Utawanyiko wa Wayunani ulikuwaje?

Utawanyiko wa Wayunani ulikuwaje?

Utawanyiko wa Wayunani unaozungumziwa katika Yohana 7:35 ulikuwaje?

Jibu: Tuanzie kusoma mstari wa 31, ili tupate maana kamili..

Yohana 7:31 “Na watu wengi katika mkutano wakamwamini; wakasema, Atakapokuja Kristo, je! Atafanya ishara nyingi zaidi kuliko hizi alizozifanya huyu?

32  Mafarisayo wakawasikia mkutano wakinung’unika hivi juu yake; basi wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakatuma watumishi ili wamkamate.

33  Basi Yesu akasema, Bado kitambo kidogo nipo pamoja nanyi; kisha naenda zangu kwake yeye aliyenipeleka.

34  Mtanitafuta wala hamtaniona; nami nilipo ninyi hamwezi kuja.

35  Basi Wayahudi wakasemezana, Huyu atakwenda wapi hata sisi tusimwone? ATI! ATAKWENDA KWA UTAWANYIKO WA WAYUNANI, NA KUWAFUNDISHA WAYUNANI?

36  Ni neno gani hilo alilolisema, Mtanitafuta wala hamtaniona; nami nilipo ninyi hamwezi kuja?”

Kabla ya kujua Utawanyko wa Wayunani ni kitu gani, ni vizuri kwanza kujua Wayunani walikuwa ni watu gani?.. Kujua Wayunani walikuwa ni watu gani unaweza kusoma hapa >>>>Nawiwa na Wayunani na wasio Wayunani.

Sasa tukirudi kwenye swali; “Utawanyiko wa Wayunani ulikuwaje”?.

Jibu ni kwamba, Utawanyiko wa Wayunani halikuwa tukio Fulani lililowatawanya Wayunani, Bali ni lugha iliyotumika kuwatambulisha Wayahudi waliotawanyika na kuishi katika nchi ya Wayunani, iliyokuwa nchi ya watu wa Mataifa.

Kumbuka si Wayahudi wote walikuwa wanaishi katika nchi ya Israeli, walikuwepo wengi waliokuwa wanaishi nchi nyingine za mbali, kama Rumi, Galatia, Misri, Babeli na ikiwemo hii ya Uyunani. Mfano wa hao utaona ni Mtume Paulo, yeye alikuwa ni Muisraeli kwa asili lakini hakuzaliwa Israeli bali katika mji wa Tarso, ambao ulikuwa upo mbali kabisa na nchi ya Israeli.

Na wengine ni wale waliomfuata Filipo na kumwomba awaonyeshe Bwana Yesu..

Yohana 12:20 “ Palikuwa na Wayunani kadha wa kadha miongoni mwa watu waliokwea kwenda kuabudu kwenye sikukuu.

21  Basi hao walimwendea Filipo, mtu wa Bethsaida ya Galilaya, wakamwomba, wakisema, Bwana, sisi tunataka kumwona Yesu”.

Na wakiwa katika hayo mataifa ya ugenini, wengi wao walikuwa bado wanashika dini yao ya kiyahudi, na hata huko walipokuwepo walijenga masinagogi yao ya ibada. (Matendo 13:43). Ni sawasawa na watu wa asili ya India, wanaoishi Tanzania leo, wakiwa huku bado wanajenga mahekalu yao na kuendeleza dini zao, na wayahudi walikuwa hivyo hivyo, walipokuwa huko katika nchi za ugenini. Walijenga mahekalu na kuendeleza desturi zao, kana kwamba wapo Israeli. Ndio maana utaona Petro anaandika waraka mmoja na kuwapelekea Wayahudi hao waliopo sehemu mbali mbali walizotawanyikia..

1Petro 1: 1 “Petro, mtume wa Yesu Kristo, kwa wateule wa Utawanyiko, wakaao hali ya ugeni katika Ponto, na Galatia, na Kapadokia, na Asia, na Bithinia”

Na zipo sababu kuu mbili zilizowafanya Wayahudi baadhi wawepo katika hizo nchi za mataifa.

1.Kuchukuliwa utumwani.

Utumwa wa Babeli, na Ashuru ndio ulikuwa sababu ya kwanza kuwafanya Israeli wabakie katika hizo nchi.. Kwani mbiu ilipotolewa ya Wayahudi warudi nchini kwao, si wote walirejea nyumbani, wengi walisalia katika nchi walizochukuliwa mateka.. na huko wakaendelea na maisha yao kama kawaida.

2. Biashara

Baadhi ya Wayahudi walikuwa wanasafiri kwenda kufanya biashara katika nchi za mbali, hivyo wengi wao walikuwa wanaanza maisha katika hiyo miji waliokuwa wanaiendea.

Kwahiyo sasa, Utawanyiko wa Wayunani  tafsiri yake ni “utawanyiko wa Wayahudi waliopo katika nchi ya Uyunani”

Kwahiyo Bwana Yesu alipowaambia Mafarisayo “kwamba mtanitafuta wala hamtaniona”….wenyewe walidhani Bwana ataenda Uyunani kuwahubiria na Wayunani, kwasababu wao wamekataa kumsikiliza.

Lakini Bwana hakumaanisha hivyo, bali alimaanisha kuwa “atakwenda zake kwa Baba (yaani mbinguni)” na “watamtafuta lakini hawatamwona”, na zaidi ya yote wao hawawezi kwenda kule aliko, kwasababu wamemkataa yeye.

Hiyo ikitufundisha kuwa na sisi tukimkataa sasa Bwana Yesu, utafika wakati “tutamtafuta lakini hatutamwona” na kule aliko “sisi hatutaweza kufika”.

Yohana 7:33 “Basi Yesu akasema, Bado kitambo kidogo nipo pamoja nanyi; kisha naenda zangu kwake yeye aliyenipeleka.

34  Mtanitafuta wala hamtaniona; nami nilipo ninyi hamwezi kuja”

Kaka/Dada ambaye bado hujaokoka, ambaye bado unaipuuzia injili kama hawa Mafarisayo, Bwana Yesu anakuambia leo “bado kitambo kidogo nipo na wewe”…. bado anakuvumilia sasa, lakini bado kitambo kidogo atakuacha… za baada ya kukuacha anasema “kule aliko wewe hutaweza kwenda”.

Ni jambo baya sana kuachwa na Mungu!..

Na mtu anaachwaje na Mungu?.. Ni pale anapoisikia injili kwa muda mrefu bila kubadilika!!.. Kikawaida Mungu ni Mungu wa uhuru, huwa hatulazimishi kufanya jambo, anachokifanya yeye kwa ule moyo mgumu, usio na toba, ni kuuacha tu!..  Utauliza hilo tunalisoma wapi katika biblia??.

Warumi 1:28  “Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, MUNGU ALIWAACHA WAFUATE AKILI ZAO ZISIZOFAA, WAYAFANYE YASIYOWAPASA.

29  Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na tamaa na ubaya; wamejawa na husuda, na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya,

30  wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao,

31  wasio na ufahamu, wenye kuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema;

32  ambao wakijua sana hukumu ya haki ya Mungu, ya kwamba wayatendao hayo wamestahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao”.

Tubu dhambi leo kwa kumaanisha kuziacha..na tafuta ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu, kukamilisha wokovu wako na Roho Mtakatifu atakuongoza kule anakotaka yeye uende.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Ni wayahudi wa aina gani wanaotajwa kuwa sinagogi la shetani? (Ufunuo 2:9, Ufunuo 3:9)

Je! wayahudi wote wataokolewa kulingana na Warumi 11:26?

YUKO WAPI MFALME WA WAYAHUDI?

Nini maana ya wokovu watoka kwa Wayahudi? (Yohana 4:22)

Je! Mtume Paulo alikuwa ni Mrumi, Myahudi au raia wa Tarso?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments