SWALI: Biblia inamaana gani inaposema jithibitisheni wenyewe kama mmekuwa katika imani, na pale pia inaposema “isipokuwa mmekataliwa”? Maana yake ni nini?
2 Wakorintho 13:5
[5]Jijaribuni wenyewe kwamba mmekuwa katika imani; jithibitisheni wenyewe. Au hamjijui wenyewe, kwamba Yesu Kristo yu ndani yenu? Isipokuwa mmekataliwa.
JIBU: Kama wakristo biblia inatuasa tuwe watu wa kufanyia mazoezi Imani yetu, ili tujithibitishe kama kweli tupo katika mstari sahihi wa Imani au la.
Ili kuelewa tuchukue mfano wa kijana mdogo ambaye anajifunza kuendesha baiskeli. Kwa hatua za mwanzo ni dhahiri kuwa atatumia baiskeli yenye miguu mitatu, ili iweze kumsaidia kumpa uwiano asianguke, na hivyo akiwa katika baiskeli Ile anaweza kuiendesha Kwa jinsi awezavyo kwasababu akikosa ule uwiano( balance), basi Ile miguu ya pembeni itamsaidia..na hivyo ataendesha bila changamoto yoyote, kama tu yule mtu anayejua kuendesha.
Lakini ijapokuwa atakuwa anaiendesha Kwa kasi au maringo kiasi gani bado hajaweza kuwa mwendeshaji kamili, Mpaka siku yatakapotolewa Yale matairi ya pembeni, na kumwacha aimudu mwenyewe ile baiskeli kama waendeshaji wengine. Pale ndipo utakapojua kweli huyu alikuwa ameshaweza au la!.
Hivyo tunaweza kusema, kama hajaweza kujisimamia mwenyewe tayari amekataliwa (yaani, hajakubalika kama mwendesha baiskeli kamili)
Ndivyo ilivyo katika ukristo. Kuna wakati utakuwa unashikwa mkono, lakini upo wakati utahitaji kusimama mwenyewe kujithibitisha, kwamfano labda ilikuwa ikifika muda wa maombi unapigiwa simu/ au unahimizwa na kiongozi wako kufanya hivyo, na kweli unaamka na unasali sana. Lakini huna budi kujijengea ufahamu huu ikiwa siku moja kiongozi wako hayupo, au amesahau kukupigia simu au amepoa je utaamka mwenyewe uombe?. Ukiona Unaweza kufanya hivyo basi tayari wewe umethibitika katika Imani. Lakini ikiwa ni kinyume chake basi bado kiroho hujakubalika.
Jiulize unapokuwa Mazingira yasiyo ya kikanisa, mazungumzo unayozungumza ni ya namna gani. Ikiwa sio ya maana, hata kama utakuwa unahubiri na kuzungumza habari za Mungu, uwapo na wapendwa muda mrefu kiasi gani..bado kiroho hujakubalika (umekataliwa)..unapaswa ujitengeneze .
Hivyo yatupasa tujijaribu Kwa namna hiyo. Ukristo ni sisi kuwa Nuru katika Giza, sio Nuru katika Nuru tu. Hatuvai vizuri tunapokwenda kanisani tu, Bali hata tunapokuwa katika Mazingira yasiyo ya ibadani. Huko ndiko kujithibitisha. Mungu anavutiwa na mkristo anayethibitisha Imani yake miongoni mwa wenye dhambi zaidi ya yule anayefanya Kwa waaminio. Jitathimini unapokuwa mwenyewe, ni Nini unatazama mitandaoni, muda wako mwingi unautumiaje,ni nani unayechati naye?. Wajibu wako Kwa Bwana unautimizaje? Huko ndiko kujithibitisha.
Lakini ikiwa tuwapo nje tunashindwa kuwa kama tuwapo ndani basi hilo Neno “isipokuwa mmekataliwa”, ndio linakuja..maana yake bado hatujakidhi vigezo vya kiroho, Mungu anavyovitazamia kwetu. Ukiwa ni kundi la kusukumwa kutenda jambo Fulani la kiroho lililo wajibu wako, bado hujakubalika.
ukiona hivyo basi yakupasa ufanye juhudi, kumaanisha wokovu wako Kwa Mungu. Kama mkristo usijisifu kwenye juhudi za kusimamiwa, jisifu kwenye juhudi za kujisimamia.
Hiyo ndio tafsiri yake, lakini Neno hilo halimaanishi kama watu wengine wanavyodhani kuwa wapo watu ambao “Mungu amewakataa” ambao hata iweje hawawezi kuupokea wokovu hapana, watu wote wanapokelewa na Mungu wanapotii sauti ya Mungu. Hakuna mtu ambaye akimfuata Mungu hata akionyesha juhudi kiasi gani atakataliwa, hapana.
Bwana akubariki.
Je! Na wewe upo kundi gani? Una habari kuwa hizi ni nyakati za mwisho? Neema ya Kristo inakuita hata Leo, ujue kuwa haitafanya hivyo milele. Ni heri utubu dhambi zako ufanye badiliko, upate ondoleo la dhambi, Yesu Akupe uzima wa milele.
Ikiwa upo tayari Kwa jambo hilo basi..fungua hapa Kwa mwongozo huo >>> KUONGOZWA SALA YA TOBA
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Mada Nyinginezo:
USIPOKUWA MWAMINIFU, NAFASI YAKO ITACHUKULIWA.
Nini maana ya “wanawake saba watamshika mtu mume mmoja”
NI NANI ATAKAYEWAPA ILIYO YENU WENYEWE?
Kwanini Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake wasichukue chochote isipokuwa fimbo tu?
UNAVYOZIDI KUWA MWENYE HAKI, NDIVYO KUJITAMBUA KWAKO KUNAVYOPUNGUA.
About the author