TUMEPEWA AMRI YA KUKANYAGA NGE NA NYOKA.

TUMEPEWA AMRI YA KUKANYAGA NGE NA NYOKA.

Jina la Bwana wetu Yesu libarikiwe. Unapomkiri Yesu kwa Kinywa, au unapojisalimisha kwa Yesu, kwa kudhamiria kabisa, dakika hiyo hiyo..Shetani anaangushwa juu yako, kama umeme…Na anawekwa chini ya miguu yako na unakabidhiwa mamlaka, juu yake.

Luka 10: 18  “Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni KAMA UMEME.

19  Tazama, NIMEWAPA AMRI YA KUKANYAGA NYOKA NA NGE, NA NGUVU ZOTE ZA YULE ADUI, wala hakuna kitu kitakachowadhuru”

Hapo kuna vitu vitatu ambavyo unapewa amri juu ya hivyo.

Amri ya kukanyaga NYOKA. 2). amri ya kukanyaga NGE na 3). amri ya kukanyaga NGUVU ZOTE ZA YULE ADUI.

  • 1. Amri ya kukanyaga Nyoka

Nyoka ni kiumbe anayeuma (au anayeng’ata kwa kutumia mdomo)..Silaha yake kubwa ni mdomo na mate yake, hana silaha nyingine kiasi kwamba ukikibana kile kichwa hakuna atakachoweza kufanya ili kukudhuru. Nyoka ni mfano wa Watu wanaotumika na shetani, kwa kujua au kwa kutokujua kukudhuru wewe kupitia maneno wanayoyazungumza…Yaani kwaufupi silaha yao ni maneno..

Zaburi 143:1 “Ee Bwana, uniokoe na mtu mbaya, Unihifadhi na mtu wa jeuri.

2 Waliowaza mabaya mioyoni mwao, Kila siku huondokesha vita.

3 Wamenoa ndimi zao kama nyoka, Sumu ya fira i chini ya midomo yao”

kobra

Fira ni nyoka aina ya KOBRA, Sasa hao Biblia imesema tumepewa amri juu yao..”kuwakanyaga”…Sasa hatuwakanyagi na sisi kwa kuwarudishia maneno.. Hapana, tukifanya hivyo na sisi tutakuwa ni nyoka kama hao. Lakini tunakanyaga vichwa kwa kuyapuuza maneno yale, na kuyazuia yasiingie moyoni mwetu..

Kwasababu ukiyaruhusu yaingie moyoni mwako, yatakuwa sumu kwako na yatakudhuru.. Hivyo unayapuuzia yale maneno na kuyapiga mateke, hiyo ni silaha kubwa sana..Ambayo kwa hiyo utaweza kuwakanyaga nyoka wote.. (Kumbuka nyoka hapo ni lugha ya rohoni, usimwite kamwe ndugu yako nyoka hata kama ni mbaya kiasi gani kwako).

  • 2. Amri ya kukanyaga NGE.

Nge ni mdudu anayeuma kwa kutumia MKIA, na si Mdomo kama nyoka. Hawa ni jamii ya watu ambao wanatumika na shetani pasipo kujua au kwa kujua. Ambao kwa mbele ni wazuri lakini kwa nyuma wanatumia mkia kukudhuru,  na kama unavyojua mkia wa nge, umepanga juu ukazunguka lengo lake ni kukuchoma wewe kwa nyuma, pasipo kujua ni nani kakudhuru.

Hivyo shetani anaweza kutumia watu wanaoonekana ni wazuri kwa nje lakini kumbe ni wenye madhara juu yako, watu wa namna hiyo tumepewa amri ya kuwakanyaga..Hatuwakanyagi kwa kuwachukia wala kufanya nao vita bila wao kujijua, tukifanya hivyo na sisi tutakuwa nge, ambao hatungati kwa mdomo lakini tunang’ata kwa mkia..Hivyo na hawa tumepewa silaha ya kushughulika nao, na hiyo si nyingine Zaidi ya MIGUU YETU, Maana yake kutotafuta tafuta wanachokiwaza juu yetu wala kukifikiri juu yako wanatuwazia nini, maana yake wewe unasonga mbele, hufuatilii wewe unaendelea mbele na mambo yako unayoyafanya.

Kama vile watu wanavyolikanyaga neno la Mungu chini, maana yake ni kwamba wanalipuuzia, wanaendelea na mambo yao,  vivyo hivyo na wewe unakanyaga maneno yao, au hila zao…kwa kuzipuuzia, na kwajinsi unavyozidi kuzipuuza ndivyo zinavyozidi kuishiwa nguvu, kwasababu utakuwa umempa Mungu nafasi kubwa ya kukupigania, na mwisho wa siku watatubu na kushawishika kumwamini Mungu wako, na utakuwa umeokoa roho zao.

  • 3. Amri ya kukanyaga nguvu zote za yule mwovu.

        Kipengele hicho ndio cha mwisho na cha Muhimu sana..Ambacho shetani hataki watu wakijue wala wakielewe, kwasababu kinamhusu yeye mwenyewe na mapepo yake, na wala hakiwahusu watu anaowatumia..

Shetani anapenda kuwaaminisha watu kuwa yeye ana nguvu sana, na hivyo akishika mahali ni ngumu yeye kutolewa..Hivyo watu wengi wamefungwa na nguvu za Ibilisi kwa muda mrefu kwasababu tu ya Imani hiyo ndani yao.  Utakuta mtu anaumwa, au anapitia tatizo Fulani, na lile tatizo ndani yake kashalikuza na kuwa kubwa mno, na kuamini kuwa inahitajika nguvu nyingi sana za rohoni kuliondoa, au  upako mwingi kuliondoa..Wengine wanatokewa kabisa na mapepo wazi, wangine yanawajia katika ndoto, wengine wananyanyaswa na mashetani usiku, kiasi kwamba hata wanaogopa kulala wenyewe. Wengine wanatishiwa na kusumbuliwa na shetani kwa namna ambayo hata wanashindwa kusimulia, mwisho wa siku wanakata tamaa hata ya kuishi. Na kundi hili lipo kubwa sana.

Sasa watu kama hawa, shetani amewashika kwa kutumia Imani yao kupata nafasi ya kuwatesa.

Biblia inasema hapo, tumepewa Amri ya KUKANYAGA… Unaelewa maana ya kukanyaga???…Kukanyaga maana yake ni KULIPOTEZEA JAMBO!!..Kulishusha hadhi, kulipunguza nguvu, kuliabisha, kulidhalilisha, kulidharau. Hiyo ndio maana ya kukanyaga, wala kukanyaga sio kuingia kwenye maombi ya mifungo ya masafa, hapana hiyo sio maana yake.. Maana yake ni kuliweka chini yako jambo. Kama tu vile watu wanavyolikanyaga chini neno la Mungu, wanafanya hivyo kwa kulidharau…Kitendo cha kukidharau kitu tayari umekikanyaga chini.

Waebrania 10.28 “Mtu aliyeidharau sheria ya Musa hufa pasipo huruma, kwa neno la mashahidi wawili au watatu.

29 Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema?”

Umeona hapo?. Watu wote wanaoihesabia damu ya agano la Yesu kuwa ni kitu ovyo, na kumdharau (au kwa lugha ya sasa, ni kuipotezea), watu hao ndio wanahesabika kama wamemkanyaga Mwana wa Adamu.

Ni hivyo hivyo, mtu anayehesabia kazi za shetani kuwa ni kitu ovyo, hapo anakuwa amemkanyaga chini, ya miguu yake.

Hivyo kwa silaha ile ile tunayotumia kukanyaga nyoka na nge, ndiyo hiyo hiyo tunayotumia KUZIKANYAGA NGUVU ZOTE ZA YULE ADUI. Wala hakuna silaha nyingine, shetani asikuogopeshe ikiwa upo tayari ndani ya Kristo..

Maana yake ni hii.

Baada ya kumkiri Yesu, kama ulikuwa unaumwa na kuamini kwamba ni ngumu kupona ugonjwa ulio nao, HILO wazo unaanza kulidharau ndani yako, kuanzia sasa (unalikanyaga!)..

> Shetani alikuwa amekutishia kwamba dhambi yako haisameheki, unalidharau hilo wazo, na kulipoteza kwenye akili yako..

> Mapepo yalikuwa yanakuhubiria kwamba utakufa kila siku kwenye mawazo yako, unayapotezea hayo mawazo na kuyadharau, na kusema hilo halipo..kwa jinsi unavyozidi kuyashusha hadhi hayo mawazo ya shetani, na uongo wake huo…ndivyo na yenyewe yanavyozidi kukosa nguvu juu yako na hatimaye kupotea kabisa.

> Maroho yalikuwa yanakukaba usiku, Hizo sauti zinazokuambia kwamba  yatarudi tena huzitilii maanani..acha kabisa kuyapa hayo mapepo heshima kubwa kiasi hicho!, yashushe hadhi..

> Mandoto ya ajabu ajabu shetani alikuwa anakutumia, anza kuyapotezea wala usiyatafakari tafakari, wala usitafute kujua maana zake, yaache yapite…yakanyage chini!.. usiyakuze, kwenye kichwa chako kana kwamba ni kitu cha muhimu sana.

> Mawazo shetani anayokuletea kwamba mapepo yatakudhuru, hayo mawaza anza kuacha kuyawaza, yakanyage chini, badala yake huo muda tumia kutafakari mambo mengine, tumia kutafakari Maneno ya Mungu, hapo utakuwa unammaliza nguvu shetani kwa kasi sana..Maana shetani kazi yake ni kukutisha wewe ili uanze kumfikiria yeye na kumkuza kwenye akili yako, ndipo apate nguvu juu yako..sasa wewe nenda kinyume naye.

>Shetani alikuwa amekuaminisha kwamba ni lazima kila siku aje akutese, yakatae hayo mawazo, wala usiyatafakari, tena yasahau kabisa kwenye kichwa chako, na wala usipate ratiba ya kufikiri jinsi anavyokutesaga..kwa jinsi unavyozidi kumpotezea, naye anapotea..

Kwasababu Miguu yetu ni silaha kubwa na ina nguvu kuliko vichwa vya nyoka, ina nguvu kuliko mikia ya nge, na ina nguvu kuliko nguvu za adui shetani.

Likumbuke hili neno..Luka 10: 18  “Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni KAMA UMEME. 19  Tazama, NIMEWAPA AMRI YA KUKANYAGA NYOKA NA NGE, NA NGUVU ZOTE ZA YULE ADUI, wala hakuna kitu kitakachowadhuru”

Bwana akubariki.

Kama hujaokoka kumbuka hizi ni siku za mwisho na Yesu anakaribia kurudi, biblia inasema itatufaidia nini tukiupata ulimwengu mzima na kupata hasara za nafsi zetu?..Tafakari neno hilo kwa makini, hivyo kama utaamua leo kumpa Kristo Maisha yako, utakuwa umefanya jambo la busara sana, ambalo hutakaa ujutia katika maisha yako, hivyo kwa msaada Zaidi na maombezi fungua hapa >> SALA YA TOBA.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

MKUU WA UZIMA AKUWEKE HURU.

SALA YA UPONYAJI/MAOMBI YA UPONYAJI.

UPONYAJI WA ASILI

KWA KUPIGWA KWAKE SISI TUMEPONA.

WEWE NI BWANA UNIPONYAYE.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Obed mwalyala
Obed mwalyala
1 year ago

Asanten sana kwamafundisho mazur BWANA MUNGU awabarikie nakuwapa aman