MIMI NI ALFA NA OMEGA.

MIMI NI ALFA NA OMEGA.

Mara nyingi Bwana Yesu amekuwa akijitambulisha kwa majina mbalimbali, kwa mfano ukisoma Ufunuo 19:13 inasema jina lake anaitwa Neno la Mungu.. Hii ikiwa na maana popote palipo na Neno la Mungu, basi Kristo yupo hapo, na mtu anayeliishi hilo, basi anamuishi Kristo maishani mwake.

Ukisoma pia Isaya 9:6 inasema

“Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani”

Hapo mwishoni inasema, jina lake ataiwa mfalme wa Amani, ikiwa na maana kuwa mahali popote amani ya kweli ile idumuyo ilipo, basi Kristo naye yupo hapo pia,kwasababu yeye ndio mfalme wa hiyo.

Lakini tukirudi katika kitabu cha Ufunuo1:8, Yesu anasema maneno haya;

“Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi”.

Anayarudia tena maneno hayo hayo katika.. Ufunuo 21:6,22:13.

Maana yake ni nini?

Alfa ni herufi ya kwanza katika lugha ya kigiriki, na omega ni herufi ya mwisho ya lugha hiyo.  Kwa lugha yetu ni sawa na tuseme Yesu ni “A” na Yesu ni “Z”, Maana yake ni kuwa yeye ni Neno la Kwanza na pia ni Neno la mwisho.

Lakini hajaishia hapo, anasisitizia kabisa kwa kusema yeye ni ‘Mwanzo na Yeye ni mwisho’. Jiulize kwanini hajasema yeye ni ‘juu na yeye ni chini’, au ‘yeye ni mashariki na yeye ni magharibi’ au ‘yeye ni mbele na yeye ni nyuma’, bali anasema yeye ni mwanzo na yeye ni mwisho?.. Ni muhimu sana kutafakari hili!!

Akiwa na maana kuwa, popote palipo na mwanzo, yeye anapaswa awepo hapo, na popote palipo na mwisho yeye ndio muhitimishaji. Jambo ambalo watu wengi hawalitambui, Na ndio maana inakuwa ngumu kumwona Yesu katika maisha yetu.

Kwasababu hatumtangulizi yeye, katika mwanzo wa mambo yetu, na vilevile hatuhitimishi na yeye katika mwisho wote wa mambo yetu. Tunachukulia kiwepesi wepesi tu, tunamweka Kristo katikati ya mambo yetu, tukidhani kuwa tutamwona akitembea na sisi. Hana kanuni hiyo!

Watu wote wanaonza na Yesu na kuhitimisha na Yesu, katika mambo yao yote, angalia maisha yao, utaona ni ya ushuhuda tu kila siku.

Hivyo haya ni maeneo muhimu sana ya kuzingatia kuanza naye, ukiyachezea haya, umeshamkosa Yesu.

  1. Siku: Unapoanza siku mpya, kabla hujafanya jambo lolote, kabla hujaangalia msg ulizotumiwa na boss wako, kabla hujawasha data kwenye simu yako. Amka piga magoti, mshukuru Mungu, chukua muda mwambie Mungu asante kwa kunipa neema ya siku mpya. Msifu, mtangulize katika mambo yako yote. Ndipo baadaye mengine yafuate. Halikadhalika unapomaliza siku, mshukuru Mungu, kwa kukushindania siku nzima, tenga muda wa kutosha kufanya hivyo, soma biblia kidogo, omba. Usikimbilie tu kitandani, na kusema nimechoka, wacha nilale, nilishashukuru asubuhi. Kumbuka yeye anasema ni Alfa na Omega, ili akamilike kwako vyote viwili vinapaswa viende sambamba.
  2. Wiki: Unapoanza wiki, anza na Bwana, siku ya kwanza ya wiki ni Jumapili, hivyo hakikisha siku hii hukosi ibadani, vilevile hakikisha jumamosi yako, unakuwepo nyumbani kwa Mungu kumshukuru. Na ndio maana kanisa kunakuwa na mikesha ya ijumaa kuamkia jumamosi, au jumamosi kuamkia jumapili. Hakikisha unakwenda kumshukuru Mungu, kwa wiki nzima. Kwa kufanya hivyo, utamwona Kristo akitembea katika wiki yako nzima kukupigania.
  3. Mwezi: Vivyo hivyo katika mwanzo wa mwezi mpya, na mwisho wa mwezi wako. Huna budi kuwepo ibada kumshukuru Mungu, na ni vema kabisa kumshukuru Mungu ukiwa na matoleo yako.  Wana wa Israeli waliagizwa kila mwezi mpya wawe na kusanyiko, hivyo na wewe usianze mwezi kama mnyama, bali tenga muda wa kumshukuru muumba wako.(Ezra 3:5)
  4. Mwaka: Ufungapo mwaka, na ufunguapo mwaka, ni sharti uwe uweponi mwa Bwana. Umealikwa kwenye sherehe,usiende, unalazimishwa uwepo kazini, omba ruhusa, ni heri ukatwe mshahara wa mwezi huo, kuliko kuliko kumkosa Yesu mwaka mzima. Yeye ni Alfa na Omega.
  5. Kazi: Biblia inasema malimbuko yote ni ya Bwana, ikiwa unaanza kazi mpya, hakikisha mshahara wako wa kwanza unampa Bwana, na pale unapoacha, na kupata nyingine, vivyo hivyo fanya kwa Bwana.(Zaburi 3:9), hata katika bishara yako, au popote panapokuingizia kipato.
  6. Uzao: Wazaliwa wote wa kwanza, ni wa Bwana, pia na wa mwisho. Ukitaka ubarikiwe uzao wa tumbo lako, embu usimzuilie Bwana watoto wako. Ana mama yake Samweli alifanya vile kwa mwanaye, Samweli, matokeo yake mpaka leo tunamsoma habari zake, lakini kama angemzuilia, tungemjulia wapi?.

Hakikisha unapompa Bwana mwanao, sio unampa kwa mdomo tu, unamwacha aje kupenda mwenyewe kanisa akiwa mkubwa, bali unamgharimikia kwa Bwana mahitaji yote yanayompasa, utampa elimu, lakini zaidi elimu ya biblia kwa bidii, unamtafutia madarasa ya biblia spesheli kutoka kwa watumishi wa Mungu, unamtoa wakfu kwa Bwana, maana yake hata akikwambia mimi sitakuja kuajiriwa bali nitakuwa mchungaji, hakuna kipingamizi chochote juu yake, unamsapoti kwa furaha yote.

Ukifanya hivyo, utakuja kuvuna ulichokipanda mbeleni. Kwake huyo mtoto na kwa wazao wako wote waliosalia. Kwasababu umemfanya Yesu Alfa na Omega kwenye uzao wako.

Hivyo popote pale, hakikisha unaanza na Kristo, na unamaliza na Kristo. Na hakika tutamwona katika mambo yetu yote.

Maran Atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

NA JINA LAKE AITWA, NENO LA MUNGU.

Nini maana ya “mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili”?

Je ni kweli ilikuwa desturi ya Bwana kuishika sabato?(Luka 4:16)

Majina mbalimbali ya Mungu na maana zake.

Nini maana ya K.K, na B.K?  (B.C na A.D).

Je tunaruhusiwa kushirikiana na wasanii wa kidunia katika kumwimbia Mungu?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments