JIBU: Vipo vyeo vitatu maalumu ambavyo vilimtambulisha Bwana Yesu Kristo…1) Mwana wa Mungu 2) Mwana wa Adamu 3) Mwana wa Daudi. Vyeo hivi kila kimoja kina maana yake..
Sasa kabla ya kuendelea mbele zaidi…ni muhimu kufahamu kuwa cheo cha “Mwana” ni cheo cha “urithi”…Maana yake ni kwamba mfano ukiwa na mtoto wako mmoja wa pekee huyo atarithi kila ulicho nacho…ikiwemo enzi yako yote, mali zako pamoja na hata jina lako…
Sasa katika biblia..mahali popote ambapo Neno Mwana linaanza kwa herufi kubwa…hilo linamzungumzia mtu mmoja tu maalumu ambaye ni Yesu Kristo…lakini ukiona neno “mwana” limeanza kwa herufi ndogo kama hivyo, basi fahamu ni mtu mwingine tofauti na Yesu anayezungumziwa hapo.. Kwa mantiki hiyo basi “wana wa Mungu” wapo wengi lakini “Mwana wa Mungu ni mmoja tu”…mimi na wewe tuliompokea Yesu ni wana wa Mungu….kadhalika wana wa Daudi wapo wengi..lakini “Mwana wa Daudi” ni mmoja tu ambaye ni Yesu…Sulemani alikuwa pia ni ‘mwana wa Daudi’, Hezekia, Yosia, Manase wote hao walikuwa ni wana wa Daudi….Hali kadhalika pia “wana wa Adamu wapo wengi”…mimi ni mwana wa Adamu(au kwa kifupi Mwanadamu)..wewe ni mwana wa Adamu lakini “Mwana wa Adamu” yupo mmoja tu ambaye ni Yesu…ni kama vile miungu wapo wengi lakini Mungu ni mmoja tu!.
Sasa tukirudi kwenye shabaha yetu ya msingi, ambapo tumeona kuwa Neno ‘mwana’ linazungumzia ‘urithi’
Hivyo basi vyeo hivyo vitatu tunaweza kuviweka katika mnyumbuliko ufuatao…1)Mrithi wa Mungu 2) Mrithi wa Adamu na 3) Mrithi wa Daudi.
Sasa unaweza kujiuliza Kristo alirithi nini kutoka kwa hawa watatu?
Kama mtu ataitwa Mwana wa Mungu maana yake ni kwamba ni Mrithi wa enzi yote ya Mungu na Ukuu …na huyo si mwingine zaidi ya Yesu Kristo, ambaye alirithishwa vyote.
Waebrania 1:1 “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi,
2 mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika MWANA, ALIYEMWEKA KUWA MRITHI WA YOTE, TENA KWA YEYE ALIUFANYA ULIMWENGU.
3 Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu”
Kwahiyo hiyo ndio sababu ya Kristo kujulikana kama MWANA WA MUNGU..Ni kwasababu amerithi milki zote za Mungu..
Mathayo 28:18 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani”.
Cheo cha pili ni cheo cha MWANA WA DAUDI/Mrithi wa Daudi..Sasa ili kujua ni kwanini Kristo aliitwa mwana wa Daudi ni vizuri kumjua kwanza Daudi alikuwa ni nani…(kwa maelezo marefu unaweza kututumia ujumbe inbox tutakutumia somo lake)…lakini kwa ufupi ni kwamba Daudi alikuwa ni mfalme pekee aliyepata Hekima ya kufikiria kumjengea Mungu nyumba ya kifalme katika wa Yerusalemu…na hivyo kumfanya Mungu kuuchagua ule mji kuwa makao makuu yake ya kifalme Duniani (yaani Yerusalemu).
Kama sio Daudi basi mpaka leo pengine Mungu asingekuwa na mji wake maalumu duniani kati ya miji ya Israeli…(Tusingelisikia hili neno Yerusalemu au Sayuni likirudiwa rudiwa katika maandiko, kwani ungekuwa mji kama miji mingine tu, wala ile Yerusalemu mpya kwenye ufunuo pengine ingeitwa kwa jina lingine)…
Lakini Daudi ndiye aliyefanya Yerusalemu ikawa mji wa kifalme wa mwokozi..na Mungu alimwahidi hatakosa mtu wa kukaa katika kiti cha kifalme kutoka katika uzao wake…na katika uzao wake huo yupo mmoja ambaye ni mkuu sana alitabiriwa kutokea huko na huyo si mwingine zaidi ya YESU KRISTO mwenyewe(kasome Mathayo 1:1-17) ambaye atakuwa mfalme juu ya Dunia nzima! Na ndiye atakayeijenga Yerusalemu mpya ile itakayoshuka kutoka mbinguni…na kukaa na watu wake. Na ndio maana Kristo ilimpasa aitwe mwana wa Daudi kufuatana na yale Daudi aliyoyafanya na kukabidhiwa.
Na cheo cha Mwisho cha Yesu Kristo ni cheo cha MWANA WA ADAMU au Mwana wa mtu,…sasa kama tunavyomjua Adamu alikuwa ni mtu wa kwanza kuumbwa na kupewa Urithi wote na mamlaka yote duniani, kwamba atawale kila kitu, na kwamba viumbe vyote vitamwogopa!….lakini kama tunavyojua aliuuza na kuupoteza ule urithi wake aliopewa na Mungu kwa adui shetani…Hivyo ili urithi huo umrudie tena mwanadamu..basi hakuna budi aje kutokea Adamu mwingine wa pili, ambaye atakaribiana sana kufanana na Yule Adamu wa kwanza,…ambaye ataurithi ule urithi na enzi yote aliyopewa Adamu ya kwanza…
1Wakorintho 15:45 “Ndivyo ilivyoandikwa, Mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi iliyo hai; Adamu wa mwisho ni roho yenye kuhuisha”.
Adamu wa pili atakuwa ni mwanamume kama Yule wa kwanza, naye atapewa mamlaka kama Yule wa Kwanza wa pale Edeni, na yeye ni lazima awe wa kwanza kuumbwa …na huyo si mwingine zaidi ya Yesu Kristo..ambaye ndiye limbuko letu rohoni na ndiye aliyekabidhiwa mamlaka yote ya duniani. Hiyo ndiyo sababu Yesu anaitwa Mwana wa Adamu…ni kwasababu amerithi mamlaka yote na enzi yote Yule Adamu wa kwanza aliyokuwa nayo (aliyopewa na Mungu)..
Mathayo 11:27 “Akasema, Nimekabidhiwa vyote na baba yangu; wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia”.
Hivyo Yesu Kristo ndiye Mwanzo na Mwisho, Alfa na Omega…Ndiye mwanadamu kamili, ndiye aliye na mamlaka yote sasa, ndiye mwenye enzi ya kifalme, ndiye Mungu mwenyewe katika mwili. Na ndiye njia ya kufika mbinguni…Kama hujamwamini wala kumpokea…ni vyema ukafanya hivyo kwasababu hakuna njia nyingine yoyote unaweza kumfikia Mungu kama isipokuwa kwa kupitia yeye..
Ufunuo 22:12 “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.
13 MIMI NI ALFA NA OMEGA, MWANZO NA MWISHO, WA KWANZA NA WA MWISHO.
14 Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake”.
Bwana atubariki. Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
KWANINI YESU KRISTO NI WA MUHIMU KWETU SASA?
USIPOKUWA MWAMINIFU, NAFASI YAKO ITACHUKULIWA.
TAZAMA, MWISRAELI KWELI KWELI, HAMNA HILA NDANI YAKE!
Kuna ufufuo wa aina ngapi?
MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.
MAJESHI YA PEPO WABAYA.
About the author