MAZUNGUMZO MABAYA HUHARIBU TABIA NJEMA.

MAZUNGUMZO MABAYA HUHARIBU TABIA NJEMA.

Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia, Neno la Mungu wetu..

Je umewahi kujua  kuwa mazungumzo mabaya, yanaharibu tabia njema?..

Biblia inasema katika.

1Wakorintho 15:33 “Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema”.

Hapo haisemi, “mazungumzo mabaya yanachochea tabia mbaya”.. La!, bali anasema “yanaharibu tabia njema”. Maana yake mtu mwenye tabia njema, na nzuri na inayovutia, anapoketi kuzungumza, au kusikiliza mazungumzo mabaya, kidogo kidogo anaanza kuiharibu ile tabia yake njema. Haijalishi, hatashiriki hayo mazungumzo, lakini hata kile kitendo cha kusikiliza tu!, tayari tabia yake itaanza kuathiriki.

Ndio maana biblia inatuonya hapo tukae mbali na mazungumzo yote mabaya!..

Na mazungumzo mabaya ni yapi?, ni mazungumzo yote yenye maudhui ya kizinzi, au usengenyaji, umbea, au wizi, au anasa na starehe za kidunia n.k,  na mazungumzo haya mabaya yanapatikana katika sehemu zifuatazo.

1.Kwenye Vijiwe.

Vijiwe ni sehemu yoyote watu wanapokutana kujifurahisha kwa maneno, au michezo.. kwamfano vijiwe vya watu wanaocheza michezo ya draft, au bao, wanaobashiri, au mipira n.k..

2. Kwenye mitandao

Unapotumia muda mwingi kukaa kwenye mitandao kama facebook, au whatsapp na unapojiunga kwenye makundi yasiyo ya neno la Mungu, au yasiyo ya na maana, hata kama huchangii chochote katika mijadala inayozungumziwa kule, wewe ni msomaji tu!, fahamu kuwa unaiharibu tabia yako njema.

3. Televisheni.

Unapotazama tamthilia za kidunia, pamoja na vipindi vingine vya kidunia na mijadala na midahalo mbali mbali katika luninga, ambayo maudhui yake ni ya kidunia, fahamu kuwa unaiharibu tabia yako njema, hata kama wewe huchangii chochote, ni mtazamaji tu!.. bado tabia yako inaharibika.

4. Vitabu vya simulizi.

Unapoketi na kusoma vitabu vya simulizi za kidunia, ambazo ni tungo za watu..ambazo nyingi maudhui zake ni kuchochea anasa, uasherati, na wakati mwingine kuamini uchawi.. Vitabu hivyo vinaharibu tabia njema uliyokuwa nayo, vinaharibu tabia nzuri, ambayo pengine Roho Mtakatifu alikuwa ameshaanza kuiimba ndani yako.

Hivyo ukitaka tabia yako isiharibike jihadhari na mambo hayo.. Kama ni mwanaume kaa mbali na kampani mbaya, nenda katika vijiwe kuhubiri injili, lakini si kusikiliza mambo yanayoendelea pale,  au kushiriki mijadala yao…kama ni mwanamke au binti, nenda vijiweni kuhubiri lakini si kwenye kusikiliza wala kushiriki mazungumzo yao.

Hebu tujifunze mfano mmoja kwenye biblia ya Binti mmoja aliyekuwa na tabia nzuri, kuliko wenzake wote katika familia yake, lakini siku alipotoka na kwenda kukutana na mabinti wengine wa kidunia, akajikuta kabadilika tabia na kuwa mwingine.

Na msichana huyo si mwingine zaidi ya Yule binti wa Yakobo, aliyeitwa Dina, Hebu tusome habari yake kidogo.

Mwanzo 34:1 “Basi Dina, binti Lea, ambaye Lea alimzalia Yakobo, AKATOKA KUWAONA BINTI ZA NCHI.

  2 Shekemu, mwana wa Hamori, Mhivi, mkuu wa nchi, AKAMWONA AKAMTWAA, AKALALA NAYE, AKAMBIKIRI. ”

Umeona chanzo cha Dina kuharibika tabia??.. Si nyingine zaidi ya kutoka na “kwenda kukutana na mabinti wa kidunia”, ambao stori zao ni huenda ni kuzungumzia wanaume tu, na hadhi zao, na Dina akiwa katika kusikiliza akajikuta kashawishika na kujikuta anazini na binti wa mfalme wa nchi, ambaye alikuwa ni mpagani!…Jambo ambalo ni baya sana, mbele za Mungu na mbele ya baba yake Yakobo!

Sasa kujua Dina alikuwa ni binti wa tabia gani hapo kwanza.. hebu tusome tena mstari ufuatao..

Mwanzo 34:19 “Na yule kijana hakukawia kulifanya neno lile, maana amependezewa na binti Yakobo, naye alikuwa MWENYE HESHIMA KULIKO WOTE NYUMBANI MWA BABAYE”.

Umeona?, Dina alikuwa ni mwenye heshima kuliko wote.. lakini ndiye aliye haribika kuliko wote..jambo linalohuzunisha sana!.. Sasa kama mwana wa Yakobo, mrithi wa ahadi za Mungu kaharibiwa.. wewe ni nani usiharibike??..

Kamwe usijivunie tabia yako, na kusema hakuna mtu anayeweza kukubadilisha wala hakuna chochote kitakachoweza kukubadilisha (na huku ni mtu wa kuzunguka katika vijiwe na mitandao).. fahamu kuwa Neno la Mungu ni thabiti.. limesema “tukae mbali na mazungumzo mabaya ili tusiharibu tabia zetu”... wewe na mimi hatuwezi kulisahihisha na kusema “si mazungumzo yanayoweza kumbadilisha mtu, bali ni mtu mwenyewe ndio anayeweza kujibadilisha”.

Watu wengi wanaorudi nyuma katika siku hizi za mwisho ni kwasababu hiyo.. wanazama katika kusikiliza na kushiriki mazungumzo mabaya na hatimaye wanajikuta tayari wameshapoa na kuikana imani kabisa.

Ndugu Kaa mbali na mazungumzo yote mabaya, na kinyume chake, tafuta mazungumzo mazuri ili ujenge tabia yako, na mazungumzo mazuri, utayapata kanisani, na kwenye biblia, na kwenye vipindi au makala za Neno la Mungu.

Bwana Yesu akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

JIHUDHURISHE, ILI AANZISHE MAZUNGUMZO NA WEWE

KAMA UNAPENDA MAISHA, NA KUTAKA SIKU YAKO IWE NJEMA.

NDIPO HUENDA AKACHUKUA PEPO WENGINE SABA.

VITA VYA KIFIKRA BAADA YA KUZALIWA MARA YA PILI

YONA: Mlango wa 4

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments