UFUFUO TUNAOUSUBIRIA UTAHITIMISHA YOTE.

UFUFUO TUNAOUSUBIRIA UTAHITIMISHA YOTE.

Siku ile Bwana Yesu alipokufa biblia inatuambia makaburi yalipasuka na miili ya watakatifu wengi iliinuka, lakini katika ufufuo huo hawakuondoka pale makaburini mpaka siku Yesu alipofufuka, Ndipo wakaanza safari ya kuuelekea mji mtakatifu (Yerusalemu), Na walipofika kule biblia inatuambia wakawatokea watu wengi sana…

Lakini lipo swali tunaweza kujiuliza kulikuwa na umuhimu gani wale wafu watoke makaburini kwa kipindi kama kile, pili na ni kwanini walielekea mji mtakatifu Yerusalemu na sio mahali pengine..

Tusome.

Mathayo 27:50 “Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake.

51 Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;

52 makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala;

53 nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi”.

Maswali kama hayo, tukiweza kuyatafakari vizuri naamini yatatupa mwanga wa jinsi siku ile kuu ya ufufuo wa wafu(katika unyakuo) itakavyokuwa.

Sasa ni kwanini, wakati ule makaburi yapasuke na watakatifu wafufuke,..Ni kwasababu Mungu alikuwa anataka kuwathibitishia baadhi ya wale watu wake, kuwa tendo la ufufuo lipo kweli, na mwanawe Yesu Kristo amefufuka kweli kweli.. Na alifanya hivyo ili baada ya hapo wakawe mashahidi wa ufufuo wa wafu kwa watu wengine..Kwasababu wakati huo yalikuwepo makundi mengi ya watu waliokuwa hawaamini suala la ufufuo wa wafu (Masadukayo), Na wengine walikuwa wanapinga na kuwatangazia watu kuwa ameibiwa..Hivyo ili Mungu kuwathibitishia kuwa suala la Ufufuo lipo ndipo akaruhusu makaburi yapasuke, wafu wafufuke waonekane na watu wengi.

Lakini Je! Hilo lilionekana na kila mtu tu?

Jibu ni Hapana, bali lilionekana na wale watu (watakatifu) waliokuwa Yerusalemu wakati ule. Kama tu vile Bwana alivyofufuka hakumtokea tu kila mtu isipokuwa wale waliokuwa wanamwamini. Na hao wafu ni hivyo hivyo hawakuwatokea watu wote isipokuwa tu wale watakatifu..

Kwasababu biblia inatuambia wafu wale walielekea Yerusalemu. Ni kwa vile tu biblia haiwezi kueleza kila kitu, lakini tukio lile liliwaacha katika butwaa kubwa sana wale watu waliokuwa Yerusalemu..Jaribu kufikiria, unatembea kila kona unawaona ndugu zako wa kale waliokufa katika Bwana, wengi sana, unawaona waliokuwa majirani zako kitambo, na wengine wanazungumza na wewe kabisa wanakuambia mimi ni Yusufu, mimi ni Sulemani, mimi ni Yeremia n.k…

Wewe unadhani watu hao walioshuhudia utaanzaje kuwaaninisha kuwa hakuna ufufuo wa wafu? kuwa Kristo hakufufuka bali aliibiwa?

Ufufuo huo uliwapa uthibitisho mkubwa sana, Ili kwamba wakawe mashahidi wa kufufuka kwake ulimwenguni kote, hilo ndio lilikuwa lengo lake..

Lakini upo ufufuo mwingine tunaoungojea sasa, ambapo upo karibu sana kutokea kuliko tunavyofikiria..Wakati huo PARAPARANDA kuu ya Mungu italia kutoka mbinguni..Na tukio kama lile lile la kwanza litatokea kwa mara nyingine, la makaburi kupasuka..Lakini safari hii watanyanyuka watakatifu wengi sana, wa vizazi vyote vilivyotangalia duniani..watu wengi sana..

Wakati huo watakatifu walio hai hawatajua chochote kwanza, wala ulimwengu pia..Ili lile Neno la kwamba hatutawatangulia wafu waliolala litimie..

1Wathesalonike 4:15 “Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika HATUTAWATANGULIA wao waliokwisha kulala mauti.

16 Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; NAO WALIOKUFA KATIKA KRISTO WATAFUFULIWA KWANZA.

17 Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele.

18 Basi, farijianeni kwa maneno hayo”

Vivyo hivyo na wao hawataonekana na kila mtu tu aliye duniani…

wataonekana na watakatifu watakaonyakuliwa, (Yaani wale watu tu waliozaliwa mara ya pili ndio watakaowaona)..…na wenyewe wataenda katika mji mtakatifu (Yerusalemu ya rohoni, soma Wagalatia 4:24-31)…

Siku hiyo sisi tuliokuwa hai siku tutakapowaona, ndio tutakapojua kuwa Ufufuo wenyewe umefika, na kitendo cha kufumba na kufumbua tutatoweka, hatutaonekana tena ulimwenguni..

1Wakorintho 15:51 “ Angalieni, nawaambia ninyi siri; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika,

52 kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika”.

Wakati huo dunia haitaelewa chochote!. Wengi watasema wameibiwa, kama ilivyokuwa kipindi cha Bwana Yesu, wengine watasema tumepotea tu! Watapatikana n.k. Lakini suala la kwamba kanisa limenyakuliwa hilo halitaaminika na wengi hata kidogo. Kwasababu tutakuwa ni kundi dogo sana kama vile Bwana Yesu alivyosema.

Hivyo ndugu, mimi na wewe tujue kuwa tunaishi katika hayo majira ya Kunyakuliwa kwa kanisa, Dalili zote zinathibitisha hilo, hakuna asiyejua.. Lakini Swali ni Je! tumejiwekaje tayari? Je! Parapanda ikilia leo, unao uhakika wa kunyakuliwa? Kumbuka baada ya wakati huo mlango wa rehema hautakuwa tena wazi kwa ajili yetu, Bali kitakachokuwa kinaendelea duniani ni kumiminwa kwa ghadhabu ya Mungu. Na hukumu.

Muda bado tulio bakiwa nao mfupi sana. Hivyo ikiwa wewe ni mmojawapo ambaye Kristo yupo mbali na wewe, basi chukua uamuzi wa leo hii kumgeukia na atakupokea na kukufanya mwana wake.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Kati ya Unyakuo,dhiki kuu, utawala wa miaka 1000 kipi kinaanza

IJUE NGUVU YA IMANI.

KUZIMU ni mahali pa namna gani, Je! huko wanaishi watu wakifa na kwenda kupata mateso au ni vinginevyo?

USIRUHUSU MUNGU AWEKE UADUI KATI YAKO NA WATU WAKO.

MIILI YA UTUKUFU ITAKUWAJE?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments