Title September 2018

KAMA UNAPENDA MAISHA, NA KUTAKA SIKU YAKO IWE NJEMA.

Biblia inasema maisha yetu yamefananishwa na chombo chochote kinachoendeshwa chenye usukani, mfano wa vyombo hivi vinaweza vikawa ni: Gari, au Meli, au ndege, n.k. vyote hivi pamoja na kwamba vina uwezo mkubwa na nguvu nyingi ya utendaji kazi, lakini haviwezi kujiongoza vyenyewe pasipo USUKANI. Upepo unaweza ukawa mkubwa sana baharini na usifanikiwe kukipeleka chombo mahali kinapotakiwa kufika lakini usukani ni kitu kidogo chenye nguvu chache tu na kikafanikiwa kupindisha merikebu yote na kuielekeza inapotakiwa iende.

Kadhalika na maisha yetu ya Kikristo yanayo usukani wake, Na usukani huo ni nini? Tukisoma biblia tutapata majibu yote:

Yakobo 3: 2-12, Biblia inasema..

“Maana twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo ni mtu mkamilifu, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu.

3 Angalieni, twatia lijamu katika vinywa vya farasi, ili wamtii, hivi twageuza mwili wao wote.

4 Tena angalieni merikebu; ingawa ni kubwa kama nini, na kuchukuliwa na pepo kali, zageuzwa na usukani mdogo sana, ko kote anakoazimia kwenda nahodha.

5 Vivyo hivyo ULIMI nao ni kiungo kidogo, nao hujivuna majivuno makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa sana.

6 NAO ULIMI NI MOTO; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum.

7 Maana kila aina ya wanyama, na ya ndege, na ya vitambaavyo, na ya vitu vilivyomo baharini, vinafugika, navyo vimekwisha kufugwa na wanadamu.

8 Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga; ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti.

9 Kwa huo twamhimidi Mungu Baba yetu, na kwa huo twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mfano wa Mungu.

10 Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo.

11 Je! Chemchemi katika jicho moja hutoa maji matamu na maji machungu?

12 Ndugu zangu, Je! Mtini waweza kuzaa zeituni, au mzabibu kuzaa tini? Kadhalika chemchemi haiwezi kutoa maji ya chumvi na maji matamu “.

Maandiko hayo yanaonyesha wazi kabisa kuwa usukani wa maisha yetu ni ULIMI. Na ulimi kama usukani ni wa kuuchunga sana kuliko vyote kwasababu Shetani akipata tu nafasi ya kuushika huo ataleta maangamizi makubwa kuliko hata angetumia njia nyingine za nje za dhoruba na tufani (ambayo ni majaribu).

Biblia inatuonya mtu anaweza akawa umezingatia kweli kuwa na Dini nzuri, kama kusaidia wajane, kutembelea yatima, kuvaa vizuri, kuzingatia ibada, kutoa sadaka, kufundisha watu,n.k (Yakobo 1:27). lakini kama hakuweza kuungoza usukani wake (Ulimi) basi dini yake yote na matendo yake mema mtu huyo yote yanakuwa ni sawa na bure. Soma.

Yakobo 1: 26 “ Mtu akidhani ya kuwa anayo dini, wala hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hali akijidanganya moyo wake, dini yake mtu huyo haifai. ”

Wewe ni mkristo lakini unakuwa mtu wa kusengenya, kila wakati kuzungumzia watu wengine kwa ubaya, kuchukua taarifa za mtu fulani kupeleka kwa mtu fulani, kutoa siri za mtu fulani na kumfunulia mwingine..Kila wakati unakuwa unatoa maneno yasiyokuwa na maana mdomoni, unatoa maneno ya mizaha ambayo ni aibu hata kwa mkristo kutamka, unatoa maneno ya uchochezi na fitna, unatamka matusi hata haionekani tofauti yako na mtu asiyeamini, kila wakati kuchangia mada zisizokuwa na maana, Sasa hapo hata kama unafanya ibada nzuri kiasi gani mbele za Mungu, au unahubiri kiasi gani, au unasaidia maskini kiasi gani, Dini yako ni bure mbele za Mungu..Ni kwasababu gani?..ni kwasababu Umeshindwa kuutawala usukani wa maisha yako ya kikristo, na umempa mwingine autawale naye ni shetani.

Wakati mwingine ajali nyingi zinazotokea huwa hazisababishwi na mazingira ya nje hapana!, unakuta nyingi zinasababishwa na matatizo ya kiuendeshaji (usukani) . Utakuta chombo ni kizuri tu, hakina matatizo yoyote, ni kipya, na kina uwezo mkubwa wa kupambana na mazingira mabaya ya nje, lakini kwa jambo dogo tu la uzembe katika uendeshaji inapelekea chombo kile kizima kupata ajali. Na ndicho hicho shetani anachokitafuta kwa wakristo, kukimbilia usukuni wa maisha yao (ULIMI) na akiupata huo kammaliza mtu huyo moja kwa moja.

Ndio hapo unajiuliza mbona najitahidi kusali, wakati mwingine kufunga, kutoa sadaka, kusaidia watu, kuhudhuria ibada, lakini siku yangu inakuwa mbaya, mbaya, sina amani na watu, sioni raha ya maisha, ni kwasababu kuna eneo moja la muhimu umemwachia shetani alitawale, usukani wako (Ulimi wako), shetani anapeleka maisha yako uliyoyajenga ya kikristo mahali anapotaka yeye,…Na ndio maana biblia inasema:

1Petro 3: 10 “Kwa maana, ATAKAYE KUPENDA MAISHA, NA KUONA SIKU NJEMA, AUZUIE ULIMI WAKE USINENE MABAYA, NA MIDOMO YAKE ISISEME HILA.

11 Na aache mabaya, atende mema; Atafute amani, aifuate sana.

12 Kwa kuwa macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake husikiliza maombi yao; Bali uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya”.

Unaona hapo?. Shetani anaamka asubuhi kuziloga siku zako kwa kutumia ulimi wako mwenyewe, Mungu amekusudia kukumulikia jua lake la mema lakini anapokuja na kukukuta unamzungumzia ndugu yako vibaya, unamsengenya, anapokuja anakukuta unazungumza maneno ya mizaha, kinywa chako kinaimba nyimbo za kidunia, una laani watu, unawalaumu watu kila wakati,ukikwazwa kidogo tu basi unatoa maneno mengi na yasiyolingana na wokovu, basi na zile Baraka zako zinatoweka, mwisho wa siku, unajikuta mambo yako hayaendi sawa.

Mithali 10: 19 “Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu; Bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili”.

Na pia inasema..

Mithali 21: 23 “ Mtu azuiaye kinywa chake na ulimi wake, Atajilinda nafsi yake na taabu. ”

Na njia pekee ya kuulinda ulimi wako haiji kwa kufunga na kuomba au kwa kuombewa na mtumishi, hapana! inakuja kwa kujizoesha maisha kuwa mbali na hayo mambo, unapoona kuna mazingira yoyote yanayokushawishi wewe kuzungumza maneno yasiyofaa au habari za mtu mwingine, suluhisho pekee ni kuyakataa hayo mazingira, ikiwa ni mtu anakuletea, habari hizo wewe zigeuze kumzungumzia kwa wema Yule mtu,..Ukiletewa mabaya ya mtu Fulani, wewe likumbuke lile moja jema ambalo mtu huyo alishawahi kulitenda na kulizungumzia hilo na yale tisini na tisa mabaya aliyoyatenda yapuuzie..Kwa kufanya hivyo utajikuta unabariki badala ya kulaani, unasifia badala ya kulaumu, unampenda badala ya kumchukia, unamfaurahia badala ya kumwonea wivu. Na ule uovu wote shetani alioupanga juu ya siku yako na maisha yako unayeyuka, Na kwa kufanya hivyo Mungu atakuona na kukuangazia siku zako na kuwa njema kwasababu umeweza kuutawala usukani wako.

Mithali 26: 20 “ Moto hufa kwa kukosa kuni; Na bila mchongezi fitina hukoma. ”..

Hivyo ndugu, huu ni wakati wa kuizoeza chemchemi yako kutoka maji matamu na sio machungu, kutoka Baraka na sio laana kwa faida zetu wenyewe, kwasababu kipimo kile kile tunachowapimia wengine biblia inasema ndio hicho hicho tutakachopimiwa. Baraka zile zile tutakazowabariki wengine ndio hizo hizo tutakazobarikiwa..kadhalika na laani zile zile tutakazowapimia wengine ndizo hizo hizo tukazopimiwa.

Mithali 18: 21 “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake. “

Swali ni je! Unapenda maisha na kuiona siku njema?? Kama ni ndio basi UZUIE ULIMI WAKO USISEME MABAYA …Na Bwana atakusaidia.

Zaburi 141: 3 Ee Bwana, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu.

Bwana Yesu akubariki sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Print this post