Uchambuzi na mwandishi wa kitabu cha Waefeso.
Kama kitabu kinavyojitambulisha “Waraka wa Paulo Mtume kwa Waefeso”. Paulo ndiye aliyeuandika waraka huu.
Aliuandika akiwa kama mfungwa kule Rumi.
Waraka huu una sura sita(6), ambazo tunaweza kuzigawanya katika makundi mama mawili.
1) kundi la kwanza ni Sura ya 1-3,
Sura hizi zinaeleza asili ya Imani yetu iliyo katika Kristo Yesu jinsi ilivyo ya kipekee kwa nguvu na mamlaka, na ubora, na uweza na ukuu, na utajiri, na utukufu usiopimika, kwa akili za kibinadamu.(1:20-23).
2) Lakini kundi la pili ni Sura 4-6
Inaeleza juu ya mwenendo wetu, jinsi unavyopaswa uwe katika imani tuliyoipokea. Kwasababu ni vitu vinavyokwenda sambamba, haviwezi kutenganishwa, katika fundisho la ukristo.
Kwa ufupi; Katika Kundi la kwanza Yafuatayo ni mambo mama ambayo mwandishi ameyazungumzia juu ya mambo tunayoyapata ndani ya mwokozi wetu Yesu Kristo.
Haya ni mambo ya muhimu sana, ambayo tunapaswa tuyafahamu juu ya Kristo tuliyempokea ndani yetu. Kulingana na mwandishi tukiyajua hayo itatufanya tusiwe watoto wachanga, wa kuchukuliwa na kila upepo wa elimu ya uongo, kwa hila za watu, na ujanja, na njia za udanganyifu (4:14).
Lakini katika kundi la pili ambalo ni sura ya 4-6;
Tunaelezwa wajibu wetu kimwenendo, baada ya kumwamini Kristo, jinsi unavyopaswa uwe, kwamba hatupaswi kuenenda kama mataifa waenendavyo, bali kinyume chake tukue mpaka kuufikia utimilifu wake.
Ambayo hiyo huja Kwa njia ya kuhudumiana kwa karama mbalimbali sisi kwa sisi katika kifungo cha umoja, kama kanisa la Kristo. (4:16)
Anaeleza pia yampasa kila mmoja binafsi auvue ule utu wa kale wa dhambi, na kuuvaa mpya mpya wa utakatifu na haki (4:20-24),
kwa kuuvua uongo, pia tusiruhusu hasira zitutawale, tusiwe wezi, vinywa vyetu visitoe maneno mabaya na matusi, tuwe wafadhili sisi kwa sisi, tusimzimishe Roho, upendo wetu udumu, uasherati usitajwe, wala aibu, wala ubishi.
Kwasababu watendao kama haya kulingana na Mungu hawana urithi katika ufalme wa Mungu.
Waefeso 5:5
[5]Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu.
Halikadhalika Mwandishi anatoa pia agizo juu ya matendo ya giza kwamba tuyaonapo tuyakemee, vilevile tujiepushe walevi, bali tujazwe Roho wakati wote, kwa kumfanyia Mungu ibada.
Waefeso 5:18-20
[18]Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho;
[19]mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu;
[20]na kumshukuru Mungu Baba sikuzote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo;
Mwandishi anazidi kugusia mienendo yetu mpaka katika ngazi za kifamilia na kikazi.
kwamba wake wanapaswa wawatii waume zao, vilevile waume wawapende wake zao. Watoto wawaheshimu wazazi wao, na wazazi wasiwachokoze watoto wao, Watumwa wawatii bwana zao, na mabwana wasiwatishe watumwa wao.(5:22-6:9)
Anagusia pia eneo la vita vyetu. Kwamba rohoni tupo vitani dhidi ya adui yetu shetani na mapepo yake, yenye kazi ya kuwapofusha watu macho, lakini pia kurusha mishale ya moto kutuangamiza. Hivyo tunapashwa tuvae silaha zote za Mungu, ili tuweze kusimama. (6:10-20). Anaorodhesha silaha hizo. ambazo zinakamilishwa kwa sala na maombi ya daima.
Na mwisho anatoa salamu zake kwa watakatifu, akiwaambia pia habari zake nyingine watakazisikia kwa Tikiko, aliyempeleka kwao.
Kwa ufupisho.
Kitabu hichi kinatupa ufahamu kuhusu ubora wa imani tuliyoipokea lakini pia wajibu wetu baada ya hapo, kwasababu tusipothamini na kulegea adui yetu shetani na majeshi yake yatashambulia imani yetu na hatimaye, tukayakosa tuliyohakikishiwa.
Ukishaamini tembea katika utakatifu. Ukiwa unapiga hatua kila siku kwenda mbali na dhambi, basi fahamu kuwa ukombozi wako ni hakika. Kwasababu msalaba una nguvu ya kukusaidia madhaifu yako.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >>
https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Je ni kweli Tumejengwa juu ya Mitume na Manabii? (Waefeso 2:20)
Rudi Nyumbani
About the author