Tunaweza kujifunza nini juu ya Kifo cha Mtakatifu Polikapi?
Polikapi aliishi kati kipindi cha mwaka 69-159 WK. Alikuwa ni askofu wa kanisa la Smirna ambaye alikuwa pia ni mwanafunzi wa Mtume Yohana.
Wakati ule wa kanisa la kwanza kama wengi wetu tunavyojua, Utawala wa Roma ulikuwa na vita vikali sana dhidi ya wakristo wote ulimwenguni. Na sababu kuu ilikuwa ni wao kukataa kuabudu miungu yao ya kipagani na sanamu za kirumi, na pale wanapoona watu wengi wanavutwa kuiacha Imani yao na kumgeukia Kristo ndipo walipozidisha mapambano makubwa dhidi ya wakristo.. Ilikuwa ni unachagua moja aidha umkane Kristo uishi au umkiri Ufe..
Ndio maana kwa kanisa la Kwanza, lile Neno la Mtume Paulo, linalosema.
Warumi 10:9 ‘Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka’.
Lilikuwa linamaana kubwa sana, tofauti na linavyotafsiriwa sasa hivi..Kwasababu ilifikia hatua ukimkiri Yesu tu kuwa ni mwokozi wa huu ulimwenguni adhabu yake ilikuwa ni kifo cha kukatwa kichwa au kutupwa katika tundu la simba. Sio leo hii watu tunasema tumemkiri Yesu, lakini tukiambiwa tu tujitwike misalaba yetu tumfuate licha ya kuuawa, utasikia watu wanasema hiyo ni dini ya itikadi kali..huo ni ulokole ule wa zamani..
Bwana atusaidie..
Sasa baada ya wakristo wengi kuuliwa katika kanisa la kwanza wengine kwa kutupwa katika viwanja vya simba na wengine kutundikwa kwenye miti, na wengine kukatwa vichwa ikafika wakati sasa wakawahitaji na wale viongozi wao wakuu wa juu kabisa wawaue, na mmojawapo alikuwa ni huyu Polikapi wa kanisa la Smirna lililokuwa Asia ndogo (ambayo ni Uturuki kwa sasa)..
Hapo ndipo harakati za kumtafuta Polikapi zilipoanza, wakatumiwa maaskari wa jeshi wengi sana kwenda kumtafuta, Lakini Polikapi aliposhauriwa na baadhi ya wafuasi wake ahame miji akimbilie mwingine, yeye alikataa, kinyume chake zile habari hata hazikumwogopesha bali alikwenda katika mojawapo ya nyumba ya marafiki zake, akawa akikaa huko usiku na mchana akiomba na kuliombea kanisa la Kristo ulimwenguni kote..Na siku tatu kabla ya kukamatwa kwake anasema aliona maono, katika maono hayo anasema aliona mto wa kulalia wa moto ulikuwa chini ya kichwa chake..Ndipo akaenda kuwaambia wafuasi wake kuwa atakwenda kuchomwa moto akiwa mzima…
Sasa wale askari walipofika na kumkuta walishtuka kidogo, kumuona mbona ni mtu mzee ambaye hakukuwa hata na haja ya kumwendea na majeshi na askari na marungu, na mapanga?…Kama tu ile picha ya Bwana Yesu alipokuwa pale Gethsemane, wale askari walipomwendea na marungu na mapanga wakidhani atakuwa bonsa mwenye ma-boardguards na misuli mikubwa, lakini walimkuta jinsi wasivyotegemea…hata wakaanza kuhisi huyo siye Yesu waliotumwa kumtafuta labda kuna Yesu mwingine…ndio maana walikuwa wanakazana kumwambia Tunamtafuta Yesu, japo Bwana Yesu alikuwa anawaambia mnayemtafuta ndiye mimi..lakini bado walikuwa hawaamini wanachokiona.
Na vivyo Polikapi alipowaona wale askari, aliwakaribisha kwake kama vile wageni wake, akawapa chakula wakala, kisha akawaomba haja moja kabla hawajamchukua, nayo ni ‘kuomba Lisaa’ limoja kisha ndio wamchukue wampeleke kwenye uwanja wa mauaji..Ndipo wale askari wakamkubalia haja yake, Polikapi akaanza kuomba lakini maombi yake yalipitiliza mpaka masaa mawili, ndipo wale askari wakiwa pale wakaanza Kujijutia mioyoni ni kwanini walitumwa kuja kumshika mtu kama huyu mkarimu asiye na hatia…Lakini hakukuwa na namna ilibidi wafanye vile kama walivyoagizwa.
Na walipomleta sasa katika uwanja wa mauaji ambapo watu wengi walikuwa wanamngoja auawe, Lakini wale pia walipomwona kuwa ni mzee wakaona haileti maana sana kumuua mzee kama yule. Hivyo utawala ukamtaka neno moja tu kwake kwamba “Amlaani Kristo, nao watamwachia”
Ndipo Polikapi akafungua kinywa chake na kuwaambia “Kwa miaka nane na mi-sita (akimaanisha miaka 86), nimekuwa nikimtumikia na hajawahi kunifanyia ubaya wowote. Nitawezaje kumkufuru Mwokozi wangu na mfalme wangu”?.
Lakini wale wakuu wa kirumi wakafanya kama,wanampa nafasi nyingine tena..wakamwambia.. “Wewe mzee Apa leo kwa mkuu wa Ngome hii na hiyo tu itatosha” tukuachie..(mkuu wa ngome ni mkuu wa miungu wanayoitumikia)..
Lakini Polikapi akawaambia.. “Kama mnamatumaini ninaweza kufanya kitendo kama hicho, nadhani mtakuwa mnajifanya kuwa hamjui mimi ni nani….Mnisikilize wote mimi ni mkristo!!
Wale wakuu wakaanza kumtishia kwa wale Wanyama wakali waliokuwa nao..Kisha wakamwambia tutakuchoma kwa moto..
Polikapi akawaambia “Mnanitishia kwa moto wa kitambo ambao baada ya muda mfupi tu utazima. Lakini mnajitoa ufahamu juu ya moto wa mateso ya milele ambao umeandaliwa kwa ajili ya watu waovu”.
Basi wakamchoma Polikapi kama vile nyama choma iliyowekwa juu ya mkaa, lakini walipoona haungui wakammalizia kwa mkuki na alipokuwa anakiribia kufa alisema,
“Ninakubariki Baba kwa kunipangia hukumu hii ninayostahili, ili kwamba katika kundi la wafia Imani nami pia nikinywee kikombe cha Kristo”.
Hivyo ndivyo alivyokufa Mtakatifu Polikapi kama mshindania Imani mwaminifu..(kifo cha mtakatifu polikapi na watakatifu wengine vimebeba ujumbe wa muhimu sana kwetu)
Vivyo hivyo na sisi biblia inatuambia..
Waebrania 12:1 “Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu, 2 tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu”.
Waebrania 12:1 “Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu,
2 tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu”.
Ikiwa sisi hatujafikia hatua ya kumwaga damu, lakini tunaona ni shida kuishi Maisha ya kikristo tungekuwa wakati huo tungesemaje?. Lakini mimi na wewe tumepewa neema ya kumpokea Kristo katika kipindi cha amani kama hichi..Sasa tukishindwa kuipokea siku ile tutajiteteaje mbele za Mungu aliye hai?. Au tutajilinganishaje na mashahidi waaminifu kama hawa, wakina Antipa, Polikapi na wengine..?
Hivyo biblia inatuasa, tuitupilie mbali dhambi ile ituzingayo kwa upesi,..tupige mwendo..Tukubali sasa kujitwika misalaba yetu na kumfuata Kristo kwa gharama zozote, tukubali kuchekwa, kudharauliwa, tukubali kusemwa tunapotupa vimini na kuacha kuvaa suruali na wigi na kuacha usengenyaji …Tunapaswa tukubali hata dhihaka tunapoacha kuongozana na kampani za watenda mabaya, na walevi, na wezi….tunapoanza kuongeza viwango vyetu vya maombi, na kumtafuta Mungu kwa bidii..tukubali kupitia vita vya kiimani n.k.Hatupaswi kukisoma tu kifo cha Mtakatifu Polikapi na vifo vya watakatifu wengine kama hadithi bali kama mfano wa kuigwa katika vipindi tunavyopitia sasa.
Bwana atusaidie sana..
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
UNYAKUO.
USIMPE NGUVU SHETANI.
SAYUNI ni nini?
IVUMBUE INJILI YA KRISTO KUTOKA KATIKA KILA JAMBO.
HISTORIA YA ISRAELI.
KUFUKIZA UVUMBA NDIO KUFANYAJE?
Rudi Nyumbani:
Print this post