LAKINI WAKATI WA TAABU WATASEMA, SIMAMA UKATUOKOE.

LAKINI WAKATI WA TAABU WATASEMA, SIMAMA UKATUOKOE.

Ulishawahi kukutana na kundi la watu ambao linakutafuta tu wakati wa shida, kama ndio, kuna hali Fulani unajisikia ambayo sio nzuri, ni kweli wapo ambao mazingira yanawabana washindwe kukutafuta nyakati nyingine, lakini wapo ambao wewe kwao ni mtu wa kuwatatulia tu matatizo, Habari nyingine na wewe hawana..

Kuna mtu mmoja alikuwa ananifuata nimtatulie tu matatizo yake, lakini baada ya hapo ukimpigia hata simu umsalimie, hapokei, na anabadilisha line ya simu moja kwa moja ili usimpate, baadaye anakuja kukutafuta tena, na jambo linalofuata hapo ni kuomba msaaada..

Unajua hata kama utamsaidia, lakini utasema kwanini iwe hivi, kwanini tusiwe na mahusiano hata na nyakati nyingine zote..

Sasa hiyo hali ndiyo ambayo Mungu anapitia sasahivi kwa wanadamu wengi duniani, biblia inasema..

Yeremia 2:27 “waliambiao gogo la mti, Wewe u baba yangu; na kuliambia jiwe, Ndiwe uliyenizaa; kwa maana wamenipa mimi visogo, wala hawakunielekezea nyuso zao; LAKINI WAKATI WA TAABU WATASEMA, SIMAMA UKATUOKOE”.

Umeona, wanadamu wengi sasa kinachowapeleka kwa Mungu, si kingine Zaidi ya kuomba, wafunguliwe, kuomba waponywe, kuomba wafanikishwe kiuchumi, kuomba kazi, n.k.

Lakini ukiangalia mahusiano waliyonayo na Mungu ni hafifu sana au hakuna kabisa.. Hana muda wa kusoma biblia kuyajua mapenzi ya Mungu ni nini katika Maisha yake, kumaliza hata dakika 20 kila siku katika kutafakari Neno la Mungu hawezi, kuomba kunamshinda, kwenda ibadani ni mara moja kwa mwezi, ikizidi sana mara mbili, na hata akienda ni ili Mungu amjibu lile ombi lake alilomuomba lakini sio kumwabudu katika Roho na Kweli.

Anachokiona  kirahisi kwake, ni kwenda kununua maji ya upako na mafuta, ili amwage kwenye biashara zake, ili mambo yake yaende sawa.. Au pale anapopitia hali mbaya sana ya magonjwa ndipo anapomfuata Mungu ili amsaidie,. Hapo ndipo atafunga na kuomba, na kusoma Neno kila siku kwa bidii..Lakini siku nyingine zote anaishi maisha ya dhambi.

Ndugu, tujue kabisa Mungu hapendezwe na huo mfumo wetu wa Maisha, Mungu ametuzira watu wengi sana na sisi hatujui, ndio maana inakuwa ngumu sana kusaidiwa na Mungu kwasababu, Maisha yetu ni ya kinafki mbele zake.

Lakini ukiendelea kusoma pale Bwana anasema..

Yeremia 2:27 “waliambiao gogo la mti, Wewe u baba yangu; na kuliambia jiwe, Ndiwe uliyenizaa; kwa maana wamenipa mimi visogo, wala hawakunielekezea nyuso zao; lakini wakati wa taabu watasema, Simama ukatuokoe.

28 LAKINI WAKO WAPI MIUNGU YAKO ULIOIFANYA? Na wasimame hao, kama wakiweza kukuokoa wakati wa taabu yako; kwa maana hesabu ya miungu yako ni sawasawa na hesabu ya miji yako, Ee Yuda.

29 MBONA MNATAKA KUTETA NAMI? Ninyi nyote mmeniasi, asema Bwana”.

Umeona tusimgeuze Mungu kama ni sehemu ya kutatulia matatizo yetu tu, ili hali Maisha yetu hayaendani na wokovu. Tusitete na Mungu, Mambo hayo kayafanye kwa waganga wa kienyeji lakini usifanye kwa Mungu, kwasababu utajikuta unaangukia tu laana badala ya baraka.

Hivyo tuanze sasa, kumtafuta Mungu nyakati zote, tuhakikishe tunayatenda mapenzi yake, tuonyeshe bidii zetu kwake, kwamba tunampenda sio kiunafiki, bali kwa mioyo yetu kweli. Tunamtafuta sio atufanye kuwa mabilionea, bali atufanye kuwa wana wake kama Yesu Kristo. Na ndio sasa hata hayo mengine atasaidia bila hata kutumia nguvu wala kumwomba..

Kumbuka katika nyakati hizi za mwisho, watakaokwenda kwenye UNYAKUO, sio kila mtu asemaye ninamwamini Mungu tu, halafu basi,..Bali ni watu wayatendao mapenzi ya Mungu kikamilifu sawasawa na Neno la Kristo.

Mathayo 7:21 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.

22 Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?

23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”

Bwana atupe jicho la kuona, na kuyatendea kazi.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

USIJARIBU KUMGEUZA MUNGU MGANGA WA KIENYEJI,UTAKUFA.

MLANGO MWINGINE WA ADUI KUTULETEA MAJARIBU.

NI KWA NAMNA GANI SHETANI ANAIZUIA INJILI?

Talanta ni nini katika biblia (Mathayo 25:14-30)

WAKATI ULIOKUBALIKA NALIKUSIKIA

JINSI UNAJISI UNAVYOMGHARIMU MTU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments