Yafuatayo ni mambo saba (7) ya kuzingatia wakati wa Mfungo.
1.MAOMBI
Mfungo wowote ili uwe ni mfungo ni lazima uambatane na Maombi.. Mfungo usiokuwa na maombi ni sawasawa na bunduki isiyo na risasi.
Marko 9:28 “Hata alipoingia nyumbani, wanafunzi wake wakamwuliza kwa faragha, Mbona sisi hatukuweza kumtoa?
29 Akawaambia, Namna hii haiwezi kutoka kwa neno lo lote, isipokuwa kwa kuomba”.
Mathayo 17:21 [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]
Kila siku utakayofunga hakikisha unaomba, (tena maombi ya masafa marefu, tofauti na siku nyingine).
2. KUWA MTULIVU.
Unapofunga usiwe mtu wa kuhangaika na kuzurura huku na kule, bali kuwa mtu wa faragha muda mwingi, wakati wa mfungo si wakati wa kuzurura kwenye makao ya watu, au vijiwe..kuwa mtulivu, tafuta maeno tulivu na omba.
3. ZUIA KINYWA.
Mfungo sio tu kujizuia kula na kunywa, bali pia kujizuia kuzungumza kupita kiasi…. Unapofunga si wakati wa kusema na kila mtu, si wakati wa kujiachia (hususani kwa watu wasio wa kiroho) bali ni wakati wa faragha wewe na Mungu wako (kwa kutafuta sauti ya Mungu kupitia maneno yake)
4. EPUKA MATENDO YA MWILI.
Kama ni mwanandoa jizuie kwa kiwango kikubwa au chote kukutana kimwili na mwenzi wako..Vile vile Kama unafanya shughuli fulani inayohusisha mwili wako, ipunguze kwa kiwango kikubwa..
5. PUNGUZA KIWANGO CHA KULA.
Mfungo sio kuhamisha mlo wa asubuhi na mchana na kuupeleka jioni..La! bali ni kuunyima mwili ili roho yako ije juu (inufaike).. Maana yake wakati wa kufungua (kufuturu) usile kiwango kikubwa cha chakula, kwa kufidia mlo wa asubuhi na mchana.. Ukifanya hivyo utakuwa hutendi dhambi, lakini mfungo wako unaweza usiwe na matokeo makubwa kama wa yule ajizuiaye kweli kweli.
6.USILE VYAKULA VITAMU-TAMU.
Wakati wa kufungua epuka kula vyakula vitamu tamu, hususani vile unavyovipenda sana, ambavyo vinakuburudisha sana.. “Kumbuka tena mfungo ni kuunyima mwili na si kuupendeza mwili”… Sasa unapoupa vile vitu ambavyo unavipenda sana, hapo bado kuna kaukasoro katika mfungo wako..
Danieli alikuwa ni mtu aliyejinyima vitu vitamu wakati wa mfungo… na hatimaye mfungo wake ukawa na matokeo makubwa.
Danieli 10:2 “Katika siku zile mimi, Danielii, nalikuwa nikiomboleza muda wa majuma matatu kamili.
3 Sikula chakula kitamu, wala nyama wala divai haikuingia kinywani mwangu, wala sikujipaka mafuta kabisa, hata majuma matatu kamili yalipotimia”.
7. USIWE MTU WA KUJITANGAZA.
Mathayo 6:16 “Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin, nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao.
17 Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso;
18 ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi”.
Mfungo unapaswa uwe siri hususani kwa watu walio wa nje (yaani wasiohusiana na wewe).. Kwa ndugu yako wa karibu sana, au mke au mume au watoto, mfungo wako ni ngumu kuwa siri kwao, kwasababu unaishi nao katika maisha ya kila siku (hata usipowaambia watafahamu tu)..Hivyo unaweza kuwashirikisha ikiwa lengo lako si upokee utukufu kutoka kwao.
Vile vile kiongozi wako wa kiroho, au mpendwa mwenzako (wa Imani moja na wewe) unaweza kumshirikisha mfungo wako (ikiwa lengo lako si kupata utukufu kutoka kwake) bali kupokea hamasa au kumhamasisha (Hilo ni jambo jema).
Lakini kama lengo lako ni wewe uonekane kwao ili utukuzwe, basi mfungo huo unaweza usizae matunda yale mtu anayoyategemea..
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Je unaruhusiwa kufanya tendo la ndoa ukiwa katika mfungo?
JUMATANO YA MAJIVU NI TENDO LA KIMAANDIKO?
About the author