MWANANCHI WA UFALME WA MBINGUNI

MWANANCHI WA UFALME WA MBINGUNI

Mwananchi ni mtu aliye na uraia wa Nchi fulani.

Kwamfano mtu aliyezaliwa Taifa la Tanzania ni mwananchi wa Tanzania, Kadhalika lipo Taifa la kimbinguni..Na hilo yeyote anayezaliwa katika Taifa hilo anaitwa Mwananchi wa Taifa la Mbinguni..Na kila mwananchi analindwa na katiba.

Biblia inasema katika..

1Petro 2:9 “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, Taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu;

10 ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema”.

Huwezi kuzungumzia Taifa bila kuhusisha mwananchi wa hilo taifa. Palipo na Taifa ni lazima pawepo na wananchi..Na Taifa la Mbinguni lina wananchi wake.

Hebu tuzitafakari dondoo chache hizi muhimu, ili zitusaidie kuelewa ni namna gani ufalme wa Mbinguni unafanya kazi.

KATIBA

  • Mwananchi wa Taifa lolote ni lazima aongozwe na kitabu kimoja muhimu kinachoitwa KATIBA,…Ambapo ndani ya kitabu hicho ndipo zinapopatikana sheria na taratibu zote za kuishi katika nchi hiyo husika…
  • Mwananchi yoyote anayeishi kulingana na KATIBA,.Ataishi kwa amani na furaha na kufanikiwa katika nchi hiyo..Kwani hatavunja sheria za nchi hiyo na hivyo kumfanya awe mwananchi bora na mwenye kukubalika.
  • Kila Mwananchi analindwa na Katiba..Licha ya katiba kutumika kama mwongozo wa kila mwananchi..lakini pia katiba hiyo hiyo inatumika kama chombo cha kumlinda mwananchi..Kwamba Mwananchi yoyote hapaswi kunyimwa haki yake, uhuru wake, pamoja na kuhatarishiwa amani yake..Hivyo mtu au kitu chochote kitakachokwenda nje na sheria hiyo..na kuipoteza amani ya raia..Basi mtu huyo au kitu hicho kitachukuliwa hatua kali ya kisheria.
  • Kila mwananchi ni mali ya Nchi husika..Hakuna mtu yeyote ambaye ni mali yake mwenyewe. Si ruhusa kisheria mtu kujiua!..Mtu yeyote hata anayejaribu kujiua anakwenda kinyume na katiba ya nchi na hivyo akibahatika kusalimika atakabiliwa na mashitaka ya MAUAJI!.

Kwa dondoo hizo chache. Tumeweza kujua Mwananchi ni nani na Majukumu yake ni yapi na usalama wake ni upi.

Hivyo tupo tayari sasa kujifunza juu ya upande wa Pili wa uraia wa MBINGUNI. Kumbuka mbingu ni Taifa kama tulivyosoma hapo juu..Kwahiyo hebu tutafakari pia dondoo chache zifuatazo ili tuelewe zaidi.

  • Kama vile Mwananchi wa kawaida anakuwa anaongozwa na katiba..Vivyo hivyo na mwananchi wa Mbinguni ni lazima aongozwe na KATIBA ya Kimbinguni..Ambayo hiyo si nyingine zaidi ya BIBLIA (Kitabu kitakatifu).
  • Kama vile raia wa nchi endapo akiishi kwa katiba ya nchi atafanikiwa, kadhalika Raia wa kimbinguni endapo akiishi kulingana na katiba ya kimbinguni ndipo atakapofanikiwa na kuishi maisha yasiyo na mashaka.Lakini akiishi kinyume na katiba ya ufalme wa mbinguni, basi atapata matatizo ya kushitakiwa, kufungwa au hata kuuawa.
  • Tatu kama vile kila mwananchi wa kawaida anavyolindwa na katiba ya nchi, vivyo hivyo Raia wa ufalme wa mbinguni anakuwa analindwa na katiba. Katiba ya nchi inasema ni wajibu wa vyombo vya usalama kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao muda wote..Hivyo jukumu la kumlinda mwananchi ni la serikali kupitia vyombo vya dola…Mwananchi wa kawaida hana ruhusu ya kubeba silaha mkononi na kutembea nayo barabarani.. silaha yake ni kuishi kulingana na katiba basi…jukumu la ulinzi ni la vyombo vya dola…Kadhalika Mwananchi wa ufalme wa mbinguni haruhusiwi kubeba silaha yoyote ya kimwili, jukumu la kupambana na maadui zetu ni jukumu la Malaika watakatifu, hao ndio wanaobeba silaha na kutupigania upande wetu…silaha yetu kubwa ni NENO LA MUNGU (katiba) huo ndio upanga wetu.

Biblia inasema katika..

Waefeso 6:11 “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.

12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.

13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.

14 Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,

15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; 6.16 zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.

17 Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; 6.18 kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote”

Hivyo Mwananchi yoyote wa Ufalme wa mbinguni hana budi Kuifahamu katiba kikweli kweli…Kama vile ilivyo jukumu la kila mwananchi kuifahamu katika ya nchi yake.

Sasa Madhara ya kutoifahamu Biblia ni nini?

Madhara ya kutoifahamu biblia(Neno la Mungu) kwa Mwananchi wa Taifa la Mbinguni,.hayatofautiani sana na madhara ya mwananchi wa kawaida kutoifahamu katiba.

Mwananchi asiyeifahamu katiba, ni rahisi kufanya makosa  na asijue kama anafanya makosa..Ni rahisi kwenda kulala na ndugu yake wa damu, na wakati hajui sheria ya nchi (katiba) inasema kwamba ni kosa mtu yeyote kulala na ndugu wake wa damu, hukumu yake ni kifungo cha maisha.

Kadhalika anaweza akagombana tu na ndugu yake na kwa hasira akaenda kumchomea nyumba yake, pasipo kujua katiba inasemaje kwa mtu anayepatikana kwa kosa la kuchoma nyumba..Kosa la kuchoma nyumba kulingana na sheria ya nchi yetu, hukumu yake ni kifungo cha maisha. Sasa mambo madogo tu kama hayo yanaweza kumsababishia akapoteza maisha yake yote kutumikia vifungo.

Hatari ya kutoijua Biblia kwa mwamini.

Vivyo hivyo mwananchi wa Taifa la mbinguni asipoielewa katiba ya mbinguni (yaani biblia) inasema nini, anaweza kujikuta anafanya mambo akidhani anampendeza Mungu kumbe anamchukiza Mungu pakubwa..na adhabu yake ikawa ni ziwa la moto milele..Mtu anaweza akawa ni mlevi akidhani ulevi si dhambi..anaweza akawa mwasherati akidhania uasherati sio dhambi..anaweza akawa mwabudu sanamu akidhani sio dhambi..n.k

Pia madhara mengine ya kutoijua katiba ni KUONEWA NA KUNYANYASWA. Mwananchi asiyeijua katiba ya nchi yake hata mtu akija tu anaweza kumtishia na kumnyima haki yake..lakini kama anaijua hawezi kubabaishwa kwasababu anaelewa vizuri sheria za nchi..Hivyo ni ngumu kupoteza haki yake..Vivyo hivyo Mwananchi wa Ufalme wa mbinguni asipoielewa vizuri biblia ni rahisi adui shetani kumnyang’anya haki yake. Utaona anapelekeshwa huku na huku, majaribu haya na yale..kuteswa huku na kule..Yote hayo ni kwasababu haijui biblia Neno la Mungu.

Na Dondoo ya mwisho kabisa ni kwamba kila mtu ili awe Mwananchi halali wa Taifa hilo ni lazima awe  amezaliwa katika hilo Taifa (Huo ndio utambulisho wake wa kwanza),.. Vivyo hivyo katika Uraia wa ufalme wa mbinguni..Ni lazima mtu azaliwe katika ufalme huo.

Na mtu hazaliwi kwa damu na nyama, bali anazaliwa kwa Roho na kwa Maji ndipo ahesabike kuwa ni Mwananchi wa Taifa la Mbinguni.

Sasa mtu anazaliwaje kwa Maji na kwa Roho?

Maana ya kuzaliwa kwa maji ni kubatizwa kwa maji mengi (Yohana 3:23) Na kwa Jina la Yesu (Matendo 2:38). Na maana ya kuzaliwa kwa Roho ni kupata ubatizo wa Roho Mtakatifu. Hatua hizo mbili ndio zinazokufanya uwe umezaliwa mara ya pili na kuwa Mwananchi wa ufalme wa Mbinguni.

Yohana 3:3 “Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.

4 Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?

5 Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.

6 Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.

7 Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili”.

Je umezaliwa mara ya PILI?. Je wewe ni Mwananchi wa Taifa teule la kimbinguni..Je wewe ni mrithi?..Kumbuka FALME NA MATAIFA YA DUNIA YOTE YATAPITA…Lakini UFALME WA MBINGUNI UTADUMU MILELE..NA RAIA WAKE WATADUMU MILELE!!.

Yapo mengi ya kujifunza juu ya ufalme huu wa mbinguni tukilinganisha na ufalme wa duniani..lakini Muda usingetosha kuyaandika yote hayo, lakini kwa haya machache, yatatupa chachu ya kuzidi kuutafuta ufalme wa mbinguni kila siku kwa bidii.

Bwana akubariki sana

Tafadhali share na wengine.

Maran atha!


Mada Nyinginezo:

INJILI NI NINI?

Mbona Mungu anaruhusu watu wapate shida, ilhali ana uwezo wa kutuepusha?

UFALME WA MUNGU HAUPATIKANI KIRAHISI.

JE! UNAYO NAFASI MBINGUNI?

KUWA MAKINI NA MITANDAO, NI SHIMO REFU.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Victor Mwandunga
Victor Mwandunga
1 year ago

Amen. Amen