Ndoto yoyote ni lazima idondoke kati ya mojawapo ya haya makundi matatu: Kundi la kwanza ni ndoto zinazotoka na Mungu, kundi la pili ni ndoto zinazotoka kwa shetani na kundi la tatu ni ndoto zinazotoka kwa mtu mwenyewe..
Hivyo ukiweza kuelewa jinsi ya kuzigawanya ndoto zako katika makundi haya basi itakuwa ni rahisi kwako kuitafsiri ndoto hiyo bila hata kutegemea msaada kutoka kwa watumishi yeyote wa Mungu.
Kwa mfano, ndoto nyingi tunazoota sisi wanadamu, zinaangukia katika kundi hilo la tatu, yaani ndoto zinazotoka ndani yetu wenyewe, hizi zinakuja kutokana na shughuli mtu anazozifanya mara kwa mara au mazingira yanayomzunguka, kwamfano kama mtu kazi yake ni kuranda mbao siku zote, moja kwa moja atajikuta ndoto anazoota mara kwa mara zinahusiana na urandaji mbao, au labda mazingira yanayomzunguka ni ya wafugaji, hivyo kujiona na yeye anachunga ng’ombe si jambo la kushangaza..
Mhubiri 5:3 “Kwa maana ndoto huja kwa sababu ya shughuli nyingi;…..”
Au utakuta mwingine kabla hajalala labda alikuwa anasikia njaa au kiu, hivyo ni jambo la kawaida katika ndoto za usiku huo kujiona anakula hashibi, au anakunywa maji halafu kiu hakikati, au mwingine mkojo umembana sana usiku , sasa kuota unakoja kitandani hakuepukiki.
Isaya 29:8 “Tena itakuwa kama mtu mwenye njaa aotapo, kumbe, anakula; lakini aamkapo, nafsi yake haina kitu; na kama mtu mwenye kiu aotapo, kumbe, anakunywa; lakini aamkapo, kumbe, anazimia, na nafsi yake inatamani;…….”
Hivyo ikiwa hujahamu bado jinsi ya kujua ndoto yako inaangukia kati ya kundi lipi, fungua kwanza somo hili ulipitie kisha tuendelee..>> NITAJUAJE KAMA NDOTO NI YA MUNGU AU YA SHETANI?
Sasa ndoto hii kwa sehemu kubwa inaangukia katika lile kundi la tatu yaani ndoto zinazotokana na sisi wenyewe, kwamfano, ikiwa umefiwa na mtu wako wa karibu labda tuseme baba au mama au kaka, au mjomba au hata rafiki, hawa ni watu ambao muda mwingi umekuwa nao katika maisha yako, wengine wamekulelea kwa muda mrefu wengine hata miaka 10 au 20 au zaidi, hivyo wanapokufa ghafla, si jambo la kushangaza sana kuendelea kuwaona katika ndoto zako mara kwa mara, kuota unaongea na mtu aliyefariki, na hiyo haitokani na Mungu au shetani..bali ni wewe mwenyewe..inaweza kuendelea hivyo hivyo pengine hata hadi wakati wa kufa kwako, hivyo ukiona ndoto za namna hiyo usiogope, ipuuzie tu,
Lakini pale inapotokea ndoto ya namna hiyo inaambata na vitisho, au unapewa maagizo Fulani, au unalishwa vitu Fulani usivyovijua, au unapelekwa mahali usipopafahamu basi fahamu kuwa hiyo ndoto ni ya kutoka kwa adui, Hivyo hapo unapaswa unapoamka kemea hiyo roho kwa jina la YESU KRISTO, mara moja na mambo hayo yataisha.
Lakini pia wakati mwingine ndoto hizi zinatoka kwa Mungu mwenyewe.. Mungu anakuonyesha kuwa kuna maisha baada ya kifo, na kwamba kama mpendwa wako alikuwa ni mtakatifu basi hajafa bali yupo hai sehemu nyingine anaishi..Lakini sio kwamba Yule unayemwona unaongea naye kwenye ndoto ndiye mwenyewe hapana, ile ni lugha tu ya ndoto Mungu anaitumia kukufikishia ujumbe unaoweza kuuelewa juu ya ndugu zako waliolala katika Kristo.
1Wathesalonike 4:13 “Lakini, ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini.
14 Maana, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye.”
Vilevile kama upo nje ya Kristo, bado Mungu anakuonyesha kuwa kifo cha hapa duniani sio safari ya mwisho, kwamba ipo ng’ambo nawe siku moja utafika huko utakutana na wale waliokutangulia, Sasa kama utaendelea kuwa mwovu basi sehemu yako itakuwa na wale waovu Jehanum, lakini kama utataka kuwa mtakatifu basi pia sehemu yako nawe itakuwa na wale watakatifu walio paradiso wakingojea ufufuo siku ile ya Unyakuo waende na Bwana Yesu mawinguni..
Hivyo kama bado upo nje ya Kristo unasubiri nini?. Tubu leo mgeukie yeye..Ndoto za namna hiyo ni kuonyesha kuwa Mungu anataka umalize safari yako salama hapa duniani, ufikie mwisho mzuri…Siku ile ukutane na watakatifu wengine kwa pamoja mkaishi milele na Mungu.
Ubarikiwe sana..
Jiunge na Group letu ya whatsapp, la masomo ya kila siku kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
Mada Nyinginezo:
TOFAUTI KATI YA NDOTO NA MAONO NI IPI?
NI JAMBO GANI LINALOMTAMANISHA SANA BWANA TUMWOMBE BILA KUKATA TAMAA?
NITAIFAHAMU VIPI KARAMA YANGU?
Shalom mtumishi wa Mungu. Nimependezwa sana na jinsi ulivyotafsiri ndoto ya mtu kuota akiwa anapaa. Binafsi mara kadhaa nimekua nikiota naogolea kwa umahiri mkubwa wakati mwingine baharini na wakati mwingine kwenye swimming pool. Binafsi sijui kuogelea ila katika ndoto nilikuwa nikiogelea kwa kasi na umbali mrefu sana na nimekuwa nikifurahia hilo. Maana yake ni nini?
About the author