HII NDIO TABIA YA WATU WA KEILA, USIIGE

HII NDIO TABIA YA WATU WA KEILA, USIIGE

(1Samweli 23:1-14)

Keila ni moja ya miji midogo  iliyokuwa Israeli, lakini kuna wakati ulipitia taabu kubwa sana ya kuvamiwa na wafilisti, wakateswa wakaibiwa nafaka zao, hivyo wakiwa katika mahangaiko hayo, na mateso hakuna wa kuwasaidia, Maandiko yanatuonesha akatokea Daudi katika maficho yake, alipokuwa anamkimbia Sauli..Akapita katikati ya mji huo,akasikia, kuwa wafilisti wapo huko wanawatesa watu wa Keila.

Lakini Daudi aliguswa sana moyo, hakujali Maisha yake na kuendelea na safari yake ya mafichoni bali alichokifanya ni kukiita kikosi chake kidogo, na kukiambia adhima yake ya kuwasaidia, japokuwa watu wake walikuwa wachache, walijitia nguvu, ndipo Daudi akaenda kumuuliza Mungu, kama akiwapigania watu wa Keila atashinda au hatashinda, Mungu akamwambia, hakika atashinda, akauliza tena na mara nyingine Mungu akamjibu hivyo hivyo kuwa watashinda.

Tengeneza picha, wenyeji wa mtu huyo wanasikia, Shujaa Daudi amekuja kuwasaidia, walifurahi kiasi gani, Na ndivyo ilivyokuwa Daudi akaenda kuwapigania watu hao, akashinda na kurejesha mateka yote, tena  na Zaidi akawarejeshea. 

Wanawake, wazee, vijana wa Keila wakahuika mioyo yao, wakafurahia kuona ng’ombe zao, ngano zao, watumwa wao, mali zao zimerudi.. Waliruka ruka na kucheza, na kumpenda sana Daudi.

Lakini habari mbaya ziliwafikia kwa ghafla watu wa Keila, biblia inasema, Sauli aliyekuwa anamwinda Daudi alipata taarifa kuwa adui yake amefika Keila, kuwasaidia watu wale. Hivyo, akatuma vikosi vyake, kwenda kumkamata. Lakini safari hii sio tena kumtafuta, bali kwenda kuwafuata wakuu wa mji huo, na kuwaambia wamkamate Daudi wamfikishe kwa Sauli ili amuue.

Lakini kabla Sauli hajatuma vikosi vyake, Daudi naye akapata taarifa kuwa Sauli amejua yupo kule, hivyo alichokifanya ni kwenda kumuuliza Mungu kama ilivyokawaida yake, kuhusiana na jambo hilo kama kweli watu wa Keila watamtoa na kumpa Sauli au La..

Matarajio ya Daudi yalikuwa ni hapana, akiamini kuwa wale watu aliowaokoa kwa mkono mkuu, watampa hifadhi watamficha, hawawezi kumsaliti, Lakini Bwana akamwambia Daudi kuwa, hao watu watakutoa kwa Sauli. Hapo Daudi akawa hana jinsi Zaidi ya kuingia tena maporini kwenda kutafuta mahali pa kujificha.

1Samweli 23:7 “Kisha Sauli aliambiwa ya kwamba Daudi amefika Keila. Sauli akasema, Mungu amemtia mkononi mwangu; kwa maana amefungwa ndani, kwa vile alivyoingia katika mji wenye malango na makomeo. 

8 Basi Sauli akawaita watu wote waende vitani, ili waishukie Keila, na kumhusuru Daudi na watu wake.  9 Naye Daudi alifahamu ya kuwa Sauli amemkusudia mabaya; akamwambia Abiathari, kuhani, Lete hapa hiyo naivera. 

10 Ndipo Daudi akasema, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, mimi mtumwa wako nimesikia hakika ya kuwa Sauli anataka kuja huku Keila, ili kuuharibu mji kwa ajili yangu. 

11 Je! Watu wa Keila watanitoa, nitiwe mkononi mwake? Je! Sauli atashuka, kama mtumwa wako alivyosikia? Ee Bwana, Mungu wa Israeli, nakusihi, umwambie mtumwa wako. Naye Bwana akamjibu, Atashuka. 

12 Ndipo Daudi akasema, Je! Watu wa Keila watanitia mimi na watu wangu mkononi mwake Sauli? Bwana akasema, Watakutia. 

13 Basi Daudi na watu wake, ambao wapata kama mia sita, wakaondoka na kutoka Keila, wakaenda po pote walipoweza kwenda. Kisha Sauli akaambiwa ya kwamba Daudi amekimbia toka Keila; akaacha kutoka nje. 

14 Basi Daudi alikuwa akikaa nyikani ngomeni, akakaa katika nchi ya milima milima kwenye nyika ya Zifu. Naye Sauli alikuwa akimtafuta kila siku, lakini Mungu hakumtia mikononi mwake.”

Maana yake ni nini habari hii?

Wenyeji waliona ni heri mmoja wao aangamie lakini mji wote upone mikononi mwa jeshi la Sauli. Hawakujali msaada mkubwa aliowapatia, wakamwogopa mtu ambaye hakuwajali hata kidogo walipokuwa katika mateso yao. Mfano Dhahiri wa watu wa kipindi kile cha Bwana Yesu.. 

Hawakujali miujiza waliyotendewa, hawakujali wafu waliofufuliwa, pepo waliotolewa, vipofu walioona, habari njema za faraja zilizohubiriwa na Yesu, Watoto wao walioponywa. Lakini Waliposikia tu kuna hatari ya Herode kuja kuwaangamiza.. Wakasema ni heri Mmoja afe ili taifa zima lisiangamie.

Yohana 11:47  “Basi wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakakusanya baraza, wakasema, Tunafanya nini? Maana mtu huyu afanya ishara nyingi.

48  Tukimwacha hivi, watu wote watamwamini; na Warumi watakuja, watatuondolea mahali petu na taifa letu.

49  Mtu mmoja miongoni mwao, Kayafa, aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule, akawaambia, Ninyi hamjui neno lo lote;

50  wala hamfikiri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, wala lisiangamie taifa zima”

Wakamsulibisha mwokozi wao.. Hata Sasa hatushangai kuona, watu wakimfurahia Kristo anapowasaidia tu nyakati za mateso yao, anapowabariki, anapowalinda, anapowaponya.. Lakini ikija tu tufani ndogo ya ibilisi kwa ajili ya Kristo, tayari wanamsaliti, wanautupilia mbali wokovu, akiambiwa anafukuzwa kazi kisa Yesu wake, anasahau, mema yote aliyofanyiwa na Bwana siku zote za Maisha yake. Anamwacha. Akiona umri umeenda haolewi, anasema huku kuvaa magauni ya nini tena, ngoja nivae vimini nitembee nusu uchi, ili nipate mchumba.

Tusiwe kama watu Keila, ambao walimsaliti shujaa wao kisa mtu asiyewajali, tusimwache Yesu kisa vitisho vya shetani vidogo vinavyopita mbeleni yetu. Kisa wazazi hawapendezwi na Imani yetu. Tukumbuke yeye ndio jemedari wetu, kama alitupigania vipindi vya nyuma atatupigania hata sasa.

Tumpende Bwana Mungu wetu kwa mioyo yetu yote, kwa nguvu zetu zote, kwa roho zetu zote, na kwa akili zetu zote.

Bwana atusaidie.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

KWANINI DAUDI ALIKUWA NI MTU ALIYEUPENDEZA MOYO WA MUNGU?

Naivera ni nini? Kwanini Daudi aliihitaji alipomtafuta Mungu?

Je! aliyemwua Goliathi ni Daudi au Elhanani.

WALA HAKUSIMAMA MTU PAMOJA NAYE, YUSUFU ALIPOJITAMBULISHA KWA NDUGUZE

UKIOKOKA, JIANDAE KUPITISHWA USIPOPATAZAMIA.

Je tunaruhusiwa kushirikiana na wasanii wa kidunia katika kumwimbia Mungu?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments