BALI WANA WA UFALME WATATUPWA NJE!.

BALI WANA WA UFALME WATATUPWA NJE!.

Mathayo 8:11 “Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni;

12 bali WANA WA UFALME WATATUPWA KATIKA GIZA LA NJE, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno”.

Je umewahi kujiuliza ni kwanini Bwana Yesu aseme maneno hayo??, kuwa Wana wa Ufalme watatupwa nje?.  Watakuwaje wana wa Ufalme halafu tena watupwe nje?…hao si ndo wangepaswa waingie ndani??.. Je Bwana Yesu alikosea?

Jibu ni la!, hakukosea..bali  ni kweli Wana wa Ufalme watatupwa nje!!.

Sasa ili tuwajue hawa wana wa Ufalme ni akina nani?. Hebu tuutafakari mfano mwingine wa Bwana alioutoa mahali pengine.

Mathayo 22:1 “Yesu akajibu, akawaambia tena kwa mithali, akisema,

2 Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanawe arusi.

3 Akawatuma watumwa wake WAWAITE WALIOALIKWA KUJA ARUSINI; nao wakakataa kuja.

4 Akatuma tena watu kwa wengine, akisema, WAAMBIENI WALE WALIOALIKWA, Tazameni, nimeandaa karamu yangu; ng’ombe zangu na vinono vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari, njoni arusini.

5 Lakini hawakujali, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake;

6 nao waliosalia wakawakamata watumwa wake, wakawatenda jeuri, na kuwaua.

7 Basi yule mfalme akaghadhibika; akapeleka majeshi yake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza mji wao.

8 Kisha akawaambia watumwa wake, Arusi i tayari, LAKINI WALE WALIOALIKWA HAWAKUSTAHILI.

9 Basi enendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini.

10 Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi IKAJAA WAGENI”.

Katika mfano huo utaona kuna makundi mawili, kundi la kwanza ni WAALIKWA, (ambao tunaweza kuwaita  kama “wana wa Harusi”, au waliostahili kuingia harusini, ambao walipewa kadi zao maalumu za mwaliko na waliandaliwa viti kabisa, na wanafahamiana na Bwana harusi).. Lakini wapo ambao hawakupewa kadi kabisa…wala walikuwa hawajaalikwa, kwaufupi hawakuwa kwenye bajeti yoyote, wala walikuwa hawafahamiani na Bwana harusi.

Lakini mwishoni tunaona wale WANA WA HARUSI, ambao walikuwa na nafasi harusini, ambao walifahamiana sana na Bwana harusi, ambao ni ndugu zake, na jamaa zake na Bwana harusi, waliokuwa wamekusudiwa hiyo sherehe, yaani kwaufupi karamu ilikuwa ni kwaajili yao na furaha yao…mwisho wa siku hakuna hata mmoja, aliyeingia katika hiyo karamu..badala yake walitokea wengine wakaingia katika karamu..ambao hawakustahili, wasiojuana hata na Bwana harusi, waliotoka kutoka njia panda za barabarani, kutoka mitaani, kutoka masokoni na kutoka sehemu mbali mbali…wakaingia karamuni..harusi ikajaa WAGENI.. (Zingatia hilo neno wageni!)

Kupitia mfano huu tayari tutakuwa tumeshajua ni kwanini Bwana Yesu aseme haya…

Mathayo 8:11 “Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni;

12 bali WANA WA UFALME WATATUPWA KATIKA GIZA LA NJE, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno”

Leo hii wana wa Ufalme duniani ni wengi sana… Kwa ufupi wote ambao wameisikia Injili, na injili inajirudia rudia masikioni mwao, lakini wanaitolea udhuru kila mara, hawapo tayari kujikana nafsi na kumfuata Yesu, hao tayari ni WANA WA UFALME,  ambao Bwana anawaalika lakini hawaalikiki!!!.

Pamoja na kwamba wamehubiriwa uzuri wote wa mbinguni, na faida za kiroho watakazozipata endapo wakiamua kubadilisha Maisha yao, na kuishi kulingana na Neno la Mungu na mapenzi ya Mungu, Pamoja na kuwa wamejihakikishia kuwa ni kweli wanaishi nyakati za kurudi Bwana wao… lakini bado watatoa udhuru..

Utasikia wanasema.. “Ni kweli natamani kusimama kiimani lakini kazi zangu zinanibana, nakosa muda wa kusoma biblia” .. “Ni kweli natamani kuwa mwombaji na kuhudhuria ibadani lakini kazi ni nyingi, nakuwa bize mpaka jumapili”“Ni kweli natamani kuacha pombe, na kuacha kuvaa kikahaba na kihuni ila naamini sikumoja tu nitaacha”.. “Ni kweli Neno linanufundisha kubatizwa, lakini siwezi kwasasa, kwasababu mchungaji wangu na familia yako hawaamini hilo” n.k n.K.

Sasa hili ndio kundi la WANA WA UFALME, ambao siku ile, biblia imetabiri WATATUPWA NJE, Kutakakowako KILIO NA KUSAGA MENO!!.

Ndugu usifurahie tu kulisikia Neno, au kulisoma Neno na kulielewa, bali furahia na kushangilia UNAPOLITENDA NENO. Biblia sio kitabu cha taarifa, au simulizi..bali ni kitabu cha MAELEKEZO ya Nini cha kufanya!..Maana yake tunapaswa tukitendee kazi kile tunachoelekezwa kwenye biblia, sio tukisome tu!!..au tuhubiriwe tu!..

Leo tunaishi katika kizazi cha watu wanaopenda sana kusikiliza mahubiri, wanapenda sana kuhubiriwa, wanaopenda sana kufundishwa biblia, lakini si wanaopenda KUTENDA KILE WANACHOKISIKIA AU WANACHOKISOMA AU WANACHOFUNDISHWA!!!!.

Yakobo 1:22 “Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, HALI MKIJIDANGANYA NAFSI ZENU.

23 Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo.

24 Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.

25 Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, HUYO ATAKUWA HERI KATIKA KUTENDA KWAKE.

Vile vile usifurahie kuwa Mtu wa UDHURU!.. Ukidhani Udhuru ni wako ndio utakaomfanya Bwana akuhurumie siku ile, la!.. Yeye siku zote analiangalia Neno lake alitimize na si udhuru zetu..

Luka 9:61 “Mtu mwingine pia akamwambia, Bwana, nitakufuata; lakini, nipe ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu.

62 Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu“.

Mathayo 10:37 “Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili.

38 Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili.

39 Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona”.

Jikane nafsi mtu wa Mungu… Unyakuo wa kanisa upo Karibu!

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

NENO LA MUNGU KATIKA UTIMILIFU WOTE.

USIMPE NGUVU SHETANI.

GHARAMA YA UFALME WA MBINGUNI.

Tofauti kati ya ufalme wa mbinguni na ufalme wa Mungu ni ipi?

Hapo ndipo, atakapompa Mungu Baba ufalme wake.

MWANANCHI WA UFALME WA MBINGUNI

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Zilper
Zilper
1 year ago

Shalom, mbona siku hizi sioni ule mtiririko wa masomo ili nichague