UMUHIMU WA YESU KWETU.

UMUHIMU WA YESU KWETU.

Umuhimu wa Yesu kwetu, ni mkubwa sana kama tunavyousoma katika kitabu cha .Waefeso 4:13 “hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na KUMFAHAMU SANA MWANA WA MUNGU, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;”

Shalom jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tena tujifunze Neno la Mungu, ambalo ndio taa ingozayo miguu yetu na mwanga wa njia zetu.(Zab 119:105).

Kama tulivyotangulia kujifunza, na kama wengi wetu tunavyojua kwamba mtu wa rohoni sio mtu mwenye uwezo wa kuwaona wachawi..kama inavyoaminika na wengi.. Wale watu wawili waliokuwa wanakwenda Emau, macho yao ya rohoni yalipofumbuliwa hawakuona wachawi, au majini yaliyokuwa yanawazunguka..Bali walimwona Yesu.(kasome Luka 24:13-33,)

Hivyo mtu wa rohoni ni Yule mwenye uwezo wa kumwona na kumtambua Yesu Kristo katika maandiko na katika maisha yake. Mtu aliyefunuliwa macho ya rohoni atamjua sana Mwana wa Mungu, Yesu Kristo Zaidi ya kitu kingine chochote,atajua dhumuni la yeye kuja duniani ni lipi, mamlaka aliyonayo nayo ni yapi, nafasi aliyonayo sasahivi ni ipi, na ni wapi kaandikwa katika maandiko, na umuhimu wa Yesu katikati ya wanadamu…Na mtu wa namna hiyo ataishia kumheshimu na kuwa mwangalifu na Maisha yake kuwa ya kipekee sana.

Ukishindwa kumwelewa Yesu Kristo, basi haijalishi unaona maono kiasi gani, au una elimu  ya dini kubwa kiasi gani, au unaelimu nyingine kubwa kiasi gani, au unaona wachawi kiasi gani, bado wewe ni mfu kiroho na macho yako ya rohoni yamefumbwa… Kiini cha kumwona na kumjua Mungu ni Yesu Kristo.

Wakolosai 2:9  “Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili”

Na ndio maana Biblia inatuambia tena katika ”..

Waefeso 4:13 “hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na KUMFAHAMU SANA MWANA WA MUNGU, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;”

Hivyo tunahitaji kumahamu sana huyu MWANA WA MUNGU, mafundisho yetu, mawazo yetu, shule yetu wakati wote inapaswa ilenge katika huyu mtu mmoja Yesu Kristo..Ili tuwe watu wa rohoni. Na leo kwa neema za Mungu tutajifunza kidogo juu ya huyu mwana wa Mungu (Yesu Kristo).

Tofauti na wengi tudhaniavyo kwamba Yesu Kristo anahitaji sana sifa kutoka kwetu..pasipo kumjua yeye ni nani?..Lakini ukweli ni kwamba Yesu Kristo anahitaji kwanza tumjue ndipo sifa zetu ziwe na maana kwake.  Hata katika hali ya kawaida, huwezi kuzithamini pongezi au sifa za mtu ambaye hakujui, ametokea tu huko ghafla na amesikia tu jina lako mitaani..halafu anakuja na kuanza kukupongeza na kukusifia kidogo utakuwa na mashaka..jambo la kwanza utamwuliza..je unanijua?…Tofauti na kama ingekuwa ni ndugu yako, ni wazi kuwa pongezi hizo utazithamini kwasababu anakujua sana,  anajua ulipotoka, uliyopitia, ulipo sasa na unapokwenda…

Hivyo pongezi zake zitakuwa na maana sana kwako kuliko za hao wengine ambao hawakujui wala hamjuani..Utafahamu ni za kinafki tu.

Kwahiyo hata sifa zetu tunazomsifia Bwana kama hazijachanganyikana na maarifa yakutosha ya kumjua yeye kiundani..basi sifa zetu ni za kishabiki tu ambazo hazina nguvu yoyote kwa Mungu.

Sasa hebu kwa ufupi tumwangalie kdogo huyu mwana wa Mungu (yaani umuhimu wa Yesu kwetu wanadamu).

Mungu alipomwumba Adamu alimpa mamlaka yote ya duniani..ikiwemo kutawala kila kiumbe pamoja na kuitiisha nchi..Adamu na uzao wake akafanywa kuwa mtawala wa vitu vyote..Hata shetani alikuwa chini yake,..hakuna kiumbe chochote kingekuwa na mamlaka ya  kusogeza hata jani moja isipokuwa kwa mamlaka ya Adamu, mamlaka hiyo Adamu aliendelea kuwa nayo mpaka  siku Hawa alipodanganywa na nyoka na kula tuna na kumpa mumewe..na wote wawili walipoasi hiyo mamlaka yote waliyopewa wakamwuzia shetani. Hivyo shetani akawa mtawala wa ulimwengu..akitaka kumtupia mwanadamu ugonjwa anweza, hata akitaka kumwua anao uwezo huo. Akitaka kuleta tufani anaweza na mwanadamu yoyote asimzuie.

Na hata funguo za kuzimu pia alizichukuwa shetani. Habari yetu sisi wanadamu ikawa imeishia pale, tukawa tumejiharibia wenyewe..Tukawa kundi moja na malaika walioasi, ambao wanasubiriwa kutupwa katika lile ziwa la moto…Kukawa hakuna tena nafasi ya kusamehewa, njia ya uzima ikafungwa kama ilivyofungwa kwa malaika walioasi mbinguni..shetani hakuwa na nafasi ya kutubu wala kuokolewa…Na sisi tukawa ndio hivyo hivyo..Hivyo likawa limesalia jambo moja tu mbele yetu, kufutwa sisi sote…

Lakini kwa huruma za Mungu..akatengeneza njia ya wokovu kwa mwanadamu….kwamba mwanadamu aokolewe..yaani ni kama bahati tu!..shetani na mapepo yake hawakupata hiyo bahati ya nafasi ya pili kama tuliyopata sisi. Na kwasababu ni mwanadamu ndiye aliyejiharibia hamna budi kwa njia ya mwanadamu huyo huyo ukombozi utokee.

Hivyo Mungu akaanza uumbaji mwingine wa mtu mwingine, ambaye huyo atakuwa kama Adamu..ambaye atapewa mamlaka yote ya duniani, atawale kila kitu na kila kiumbe,na vitu vyote viwe chini yake, kama Adamu, mtu huyo Ataumbwa akiwa mkamilifu na bila dhambi kama alivyoumbwa Adamu. Na huyo si mwingine zaidi ya YESU KRISTO..Huyu Yesu ni Adamu wa Pili….Ameumbwa kwa viganja vya Mungu kwa uweza wa Roho katika tumbo la Bikira. Huyu alikuwa ni mwanadamu kabisa, lakini kuna SIRI kubwa iliyokuwepo ndani yake…japokuwa alionekana kama mwanadamu lakini alikuwa ni Mungu mwenyewe aliyeuvaa mwili..(kasome 1Timotheo 3:16). Lakini hilo halikuwa la muhimu sana sisi kulijua ndio maana biblia ikaliita ni siri..

Hivyo wakati wa Yesu Kristo kama Adamu wa pili kuzaliwa, kulikuwepo na kizazi pia cha Adamu ambacho kilishaasi na hivyo kinapaswa kiondolewe kibaki kizazi cha Yesu Kristo tu!.. Sasa Yesu Kristo hakuwa na mke wa kimwili kama Adamu wa kwanza..wala hakuwa na watoto wa kimwili…Kwasababu hiyo basi ili sisi tusiangamie na hiyo ghadhabu ya Mungu itakayomwangwa juu ya uzao wote wa Adamu ulioasi akatutwaa sisi na kutufanya kuwa kama uzao wake, na ndugu zake wakike na wakiume..(akatu-adopt).

Ulishawahi kuona mtu ambaye ni tajiri sana hana watoto, anakwenda nchi ya mbali  kutafuta mayatima ambao maisha yao yapo hatarini na kuwaleta kwake na kuwafanya kuwa wanawe? (anawaa-adopt)..Ndio hicho hicho, Bwana Yesu alichokifanya kwetu…alitutwaa sisi ambao tayari tulikuwa tumeshatamkiwa hukumu na kutufanya kuwa wake..Hivyo kwa yeyote ambaye atatii na kumkubali na kujiunga naye atahesabiwa kuwa ni uzao wa Yesu Kristo,  naye pia atashiriki pamoja naye katika ufalme aliopewa na Mungu kwamba akatawale viumbe vyote, na kila kitu kilichopo duniani, na vitu vyote.

Mathayo 28:18 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani”.

Sasa kabla ya wakati wa kuondolewa uzao wote wa Adamu ulioasi haujafika,Bwana Yesu  anatuma kwanza mwaliko, kwamba popote pale wanadamu wote walipo walio wa uzao wa Adamu wa kwanza walioasi ambao wanapenda maisha, waje kwake naye atawapokea…kwamba wamwendee huyu Yesu Kristo aliyekabidhiwa mamlaka yote ya mbinguni na duniani wapate uzima.

Na huyu Yesu alianza kutuma mwaliko huo tangu vizazi vyuma na hata sasa anatuma..kwamba ufalme wake kuanza kutawala dunia umekaribia..kwamba muda ni mchache tu tuliobakiwa nao wa sisi kuitikia wito wa kuingia ndani ya hiyo neema..Utafika wakati wa utawala wake kuanza ambapo kutakuwa hakuna tena nafasi ya mtu yoyote kuingia..Mlango wa neema utafungwa.

Luka 13:23 “Mtu mmoja akamwuliza, Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache? Akawaambia,

24 Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze.

25 Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana, tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako;

26 ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu.

27 Naye atasema, Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu”.

Wakati huo huyu Yesu Kristo tunayemwona sasa ambaye anatusihi sasa hatakuwa hivi tunavyomwona leo..Atageuka na kuwa miale ya moto,na  Mungu atakihukumu kizazi chote cha Adamu kilichoasi na kumkataa mwanawe mpendwa…na kuwanusuru wale wote waliomkimbilia Mwanawe pekee Yesu Kristo.

Unaweza kuona jinsi hiyo neema ilivyo ya ajabu..Sisi kupata nafasi ya kufanyika Uzao wa Yesu Kristo?…Watu ambao tulikuwa tumewekwa kundi moja na malaika walioasi?..

1Petro 2:9 “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu;

10 ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema”.

Ndugu Bwana Yesu ndiye aliyekabidhiwa kila kitu sasa…Hajaanza kutawala kwa utukufu wake sasa wala kuushusha  ufalme wake, kwasabababu bado anataka watu watubu ili wasiangamia…lakini fahamu kuwa ufalme wake umekaribia sana…na siku atakapokuja mataifa yote waliomkataa wataomboleza na kulia….Kama ulikuwa unamfahamu tu Yesu Kristo kama “mwanadamu wa kawaida ambaye hana umuhimu sana”..leo futa hayo mawazo…Yule sio wa kawaida kabisa…kashakabidhiwa mambo yote na sasa hivi yupo mbinguni,  angekuwa ni wa kawaida angekuwa duniani sasahivi au kaburini…lakini yupo mbingu ya juu sasa, ambako hakuna aliyewahi kufika hata sasa,  anasubiri mtu wa mwisho kuingia ndani, mlango ufungwe ashuke kuja kutawala…

Mathayo 28.16 “Na wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda Galilaya mpaka mlima ule aliowaagiza Yesu.

17 Nao walipomwona, walimsujudia; lakini baadhi yao waliona shaka.

18 Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, NIMEPEWA MAMLAKA YOTE MBINGUNI NA DUNIANI”.

Je bado unamchukulia kama ulivyokuwa unamchukulia?..Je bado unaichezea neema yake hiyo?..na kuendelea kuupenda ulimwengu?..bado unaendelea kuwa mzinzi, mtukanaji, mlevi, washerati, mvaaji nusu uchi, muwekaji make-up, mvaaji suruali,mpakaji wanja, lipstick, mvaaji mawigi na maherini? bado mtazamaji picha chafu mitandaoni, mfanyaji masturbation na mhudhuriaji disko,mtoaji mimba, bado unaendelea kuishi na mwanamke/mwanamume ambaye hamjaoana n.k?..

Itakuwa ni vizuri kama utamgeukia leo..Yeye atakupokea, na wokovu ni leo na si kesho kwasababu hujui mwisho wako ni lini..Hivyo kama umeamua kuingia na kufanyika mwanawe..unachopaswa kufanya hapo ulipo ni kijitenga binafsi kwa dakika chache peke yako..Kisha piga magoti na nyosha mikono yako juu kuonyesha kuwa umejishusha na umejitambua wewe ni mkosaji..

Halafu anza kutubu kwa kuyakiri makosa yako yote, na yeye atakusamehe..na ukishatubu kwa namna hiyo hakikisha unaacha yale mambo uliyokuwa unayafanya..unaacha uzinzi, unatupa makeup zote, unachoma nguo zote za kikahaba ulizokuwa unavaa, unaacha kwenda bar, unaacha pia kuvuta sigara na kujitenga na makundi yote yanayochochoe hivyo vitu.

Na ukishaacha vyote kwa namna hiyo, toba yako itakuwa thabiti..Hatua inayofuata katafute ubatizo kama hujabatizwa, ubatizo sahihi ni ule wa maji tele (Yohana 3:23), na kwa jina la Yesu Kristo (Matendo 2:3)Na Mungu atakupa uwezo wa ajabu wa kushinda hizo dhambi..haitakuwa ngumu kwako kuishi bila kuzifanya. Na Roho Mtakatifu atakuongoza kufanya yaliyosalia..Na kuzidi kukufundisha umuhimu wa Yesu katika maisha yako na ya watu wengine.

Kumbuka ufalme wake umekaribia..na yeye ajaye aja upesi na wala hatakawia.

Bwana akubariki.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine:


Mada Nyinginezo:

MWANA WA MUNGU.

SIRI YA MUNGU.

KWANINI YESU KRISTO NI MWANA WA DAUDI?

KWANINI MUNGU ALITUUMBA WANADAMU.

JE ADAMU ALIKUWA NA KITOVU?

JE ! BWANA YESU ALIKUJA DUNIANI KUAMUA NINI?

Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Ismaël Simon
Ismaël Simon
2 years ago

Nahitaji mafundisho haya kupitia email yangu hii