SWALI: Neno ‘huisingizia sheria na kuihukumu sheria’ maana yake nini? (Yokobo 4:11)
Yakobo 4:11 Ndugu, msisingiziane; amsingiziaye ndugu yake, au kumhukumu ndugu yake, huisingizia sheria na kuihukumu sheria. Lakini ukiihukumu sheria, huwi mtenda sheria, bali umekuwa hakimu.
JIBU: Ili kuelewa vifungu hivyo Mtume Yakobo kwa uongozo wa Roho alikuwa na maana gani aliposema Mtu amsingiziaye ndugu yake au amuhukumuye ndugu yake huisingizia sheria na kuihukumu sheria, Tafakari mfano huu.
Raisi ya nchi amendea mahali Fulani kwa ajili ya shughuli zake za kimaendeleo, lakini katika kupita pita kwake akaona familia moja iliyo fukara sana, na alipotathimini tatizo nini akaona walikuwa wote ni walemavu hawawezi kufanya kazi kabisa, hivyo kwa huruma zake akaagiza wajengewe nyumba, wapewe na msaada wa chakula kutoka serikali kila mwezi, walipiwe na pia bili za maji na chakula kwa kipindi chote wawapo hai.
Lakini Yule raisi alipoondoka, mkuu wa mkoa wa eneo lile, akaenda kuitazama ile familia ikoje, badala ya kutekeleza agizo la mkuu wake, akaanza kuwashitaki na kusema hawa hawana ulemavu wa kuwafanya wasifanye kazi, wanajifanya tu wadhaifu, ni wavivu, wanaweza kuendesha maisha yao, hakuna haja ya kuwapa chochote, hivyo akaanza kuwaonea na kuwashutumu, na kuwanyima mahitaji yao kwa wakati, na kuwashurutisha wajitume.
Sasa Kimsingi mtu kama huyu, ni rahisi kudhani, anawaudhi na kuwashutumu tu wale maskini, Lakini kiuhalisia anamudhi na kumshitaki raisi aliyetoa amri ile kwamba walishwe. Kwa tabia hiyo ni kwamba anamshtaki raisi hafikirii vizuri, anatumia fedha za uma vibaya, anatafuta sifa kwa watu, ana maamuzi yasiyokuwa na maana, hata kama huyo mkuu wa mkoa hawazi hivyo, anampenda raisi wake, na anathamini mali zake, lakini kitendo tu cha kuwashutumu wale, ni sawa na anamshutumu aliyewafadhili.
Ndivyo ilivyo na katika kifungu hicho, Wewe kama mwamini, unapomsingizia ndugu yako, Maana yake unakwenda kinyume na sheria ya Kristo tuliyopewa ya kupendana, unapomhukumu ndugu yako unakwenda kinyume na sheria ya Kristo inayosema Usikuhukumu (Mathayo 7:1).
Hivyo unaihukumu hiyo sheria kwamba ina makosa, wakati Bwana aliiona ni bora, lakini wewe unakwenda kinyume na hiyo.
Hivyo sisi kama wana wa Mungu hatujaitwa tuwashutumu watu, tutafute kasoro ndani ya ndugu zetu, kana kwamba sisi, hatuna maboriti kwenye macho yetu, ila tumeitwa tuitende sheria, na kuonyana, na kuelekezana, na kujengana, katika upendo, lakini sio kutoa hukumu kwa wengine, kana kwamba sisi ni mahakimu.
Tumeagizwa tunapomwona ndugu yetu ameghafilika tumrejeshe kwa upendo, sio kwa mashutumu, hiyo ndio sheria ya Kristo.
Wagalatia 6:1 Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe.
2 Mchukuliane mizigo na KUITIMIZA HIVYO SHERIA YA KRISTO. 3 Maana mtu akijiona kuwa ni kitu, naye si kitu, ajidanganya nafsi yake.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Mafundisho mengine:
Je Yesu ni Mungu au Nabii?
MANENO YA MUNGU YANAPINDULIWAJE?
JE! UMEYABATILISHA MAMBO YA KITOTO?
Print this post