji …

Kinyume chake unapokosea jione kama ulikuwa unapitishwa katika funzo ambalo sasa unapewa nafasi nyingine usiitmie vibaya…

Watu wengi, unaowaona wamekata tamaa, wamepoa, hawana mabadiliko tena, wamejitenga, lakini hapo zamani walikuwa vizuri, wana mashaka na hofu ya ndani kwa ndani, asilimia kubwa ni majuto mabaya yanawasonga ndani yao.

Daudi alipoanguka katika dhambi ya uzinzi, alimrudia Bwana kwelikweli, ijapokuwa ilimgharimu pakubwa…hakwenda kujificha na uso wa Mungu kama Adamu.

Lakini ya ki-Mungu huturudisha kumtazama Mungu…Rudi umwangalie Mungu wako kisha chukua hatua nyingine, kwani hiyo huwa na nguvu na matokeo ya haraka zaidi ya mwanzo.

Petro baada ya pale alikuwa na ujasiri mkubwa wa kumshuhudia Kristo, zaidi ya mitume wengine wote, ikiwa umefeli mahali fulani embu amka tena kwa nguvu, usikubali kunyong’onyea kama Yuda na mfalme Sauli ambaye alijiua..

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

KUWA MWOMBOLEZAJI.

NI KIPI KINAKULEWESHA?

TUNASHINDA NA ZAIDI YA KUSHINDA

Print this post

IPO NJIA YA MKATO YA KUFIKA KIWANGO VYA MBALI VYA KIROHO.

Maisha ya mwilini mara nyingi hubeba mafundisho ya rohoni, ndio maana Bwana Yesu alitumia sana mifano ya kidunia kuwafundisha siri za ufalme wa mbinguni.

Katika jamii ili mtu aitwe profesa au daktari(kitaaluma) anapaswa awe ni msomi wa kukaa darasani kwa muda mrefu, awe na ujuzi lakini pia na uzoefu wa tafiti nyingi..yaani kwa ufupi haiwezekani ukaitwa daktari(kitaaluma) halafu usiwe msomi wa elimu za juu.

Lakini kuna udaktari ambao mtu anaweza kupewa kwa kutunikiwa, na mara nyingi huu huja pale mtu anapotoa mchango fulani mkubwa katika jamii…mtu kama huyu anaweza kutunukiwa udaktari hata kama yale mafunzo ya ndani ya kitaaluma hana.

Sasa kiroho ni vivyo hivyo unaweza pia ukawa mkufunzi, mwenye ukomavu mkubwa, zaidi ya mababa zako wa kiroho, hata zaidi ya wachungaji wako, au maaskofu wako, au wazee wako wa kiimani, kwa namna gani?

Mstari ufuatao unatupa jibu;

Zaburi 119:99-100

[99]Ninazo akili kuliko wakufunzi wangu wote,

Maana shuhuda zako ndizo nizifikirizo. Ninao ufahamu kuliko wazee, Kwa kuwa nimeyashika mausia yako.

Ukitafakari huo mistari, utaona ni mwanafunzi anayejisifia kuwa ana akili zaidi ya waalimu wake…sio kwamba ameshahitimu, hapana bado yupo chini ya waalimu wake lakini akili zake zimewapita, bado ni kijana lakini ufahamu wake umeshawazidi wazee wake.

Imewezekanikaje?

JE anasoma sana? Au ana kiwapa cha asili tofauti na wengine? Hapana…anasema kwasababu shuhuda za Mungu ndizo anazozitafakari, lakini pia anayashika mahusia ya Mungu .

Hiyo ndio siri yake, usiku na mchana ni kufikiri juu ya “KWELI”, Yaani Neno la Mungu, na na namna ya kulifanya kuwa sehemu ya maisha yake..(kujiepusha na dhambi.)

Hiyo ndio namna inayomkomaza mtu kiroho kwa haraka sana kuliko hata maarifa mengi ambayo wengi hudhani, au mafunuo mengi, au kuhubiri kwingi, au kufundisha kwingi…

Mtu mmoja anaweza akawa na uelewa mkubwa, mwalimu mzuri, mtume mwenye ushawishi mkubwa, lakini bado asimkute mwanafunzi wake ambaye maisha yake anajitahidi kuliishi Neno la Mungu.

Hivyo ndivyo Mungu anavyowatambua wakufunzi wake (kiroho), uwezo wa “kumcha Mungu” haijalishi utapoteza sifa nyingine zote za maarifa,mafunuo, lakini akiwa na hiyo huyo amefika mbali sana.

Kwasababu Biblia inasema hakuna mwisho wa usomi, (kujua maarifa), ila mtu akizingatia kumcha Mungu na kuziishika amri zake, ni zaidi ya usomi wa vitabu vyote.

Mhubiri 12:12-13

[12]Tena, zaidi ya hayo, mwanangu, kubali maonyo; hakuna mwisho wo wote wa kutunga vitabu vingi; na kusoma sana huuchosha mwili.

[13]Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa;

Mche Mungu, nawe uzishike amri zake, Maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu.

Tuwekeze nguvu zetu zote katika kuliishi Neno na neema ya Mungu itusaidie..

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

JE! UNATAKA UITWE MSOMI NA MUNGU?

USIKWEPE CHUO CHA UTAKATIFU.

HAWEZI KUWA MWANAFUNZI WANGU.

Print this post

KAMA NISIPOKUTAWADHA, HUNA SHIRIKA NAMI

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo, karibu katika kuyatafakari maneno ya uzima

Tengeneza picha Mungu amekutokea amesimama mbele yako, wakati ukiwa na mawazo ya kumwangukia chini umsujudie, unashangaa yeye moja kwa moja anakuwa wa kwanza kuinama na kukusafisha miguu yako…

Hivi utajisikiaje? Ukweli ni kwamba hutajisikia huru hata kidogo, kwa ufupi hutakubali kitendo hicho kifanywe na yeye kutoka na ukuu wake, na heshima yake iliyozidi vyote, ni sawa na uone baba amemnunulia mtoto wake zawadi halafu yeye ndio anayekuwa wa kwanza kumshukuru mtoto, tena kwa kumwinamia..ni wazi kuwa hilo halijakaa sawa, au mtu aliyeibiwa mali zake nyingi, halafu amekutana na aliyemwibia badala ya mwenye mali kungojea kuombwa msamaha, yeye ndio anajionyesha kama ni mkosaji kwake…unaona ni jambo ambalo halina uhalisia, halikubaliki kifikra hata kidogo…

Kwa namna ya kawaida hali kama hizi akitendewa mtu hawezi kuridhia…lakini Mungu anatutendea sisi na anasema kama hutukubali kutendewa naye hivyo kamwe hutuna ushirika naye.

Ndicho kilichotokea kwa mitume na Petro. Wakati ule walipomwona Bwana Yesu, anashika kitambaa na maji kisha akaanza kuwaosha na kuwapangusa miguu yao…Petro hakuweza kuridhia akasema Bwana hutanitawadha miguu kamwe. Lakini Yesu akamwambia usipokubali huna ushirika nami.

Yohana 13:8

[8]Petro akamwambia, Wewe hutanitawadha miguu kamwe. Yesu akamwambia, Kama nisipokutawadha, huna shirika nami. 

Hii ni kufunua nini…

Ni lazima tumjue Kristo, ni kweli anasimama kwetu kama mfalme, kama Bwana, kama Mungu…tunamwabudu…lakini pia anasimama kama mtumishi wetu..Ni jambo ambalo haliwezi kuingia akilini  lakini ndivyo alivyo, amependa yeye kuwa hivyo kwetu.

Ni mfalme mwenye taji la kifalme lakini wakati huo huo pia mfalme aliyebeba kitambaa cha kuwasafisha watu miguu.

Hiyo ndio sifa ya ufalme wake. Amesimama kama muumba wetu tumwabuduye, lakini pia anatutumikia, katika kutuponya magonjwa yetu, kutulisha, kutuvisha, kutuombea, kutulinda, kutufuta machozi, na kuchukua mizigo yetu mfano wa punda na hata kufanya mambo ambayo sisi hatuwezi stahimili akitufunulia yote kwa jinsi anavyojishusha na kujishughulisha sana na mambo yetu…. Na mfano tukikataa yeye asituhudumie hivyo anasema wazi kuwa hatuna ushirika naye.

Maana yake ni fahari yake kututendea hayo, wala yeye hayahesabu kuwa ni kitu.

Anatufundisha nini?

Tuwe watumishi pia wa wengine kwa namna hiyo, kama yeye alivyo kwetu…kujitoa kwake sio kutimiza wajibu bali ni fahari yake ambayo isipokubaliwa inaharibu moja kwa moja mahusiano.

Kumsaidia mpendwa mwenzako iwe ni furaha..kujinyenyekeza kwake isiwe ni sababu za umri au cheo bali fahari..Kumwombea iwe ni fahari yako, kumsikiliza iwe ni furaha yako…hivyo ndivyo Bwana anavyotaka.. na ndivyo alivyomwambia Petro.

Yohana 13:12-17

[12]Basi alipokwisha kuwatawadha miguu, na kuyatwaa mavazi yake, na kuketi tena, akawaambia, Je! Mmeelewa na hayo niliyowatendea? 

[13]Ninyi mwaniita, Mwalimu, na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo. 

[14]Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi. 

[15]Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo. 

[16]Amin, amin, nawaambia ninyi, Mtumwa si mkuu kuliko bwana wake; wala mtume si mkuu kuliko yeye aliyempeleka. 

[17]Mkiyajua hayo, heri ninyi mkiyatenda. 

Neema ya Bwana itusaidie.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

WEWE NI ZAO LA MAHUSIANO NA USHIRIKA.

USHIRIKA WA ROHO MTAKATIFU UKAE NANYI NYOTE.

WENGINE WANAKESHA KWAAJILI YAKO.

Print this post

Wale mbweha wadogo, Waiharibuo mizabibu.

Wale mbweha wadogo, Waiharibuo mizabibu

Wimbo ulio bora 2:15

15 : Tukamatie mbweha, Wale mbweha wadogo, Waiharibuo mizabibu, Maana mizabibu yetu yachanua.

Kitabu cha wimbo ulio Bora ni kitabu kinachoeleza asili ya upendo wa Kristo kwetu na jinsi tunavyopaswa kuuitikia.

Kuwa urefu wa masomo yaliyo nyuma ya kitabu hiki fungua hapa >>> NYAKATI TOFAUTI- TOFAUTI ZA UPENDO.

Lakini kwenye mstari huu, tunaona ni kama vile mtu kwa lugha ya picha anaona mbweha “ Wadogo” wamevamia shamba lake la mizabibu inayochanua na hivyo hawapuuzii kwasababu ya udogo wao, bali anatoa tamko la kukamatwa na kuondolewa…ili shamba lake linalochanua liwe salama.

Kimsingi mbweha si mnyama anayekula nyama tu, bali hula pia mizazibu, na mingine kuiharibu.

Hii ni kufunua nini katika hali zetu za rohoni.. 

Adui akishaona mahusiano Yetu na Kristo yanazaa matunda, huinua vitu Vidogo vidogo ili kuharibu mahusiano wakati mwingine unaweza usione kama vina madhara sana au vina nguvu sana, lakini katika eneo la kiroho kitu kidogo kina nguvu sawa na kitu kikubwa…

Hivi ndio vinavyoitwa mbweha wadogo..

Mambo Kama haya ni kama vile kuendekeza vishawishi vya dhambi kwenye maisha yako.

Kwa mfano wewe ni binti halafu kila siku unaona wanaume wanazungumza na wewe maneno ya mizaha, sasa kama usipokemea tabia hiyo, ukaona ni kawaida, tabia hizo ndogo ndogo ndizo zinazopelekea mtu baadaye kuanguka kwenye dhambi za uzinzi.

Samsoni, alipoona ushawishi wa delila unaendelea, badala aukatishe yeye akapuuzia mwisho wa siku akatekwa..

Hao ni mbweha wadogo wanaoharibu shamba lako, kila kichocheo na kishawishi kiwe kidogo kiasi gani usikipuuzie.

Wakati mwingine kuendekeza uvivu wa kiroho, yaani kupuuzia maombi, kupuuzia ibada, kidogo kidogo hupelekea kupoa kiroho, na hatimaye unajikuta kabisa umerudi duniani..mpaka unajiuliza nimefikaje hapa? Ni kwasababu uliendekeza uvivu wa kiroho..ulisema. nitaomba kesho, nikesha kesho, nitamtumikia Mungu mwezi ujao..mwishowe ukawa hivyo ulivyo leo…

Angalia ni eneo lipi la maisha yako limevamiwa na hawa mbweha wadogo, kisha chukua hatua za haraka kurekebisha.

Shalom

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Mwandishi wa kitabu cha wimbo uliobora.

Nini maana ya Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, (Wimbo 2:7)

Pambaja ni nini katika Biblia kama tunavyosoma katika kitabu cha Wimbo ulio bora 1:2?


 

Print this post

WEWE NI NANI PALE AMBAPO WATU HAWAKUONI?

Tunasahau sana maisha yetu ya sirini, na kuweka nguvu kubwa, katika kuonekana kwetu kwa  nje mbele za watu, hatujui kuwa Darasa kubwa la Mungu kwa mwanadamu lipo katika maisha yake ya sirini.  Na Mungu humlipa mtu kwa hayo na si mengine.

Mathayo 6:4….na Baba yako aonaye sirini atakujazi.

Kujazi maana yake ni kulipa.

Ikiwa na maana, unayoyatenda sasa iwe ni mema au mabaya kwa siri, malipo yake utayaona baadaye kwa wazi.

Yusufu, kabla ya kuwekwa kuwa msimamizi wa mali yote ya Farao, alitumika kama wakili mwaminifu katika nyumba ya potifa, kwa muda mrefu. Baadaye Mungu akamlipa kwa kumpa Misri yote.

Yuda mpaka kuingiwa na shetani, hadi kumuuza Bwana wake, ni matokeo ya wizi aliokuwa anaufanya kwa siri kwa muda mrefu.

Daudi kabla ya kujazwa mafuta ya kumwangusha Goliathi, ni maisha ya sirini ya Imani aliyokuwa anayadhihirisha kule maporini kwa Mungu wake, mbele ya simba na dubu walipokuwa wanakuja kulishambulia Kundi. 1 Samweli 17:34-37)

Vilevile, kwa mtu yeyote yule, kupata kibali, kutumiwa na Mungu, kuinuliwa viwango vya kiroho..hutegemea sana hali zetu za sirini zinazoendelea sasa, Kwamfano utakuta labda huyu ni mwanakwaya, au mtumishi wa Mungu, lakini katika maisha yake ya sirini, anajichua, ni mzinzi, anakunywa pombe, Lakini kwa nje, anajionyesha kuwa ni mwema, anautunza ushuhuda wake, anavaa mavazi ya kujisitiri, anaongea kwa staha, ana juhudi katika utumishi, akidhani kuwa hilo ndio litamshawishi Mungu kumwongezea neema.

Ukweli ni kwamba hapo anapoteza nguvu, kwasababu tusipokuwa waaminifu katika madogo ya sirini, Bwana Yesu hawezi kutuaminisha katika makubwa.. Tabia mbaya za sirini, zinaharibu huduma zetu, utumishi wetu wa baadaye.

Mtu anataka apandishwe labda cheo kazini, lakini katika nafasi hiyo hiyo ya chini, anaiba,  mwingine anataka apewe cheo lakini pale pale alipo hawajali watu walio chini yake, ni mwenye wivu, . Unategemea vipi Mungu amlipe mtu kama huyu?

Kabla hujalipwa na Mungu, unakaguliwa kwanza na Mungu.

Shughulika na maisha yako ya binafsi ya sirini, kwasababu hayo ndiyo yanayokueleza utakuwa nani mbele za watu baadaye.

Nini cha kufanya..

Mwalike Bwana, akuchunguze, sirini mwako, Mawazo yako, tabia zako, matendo yako. Kisha mwombe akuponye, na baada ya hapo anza kutendea kazi uliyoyaomba.

Simamia andiko hili;

Zaburi 139:23-24

23 Ee Mungu, unichunguze, uujue moyo wangu, Unijaribu, uyajue mawazo yangu;
24 Uone kama iko njia iletayo majuto ndani yangu, Ukaniongoze katika njia ya milele

Mungu akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

USIIHARIBU TABIA YAKO KWA MAZUNGUMZO YAKO.

NIONYESHE MARAFIKI ZAKO, NIKUAMBIE TABIA ZAKO.

HII NDIO TABIA YA WATU WA KEILA, USIIGE

Print this post

PALE MAOMBI YANAPOGEUKA KUWA MAPAMBANO.

Si kila wakati maombi yatakuwa ni mazungumzo ya utulivu na amani, wakati mwingine maombi hugeuka kuwa mapambano, na ung’ang’anizi, na usumbufu. Kuna nyakati Mungu anabadilika tabia, kuonyesha kama hakujali hivi, hakusikii hivi, Sio kwamba anakuonea, au anafurahia wewe kuendelea kuteseka katika hali hiyo, hapana bali anafanya hivyo ili kukutengeneza wewe, kwa namna usiyoijua.

Ni lazima ufahamu, Mafanikio ya maombi si lazima yawe majibu, bali mafanikio ya maombi ni mabadiliko yako.  Mungu akitaka kukutengeneza, ili tegeo lako lote liwe kwake, hukawia kutimiza ombi Fulani, ili uongeze tegemeo lako lote kwake.

Imani, tumaini, ukomavu, na Upendo wa ki-Mungu, mara nyingi hujengwa katika namna hiyo ya maombi ambayo yanakugharimu kumtaabisha Mungu.

Yakobo alipomtaka Mungu ulinzi, Mungu hakuonyesha kujali hata kidogo, Hivyo mazungumzo yao, yakabadilika kutoka kuwa ya amani, hadi mapambano, wakapigana mweleka usiku kucha mpaka akajeruhiwa uvungu wa paja, ijapokuwa maombi yalikuwa ni ya ung’ang’anizi sana, ya kuumwa, ya kudhoofika, ya kuchakaa, ya kukonda, ya njaa, lakini hakujua anakwenda kubadilisha hali yake ya ndani,  alikuwa anaandiliwa kuwa ISRAELI, na sio Yakobo tena mdhaifu.(Mwanzo 32:24-28)

Fahamu kuwa maombi hufanya jambo la ziada juu ya majibu. Wakati mwingine unaweza usijibiwe kabisa hata hilo ombi unaloliomba lakini fahamu kuwa hutabaki kuwa yule yule.. Mtume Paulo, alimlilia sana Mungu (maombi ya ung’ang’anizi), kuhusu mwiba uliokuwa ubavuni mwake uondolewe, ukweli ni kwamba haukuondolewa, lakini alitoka na ufunuo mpya wa “Neema ya Mungu” ukambadilisha mtazamo wa maisha yake moja kwa moja kuhusu Mungu, Maana yake ni kuwa kama mwiba ule usingemtesa na kumlilia sana Mungu asingeielewa neema ya Mungu, ambayo mpaka leo hii tunajifunza kupitia masumbufu yake.

2Wakorintho 12:7-10

Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi.
Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke.
Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.
10 Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.

Hii ni siri ambayo wengi hawaijui, Uonapo upo kwenye Wakati mgumu na umeomba kwa namna ya kawaida huoni dalili yoyote ya kujibiwa, anza maombi ya kung’ang’ana, funga zaidi, lia zaidi, kemea zaidi, zama zaidi …Fanya hivyo kwasababu ipo kazi ya ziada Mungu anataka kuitenda ndani yako zaidi ya  majibu unayoyataka,. Usiridhike tu na maombi ya utulivu, shindana na Mungu wako, ng’ang’ana sana, ikiwa hujajibiwa jana, endelea leo, tena kwa nguvu zaidi, ukiona hali imekuwa mbaya, usipoe, shughulika na Mungu zaidi na zaidi, hakuna kukata tamaa, hakuna kurudi nyuma, kwasababu Maombi hufanya kazi nyingine ya ndani zaidi ya majibu tu..

Mwisho utauna uzuri wa Mungu, jinsi atakavyokuleta  katika matokeo bora zaidi, ambayo utamshukuru Mungu maisha yako milele. Hivyo fahamu kukawia kwake ni kwa faida yako.

Maombolezo 3:31-33

31 Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtu Hata milele.
32 Maana ajapomhuzunisha atamrehemu, Kwa kadiri ya wingi wa huruma zake.
33 Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu. Wala kuwahuzunisha

Mungu akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

NGUVU YA MAOMBI

MWONGOZO WA MAOMBI YA FAMILIA

MWONGOZO WA MAOMBI YA KUJIKUZA KIROHO.

Print this post

WEWE NI ZAO LA MAHUSIANO NA USHIRIKA.

Ulishawahi kujiuliza, kwanini Mungu atumie  namna ya “wingi”, alipomuumba mwanadamu, na sio, “umoja”, kama alivyokuwa anafanya kwenye uumbaji wa vitu vingine?

Mwanzo 1:26-28

26 Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.
27 Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba

Anasema na “tumfanye” mtu kwa mfano wetu, na si “nimfanye mtu”? Ni kuonyesha hali ya asili ya anaye muumba, kwamba si wa kibinafsi, bali ya kimjumuiko..asili yake ni jumuiya. Ijapokuwa ni Mungu mwenyewe ndio aliyemuumba mwanadamu, lakini wazo lake aliwashirikisha Malaika zake, ambao walikuwepo kabla yetu sisi..Ndio maana ya hiyo “na tumfanye mtu”

Ni kufunua kuwa sisi ni zao la muunganiko, na ushirika, na ndivyo ambavyo tunaweza pia kuzaa, au kufanikiwa katika namna hiyo hiyo.. Ndio maana, hata sisi tukitaka kumleta mwanadamu mwenye asili yetu, sio jambo la mtu binafsi kujitakia pekee yake, ni lazima mwanamume, atakutana na mwanamke, kila mmoja atachangia alichonacho, na mwishowe, anatokea kiumbe kama wao. Hiyo ni kanuni..sisi  kuwepo ni kazi ya “mchango” iliyofanywa na watu wawili.

Hata katika maendeleo yetu, na mafanikio yetu. Jambo lolote tukitaka lifanikiwe, ni sharti tukubali michango.. Haiwezekani mtu kusimama mwenyewe mwenyewe kufanikisha kila jambo., Ukuaji wa kiroho, unahitaji kanisa,  ukutanapo na watakatifu wenzako,(wawili, watatu, mia) ndipo unajengwa na kukua, tofauti na kujisukuma mwenyewe mwenyewe, hakuna mafanikio .

Vilevile na katika maendeleo ya mambo mengine yote ya mwilini na rohoni, wanaofanikiwa, ni watu wenye kuruhusu, michango, kusaidiwa, kujihusianisha, kujishusha, kujengwa, kufundishwa, kushauriwa, kuwezeshwa, na wengine..Na hatimaye kufanikiwa..Mafanikio ya moyoni yaani furaha, amani, utulivu, ni mahusiano mazuri na mema uliyonayo na wengine, katika ushirika wa Roho Mtakatifu.

Mwanadamu kamili, huishi kwa mahusiano. Kuanzia sasa usipuuzie mahusiano, Jenga mizizi yako vema, tafuta kwa bidii kuishi kwa amani na watu wote (Waebrania 12:14). Kwasababu wewe ni zao la Mahusiano, tangu mwanzo.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Print this post

TUNAFAHAMU KWA SEHEMU, TUNAFANYA UNABII PIA KWA SEHEMU.

1 Wakorintho 13:9-10

[9]Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu;

[10]lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika.

Biblia inatupa dira kamili wa maisha yetu, na namna ambavyo tunapaswa kumwelewa Mungu na utendaji kazi wake kwetu sisi. Ni vizuri wewe kama mtoto wa Mungu, kujua ni kipi umewezeshwa kujua na kipi hujawezeshwa..

Watu wengi tunapopitia hili andiko, tunashindwa kulitafakari kwa ndani zaidi, na matokeo yake yanakuwa ni kuishi maisha ya kuhangaika na kutaabika tukidhani kuwa Mungu hasemi au Mungu hajibu.

Roho Mtakatifu anatufundisha kuwa katika eneo la kujua mambo yote, sisi hatujakusudiwa kwa sasa. Hujakusudiwa kuishi duniani ujue kila kitu.

Bali kwa sehemu ndogo tu.. kwa mfano wa sasa tunasema unapewa vidokezo(trailer) vya filamu. Lakini picha nzima ya filamu yote hutaijua sasa, mpaka utakapovuka ng’ambo.

Ndivyo ilivyo katika mambo yote, kwamfano ikiwa mtu unamwomba Mungu akupe kujua jambo Fulani, au akufunulie kila kitu kinachoendelea au kitakachoendelea, au akufunulie kila kitu kinachohusu maisha yako ya sasa au ya baadaye…usitarajie utaonyeshwa taswira yote, kwamba leo itakuwa hivi, kesho vile, mwaka vile, wiki ijayo vile n.k. ndugu haiwi hivyo Mungu atakugusia kwa sehemu tu..ndogo ndogo ambazo hizo zitakupa picha fulani…lakini si taswira yote, kwasababu tumepewa kujua kwa sehemu.

Ikiwa wewe ni nabii, Mungu amekuonyesha jambo, toa unabii kama ulivyoonyeshwa usianze kuweka matukio yako ambayo hujaonyeshwa ..mwisho wa siku utajichanganya mwenyewe au jamii unayoitabiria..kwasababu hata iweje huwezi jua kila kitu, huwezi funuliwa kila jambo hata ulieje.

Ndio yaliyomkuta Yohana Mbatizaji.. aliweka matarajio yake, fikra zake, na kuziamini sana mwisho wa siku akamwona hata Kristo siye…ilihali alimshuhudia mwenyewe ndiye.

Kwamfano leo utaenda kwa nabii, kisha akaonyeshwa kwenye maono umebeba mtoto wa kiume, sasa kwasababu atataka kujifanya yeye ni nabii mwenye viwango vya juu ataanza kutoa simulizi zake za uongo…Bwana ananionyesha utabeba mtoto wa kiume hivi karibuni, hivyo andaa nguo zake, pia mwombee, mwandalie na sadaka ya shukrani.

Lakini kumbe Mungu hakumaanisha atampa mtoto, alimaanisha atamfanikisha na kumfanya mlezi wa mayatima.. kwa taswira ile ya mwanamke aliyembeba mtoto.

Matokeo yake yule mwanamke anaweka matarajio yake hapo, miaka inapita hapati mtoto, baadaye yule nabii anaonekana mwongo. Kumbe sio..ni kwasababu alijaribu kuvuka kipimo cha unabii alichopimiwa.

Angesema Bwana amenionyesha hivi na hivi.. zaidi ya hapo sijui, Mungu atakufunulia mwenyewe, ingetosha kumpa yule mama wigo wa kutafakari maono yake, na yatakapotimia atajua kuwa kumbe tafsiri yake ndio ile.

Vivyo hivyo hata wewe mwenyewe..utamwomba Mungu akuthibitishie jambo Fulani, utagundua mara nyingi hupewi taarifa za kujitosheleza juu ya hilo jambo, utapewa ishara tu, wakati mwingine alama Fulani, .

Ukiona hivyo usihangaike sana kupata picha yote ya kila kitu, bali chukua hatua na Bwana atakuwa na wewe..

Ikiwa ndio hivyo tufanyaje?

Kuishi kwa Imani.

Jambo kuu tuliloumbiwa na Mungu, ni kuishi kwa imani sio kwa kuona.

Jambo lolote lifanye kwa imani, kwasababu hujapewa kujua kila kitu kwa ufasaha wote sasa..

Ikiwa na kushuhudia huwezi kungoja kwanza Mungu akuonyeshe jina la mtaa, aina ya mtu utakayekutana naye, nguo aliyovaa na jina lake ndipo uende…hapo ndugu utangoja sana..

Lakini unaenda kwa imani,.ukiamini lile Neno kwamba “nitakuwa pamoja nanyi mpaka ukamilifu wa dahari,” na matokeo yake unakutana na yule mtu ambaye Mungu amemkusudia kati ya wengi.

Hivyo ndugu fahamu kuwa tunajua kwa sehemu, tunatoa unabii kwa sehemu..

Ndio maana anamalizia kwa kusema;

1 Wakorintho 13:12

[12]Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana.

Tembea kwa Imani. Unabii, maelekezo, taarifa, vinapokuja machache, ni wakati sasa wa kuchukua hatua ya kutenda kuliko kusubiri hapo muda mrefu.

Bwana akubariki

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

HEKIMA NANE(8) ZA KIUINJILISTI, KATIKA KUWAVUA WATU KWA KRISTO.

KUSUDI LA KWANZA LA KUCHAGULIWA NA MUNGU NI LIPI?

PELEKA INJILI KOTE KOTE KWA SADAKA YAKO.

Print this post

UNAJISIKIAJE, KUTEMBEA NA SANDA?

Yohana 11:44

[44]Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake amefungwa leso. Naye Yesu akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake.

Nakusalimu Katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Nataka tujifunze jambo moja Kwa Lazaro aliyefufuliwa…

Kama tunavyojua mtu huyu alikufa, akazikwa na akaoza pia..lakini Bwana Yesu alipofika kaburini Alifanya muujiza mkubwa wa kumfufua.

Na kweli Lazaro alitoka kaburini akiwa mzima kabisa bila shida yoyote…Lakini wengi wetu tunaishia hapo, na kusema Bwana Ametenda muujiza…Lakini Yesu alipomwangalia aliona bado akatoa agizo akisema mfungueni mkamwache aende zake.. Maana yake ni kuwa ufufuo, ulimpa uzima kweli lakini sio uhuru..

Ilihitaji afunguliwe, maana kaburi lilimfunga mikono yake, miguu yake pamoja na uso wake…hata alipofufuka bado liliacha mizizi yake kwa mtu.

Maana yake ni nini..

Ufufuo unafananishwa na wokovu, Mtu anapomwamini Yesu anakuwa tayari amefufuka kutoka katika wafu…lakini hilo peke yake halitoshi, bado Anakuwa na kamba za makaburini (maisha ya kale), hivyo anapaswa afunguliwe…

Ukiokoka haimaanishi, tabia za kale zote zitaondoka siku hiyo hiyo, unahitaji kukubali kufunguliwa, ili uwe huru kwelikweli..

Sanda, zilizomzinga Lazaro, uso wake, miguu, mikono, kama wavu wa bui-bui, hutembei, Hushiki wala huoni…ndio maisha Ya wakristo wengi baada ya kuokoka yalivyo..

Zile tabia za kale wanaendelea nazo, uchungu, wivu, hasira, uadui, maumivu, vinyongo, hofu, wasiwasi, wanashindwa kuendelea mbele kwasababu hawatoi nafasi ya kufunguliwa…

Angalia hapo Bwana Yesu anasema..”Mfungueni, mkamwache aende zake…”

Hasemi jifungue…bali mfungueni…yapo mambo huna budi kukubali kusaidiwa ili upone..

Ndio hapo Mungu akaweka…Kanisa.

Ambapo..

Utakutana na wachungaji.. kukusimamia na kukulisha mpaka utakapokomaa Na kukua vizuri kiroho…kuishi bila kanisa yaani mwenyewe mwenyewe tu, ni sawa na kutembea na sanda lako,

Kumbuka Bwana anatarajia umzalie matunda mara baada ya wokovu wako…yapo majukumu ya kufanya baada ya kuokoka..lakini ikiwa miguu na mikono na uso umefungwa unatarajia nini hapo?

Kubali kufundishika, Kubali kuchungwa, kubali mashauri na kuonywa, kubali kuombewa, kubali kuishi na ndugu (katika Bwana), kubali kusoma Neno, kuomba na wenzako utafunguliwa sana.. zaidi ya kuridhika tu na wokovu ulioupokea ukidhani utazalisha chochote katika hali hiyo hiyo ya kiroho ambayo upo peke yako peke yako.

Mara nyingine hata maono yako huwezi kuyafikia kwasababu umefungwa miguu yako. usisonge mbele.. Ogopa sanda, kama vile unavyoogopa mauti.

Ukijiona  una tabia ambazo haziendani Na hali mpya ya wokovu ulioupokea basi ndio wakati wa kushughulika na sanda lako, kwa kutii na kufuata hayo maagizo. Jiwajibishe, tendea kazi wokovu Wako, kwasababu kila mtu anawajibu wa kufanya hivyo.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Hofu ya Bwana ni nini? (2Wakorintho 5:11)

Sheria ya uhuru ni ipi? (Yakobo 2:12)

Kutawa ni nini? Sawasa na Luka 1:24

Print this post

JE! UMEFIKIA VIGEZO VYA KUWA BABA ROHONI?

Kitabu cha Waraka wa kwanza wa Yohana ni kitabu ambacho kilielekezwa mahususi kwa makundi matatu (3) ya watu, Watoto, vijana, na Wababa.  Sasa sio Watoto au vijana au wababa kimwili, Hapana, bali alikuwa anazungumzia ngazi hizo katika roho, yaani Kundi la Watoto kiroho, vijana kiroho na wababa kiroho.

1Yohana 2:12-14

12 Nawaandikia ninyi, watoto wadogo, kwa sababu mmesamehewa dhambi zenu, kwa ajili ya jina lake.
13 Nawaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nawaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mmemshinda yule mwovu. Nimewaandikia ninyi, watoto, kwa sababu mmemjua Baba.
14 Nimewaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nimewaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu.

WATOTO:

Na kila mmoja wao ameelezwa sifa zao, zinazowafanya wawe vile. Kwamfano Watoto kiroho, anasema  ni kwasababu wamesahewa dhambi, lakini pia wamemjua Baba, tafsiri yake ni nini? Kwa mtu ambaye ni mchanga kiroho, anapokuja kwa Kristo, jambo la kwanza, ambalo atalipitia kwenye maisha yake, ni kutuliwa mizigo, mizito ambayo alikuwa anasumbuka nayo, ambayo asili yake ni dhambi. Ndio hapo ataanza kujiona mwepesi, anapokuja kwa Kristo, anajiona huru, katika kifungoni, anajiona na amani ambayo hajui chanzo chake ni nini, anajiona anapendwa,..Na ndivyo ilivyo upendo wa Mungu kwa huyu mtu unakuwa wa kipekee sana, ndio sababu kwanini anasema nimewaandikia nyinyi Watoto wadogo kwasababu mmesamehewa dhambi zenu, na mmemjua Baba. Hayo ni mambo mawili ambayo walio wa changa kiroho huyapitia.

VIJANA:

Lakini kwa vijana, anasema nimewaandikia kwasababu mmemshinda yule mwovu. Hatua hii ya ujana ni ya kipindi cha ukuaji kiroho, hapa mara nyingi mwamini hukutana sana na majaribu ya shetani, mapingamizi makubwa, vita vya kiimani, misukosuko kwa sababu ya Kristo. Kiroho mtu kama huyu huitwa kijana, kwasababu wakati huu, ijapokuwa atasongwa lakini huwa haachi kumng’ang’ania Mungu, moto wake hauzimiki, hata kidogo, kama ni maombi, kasi huwa ni ile ile, usomaji Neno haupungui,  hata akiumwa haiwi vyepesi kumwacha Mungu, kwasababu ni wakati wa Nguvu za Mungu nyingi Kutenda kazi ndani yake, na kumshinda mwovu kotekote.

WABABA:

Lakini Wababa kiroho, sifa yao pia ni tofauti na hao wengine, Sifa yao ni kuwa “ wamemjua yeye aliye tangu mwanzo”.

Maana yake ni nini? Kwanini hasemi kwasababu mmehubiri sana?, au kwasababu mmedumu sana ndani ya Kristo? Bali kwasababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo?

Kumfahamu Mungu, tangu mbali, ni kigezo kikuu sana cha ukomavu rohoni. Mpaka mitume kuitwa baba zetu, ni kwasababu walipewa kumwona Mungu kutokea mbali, tofauti na waandishi na makuhani..Ndio maana waraka tu huu ulipoanza anasema..

1Yohana 1:1 Lile lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono yetu ikalipapasa, kwa habari ya Neno la uzima;

Hili lilikuja kudhihirika pale Yesu alipoanza kuwaeleza mambo yake mwenyewe aliyoandikiwa tangu, Torati ya Musa, Zaburi na Manabii, jinsi alivyokuwepo na watu wake, jangwani, kupitia ule mwamba, Mana, nyoka wa shaba, jinsi alivyo mtokea Ibrahimu kama Melkizedeki, jinsi alivyojidhihirisha kwao kwa namna mbalimbali kupitia tumbo la Samaki kwa Yona n.k. lakini hawakumwelewa.

Luka 24:44

44 Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii na Zaburi.
45 Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko.

Sasa, mtu akishamwona Mungu kwa namna hiyo, basi Mungu kwake hawi wa “matukio” bali wa wakati wote. Yaani alikuwa nasi jana, yupo nasi leo, na atakuwa nasi hata milele.. Watoto wachanga kiroho, hawawezi kumwona Mungu jana, wenyewe Mungu wao, ni wa matukio ya leo.

Maeneo matatu ambayo macho yako yanapaswa yafunguke kuhusu, kumjua Mungu tangu mwanzo.

  1. Maandiko: Ili uwe Baba kiroho, ni sharti umwone Kristo tangu mwanzo wa uumbaji wote kama alivyowafundisha mitume (Luka 24:44).
  2. Maisha: Ni lazima umtambue Mungu madhihirisho yake tangu mwanzo wa maisha yako (Siku ulipozaliwa), Daudi mpaka kufanywa mchungaji wa Israeli, ni kwasababu alimwona Mungu tangu akiwa machungani, wakati ule alipokutana na dubu na Simba, aligundua kuwa ni Mungu ndiye aliyemsaidia (1Samweli 17:37)..Vivyo hivyo na mtu aliyekomaa kiroho, ataweza kumtambua Mungu, katika matukio mengi ya maisha yake, hata kabla hajaokoka, Na kujifunza Sauti yake
  3. Baada Ya kuokoka: Baada ya wokovu, mtu huwa anaanza maisha mapya, Na sasa ameshakaa muda Fulani mrefu, ni lazima ujifunze kumtambua Mungu katika nyakati mbalimbali alizokupitisha na uijue tabia yake kwako. Nyakati za taabu, za shida, za kufanikiwa na kupungukiwa..umwone Mungu, Jifunze kumjua yeye.. tangu mwanzo.. Ili usiwe tena mtoto mchanga.

Hivyo ile uwe Baba, ni lazima umjue Mungu aliyekuwepo tangu Mwanzo, usiwe mtu wa matukio ya leo leo, kama mtu uliyeokoka jana, Kaa chini, tafakari sana, hatua moja baada ya nyingine ya maisha yako, anzia kwenye maandiko uone jinsi Mungu alivyokuwa na watu wake tangu zamani, ambao wengine kwa kukosa kumjua wakawa wanalalamika tu, wanaishi kiwepesi wepesi, na hatimaye kumsulubisha, lakini wale waliomjua waligeuzwa na kuwa mitume wake,

Kuwa baba rohoni.

Mungu akubariki.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Je umewaonea utungu watoto wako?

Kwa jina lake Ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa.

LAKINI SISI HATUKUIPOKEA ROHO YA DUNIA.

Print this post