Jibu: Tusome..
Waefeso 2: 20 “Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni”.
Katika mstari huo yapo mambo makuu mawili ya kuzingatia kwa makini.
1) Msingi na 2) Mitume na manabii
Tukianza na Msingi.
Hapo anasema mmejengwa juu ya “Msingi” na si “misingi”. Maana yake ni msingi mmoja tu, na si mingi.. Na anaendelea kwa kusema..”mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii”..na sio “mmejengwa juu ya mitume na manabii”.. Maana yake ni kwamba msingi waliokuwa nao mitume na manabii ndio sisi pia tunajengwa juu ya huo.. Mtu akisema “natembea juu ya misingi na kanuni za Baba yangu au babu yangu, hajamaanisha anatembea juu ya baba yake”..Bali juu ya kanuni na taratibu alizorithishwa na Baba yake, ambazo hata baba yake alikuwa anazifuata na kuziishi….Kadhalika na hapo, Neno la Mungu linasema, mmejengwa juu ya msingi wa Mitume na manabii, maana ya kuna msingi ambao Mitume na manabii walikuwa wanaiishi na kuifuata, na hatimaye wakairithisha kwa kizazi kinachofuata. Kwa misingi hiyo ndio sisi tunajengwa.
Sasa kabla ya kujua vizuri huo msingi ni nini, hebu tujue kwanza hawa Mitume na Manabii wanaozungumziwa hapo ni wakina nani?..
Tofauti na inavyodhaniwa kwamba Mitume na Manabii wanaozungumziwa hapo, ni kundi la manabii na Mitume wanaozuka leo… unakuta inatokea mtu fulani mahali fulani anayejiita Mtume au Nabii, anaanza kujigamba kwamba karama yake ndio karama kuu yakulijenga kanisa. Na kwamba yeye ndio msingi na kanisa, limejengwa juu yake. Jambo ambalo ni uongo, tena kwa asilimia zote.
Mitume na Manabii wanaozungumziwa hapo ni Manabii wote wa agano la kale, na Mitume wa kanisa la kwanza wa agano jipya. Hao Msingi waliouweka na kuufuata ndio msingi sisi tunaojengwa juu ya huo na huo si mwingine zaidi ya biblia takatifu, ambapo ndio tunanukuu maneno kutoka huko. Ndio maana leo hii, msingi ni biblia takatifu, Maneno yaliyoandikwa na Mitume kama Paulo, Petro, Yohana, Yakobo n.k hayo ndio msingi wetu leo hii, ndio maana leo hatunukuu Neno la Nabii yeyote aliyepo leo, wala Mtume yeyote aliyepo leo na kulihubiri hilo, kana kama ni Neno la Mungu, badala yake tunanukuu maneno yaliyoandikwa na Mtume Paulo, au Nabii Isaya, au Nabii Yoeli n.k..Hao ndio mitume na manabii ambao tumejengwa juu ya msingi wao.
Kwahiyo mtu yeyote anayejiita mtume au nabii au mwalimu au muinjilisti, na anasema na kujivuna kwamba kanisa limejengwa juu yake, na kujivuna kwamba yeye ndio nguzo kuu, au karama yake ndio karama kuu…kwa kufuatia huo mstari, mtu huyo anadanganya aidha kwa kujua au kwa kutokujua.
Msingi wetu sisi ni biblia takatifu, ambayo imeandikwa na mitume wa Yesu na manabii wa agano la kale, hao ndio Mababa. Na kiini cha biblia takatifu ni YESU KRISTO. Vitabu vyote katika biblia vimebeba habari au unabii wa Yesu Kristo, hakuna kitabu hata kimoja kisichobeba ufunuo wa Yesu Kristo ndani ya biblia. Kwasababu yeye ndio Mungu mwenyewe katika Mwili. (1Timotheo 3:16).
1Wakoritho 3:11 “Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, Yesu Kristo”.
Je umemwamini Yesu?, umepokea Roho Mtakatifu?..Kama bado mwamini leo na kumkabidhi maisha yako, naye atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu (Matendo 2:38)
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mafundisho mengine
Mada Nyinginezo:
Mtume Paulo alikuwa na maana gani kusema katika 1Wakorintho 15:31″…NIKAKUFA KILA SIKU?
About the author