JIBU: Tusome mstari wenyewe.
Mhubiri 1:15 “Yaliyopotoka hayawezi kunyoshwa, Wala yasiyokuwapo hayahesabiki”.
Hapo utaona vipengele viwili, cha kwanza ni: Yaliyopotoka hayawzi kunyoshwa. Na cha pili ni yasiyokuwapo hayahesabiki.
Tukianza na hicho cha kwanza cha Yaliyopotoka hayawezi kunyoshwa,..Tukumbuke kuwa kitabu cha Mhubiri ni kitabu kinachoeleza juhudi za mwanadamu za kutafuta suluhu ya mambo yote yaliyopo duniani kwa nguvu zake mwenyewe pasipo kumuhusisha Mungu. Na ndio maana utaona mhubiri ambaye ndiye aliyejibidisha katika kufanya hivyo, mwisho wa siku anaishia kusema ni UBATILI Mtupu, mambo yote na hekima yote ya mwanadamu ni ubatili tu, ni sawa na kuufuata upepo ambao mwanzoni unaweza kukupa matumaini kuwa utakufikisha mahali, lakini mwishowe unapotea tu ghafla njiani, hujui ulipoelekea umekuacha tu hewani. Ndivyo alivyo mwanadamu anayehangaika kukimbizana na ulimwengu huu.
Sasa aliposema “Yaliyopotoka hayawezi kunyoshwa” Ni kuwa aliona, kuna mambo ambayo yalikatazwa na Mungu, au kwa namna nyingine tuseme hayapo katika uhalisia wake, na pengine anaweza kuyaweka sawa na kuyafanya yaonekane yanafaa katika jamii, Umeona? Ndipo kwa hekima yake akajaribu kufanya hivyo aone kama yatakuwa kweli ni sawasawa, lakini mwisho wa siku akagundua hata ufanyaje kile kilichokataliwa na Mungu (yaani kupotoshwa) hakiwezi kufanywa kiwe sawasawa. Ni kujitafutia tu matatizo na shida zisizokuwa na sababu.
Mbeleni kidogo utaona anasema..
Mhubiri 7:13 “Tafakari vema kazi yake Mungu; kwa sababu ni nani awezaye kukinyosha kitu kile alichokipotosha yeye?
Ni kama leo tu, watu wanatafuta namna ya kuhalalisha ndoa za jinsia moja..wanajaribu kufanya kila mbinu, ionekane kuwa ile ni ndoa iliyokubaliwa na Mungu, lakini bado haiwezi kuwa ndoa, na hilo wanalijua, wengine mpaka wanajibadilisha jinsia waonekane kama wanaume, au wanawake, lakini bado zile jinsia zao zinaendelea kubakia nao ndani yao.. Na matokeo yake wanaishia kupata matatizo mabaya ya kiafanya na kuishia kufa.
Ndivyo walivyo hata na mashoga, wanapojaribu kuwa kama wanawake, maumbile yao yanaharibika wanashindwa kukaa hata katika jamii na watu wengine wakihofia aibu. Kwasababu yaliyopotoshwa hayawezi kunyoshwa, Unaona? Si hilo tu Wapo wengine wanajichubua ngozi zao ili wabadili rangi ya miili yao wawe weupe, sote tunajua mwisho wao watu wa namna hiyo ni nini, ni kuishia kupata kansa ya ngozi na kufa.
Inastaajabisha leo hii, kuona wanawake nao wanasema suruali ni mavazi ya jinsia zote. Haijalishi wataihalalisha vipi wataitengeneza kwa muundo gani unaoonekana wa kike, lakini bado vazi la suruali litabakia kuwa vazi la kiume tu, wewe unayejaribu kukinyosha kitu ambacho Mungu kakipotosha kwako unajitafutia matatizo na hukumu.
Unaweka mawigi, kucha za bandia, ili uonekane wa tofauti na Yule wa kwanza ambaye Mungu alikuumba..Embu Itafakari vema kazi ya Mungu, na uache kukinyosha kile ambacho Mungu kakipotosha. Hiyo ndio maana ya kifungu hicho.
> Sasa tukirudi kwenye kile kipengele cha pili ambacho kinasema “Wala yasiyokuwapo hayahesabiki”.
Hii dunia imejawa na mambo mengi ya Mungu, ambayo bado mwanadamu anazidi kuyavumbua kila siku, lakini mpaka sasa takwimu zinaonyesha, bado asilimia 86 ya viumbe havijajulikana duniani, japokuwa ameishi duniani kwa muda mrefu sasa
Mambo yasiyojulikana ni mengi kuliko yanayojulikana, wanasayansi wanalijua hilo, kila siku wanavumbua mambo mapya, wanashangaa kumbe na hili lipo na lile lipo..Hiyo inawafanya wawe buzy usiku na mchana kutafuta na kutafiti tu, siku zinakuja siku zinakwenda, wanaendelea tu hivyo hivyo, wanasahau mpaka na mambo ya msingi ya roho zao.. Wanadhani katika kuvumbua huko ndio siku moja watapata jawabu la maisha ya mwanadamu hapa duniani.
Mhubiri anasema hayo yote ameshayafanya, lakini amegundua ni ubatili mtupu, kwamba yasiyokuwepo hayahesabiki, hata kama nitakuwa buzy miaka yangu yote kutafiti, kamwe sitavumbua yote. Ni sawa na kuufuata upepo. Huoni leo hii wanadamu walivyo buzy na mambo ya duniani wanasahau mambo ya mbinguni ambayo ni ya kudumu milele? Kiasi kwamba huwezi kuwaeleza chochote, nje ya sayansi wanayojitumainisha nayo.
Lakini Mhubiri mwishoni anatoa jumla ya mambo yote, anasema, linalompasa mwanadamu kufanya ni KUMCHA MUNGU, NA KUZISHIKA AMRI ZAKE (Mhubiri 12:13) basi. Na wewe pia hakuna mahali popote utakapoweza kupata jawabu la maisha isipokuwa kwa Kristo tu peke yake. Hii dunia itakutesa sana, lakini Ukimpa leo maisha yako,ayaongoze, ukaanza naye upya ameahidi kukupa pumziko la roho, hiyo ni ahadi yake.
Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;
30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”.
Hivyo kama upo tayari leo kutubu na kuanza naye upya, basi fungua hapa kwa maelekezo ya sala ya Toba..>>. SALA YA TOBA
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mafundisho mengine
Mada Nyinginezo:
About the author