UTAKAPOKUWA MZEE, UTAINYOSHA MIKONO YAKO. NA MWINGINE ATAKUFUNGA

UTAKAPOKUWA MZEE, UTAINYOSHA MIKONO YAKO. NA MWINGINE ATAKUFUNGA

Bwana Yesu asifiwe,

Ufukufu na Heshimu ni vyake milele na milele. Amina.

Napenda tutafakari, Pamoja kwa makini maneno haya ambayo Bwana Yesu alimfunulia mtume wake Petro, ni maneno ambayo yatakufaa sasa wewe kijana ambaye bado una nguvu za kufanya utakalo hivi sasa..

Embu Tusome;

Yohana 21:18 “Akasema, Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na MWINGINE atakufunga na kukuchukua usikotaka”.

Hii kauli ni ya kuitafakari sana, sio ya kuichukulia juu juu, Hapa Bwana anamweleza Petro jinsi ujana wake unavyoweza kumpa uhuru wa ‘nani wa kujifunga chini yake’, na kumtumikia, mfano akiamua, ajifunge na kuwa mtumwa wa mali, uamuzi ni wake, akitaka ajifungue kisha ajifunge kwa mwingine tena, bado uwezo huo anao, leo anaweza akajifunga kwa Mungu, kesho kwa shetani, ni jinsi apendavyo kwasababu nguvu hizo anazo rohoni.

Hapo ndipo lile neno linalosema, “nimewaandikia ninyi vijana kwasababu mna nguvu ya kumshinda yule mwovu”(1Yohana 2:14), linapotimia, maana yake, uwezo wa kujifungua au kujifunga kwa shetani, unao, angali  bado una nguvu..

Lakini tunaona Bwana Yesu anampa angalizo lingine na kumwambia, utakapokuwa mzee, “MWINGINE”..Atakufunga na kukuchukua usikotaka..

Sasa ulishawahi kutafakari huyo ‘mwingine’ ni nani?

Huyo mwingine ni Aidha “Mungu” au “Shetani”.. Maana yake ni kuwa utafika wakati, ambapo kama hutajiweka chini ya Mungu tangu sasa, shetani atakuweka chini yake kipindi hicho, penda usipende,..yaani utamilikiwa na shetani asilimia mia ya Maisha yako, na kukufanyia chochote apendacho juu yako..

Ukishafikia hii hatua, kamwe huwezi tena kumgeukia Mungu, wala hata kuzielewa Habari za Mungu, kwasababu tayari wewe ni mfungwa wa shetani.

Hali kadhalika kinyume chake ni kweli, unapofanyika chombo cha Mungu sasa angali una nguvu..utafika wakati huna nguvu, Mungu atakuchukua moja kwa moja na kukupeleka atakapo yeye.. Huko ndipo wakati ambapo uzee wako unaishia vema..hata kama ni kwa kifo kwasababu ya ushuhuda, lakini kamwe hutakaa upotee tena milele..kwasababu umeshafungwa tayari na Mungu, hivyo hakuna namna yoyote utakaa upotee au uanguke mikononi mwa shetani.

Ndio maana biblia inasema..

Mhubiri 12:1 “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo”.

Maana yake ni kwamba usipomkumbuka muumba wako leo, wakati una nguvu (wakati wa ujana wako) utafikia wakati, utapoteza furaha yako yote ya maisha.. Hicho ndicho kipindi cha kufungwa na ibilisi, na kupelekwa usipotaka..Angalia vema utaona wazee wengi ambao wamekuwa wakipuuzia injili tangu ujanani, mwisho wao huwa hauwi mzuri, kunakuwa na ugumu mkubwa sana kuwashawishi kwa Habari ya wokovu. Huwa wanapitia wakati mgumu sana kiroho kwasababu tayari “mwingine” ameshawafunga na kuwachukua wasipotaka..

Hivyo Bwana Yesu alikuwa anamtahadharisha Mtume Petro, sio tu kwa Habari ya kifo chake, lakini pia kwa maamuzi anayoyachukua sasa..lazima yawe ya busara.. Utumwa anaouchagua sasa, ndio utakaomuhifadhi baadaye..

Kama ni Kristo, basi Kristo atamwokoa, lakini kama ni shetani basi shetani atampeleka alipo yeye..

Ndugu, siku hizi ambazo waweza kusikia injili, na ukashawishika moyoni, ndizo siku zako za ujana, embu sasa anza kujiweka chini ya Kristo, akuongoze, achana na ulimwengu na mambo yake, wanadamu hawawezi kukufaidia chochote kwa siku zijazo.

Anza kuisafisha njia yako sasa, kama vile biblia inavyotushauri katika..

Zaburi 119:9 “Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako”.

Kumbuka, ni kipindi kifupi sana tumebakiwa nacho hadi kurudi kwa Bwana Yesu mara ya pili, Kama unadhani, Unyakuo bado sana, fikiria mara mbili, dalili zote zimeshatimia, injili inayoendelea sasa sio ya kubembelezewa wokovu, bali ni ya kujiingiza katika ufalme kwa nguvu. Huna sababu ya kuendelea kufichwa uhalisia, dakika hizi ni za majeruhi, siku yoyote, parapanda  inalia, PARAPANDA INALIA!!

Bwana atusaidie.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

PETRO AKAMWAMBIA YESU “BWANA NA HUYU JE”?

NI YESU YUPI UMEMPOKEA?, NI ROHO IPI UMEIPOKEA? NA INJILI IPI UMEIPOKEA?

Je! Ni kanisa lipi sahihi kumuabudia Mungu?

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita.

Ni sahihi kusema sikuitiwa kuhubiri ubatizo kama Paulo alivyosema (1Wakorintho 1:17)?.

LAKINI WAKATI WA TAABU WATASEMA, SIMAMA UKATUOKOE.

KUNA AINA NGAPI  ZA MAOMBI?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Prisca komba
Prisca komba
2 years ago

Amina