Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo Bwana wetu, Karibu tuzidi kuyachambua maandiko;
Mwanadamu anasongwa na mambo mawili pale linapokuja suala la kuamua hatma ya maisha yake ya milele. Je! Atii au apate maarifa kwanza?. Pale Mungu anapomwambia Usizini? Je, asifanye hivyo? Au achunguze kwanza ni nini kipo nyuma ya tendo hilo, ndipo awe huru sasa kuchagua kuzini au kutokuzini?
Ukweli ni kwamba asili ya mwanadamu ni kutaka maarifa kwanza, ya kitu ndipo baadaye atii, Lakini Je! Biblia inatufundisha nini kuhusiana na maamuzi sahihi na Salama ambayo Mungu aliyaweka kwa mwanadamu.
Tukisoma ile habari ya pale bustanini biblia inatuambia,.. Mungu alipanda miti yake, kisha alipomaliza akatoa maagizo kuhusiana nayo akasema..
Mwanzo 2:16 “Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, 17 walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika”.
Lakini mwanadamu akaona, hayo maelezo ya Bwana Mungu hayajitoshelezi, kwanini atuzuie tusile, hajui kuwa sisi tunataka tupate sababu kwanza, (tupate maarifa), kujua ni nini kwanza kipo nyuma ya mti huo, ndipo tuwe sasa huru kuchagua kuula, au kutoula. Ndipo wao wakauendea na kuula.
Mwanzo 3:4 “Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, 5 kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya. 6 Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni MTI WA KUTAMANIKA KWA MAARIFA, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala”.
Lakini walipofanya vile, hawakuvuna chochote, matokeo yake wakajikuta tayari wameshaingia kwenye matatizo ambayo mpaka sasa tunayashiriki, yale maarifa waliyoyategemea kuwafanya wawe bora, yakawa mauti kwao.
Asili yetu sisi wanadamu hatukuumbwa kwenye kupata maarifa kwanza, ndio tuishi, bali kwenye kutii kwanza.. Ndivyo tulivyotengenezwa na Mungu.. Kwamba tukitembea katika kutii tutakuwa salama sikuzote,..hayo mengine yatakuja baadaye. Ndicho alichokifanya Ibrahimu alipoambiwa akamtoe mwanawe sadaka ya kuteketezwa alitii kwanza, hakudadisi na kusema kwanini huyu Mungu atoe maagizo ya kishetani kama haya ya kuua watu, yeye alitii, ndipo akaja kujua sababu baadaye.
Hii ikiwa na maana kuwa,..Kama Yesu katuambia wazinzi wote, na waongo wote, hawataurithi uzima wa milele, bali sehemu yao ni katika lile ziwa la moto. Tunahitaji nini tena, kutafuta uzuri uliopo nyuma ya uzinzi, mpaka tukaujaribu.au kutafuta eneo la kijeografia la jehanamu, tulione ndio tuamini?
Ufunuo 21:8 “Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili”.
Bwana Yesu anasema.. Yeye ndio njia, na kweli na uzima, mtu hafiki kwa Baba isipokuwa kwa njia yake yeye (Yohana 14:6), FULL STOP!..Sasa kwanini tutafiti njia zetu wenyewe za kutupa wokovu? Kwanini uishi kwa mitazamo yako, au ya wanadamu, wanaokuambia hakuna mwisho wa dunia, au hakuna maisha baada ya kifo
Katika nyakati hizi za hatari ambazo biblia inazitaja (2Timotheo 3:1), ni lazima “tuongeze maarifa ya kulijua Neno la Mungu, na sio maarifa ya kuyadadisi maneno ya Mungu, kama Adamu na Hawa”..Tutapotea haraka sana, tukiwa watu wa namna hii, kutilia mashaka maneno ya Mungu, kila andiko tunalolisoma, tunasema kwanini iwe hivi, au iwe vile?, kwani kuna shida gani, nikinywa bia yangu na simdhuru mtu? Acha kabisa hayo mawazo ya ibilisi..Utapotea…Wewe tii sasa, sababu utakuja kuzijua mbeleni. Sayansi itakuambia haipo hivyo, ukweli ni huu, mwanadamu wa kwanza alikuwa ni sokwe, uthibitisho umepatikana, hakuna Mungu..Ndugu hapo ndio umepotea kabisa, Kumbatia Neno la Mungu.
Tunapohubiriwa tuache anasa, jambo la kwanza ni kutii, hilo Neno, haijalishi itatugharimu kiasi gani..Tunapohubiriwa tuvae mavazi ya kujisitiri, tuache vimini, tuache rushwa. Tusiulize ulize kwanini..Ni kuweka kando kwanza..Sababu tutakuja kujua huko mbeleni.
Tunusuru roho zetu…Tulipokee Neno la Mungu kama lilivyo.
Bwana atusaidie sana.
Maran Atha.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Tofauti kati ya Hekima, ufahamu na maarifa, ni ipi?
Maana ya watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa.
AINA SABA (7) ZA UNAFIKI, AMBAZO UNAPASWA UJIEPUSHE NAZO.
Bilauri ni nini kibiblia?(Ufunuo 21:11,22:1)
TUYATENDE MAMBO YOTE KWA UZURI NA UTARATIBU.
About the author