Kama kinavyoanza kwa utambulisho wake, ‘Waraka wa Paulo mtume kwa Wakolosai’.
Paulo ndiye mwandishi wa waraka huu.
Madhumuni makuu ya waraka huu ulikuwa ni kuwasisitiza Wakolosai jinsi Yesu alivyo UTOSHELEVU WOTE, ambaye kwa kupitia yeye Uumbaji wote umekamilishwa ndani yake, lakini si hilo tu bali na utimilifu wote wa ki-Mungu unapatikana ndani yake, pamoja na hazina zote za hekima na maarifa.
Akiwa na maana kuwa mtu akimpata Kristo, hahitaji kitu kingine cha pembeni kumkamilisha yeye, Utoshelevu wote upo kwake.
Hivi ni vifungu mama,
1:15-17
“15 naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. 16 Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. 17 Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye”.
2:3
ambaye ndani yake yeye hazina zote za hekima na maarifa zimesitirika.
2:9
“Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili”.
Anaeleza kwa undani katika sura ile ya pili, kwamba ni kutokana na uwepo wa watu waliolivamia kanisa na kuwadanganya kwa maneno ya ushawishi, nia zao ni kuwafanya mateka kwa elimu isiyo na matunda, ya mapokeo ya kibinadamu, yasiyo ya Kristo (2:8). Kwamba mtu akishika hayo, ndio utimilifu wote unapatikana.
Vilevile kuonekana kwa baadhi ya desturi za kiyahudi ndani ya kanisa, kama vile kushika sikukuu, tohara, sabato, na mwandamo wa mwezi. Vikidhaniwa kuwa vitu hivyo vinaweza kuleta ukamilifu wote pamoja na Kristo (2:11-23)
Na pia kuzuka kwa ibada bandia za kuabudu viumbe vya rohoni (malaika), kwa mawazo kuwa mtu ataupokea ukamilifu.(2:18)
Paulo anaeleza yote hayo hayana wokovu, isipokuwa kwa njia ya haki tuliyoipokea kwa msalaba wake uliofuta hati ya mashtaka yetu, kwa mateso yake pale msalabani ambayo kwa kupitia njia hiyo tumepokea msamaha wa dhambi, pale tu tunapoamini na kubatizwa (2:12-17)
Sehemu ya tatu Paulo anaeleza kwamba kuamini ni pamoja na kuuvaa utu upya wa Kristo. Hivyo huyu mtu hatarajiwi kuendelea kuishi hivi hivi tu, kisa Kristo amemkamilisha kwa kila kitu, bali anapaswa aenende kwa Kristo mwenyewe, ayafikiri yaliyo juu, (3:1-17),
Kwa namna gani?
Kwa kuzifisha tabia za mwilini, kama uasherati, uchafu, kutamani, mawazo mabaya, ghadhabu, matusi. Lakini pia kujivika utu wema, moyo wa rehema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, kusameheana, upendo, ibada. Vilevile si tu katika mambo ya rohoni , bali mpaka kwenye ngazi za kifamilia, kwamba wake kuwatii waume zao, na waume kuwapenda wake zao, na watoto kuwatii wazazi. Hizo ndio tabia za utu mpya.
Katika sura ya 4.
Bado Paulo aendelea kueleza huo mwenendo ndani ya Kristo, unapaswa uonekane mpaka kwa mabwana, kwa watumwa wao. Kwamba mabwana wawape watumwa haki zao, Lakini pia watakatifu wote, wanapaswa kudumu katika maombi, na kuenenda kwa hekima kwa watu wasioamini, katika usemi bora, na kujifunza kuukomboa wakati.
Na mwisho.
Paulo anawasilisha salamu za washirika wenzake wa injili, kwa Wakolosai ikiwemo, Epafra, Luka, Dema, marko, Aristarko, Yusto.
Hitimisho.
Kwa ufupi waraka huu, hueleza kwamba utoshelevu wote upo ndani ya Kristo tu na sio zaidi ya hapo, hatuhitaji kitu kingine cha pembeni kutukamilisha sisi, Lakini ni wajibu wa huyu mkristo kutembea katika maisha mapya ndani yake. Kwasababu mambo yote mawili yanakwenda sambamba hayatengani. Kristo huokoa na kutakasa wakati huo huo. Unapookolewa, saa hiyo hiyo umevikwa utu upya. Huwezi kuendelea katika dhambi.
Ni kipi cha ziada tunachoweza kujifunza katika waraka huu?.
Maombi ya Paulo na Eprafa yasiyokoma kwa kanisa hili(1:3, 9, 4:12):
Hatuna budi kujijengea desturi ya sikuzote kuliombea kanisa la Bwana, hususani mahali tulipo, pamoja na watakatifu wengine tuwajuao. Kwasababu kusimama kwa kanisa hutegemea sana maombi yasiyokoma.
Bwana akubariki. ||kiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii. Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Nijapokuwa sipo kwa mwili, lakini nipo pamoja nanyi kwa roho,
Rudi Nyumbani
About the author