UDHURU NI NINI KIBIBLIA?

UDHURU NI NINI KIBIBLIA?

Shalom, karibu tujifunze na tujikumbushe wajibu wetu sisi kama watakatifu katika safari yetu ya Imani hapa duniani.

Kuna mambo ambayo tunaweza tukashindwa kumfanyia Mungu, tukadhani kuwa “Mungu anaelewa”, kumbe yanatafsirika kama Ni UDHURU mbele zake.

Tofauti na sisi tunavyoweza kutafsiri Neno udhuru. Kwamba ni kutoa sababu za uongo, ili tu kuepuka jukumu au wajibu Fulani, kwamfano, labda mtu kakuambia naomba ukanipakilie mzigo wangu kwenye gari pale stendi unitumie.. Sasa pengine wewe hutaki kwenda, ili kupindua hiyo safari, saa hiyo hiyo unaunda safari yako ya uongo na kumwambia, hapana sitaweza kwenda, kwani ninamgeni wangu natarajia baadaye, nikamchukue hotelini sijui atatoka muda gani..Lakini unajua kabisa, jambo kama hilo hukuwa na mpango nalo, huo ndio udhuru tunaoufahamu sisi.

Lakini kwa Mungu udhuru, ni kutoa sababu za kweli tena  zenye maana na mashiko kabisa.. ambazo wakati mwingine ni kweli kabisa zinastahili kufanywa.. Ili kuelewa vizuri Embu tusome tena Habari hii kwa utulivu, naamini umeshaipitia mara kadhaa, lakini isome tena, na tena, uone ni nini Mungu analenga, na ujiangalie na wewe katika nafasi yako, Je! Mambo kama hayo yapo?,,Tusome..

Luka 14:16 “Akamwambia, Mtu mmoja alifanya karamu kubwa akaalika watu wengi,

17 akamtuma mtumwa wake saa ya chakula awaambie wale walioalikwa, Njoni, kwa kuwa vitu vyote vimekwisha kuwekwa tayari.

18 Wakaanza wote kutoa udhuru kwa nia moja. Wa kwanza alimwambia, Nimenunua shamba, sharti niende nikalitazame; tafadhali unisamehe.

19 Mwingine akasema, Nimenunua ng’ombe jozi tano, ninakwenda kuwajaribu; tafadhali unisamehe.

20 Mwingine akasema, Nimeoa mke, na kwa sababu hiyo siwezi kuja.

21 Yule mtumwa akaenda, akampa bwana wake habari ya mambo hayo. Basi, yule mwenye nyumba akakasirika, akamwambia mtumwa wake, Toka upesi, uende katika njia kuu na vichochoro vya mji, ukawalete hapa maskini, na vilema, na vipofu, na viwete.

22 Mtumwa akasema, Bwana, hayo uliyoagiza yamekwisha tendeka, na hata sasa ingaliko nafasi.

23 Bwana akamwambia mtumwa, Toka nje uende barabarani na mipakani, ukawashurutishe kuingia ndani, nyumba yangu ipate kujaa.

24 Maana nawaambia ya kwamba katika wale walioalikwa, hapana hata mmoja atakayeionja karamu yangu.

Embu zitafakari hizo sababu, uone kama hakuna hata moja isiyo na mashiko, ni kweli, sherehe tu, huwezi ifananisha na mke mpya..mwingine kanunua ng’ombe, wengi, hivyo ni lazima siku hiyo akawajaribu kwanza, vinginevyo wakiwa sio bora na siku imeshapita hawezi tena kuwarudisha,tayari ni hasara, mwingine kanunua shamba tayari, lakini bado hajaliona, hivyo ni lazima akalihakiki, kama ni lenyewe au kama ameuziwa dimbwi, na siku yenyewe ndio hiyo hiyo ya karamu aliyoalikwa hawezi kuacha kwenda?

Umeona, zote hizo zilikuwa ni sababu, lakini mwenye karamu anazitafsiri kama ni Udhuru. Kwasababu gani? Kwasababu wameyathamini mambo yao, Zaidi ya ile karamu yake kubwa.

Leo hii,watu wengi hata jumapili wameacha kwenda kanisani kabisa, wanasema, boss wangu hataki, wanazitetea kazi zao, ili wasifukuzwe..halafu kwenye vichwa vyao wanasema BWANA ANAELEWA!…Kama ingekuwa sio huyu boss wangu kunizuia, mimi nisingekosa kanisani hata siku moja..

Ndugu kwa Mungu huo ni udhuru..Kama unaweza kuitumikia kampuni yako, kwa siku 6 za wiki, hadi siku ya Mungu unaiiba, fahamu tu, Mungu hawezi kukuelewa, anautafsiri kama Udhuru. Haiwezekani wiki nzima, usijiwekee ratiba kwa Mungu wako ya kumwabudu yeye, hata siku moja.

Danieli hakuruhusu udhuru, hata alipokatazwa na mfalme wa dunia yote,(kumbuka Sio boss wa ka-kampuni fulani) kuabudu Mungu wake, na vitisho vyao vya kuwatupa katika tundu la simba wote watakaokaidi. kinyume chake Danieli ndio alifungua madirisha yake, akawa anamwabudu Mungu, wakati wengine, wanasema Mungu anaelewa, hali halisi ya sasa, tumekatazwa na mfalme, sisi ni nani tupinge..

Na walipomkamata na kumtupa katika tundu la Simba, Tunaona Mungu alikuwa naye..

Vivyo hivyo na akina Shedraka, Meshaki, na Abednego, walikataa udhuru wa Nebukadreza wa kuabudu sanamu, wakati wengine wanasema, Mungu anaelewa..wenyewe wakakataa kumvunjia Mungu heshima, ndipo walipotupwa katika tanuru la moto..Bwana aliwapigania na kuwaokoa.

Lakini ikiwa sisi kila jambo tutazama, hali zetu, tusijidanganye kuwa Mungu anaelewa! Hizo zote ni udhuru. Usiruhusu kazi ile muda wa Mungu wako, usiruhusu, familia, mihangaiko, mali zitafune muda wa Mungu wako. Wengine wanasema jumapili ndio faida ninapata, ndugu ziache hizo faida zipite, Ni nani kakuambia Mungu hatakupa hizo siku nyingine? epuka udhuru..

Na ndio maana mwishoni kabisa mwa ile Habari, Bwana anasema…

“Maana nawaambia ya kwamba katika wale walioalikwa, hapana hata mmoja atakayeionja karamu yangu”.

Watu wanaotanguliza mambo yao mbele Zaidi ya Mungu katika kipindi hichi cha siku za mwisho, kwenye Unyakuo, kwenye karamu ya mwanakondoo mbinguni hawataenda. Swali je! Na wewe ni mtu wa udhuru kwa Bwana? Jibu unalo.

Maran atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Maswali na Majibu

UFUNUO: Mlango wa 19

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 3

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

KWASABABU MUDA TULIOBAKIWA NAO SI MWINGI.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments