JE UMEUFIKIA ULE UTUKUFU HALISI WA MANA? 

JE UMEUFIKIA ULE UTUKUFU HALISI WA MANA? 

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo, karibu katika kujifunza Neno la uzima.

Ni vizuri kufahamu mana waliyopewa wana wa Israeli jangwani, ijapokuwa ilikuwa ni ileile lakini haikuwa na ubora sawa. Utajiuliza kwa namna gani?

  1. Ipo mana iliyodumu kwa siku moja (1): Ndio ile waliyokuwa wanaiokota kila siku asubuhi, na kuipika, jua lilipozuka iliyeyuka, lakini pia iliposazwa siku ya pili yake ilivunda.
  2. Mana ya pili ni ile iliyodumu kwa siku mbili(2). Mungu aliwaangiza siku moja kabla ya sabato waokote mana ile, ambayo wataila, mpaka siku ya sabato, na itakuwa sawa. Lakini ikisazwa hadi siku ya tatu, inavunda.
  3. Mana ya tatu, ilidumu daima: Hii haikuharibika kwa vizazi vyote. Ni ile aliyoambiwa Musa aichukue na kuihifadhi ndani ya sanduku la agano. Iwe kumbukumbu kwa vizazi vyote vijavyo.

Habari hiyo utaisoma kwenye Kutoka 16:19-36

Je hili hufunua nini katika agano jipya?

Mana ya kwanza:

Kama vile tunavyojua mana ni chakula walichopewa na Mungu wakile na kuishi, katika mazingira magumu (ya jangwani).Na katika hiyo hawakuugua, wala miguu yao kupasuka.

Vivyo hivyo kwa sasa Mana ni chakula cha rohoni ambacho tumepewa tukile sisi tuliookoka, katika huu ulimwengu wa upotovu, ili katika hicho tusiathiriwe na dhambi au mauti, mpaka siku ya ukombozi wetu.

na chakula chenyewe ni “ufunuo wa Yesu Kristo” au kwa lugha nyingine ni “Neno la Mungu lililofunuliwa”(Yohana 6: 30-35)

Mtu yeyote anayeokoka, lazima ajue hapaswi kukaa tu, na kusema imekwisha, Yesu aliyamaliza yote. hapana vinginevyo atakufa kiroho. Bali anapaswa aanze kula NENO (ndiyo mana) ili aukulie wokovu, kama Israeli walivyokula jangwani. Na hiyo huchangiwa na kufundishwa injili ya kweli kutoka kwa walimu sahihi, huku na yeye mwenyewe akionyesha bidii katika kutamani kufundishwa pamoja na kusoma Biblia kila siku.

Sasa mtu kama huyu rohoni akifanya hivyo anaonekana anakula mana lakini sasa mana yake kwa mwanzoni, humtia nguvu ya kitambo kidogo, ni sawa na mtu anayekunywa maziwa na yule anayekula ugali ipo tofauti, ni kweli vyote vinafaa mwilini lakini vyote vina nguvu tofauti.

Ndivyo ilivyo kwa mtu aliye mchanga kiroho, hufunuliwa  lile neno la awali (Maziwa).

Hivyo fadhili za Mungu zitamlinda mtu huyu, siku kwa siku kwa jinsi anavyozidi kufundishwa na kujisomea, ndio maana Mtu aliyemchanga kiroho akikosa Neno au fundisho kwa muda mrefu, ni rahisi sana kufa, Haiwezekani mtu akasema nimeokoka halafu hana habari na kufundishwa. Kujipima kama wewe ni hai au umekufa angalia usomaji wako/kujifunza kwako Neno.

Mana ya pili:

Lakini kwa jinsi mtu huyu anavyojenga uhusiano wa karibu na Mungu wake siku baada ya siku, basi Neno lile linapokea nguvu, ya kumuhifadhi kwa kipindi kirefu kidogo,. Wana wa Israeli kwasababu walikuwa wanaingia  katika sabato kwa Mungu wao,ili kumwabudu na kumsifu, ile mana ilipokea nguvu kwa hiyo siku yao ya sabato haikuharibika.

Halikadhalika na mtu awapo katika kujibidiisha na kazi ya Mungu, utumishi wa Mungu, huduma ya Mungu. Lile Neno linapokea nguvu ya kumuhifadhi wakati wote huo ahudumupo. Maana yake uwezo wa kuhifadhiwa na Mungu unakuwa mkubwa. Huyu mtu anayejibiisha na Mungu, hawi mwepesi kuanguka dhambini, hawi mwepesi kurudi nyuma ovyo, hawi mwepesi kushambuliwa na mwovu hata kukosa shabaha kabisa, hawi mwepesi kupungukiwa kabisa.

Fadhili za Mungu hukaa juu yake, huyu mtu kwa wakati wote amtumikapo Mungu kwa moyo wa dhati, au azingatiapo ibada nyingi. Mungu humuhudumia yeye. Lakini kwamfano akianza kupoa, na kulegea, ataanza kuona tu nguvu za Mungu zinaisha ndani yake ukame unatokea, uzito unakuja, ugumu unaamka tena ndani yake. Hufananishwa na kile chakula alichopewa Eliya na malaika, akaweza kuenda na nguvu ya chakula hicho kwa siku arobaini. Hiyo ndio mana ya pili ambayo Bwana atakulisha wewe utumikaye mbele zake.

Mana ya Tatu:

Lakini ile mana ambayo hudumu milele. Utakumbuka kuwa sharti yake ni ikae ndani ya sanduku. Na sanduku letu ni Kristo, ambaye ndani yake hazina zote za hekima na maarifa  zimesitika (Wakolosai 2:3).

Kwa jinsi mtu unavyoendelea kudumu ndani ya Kristo, kwa uaminifu, kwa wakati fulani mrefu, Bwana hujifunua kikamilifu kwao. Na hapo fadhili za Mungu hazikomi, wala kupungua juu yao milele. kwasababu wameufikia ule utukufu halisi wa Mana iliyofichwa, ambayo si kila mtu anaifikia. Hatua hii, humfanya huyo mtu wakati wote kuwa chini ya fadhili nyingi za Mungu, neema nyingi zinakuwa juu yake, sikuzote ni kwenda mbele tu hakuna kurudi nyuma, wala kupoa, wala hakuna siku atapoa ki-upendo kwa Mungu, Mungu atajifunua kwake kwa namna yake mwenyewe.

ndio maana alitoa ahadi hiyo kwa kanisa la Pergamo akasema..

Ufunuo 2:17

[17]Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. YEYE ASHINDAYE NITAMPA BAADHI YA ILE MANA ILIYOFICHWA, nami nitampa jiwe jeupe, na juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya asilolijua mtu ila yeye anayelipokea.

Kushinda nini?

Ukianzia juu (Ufunuo 2:12-17) utaona anasisitiza,

kutoikana imani na kuendelea kuwa mwaminifu, kwa kutojichanganya na mafundisho ya uongo, ambayo yanakufanya usiwe mtakatifu Rohoni. Mafundisho hayo yalifananishwa na yule Balaamu aliyewaletea Israeli wanawake wa kimataifa ili wawaoe  kisha wafundishwe kuabudu miungu, ili wamkosee Mungu. Ndugu epuka mafundisho ya kidunia, baki kwenye Neno likufanyalo kuwa mtakatifu, tembea katika huo. Fahamu tu Mana hiyo ipo sandukuni imefichwa, si kila mtu anaweza kuifikia hivyo huna budi na wewe kuingia humo, kwa kuishi maisha ya kumtii Kristo. Fikia utukufu huo wa mana.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

USIWE NA TAMAA YA CHAKULA KINGINE.

MNGOJEE BWANA

CHAKULA CHA ROHONI.

(Opens in a new browser tabUSIPOTEZWE NA MANENO YA MANABII WA UONGO.(Opens in a new browser tab)

Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments