SHUGHULIKA SANA NA DHAMBI YA KUSAHAU.

SHUGHULIKA SANA NA DHAMBI YA KUSAHAU.

Nakusalimu katika jina kuu sana na lenye nguvu la Bwana wetu Yesu Kristo. Karibu tujifunze maneno ya uzima ya Mungu wetu.

Sisi kama Wanadamu Kila mmoja wetu haijalishi ameokoka au hajaokoka, ndani yake ameumbiwa kiwango cha “kusahau”. Hii ni karama ya Mungu na ni vizuri kumshukuru Mungu Kwa jambo hili, kwasababu kama tungeikosa wanadamu wote tusingeishi hivi tulivyo Leo.

Lakini kusahau kukisimama Mahali pasipo-papasa, inageuka kuwa hatari kubwa sana, Tena dhambi yenye matokeo mabaya sana rohoni.

Kuna aina ngapi za kusahau?

Sasa kusahau kunaweza kuwa aidha kupoteza kumbukumbu ya lile jambo au tukio, Moja Kwa Moja akilini mwako, uwe kana kwamba hujawahi kulipitia. 

Au kunaweza kuwa kulipoteza tu Kwa muda katika kumbukumbu lakini utakapokumbushwa unalikumbuka Tena.

Kusahau kwenye madhara ni kupi?.

Kabla ya kutazama ‘kusahau’ kwenye hasara tuone kusahau kwenye faida kukoje.

Kusahau kwenye faida kunatimia katika mambo yasiyo na maana, au yenye maudhui hasi kwako. Kwa mfano pale mtu unapotukanwa, au unapopigwa kikumbo barabarani na mtu usiyemjua, unaposikia miziki isiyokufaidia huko nje, unapofiwa, unapodhulumiwa, unaposemwa, unapovunjiwa heshima, unapoaibishwa, unaposingiziwa n.k… Mazingira kama haya ambayo ni hasi…kusahau Kunahitajika sana na ni lazima ujifunze kuruhusu jambo hili liumbike ndani Yako ili uponyeke kwa haraka,.maana ndio sehemu yake hiyo inapopaswa itumike.

Lakini kusahau kusikokujenga ni pale unaposahau Matendo mema, au mambo chanya yakupasayo kutenda. Kwamfano Sheria inasema ” usitupe taka hapa” Halafu inapita wiki Moja umesahau agizo hilo, unarudia tena kutupa taka pale pale ulipokatazwa..Hapo utakuwa hujitafutii jambo lingine zaidi matatizo?

Vivyo hivyo katika Neno la Mungu pale unaposahau sahau Neno la Mungu hapo ndio pabaya sana. Wakristo wengi hatujui kuwa Mungu “anayorudia kutuambia ni mengi kuliko Yale mapya anayotaka kusema nasi”..Ni Kwanini? ni kwasababu tumekuwa wepesi wa kusahau Sheria zake.

Mambo yamekuwa kinyume chake, badala tusahau yaliyo mabaya tukumbuke yaliyo mema, tunasahau mema tunakumbuka mabaya sikuzote.

Ni shambuliko kubwa sana ambalo ibilisi amelipanda mioyoni mwa wanadamu. Ndio sababu uchungu haukomi, masengenyo hayaishi, vita vinazuka Kila siku, fitna, unafki, na uongo havina mwisho ni kwasababu Hali Ile Ile tuliyokuwa nayo nyuma mpaka sasa tunairuhusu ikae kwenye akili zetu.

Wakati nguvu hiyo tungepaswa tuitumie kulihifadhi Neno la Mungu mioyoni mwetu ili Matendo chanya yaendelea kutokea ndani yetu, hatufanyi hivyo.. maandiko yanasema..

Yakobo 1:22-25

[22]Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.

[23]Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo.

[24]Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.

[25]Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake.

Tuweke mfano, tunaweza kusoma kwenye biblia kwamba Upendo hauhesabu mabaya, Wala haujivuni, Wala hauoni uchungu n.k(1Kor 13).. Sasa wakati uliposoma hili  neno, moyoni mwako unasema nitaliishi hili Neno, lakini inapita siku mbili unashangaa umerudia kule kule, unaanza ishi maisha ya namna Ile ya kwanza,. Tatizo lipo hapo kwenye kusahau. Laiti.hilo Neno lingekuwa limeganda viizuri kwenye moyo wako, ingekuwa breki pale tu mambo mabaya yanapojaribu kuvuka mipaka.

Sasa tunawezaje kuishinda Hali hii ya kusahau sahau?

Ni kama vile mwanafunzi darasani, mara nyingi anakuwa ni mtu wa.kurudia rudia kusoma na kufanyia sana mazoezi kile alichofundishwa..lengo la kufanya vile ni kulazimisha akili yake inakili Yale mafundisho kwa muda mrefu ili atakapoingia kwenye mtihani asisahau chochote…Lakini kama akisema Mimi ni ‘genius’ sina muda wa kurudia nilivyofundishwa..ni wazi kuwa mambo mengi yatamruka, na atafeli.

Hivyo na sisi sote ni wanafunzi wa Biblia. Soma biblia Kila siku ifanye kuwa rafiki Yako, usiwe mtu wa kusoma Leo, Tena wiki ijayo au mwezi ujao, ndio unakuja kusoma tena..SoMo tafakari mambo uliyoagizwa mule na Mungu Kila siku..Ndivyo itakavyokuwa rahisi kuliishi Neno la Mungu, kinyume na hapo usijidanganye Utasahau…kwasababu mwisho wa siku yatatoka moyoni mwako, na hivyo dhambi yoyote itakayokatisha mbele Yako, utashindwa kukabiliana nayo mapema. Mungu hapendi tuwe na tabia hii ya kusahau sahau Neno lake.

Kumbukumbu la Torati 6:6-9

[6]Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; [7]nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo. [8]Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako. [9]Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako.

Piga vita kusahau Neno la Mungu.

Bwana akubariki.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Wivu ni nini na kuna aina ngapi za Wivu? Na je ni dhambi kuwa na Wivu?

Utii ni nini? na ni nani tunayepaswa kumtii au kutokumtii?

NINI MAANA YA SISI KUWA WATOTO WA MUNGU?

JE NI KUTII AU KUPATA KWANZA MAARIFA?

YESU ANA KIU NA WEWE.

DHAMBI YA MAUTI

PALE AHADI ZA MUNGU ZINAPOKUJARIBU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments