Shalom. Jina kuu la Mwokozi wetu Yesu Kristo, libarikiwe.
Karibu tujifunze biblia.
Mathayo 3:5 “Ndipo walipomwendea Yerusalemu, na Uyahudi wote, na nchi zote za kandokando ya Yordani;
6 naye akawabatiza katika mto wa Yordani, huku wakiziungama dhambi zao.
7 Hata alipoona wengi miongoni mwa Mafarisayo na Masadukayo wakiujia ubatizo wake, aliwaambia, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja?
8 Basi zaeni matunda yapasayo toba;
9 wala msiwaze mioyoni mwenu kwamba, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba Mungu aweza katika mawe haya kumwinulia Ibrahimu watoto.
10 Na shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni”
Soma tena mstari wa 7 “Hata alipoona wengi miongoni mwa Mafarisayo na Masadukayo wakiujia ubatizo wake, aliwaambia, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? ”
Tunaweza kuiweka vizuri hiyo sentensi kwa namna hii “Enyi wazao wa nyoka ni nani aliyewadanganya(maana yake ni nani aliyewaonya) kwamba mtaiepuka hukumu inayokuja kwa njia hiyo mnayoitaka nyie?”..Njia gani?…Njia hiyo ya kuja kutaka kubatizwa na huku bado hamtaki kuacha dhambi zenu…Ni nani aliyewahubiria kuwa mtaikwepa hukumu kwa namna hiyo?…Maana yake mnafikiri kuwa kwa kuja kubatizwa tu hiyo inatosha kuikwepa hukumu itakayokuja….Mnajidanganya!…ZAENI MATUNDA YAPATANAYO NA TOBA!…Maana yake ni kwamba baada ya kutubu ishini kulingana na kutubu kwenu..Kama ulikuwa ni mwasherati, tubu na UACHE UASHERATI! Usiufanye tena, kama ulikuwa na kiburi tu na uache kuwa mwenye kiburi tena, kama ulikuwa mlevi unatubu na kuachana na ulevi wako, n.k..Huu ubatizo hautakuwa na msaada wowote kwenu kama mtakuja tu kubatizwa na huku bado hamjaacha matendo yenu mabaya. Huo ndio ujumbe Yohana Mbatizaji alikuwa anataka kuwapa wale Mafarisayo na Masadukayo.
Mafarisayo walisikia injili ya Yohana, wakaogopa, lakini wakasema aah ngoja tukabatizwe na sisi ili pengine tutaokoka huko mbeleni, lakini mioyoni mwao walikuwa hawana mpango wa kubadilika haka kidogo,..Walitaka kuugeuza ubatizo wa Yohana kama dini tu!..kama ni Liturujia mpya tu ya kufuata, kama katekisimo tu!..lakini walikuwa hawajui lengo kuu la ule ubatizo ni nini.. Lengo lake kuu lilikuwa ni kutubu na KUACHA DHAMBI!..sio kwenda kulowekwa kwenye maji na kurudi kuendelea na Maisha yako ya dhambi kama kawaida, na jina lako liwe limeshaandikwa mbinguni. Sio hivyo kabisa.
Vivyo hivyo na leo, ubatizo sio dini, na wala sio lebo ya kwamba Mungu anataka watu waliobatizwa ndio wawe wamepata tiketi ya kuingia mbinguni haijalishi wanaishije, yeye anataka tu watu wabatizwe.. hapana! Mungu anataka watu waliotubu na KUACHA DHAMBI. Hao ndio mbele za Mungu ubatizo wao una maana lakini kama mtu hujatubu kwa KUACHA DHAMBI, mtu huyo anamdhihaki Mungu.
Ukimuuliza mtu je umeokoka anakujibu, mimi nimebatizwa!..ukimuuliza tena je una uhakika wa kwenda mbinguni anakujibu ndio nilishabatizwa. Ubatizo hauna uhusiano wowote na kwenda mbinguni kama hujatubu kwa kuacha dhambi..Ndicho mafarisayo walichokuwa wanaenda kufanya kwa Yohana.
Umesema tu umetubu lakini bado unaendelea kuvuta sigara, bado unaendelea na uasherati, unaendelea na ulevi na ulawiti na usagaji, na pornography, halafu unasema umebatizwa au unakwenda KUTAFUTA UBATIZO, Ukidhani ndio unampendeza Mungu, na kwamba ndio utakwenda mbinguni..nataka nikuambie hapo unakwenda kujitafutia tu Laana badala ya Baraka.
Kutubu maana yake ni kugeuka na kuacha kile ulichokuwa unakifanya, na sio kusema tu mdomoni nimeacha na ilihali Maisha yako bado yapo vile vile. Ikiwa haupo tayari kuokoka, basi ni heri usiugize wokovu, wala usijiite hivyo, kwasababu ndivyo unavyomtia Mungu wivu kwa mienendo yako.
Watu wa Ninawi Mungu aliwasamehe kwasababu Aliona matendo yao kwamba wamegueka, wameacha mambo maovu waliyokuwa wanayafanya, hiyo ndiyo ikawafanya Waepukane na hukumu ile ambayo ilikuwa inawajia, na Mungu hakuona midomo yao kwamba wametubu kwa midomo ndipo awasamehe, hapana! bali matendo yao ndiyo yaliyosababisha wao kusamehewa.
Yona 3:10 “Mungu akaona MATENDO YAO, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende”
Hali kadhalika, usifanyike kuwa mzao wa nyoka, kwa kutafuta kutimiza maagizo ya Mungu na huku moyoni huna mpango wa kutenda mapenzi yake. Hizo ni tabia za Nyoka kibiblia. Mafarisayo wanamwendea Yohana kubatizwa na huku mioyoni mwao ni wale wale watu wenye viburi, wanaopenda utukufu, wenye wivu, wenye chuki, …maana japokuwa walikuwa wanamwendea Yohana kubatizwa lakini mioyoni mwao walikuwa wanamchukia n.k
Kama umeamua kumfuata Yesu leo, basi kubali pia kubeba na msalaba wako, kabla ya kwenda kubatizwa piga gharama kabisa kwamba unakwenda kuacha dhambi moja kwa moja, kwamba dunia ndio umeipa mgongo hivyo, msalaba mbele, ulimwengu umeuacha nyuma..Na kwa kufanya hivyo ndipo utaona nguvu za Mungu katika Maisha yako zikikusaidia na kukuongoza na ndivyo Mungu atakavyokukaribia Zaidi na kukupenda. Na kukubariki.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
AINA YA MAADUI UTAKAOKUTANA NAO KATIKA SAFARI YAKO YA WOKOVU.
About the author