MAFUNDISHO MAALUMU KWA WANA-NDOA; FAMILIA TAKATIFU: Marimu na Yusufu.
Karibu katika mwendelezo ya Masomo ya wanandoa . Ikiwa wewe ni mwanandoa au unajiandaa kuingia katika ndoa, basi masomo haya ni muhimu sana kwako kuyajua.
Tulishatazama, huko nyuma jinsi ndoa ya kwanza ya wazazi wetu Adamu na Hawa ilivyokuwa, na changamoto walizokutana nazo, na jinsi walivyoweza kukabiliana nazo. Ikiwa hukupata masomo hayo, basi utatumia ujumbe inbox tukutumie.
Leo tutatazama familia nyingine takatifu. Ambayo ni ya Yusufu na Mariamu. Yapo mambo mengi sana ya kujifunza, juu ya wanandoa hawa, Na ndio maana kwanini Mungu alikusudia mwokozi wa ulimwengu aje kwa kupitia watu hawa, Ni Kwasababu kuna mengi ya kujifunza kwao. Tutaona pia utaratibu Mungu aliowawekea katika kutimiza kusudi lake hapa duniani.
Alikuwa ni mtu aliyeepuka madhara kwa wengine: Yusufu hakuwa kama Samsoni, ambaye alipoona mwanamke aliyemchumbia amepewa rafiki yake, akakasirika, na kwenda kuchukua mbweha mia tatu, na kuwapeleka kwenye shamba la ngano la wafilisti, kuyateketeza ili ajilipizie kisasi (Waamuzi 15:1-20).
Lakini Yusufu hakuwa hivyo, yeye alipoona binti aliyemchumbua ana mimba, alitafuta njia ya kuepusha madhara kwa dada huyo, hivyo akakusudia ‘’kutomuabisha’’. Akapanga mipango yake ya kumuacha kwa siri,..huenda alipoulizwa vipi mbona humwoi msichana huyu, akawa anasema bado sijafikia muafaka, nitawapa majibu.
Mathayo 1:18 “Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu.
19 Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri”.
Sasa Ikiwa alikuwa na hofu ya kumwaibisha asipigwe mawe, unatazamia vipi mtu kama huyu, angeweza kumpiga mke wake hata baada ya ndoa , au awe anatoa siri za madhaifu ya mke wake kwa watu wa nje?
Mwanamke anapoteleza, sio lazima wakati wote upeleke taarifa kwa jamii, aaibike au umpige, au umfukuze, bali ni kumvumilia, kwasababu mengine yanatokea kwa sababu ambazo utakuja kuzijua mbeleni. Tabia hii alikuwa nayo Baba-wa-Yesu (kimwili)
Alikuwa ni bikira: Ni binti ambaye alijitunza tangu anazaliwa mpaka anakuwa mwanamke, Na hiyo ikapelekea kupata neema ya kuchumbiwa na mzao wa Daudi (Yusufu). Kumbuka ahadi ya kuzaliwa Kristo haikuwa kwa Mariamu, bali ilikuwa kwa uzao wa Daudi. Hivyo Mungu alipomuona Mariamu, na ukamilifu wake katika mwili ndipo akasema huyu anafaa kupata neema ya kukutana na Yusufu atimize kusudi la Mungu.
Maana yake ni nini, upo umuhimu sana, wa msichana kujitunza sana mwili wake, kwani hiyo itakupelekea kupata mwanaume bora, na uzao bora. Ni kweli si wote wataingia katika ndoa wakiwa bikira, lakini ikiwa umetambua sasa, wajibu wako, na umeokoka, huna budi kujitunza sana, na hata baada ya ndoa, ili hicho kitakachotoka tumboni mwako kiwe kitakatifu.
SASA BAADA YA KUONA SIFA HIZI KUU (2), WALIZOKUWA NAZO HAWA WANANDOA, TUONE UTARATIBU WA KIMAJUKUMU JINSI MUNGU ALIVYOUGAWANYA KWAO.
Malaika Gabrieli alitumwa kwa Mariamu, ili kumpa taarifa ya kupata mimba kwa uweza wa Roho na kwamba mtoto huyo ataitwa Yesu.
Lakini baada ya hapo, Mungu hakuendelea tena kusema na Mariamu moja kwa moja. Bali alimgeukia mumewe Yusufu, na kumwagiza kuwa atakapozaliwa amwite jina lake YESU.
Mathayo 1:20 “Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu.
21 Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao”.
Na utaona baada hapo, wakiwa kule Bethelehemu, bado Malaika anamtokea Yusufu tu, na kumwambia, mchukue mtoto na mama yake, wapeleke Misri, kwasababu Herode anataka kumuua mtoto.(Mathayo 2:13-14)
Tengeneza picha Mariamu angekuwa ni mwanamke kiburi, angesema, mbona Mungu hajasema na mimi kuhusiana na hilo?, Kwanza si wewe uliyembeba masihi, mateso huyajui, huko Misri ni nani unayemjua, nangojea Mungu anithibitishie kwanza mimi..lakini hakuwa hivyo alikubali kutii, bila kujadili jadili.
Bado utaona, akiwa kule Misri, malaika anamtokea tena Yusufu peke yake na kumwambia, mchukue mke na mtoto urudi nao Israeli kwasababu Herode amekufa. Safari tena ya mihangaiko ikaanza, huku Mariamu akisikiliza maagizo ya mumewe na kutii (Mathayo 2:19-20).. Lakini wakiwa pale Bethelehemu, wametulia ili sasa waanze maisha, saa hiyo hiyo, Yusufu anamwambia mke wake, tuondoke hapa tuende tena Nazareti, Mungu ameniagiza hivyo (Mathayo 2:22-23).
Mariamu hakuwa na kigugumizi kumsikiliza mume wake, hakuwa na kazi nyingine yoyote zaidi ya kupokea maagizo ya uongozi kuhusu familia au mtoto kutoka kwa mumewe.
Kwa mwanamke: Tambua kuwa mume ndio kichwa cha familia, Mungu atamtumia yeye, kuyalinda na kuyatamia maono yako, huwezi kufanikiwa bila yeye. Haijalishi Mungu kakuonyesha mambo makubwa kiasi gani hapo mwanzoni. Ikiwa humtii mume wako, ujue kuwa unajiharibia wewe mwenyewe. Utiifu ni muhimu sana, hata wakati ambapo unaona sehemu unapopelekwa sio pa kuvutia.
Ndio maana unawajibu sana wa kumwombea mume wako, ikiwa ni mwenye dhambi, Mungu ambadilishe. Kwasababu yeye ndio usalama wa maono yako.
Kwa mwanaume: Umewekwa kama kichwa, ni lazima utambue kulinda maono mema ya mkeo, Si kila taarifa nzuri itakufikia wewe wa kwanza, Wakati mwingine inaanzia kwa mwanamke, kama ilivyokuwa kwa Mariamu, kisha wewe baadaye, hivyo uonapo hivyo, usipige vita, bali, sikiliza, tafakari, pia tendea kazi, Hapo ndipo Mungu atakapokutumia, kuijenga familia bora. Wewe kama mlinzi huna budi, kutimiza wajibu wako,wa kumtunza mkeo na kumpenda kama maandiko yanavyosema. Jambo lolote linaloihatarisha familia yako, shughulika nalo kwelikweli usimwachie mwanamke alitende.
Hivyo kwa kuzingatia mambo hayo, Ndoa zetu zitakuwa bora, mfano wa ile ya Yusufu na Marimu. Na Bwana atatupa zawadi ya kuzaa vitakatifu kama Ilivyokuwa kwa Yesu na wadogo zake wote. Tambua wajibu wako, simama katika nafasi yako.
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
WANA-NDOA: Baba Mkwe, Na mama Mkwe.
ONDOA TAKATAKA KATIKA FEDHA, NA CHOMBO KITATOKEA KWA MTAKASAJI.
About the author