Misukule ni nini? ni kweli ipo? Na je! inaweza kurudishwa?

Misukule ni nini? ni kweli ipo? Na je! inaweza kurudishwa?

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe.

Misukule kwa tafsiri inayojulikana na wengi, ni watu waliotekwa kichawi, kwa lengo la kutumikishwa..ambapo kabla ya kutekwa huko, mtu yule anakuwa anatengenezewa kifo bandia, na kuonekana kama amekufa, na hata kuzikwa kabisa..lakini anakuwa hajafa, na kile kilichozikwa kinakuwa si yeye, bali ni kipande kidogo cha gogo, au mgomba.

Ambapo kipande hicho kinageuzwa kimazingara na kuchukua taswira ya yule mtu aliyetekwa. Na hivyo ndugu wa huyu aliyechukuliwa wanakuwa wanadhani wamemzika mpendwa wao kumbe sio.

Sasa swali ni Je! Ni kweli hiyo aina ya ushirikina ipo?.

Jibu ni ndio ipo!. Shetani anao uwezo wa kufanya jambo hilo na mengine Zaidi ya hayo, aliweza kugeuza fimbo kuwa nyoka aliye hai mbele ya Farao, si zaidi fimbo kuwa nyoka aliyekufa?, au fimbo kuwa maiti ya mtu aliyekufa!!..hivyo hilo ni jambo ambalo linawezekana.

Lakini pamoja na kwamba anaweza kufanya hayo,  lakini si rahisi kwake yeye kufanya hivyo, kuna ugumu mkubwa sana kwake….tofauti na wengi tunavyodhani kuwa shetani mambo yote kwake ni mteremko, kwamba lolote atakalojiamulia kwake ni rahisi kulifanya. Nataka nikuambie hata kwa shetani mambo mengine si rahisi kwake bali anapambana sana ili afanikiwe.

Ingekuwa kila kitu kwake ni mteremko, sidhani mpaka leo dunia ingekuwepo..vile vile angewafanya watu wote leo kuwa wabaya kupindukia, lakini utaona ijapokuwa kuna watu wengi walio waovu na ambao hawajampokea Yesu, LAKINI BADO SI WABAYA KUPINDUKIA!!. Si kwamba shetani hapendi kuwafanya wawe wabaya sana!.. anatamani kuwafanya kuwa wabaya kupindukia..Lakini anashindwa na kukwama kwa wengi.. Kwasababu si kila mlango ni mrahisi kwake kuuingia.

Ndio maana utaona ataweza kumshawishi na kumfanya mtu kuwa mwasherati, na mlevi lakini kumshawishi kuwa mkatili na gaidi inakuwa ni ngumu!.. Hiyo ni kwasababu kuna milango ambayo si mirahisi kwa shetani kuiingia kwa mwanadamu.. ataweza kumshawishi mtu kuwa mwongo na mtukanaji na mzinzi wa kupindukia lakini akashindwa kumfanya awe Jambazi linaloua watu kikatili!..utaona ni watu baadhi tu miongoni mwa watu wake anaofanikiwa kufawanya magaidi.

Vivyo hivyo ni watu baadhi tu ndio ataweza kuwateka na kuwageuza kuwa Misukule, na kuwatumikisha, lakini si jambo rahisi kwake, ambalo linaweza kufanyika kwa jinsi anavyotaka yeye au kwa mtu yeyote.

Jambo la mtu kuchukuliwa msukule, ni gumu sana kutokea kwa mtu, kama vile, ilivyo ngumu kwa kahaba, au mlevi kuwa gaidi yule wa kuchinja watu!.. Mtu anaweza asiwe hata ndani ya imani ya kikristo na ikawa ngumu kwa shetani kumchukua msukule. Ni kwasababu kuna ulinzi Fulani ambao upo duniani wa Roho Mtakatifu.

Ni watu wachache sana ambao ndio wanaweza kuchukulika msukule na kutekwa kwa namna hiyo.. (tutakuja kuliona hilo kundi mbele kidogo)..Kama tu vile ilivyo ni watu wachache sana walio katika ufalme wa giza wanaoweza kufanywa kuwa magaidi na shetani…

Wapo wengi walio waovu duniani, wazinzi, waongo, lakini bado isiwe rahisi kwao kuchukuliwa msukule..

Hivyo msukule sio jambo kubwa na linalofanyika kirahisi kama linavyotukuzwa leo. Kiasi kwamba leo hii kati ya misiba 10 inayotokea kiajabu ajabu.. basi 2 au 3 katika hiyo, utasikia watu wakisema huyo mtu kachukuliwa msukule, hajafa!.

Jambo ambalo si kweli!.. ambalo lengo lake ni kuukuza ufalme wa giza na kupachika hofu..

Ingekuwa hivyo ndivyo nadhani shetani angeshamaliza watu wote duniani, kuwachukua misukule..Maana walio nje ya Imani, ni wengi kuliko walio ndani ya Imani. Nchi ya  India na China tu zina mabilioni ya watu wanaoabudu miungu, ambao hata hawamjui Mungu wa kweli, hao nadhani angeshawamaliza wote.. Lakini wengi wa hao wapo salama tu!.

Nchi za Ulaya na Marekani, zina idadi kubwa  ya watu wasioamini kama Mungu yupo, lakini wengi wao wapo huru, hawajachukuliwa misukule. Hata katika jamii zetu, wapo wengi walio waovu lakini wapo wanaishi.. Je! Unadhani shetani hawaoni na kuwatamani??.. anawaona na kuwatamani sana… lakini si rahisi kwake, kwasababu yupo Roho Mtakatifu duniani ambaye anamzuia shetani kujiamulia kufanya baadhi ya mambo.. Maandiko yanasema baada ya huyo kuondolewa duniani ndipo mambo yatabadilika ulimwenguni (2Wathesalonike 2:7).

Sasa wengi wa wanaochukuliwa Msukule, wanakuwa ni watu wanaoangukia katika mojawapo ya makundi haya matatu

1. Wachawi na Washirikina.

Hili ni kundi la kwanza, ambalo ni rahisi sana kuchukuliwa msukule. Wengi wa wanaochukuliwa msukule ni aidha wao wenyewe walikuwa wachawi, au washirikina. Hivyo kama ni mshirikina au mchawi basi, ni rahisi kwako kutekwa na adui.

2. Watu wanaohudhiria kwa waganga wa kienyeji.

Mtu yeyote ambaye anakwenda kwa mganga wa kienyeji, maana yake kamsogelewa shetani kwa hiari yake mwenyewe, hivyo kajiuza kwa shetani na shetani anaweza kumfanya lolote, ikiwemo kumchukua msukule.

3. Watu wanaoyadharau Maneno ya Mungu kwa makusudi.

Hili ni kundi lingine ambao li karibu sana na kuchukuliwa msukule. Mtu yeyote anayeidharau injili kwa muda mrefu, na makusudi, huyo anajiondolea ulinzi wa kiMungu kwa haraka sana pasipo yeye kujijua..na anakuwa amejiuza kwa shetani bila yeye kujua.

Utauliza kivipi?

Kuna mfano mmoja wa mtu aliyechukuliwa Msukule na shetani mwenyewe kwenye biblia..huyo alikuwa ni mtu wa kuyadharau maneno ya Mungu, alipoonywa mara nyingi atubu alishupaza shingo..na ndipo walinzi wa mbinguni ambao kazi yao ni kuwalinda wanadamu, waliopoondoa ulinzi juu yake.. na kumruhusu shetani amchukue. Na huyo si mwingine zaid ya Mfalme Nebukadneza..

Danieli 4:23 “Tena, kwa kuwa mfalme alimwona mlinzi, naye ni mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni, akisema, Ukateni mti huu, mkauangamize; ila kiacheni kisiki cha shina lake katika ardhi, pamoja na pingu ya chuma na shaba, katika majani mororo ya kondeni; kikatiwe maji kwa umande wa mbinguni, na sehemu yake iwe pamoja na wanyama wa kondeni, hata nyakati saba zipite juu yake;

24 tafsiri yake ni hii, Ee mfalme, nayo ni amri yake Aliye juu, iliyomjia bwana wangu, mfalme

25 ya kuwa utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa kondeni, nawe utalazimishwa kula majani kama ng’ombe, nawe utatiwa maji kwa umande wa mbinguni, na nyakati saba zitapita juu yako; hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa yeye amtakaye, awaye yote.

26 Na kwa kuwa waliamuru kukiacha kisiki cha shina lake; ufalme wako utakuwa imara kwako, baada ya wewe kujua ya kuwa mbingu ndizo zinazotawala.

27 Kwa sababu hiyo, Ee mfalme, shauri langu lipate kibali kwako; ukaache dhambi zako kwa kutenda haki, ukaache maovu yako kwa kuwahurumia maskini; huenda ukapata kuzidishiwa siku zako za kukaa raha.

28 Hayo yote yakampata mfalme Nebukadreza.

29 Baada ya miezi kumi na miwili, alikuwa akitembea ndani ya jumba la kifalme katika Babeli.

30 Mfalme akanena, akasema, Mji huu sio Babeli mkubwa nilioujenga mimi, uwe kao langu la kifalme, kwa uwezo wa nguvu zangu, ili uwe utukufu wa enzi yangu?

31 Hata neno lile lilipokuwa katika kinywa cha mfalme, sauti ilikuja kutoka mbinguni, ikisema, Ee mfalme Nebukadreza, maneno haya unaambiwa wewe; Ufalme huu umeondoka kwako.

32 Nawe utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa kondeni; utalishwa majani kama ng’ombe, na nyakati saba zitapita juu yako, hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, awaye yote.

33 Saa iyo hiyo jambo hilo likatimizwa, likampata Nebukadreza; alifukuzwa mbali na wanadamu, akala majani kama ng’ombe, na mwili wake ulilowa maji kwa umande wa mbinguni, hata nywele zake zikakua, zikawa kama manyoya ya tai, na kucha zake kama kucha za ndege”

Umeona?.. huyu alitekwa na shetani mwenyewe kwa ruhusa ya Mungu.. kwasababu alikuwa anayadharau wazi maneno ya Mungu, akachukuliwa msukule, maandiko yanasema akalishwa majani kama ng’ombe. Misukule ya siku hizi inalishwa pumba, na vitu visivyofaa..

Hiyo inatufundisha na sisi kutoyadharau maneno ya Mungu na kutokuwa na kiburi. Mungu akitukataa hakuna atakayetukubali.. Na Mungu akiondoa ulinzi wake juu yetu, kama alivyoondoa kwa Nebukadneza, unadhani ni nini shetani atakachokuwa amebakiwa nacho kwetu, Zaidi ya kutuchukua mateka?.

Na Mwisho, je! mtu anatokaje kama tayari kashachukuliwa Msukule?

Mtu anapokuwa katika kutekwa huko, akili zake zinakuwa zimefungwa anakuwa kama kichaa.. Hivyo kama hatakutana na mtu atakayemwombea huko basi atabaki katika hali hiyo hiyo mpaka Bwana atakapomfungua mwenyewe, kama alivyomfungua Nebukadneza..

Na kumbuka watu hawa(Misukule) wanakuwa wapo katika mwili, na si katika roho, kwasababu hawajafa.. Ni ngumu kuwaona kwasababu waliowashika wanawaficha katika nyumba zao..kama mtu anayeficha almasi ndani kwake….hivyo ni ngumu kujua, lakini wapo katika mwili na wanaonekana kwa macho kabisa.. hivyo wanapoonekana ni kama vile kichaa aliyeonekana barabarani.. hivyo anaweza kuchukuliwa na kufanyiwa maombezi, ili akili zake zimrudie..na anapofunguka anarudia hali yake ya kawaida, kama mtu aliyepona ukichaa. kwasababu alikuwa hajafa. (lakini kumbuka si kila kichaa ni msukule)… Na si kila misiba ni misukule.

Na vile vile hakunaga huduma ya kwenda kutafauta misukule, au kuichimbua..au kuiita huko iliko na kuirudisha.. kwasababu hujui ni nani na nani ndio kachukuliwa. Roho Mtakatifu ndiye anayefunua kwamba mahali Fulani katika nyumba Fulani kuna mtu kafungwa, anahitaji kuombewa afunguliwe..Hivyo!, na si kwenda kuzunguka na kutafuta msukule!.

Na Ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko ufalme wa giza. Roho ya Mungu duniani ni KUU kuliko roho ya shetani.

Hivyo hatuhitaji kuishi kwa hofu ya kuchukuliwa msukule, wala watoto wetu kuchukuliwa msukule, wala hatuhitaji kufuatilia sana habari za kichawi, kama tayari tupo ndani ya Kristo. Tunapokuwa ndani ya Kristo, tunapaswa tuongeze bidii katika kumjua sana Mungu Zaidi ya shetani.. Tukimjua sana Yesu na neema yake na utukufu wake..maarifa hayo yanatosha kutulinda na kutuhifadhi, hata kama hatujawahi kusikia neno uchawi katika maisha yetu.

Jambo la hatari shetani analolifanya katika siku hizi za mwisho, ni kuhakikisha anaupandisha hadhi ufalme wake, ambao tayari upo chini. Ndio hapo atanyanyua hata watu wahubiri ili kusifia kazi za shetani, na uchawi wake. Wakati kiuhalisia uchawi, si kitu kwa walio ndani ya Kristo, na wala Bwana Yesu hajawahi kutupa maagizo tukajifunze juu ya uchawi, ili tumwelewe yeye, au tumpendeze yeye. Anachotaka kwetu ni SISI tumjue yeye, na si tujue majina ya mapepo na elimu ya kuzimu.

Hivyo kama umempokea Yesu, tafuta kumjua Zaidi Yesu, na kama bado basi mpokee leo. Na tafuta kumjua.

Bwana akubariki.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Jiunge na Group letu ya whatsapp, la masomo ya kila siku kwa kubofya hapa > Group-whatsapp


Mada Nyinginezo:

KUOTA NYOKA.

EDENI YA SHETANI:

EDENI YA SHETANI:

Kwa maana kahaba ni shimo refu; Na malaya ni rima jembamba.

Kwanini Mungu awachome watu kwenye ziwa la moto na hali yeye ndiye aliyewaumba?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments