HAUWEZI KURUKA MADARASA YA MUNGU!

HAUWEZI KURUKA MADARASA YA MUNGU!

Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujinze biblia, Neno la Mungu wetu.

Yapo mambo ambayo watu wa Mungu wanatamani kuyapata au kuyafanya kwa muda waliopanga wao, lakini pasipo kujua pia upo muda wa Mungu wa kuruhusu mtu wake apate anachokitaka au afanye analolitamani. Ni muhimu sana kujua hilo.

Kikawaida pale tunapokuwa tumeokoka, na Kristo kakaa ndani yetu, basi tunapompelekea Mungu maombi yetu, au haja zetu au mahitaji yetu, basi anakuwa anayasikia na siku ile ile anayajabu kama tumeomba sawasawa na mapenzi yake.

Lakini sasa Matokeo ya majibu hayo yanaweza kuwa ni tofauti na mategemeo yetu.. Wengi tunatamani Bwana Mungu atupatia jambo Fulani na tunataka saa hiyo hiyo tukipate kile tulichoomba, pasipo kujua kuwa Mungu hataki tuangamie katika yale tunayomwomba..

Mithali 1:32 “….Na kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza”.

Kwahiyo Mungu kabla hajakupa kile ulichomwomba, ni lazima kwanza aondoe upumbavu ndani yako… Na upumbavu mwingi tunakuwa tunazaliwa nao, kutokana na udhaifu wa mwili, na mwingine tunaupata kutokana na maisha ya dhambi tuliyokuwa tunayaishi…..Hivyo Mungu hawezi kutupa kitu kizuri halafu hatimaye kije kutuharibu .. vinginevyo atakuwa sio Baba mzuri na mwenye hekima.. Kwahiyo kipindi cha kuondolewa kwanza upumbavu mpaka kupokea majibu ya maombi, hapo ndio pana nafasi (inaweza kuchukua kipindi kirefu sana kuondolewa upumbavu).

Ili tuelewe vizuri tutafakari mfano ufuatao..

Wewe ni mzazi mwenye uwezo (tajiri) na mwanao ambaye anasoma chekechea anakuomba umpe Gari.. Kwa mzazi mwenye upendo na hekima, huwezi kuchukua gari na kumpa pale pale, bali utamwahidia kumpa gari!, ila si wakati ule, kwasababu bado hajajua hata kusoma na kusoma, hajajua kuhesabu, atawezaje kuendesha gari barabarani?.. Hivyo utakachofanya ni wewe kumpeleka kwanza shule ili upumbavu uondoke kichwani mwake, akajifunze gari ni nini, vile vile kanuni za kuendesha gari, na sheria za barabarani ili asisababishe ajali.. Hali kadhalika akajifunze matumizi ya gari si kwaaajili ya anasa bali kwaajili ya usafiri na kwaajili ya kazi.

Sasa wakati ambao umemwahidi gari mpaka siku ya kumpa hilo gari, inaweza kuchukua hata miaka 15.. Maana yake atakuja kulipata hilo gari akiwa na miaka 25, na ili hali yeye aliliomba akiwa na miaka 10.

Sasa jiulize! Kama sisi wazazi tuna hekima kama hiyo si zaidi Mungu!.. Huwezi kumwomba Mungu akupe jambo Fulani kubwa halafu akakupa papo kwa hapo, kwa akili uliyonayo hapo!… ni lazima akutengeneze kwanza!..na kutengenezwa kunaweza kukugharimu hata miaka kadhaa!… utakapofikia vigezo anavyovitaka yeye ndipo akupe kile ulichokiomba.

Ukiona bado hujakipokea kile ulichokiomba maana yake bado hujamaliza madarasa!… endelea kumngoja Bwana.

Huwezi kumwomba Mungu akupe mali nyingi na halafu akili yako inawaza anasa!..hawezi kukupa kwa wakati unaoutaka wewe,..itakugharimu kwamba upumbavu uondolewe ndani yako ndipo akupe!… huwezi kumwomba Mungu akupe nyumba na huku kichwani unawaza kuwakomoa watu au kuwaonyesha watu Fulani au kujivuna… hawezi kukupa kwa muda huo!, bado unao upumbavu ndani yako, ambao utakuharibu wewe endapo akikupa hiko kitu kwa muda huo!… atakachofanya kwaajili yako ni kuondoa kwanza upumbavu ndani yako kupitia madarasa yake,(na wakati mwingine hata ya kupitia umasikini), ili kupitia umasikini ule ujue kuwahurumia wengine, na siku utakapopata chako uweze kuwasaidia wengine… na kama ni mwepesi wa kumwelewa Mungu na upumbavu ukawahi kutoka ndani yako, basi ahadi utaipokea mapema, lakini kama ni mgumu, basi ndivyo ahadi yako itakavyozidi kuchelewa!.

Huwezi kukwepa hayo madarasa ya Mungu (hata ufanye nini).

Huwezi kumwomba Mungu akupe karama Fulani na huku moyoni mwako unawaza kujivuna, au kuwaonyesha watu Fulani, au kuwakandamiza wengine katika mwili wa Kristo…. Ni kweli umeomba jambo jema na siku ulipoomba alikusikia lakini hawezi kukupa kwa wakati huo, ambao akili yako inawaza mabaya… Ni sharti kwanza akupeleke kwenye madarasa yake maalumu, akufundishe nini maana ya karama za roho, nini lengo la karama za rohoni ndani ya mwili wa Kristo, n.k.

Ukishayaelewa madarasa hayo, kwa vipimo vyake yeye atakuhakiki na akiona umevikidhi vigezo ndipo anakupa, kwasababu anajua utavitumia vizuri kwa faida ya wengine na si kwa faida yako binafsi.

Na mambo mengine yote ni hivyo hivyo, Utakapomwomba Mungu fahamu kuwa ni lazima akuandae ndipo akupe ulichomwomba, kwasababu yeye ni Baba mwema ambaye hapendi kutupa vitu ambavyo mwishoni vitatangamiza sisi wenyewe.

Hivyo kuanzia leo ndugu yangu, tafuta kuyajua mapenzi ya Mungu, kwasababu unapoyajua mapenzi ya Mungu, basi ni rahisi kupokea majibu ya maombi yako pale tu unapoomba kwasababu kunakuwa hakuna upumbavu mwingi ndani yako… Lakini kama huyajui mapenzi ya Mungu na huyafanyi basi majibu ya maombi yako yatakawia sana, haijalishi utaombewa na watumishi wote ulimwenguni!, bado kanuni za Mungu zitabaki kuwa zile zile..

Yakobo 4:2 “Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi,

3  Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu MWAOMBA VIBAYA, ili mvitumie kwa tamaa zenu”.

Kama unamwomba Mungu mtoto halafu kichwani unawaza kuwakomesha maadui zako, au kuwafumba kichwa watu fulani, huenda ombi lako hilo likachukua muda kidogo kupata majibu.. Lakini kama utamwomba Mungu akupe mtoto, kwasababu tu unahitaji kulea kwa fahari yako wewe mwenyewe, na si kwa sababu ya watu Fulani wa nje au maadui zako wakuone, basi huenda maombi yako yakachukua muda mfupi sana kujibiwa..

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Ni nani aliyemshawishi Daudi akawahesabu Israeli? Ni Mungu au shetani?

VITA DHIDI YA MAADUI

KIFO CHA MTAKATIFU PERPETUA NA FELISTA.

CHAMBO ILIYO BORA.

NJIA MOJAWAPO YA KUPATA MSAADA KUTOKA KWA MUNGU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Renson
Renson
2 years ago

Mmh umenigusa moyo mtumishi

Paschal
Paschal
2 years ago

God bless you all