NI NANI ATAKAYEWAPA ILIYO YENU WENYEWE?

NI NANI ATAKAYEWAPA ILIYO YENU WENYEWE?

Nakusalimu katika jina kuu sana la Bwana wetu Yesu Kristo, karibu tujifunze maneno ya uzima.

Ulishawahi kuutafakari kwa ukaribu huu mstari ambao Bwana Yesu aliusema katika..

Luka 16:12 “Na kama hamkuwa waaminifu katika mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe?

Kauli hii ni kinyume na sisi tunavyoweza kuitafsiri. Kwa kawaida, ni sharti kwanza mtu atazame uaminifu wa kile cha kwako kwanza, ndipo ashawishike kukuongezea kilicho cha kwake. Ukienda kukopa Benki ni sharti waangalie mipango/ mikakati yako na matumizi yako kwa kile ambacho tayari umeshaanza kukifanya, ndipo wakupe mkopo wa kuongezea biashara yako.

Vinginevyo ukienda hoe hae, huna malengo au mipango, ni wazi kuwa hutaambulia chochote, kwasababu wanahofia kama tu hicho cha kwako kidogo kimekushinda kukitazama, ukiongezewa kikubwa utawezaje?

Kama cha kwako mwenyewe haukijali, utajali vipi vya wengine?. Kama unajiibia mwenyewe ofisini kwako, utayahurumiaje mashirika ya wengine uliyopewa uyasimamie..

Lakini kwa Mungu ni tofauti, ili akupe kitu chako mwenyewe, ni sharti kwanza ukijali cha mtu mwingine. Ni sharti kwanza uonyeshe uaminifu kile cha mwingine ulichowekewa dhamana.

Unataka Mungu akupe uchungaji wako, Atakuangalia Je ulishawahi kuwajali kondoo wa Mungu, katika hilo kanisa ulilowekwa chini yake sasa? Ulishawahi kuwahudumia kwa upendo kabisa na kuwajali kama Mungu anavyotaka, Kama hukuweza basi ni ngumu sana Mungu kukupa cha kwako.

Mtu anamwomba Mungu ampe watoto wa kulea, lakini watoto wa familia nyingine hawajali, wala hata hana mpango nao kisa tu hajawazaa yeye.. Mungu akishaona hivyo, anasema, hata akikupa wa kwako hutaweza kuwalea, ni heri tu ubaki hivyo hivyo ..

Leo watu wengi wanamwomba Mungu awape ofisi zao wenyewe, Je, pale ulipowekwa kama muajiriwa unatumika kwa uaminifu?.

Unataka Mungu akupe nyumba yako mwenyewe, Je! Umekuwa mwaminifu katika hiyo nyumba ya mwingine Mungu aliyokuweka chini yake? Unaijali, unaitunza, unaipa thamani kama vile ni ya kwako?

Chochote tunachokitaka kwa Mungu, tujue kuwa atatujaribu kwanza kwa kutuletea hicho hicho kutoka kwa wengine,aupime uaminifu wetu. Mungu alimpima Yusufu katika nyumba ya Potifa kama je! Atakuwa mwaminifu? Na alipouona uaminifu wake, ndipo akampa cha kwake, akawa waziri mkuu kule Misri.

Hata katika ufalme wa Mungu, hatutapewa miji yetu wenyewe tuimiliki kule kwenye mbingu mpya na nchi mpya kama hatutakuwa waaminifu hapa duniani, kwa utumishi Mungu aliotuwekea chini yake katika kanisa lake.

Ikiwa tunalegea legea, au tunavipuuzia vya Mungu, au tunafanya mambo ya aibu, tusahau kule kupewa chochote na Mungu wetu ili tumiliki.

Tafakari tena habari hii..

Luka 19:12 “Basi akasema, Mtu mmoja, kabaila, alisafiri kwenda nchi ya mbali, ili ajipatie ufalme na kurudi.

13 Akaita watu kumi katika watumwa wake, akawapa mafungu kumi ya fedha, akawaambia, Fanyeni biashara hata nitakapokuja.

14 Lakini watu wa mji wake walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale.

15 Ikawa aliporudi, ameupata ufalme wake, aliamuru waitwe wale watumwa aliowapa fedha, ili ajue faida aliyopata kila mtu kwa biashara yake.

16 Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi.

17 Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi.

18 Akaja wa pili, akasema, Bwana, fungu lako limeleta mafungu matano faida.

19 Akamwambia huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano.

20 Akaja mwingine akasema, Bwana, hili ndilo fungu lako, ambalo nililiweka akiba katika leso.

21 Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa usichoweka, wavuna usichopanda.

22 Akamwambia, Nitakuhukumu kwa kinywa chako, mtumwa mwovu wewe. Ulinijua kuwa ni mtu mgumu, niondoaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda;

23 basi, mbona hukuiweka fedha yangu kwa watoao riba, ili nijapo niipate pamoja na faida yake?

24 Akawaambia waliosimama karibu, Mnyang’anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi.

25 Wakamwambia, Bwana, anayo mafungu kumi.

26 Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang’anywa hata alicho nacho”.

Hivyo tuwe waaminifu, mahali popote Mungu alipotuweka. Kwasababu hiyo ndio itakayofungua milango ya kuwepa vya kwetu wenyewe.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

KUWA MWAMINIFU KWA MANENO YAKO MWENYEWE,

NI SAA KUMI NA MBILI (12) TU, ZA KRISTO KWAKO.

YESU NI MFALME WA AINA GANI KWAKO? 

KUNA MAJIRA MUNGU ATAIVURUGA MIPANGO YETU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments