VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 12 (Kitabu cha Isaya)

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 12 (Kitabu cha Isaya)

Jina la Bwana YESU Kristo libarikiwe, karibu katika mwendelezo wa uchambuzi wa vitabu vya biblia, Tumekwisha kuvitazama vitabu kadhaa nyuma, na leo kwa neema za Bwana tutapiga hatua moja mbele, kukitazama kitabu cha Isaya.

Kabla ya kuendelea mbele,  ni muhimu kufahamu kuwa huu ni ufupisho tu!, na sio utimilifu wenyewe! hivyo kila mtu analo jukumu la kukisoma kitabu hichi cha Isaya kabla na baada ya kusoma ufupisho huu. Na vile vile, kama hujapitia uchambuzi wa vitabu vilivyotangulia, ni vizuri uupitie kwanza ili tuweze kwenda pamoja katika vitabu hivi vya mbeleni.

Kama hujapata uchambuzi huo basi unaweza kufungua hapa >>> Vitabu vya Biblia: Sehemu ya kwanza (www.wingulamashahidi.org) au unaweza ukatujuza kupitia inbox kwa namba zilizopo mwisho wa somo ili tuweze kukutumia.

Mwandishi wa kitabu cha Isaya ni Nabii Isaya mwenyewe, kitabu cha Isaya kina sura 66 sawasawa kabisa na jumla ya vitabu vyote vya biblia, ambavyo ni 66.

Tofauti na vitabu vingine vya kinabii kama Hosea, Zekaria, Hagai, Obadia, Yona, Habakuki, Malaki na vingine baadhi, ambavyo vimebeba Nabii za kipindi fulani tu au za jamii ya watu fulani tu!, labda kuhusu Mwisho wa dunia, au kuchukuliwa kwa Israeli kwenda Babeli, au hukumu ya Taifa fulani litubu!, vinakuwa havijabeba, au vinabeba kwa sehemu ndogo sana..

Lakini kitabu cha Isaya  ni kitabu ambacho kimebeba UNABII wa mambo karibia yote kwa mapana na marefu.

Kitabu cha Isaya, kina unabii kuanzia Israeli kuchukuliwa Mateka na kupelekwa Babeli, vile vile kina unabii wa kurejeshwa kwao, kina unabii wa kuanguka kwa Babeli, na hukumu ya Babeli, kina unabii wa kujengwa tena hekalu lililobomolewa, kadhalika kina unabii kuanguka na kunyanyuka kwa Mataifa mengine nje ya Israeli, vile vile kina unabii wa UJIO WA MASIHI, (Hakuna kitabu kingine chochote kilichotabiri kwa kina jinsi Masihi atakavyokuwa na tabia zake kama kitabu hiki, tutakuja kuliona hilo vizuri mbele kidogo)..

Kitabu cha Isaya pia kimetabiri Siku ya Ghadhabu ya Mungu, ambayo itakuja  baada ya Unyakuo wa kanisa kupita!, kimetabiri mpaka kipindi cha utawala wa miaka 1000,wakati ambao Kristo atatawala na watakatifu wake kwa miaka elfu akiwa hapa duniani, na mambo mengine mengi.

Leo tutazitazama nabii hizi chache, Lakini kabla ya kwenda kuzitazama.. Ni vyema pia kufahamu jambo lingine la muhimu, kwamba Kitabu cha Isaya hakijaandikwa kwa muda wa siku moja, au mwezi, au mwaka mmoja. Hapana!.

Kitabu cha Isaya kimeandikwa kwa kipindi cha Miaka 58 kuanzia mwaka (739KK-681KK)

Kwa kadiri Isaya alivyokuwa anapewa maono ndivyo alivyokuwa anaandika, na sio kila siku alikuwa anapewa maono, wakati mwingine ilipita kipindi kirefu hata zaidi ya mwaka, pasipo kupokea unabii wowote wa kuandika.. Hivyo Sura zote 66 za kitabu hicho, ni mfululizo wa Maono aliyoyaona Isaya, katika kipindi chote cha Maisha yake, tangu alipoanza kuona maono mpaka alipokufa (yaani miaka 58).

Ndio maana utaona maono ya kitabu hicho ni kama yamechanganyikana..Ni kwasababu hakupewa kipindi kimoja.. Leo anaweza kupewa Ono linalomhusu Masia, akaliandika katika Sura moja, mwezi ujao au mwaka ujao akapewa linalohusu kuanguka kwa Babeli akaliandika chini katika sura ya pili, baada ya miaka miwili tena anapewa ono linalomhusu Masia tena (Yesu Kristo), tofauti na lile la kwanza, akaliandika katika sura ya 3, baada ya miezi kadhaa anapewa unabii tena kuhusu Utawala wa miaka elfu n.k Kwahiyo ni unabii juu ya unabii, kwa vipindi tofauti tofauti.

MAISHA YA ISAYA.

Isaya alikuwa ni Mwana wa mtu aliyeitwa Amozi, biblia haijaleza huyu Amozi, baba yake Isaya alikuwa ni mtu wa namna gani, lakini ni wazi kuwa alikuwa ni mtu maarufu, aliyekuwa anajulikana). maana ya jina Isaya ni “Bwana ni Wokovu”..(Isaya alianza kuona maono ya Mungu baada ya kifo cha mfalme Uzia (Isaya 6:1), Na ni nabii aliyetokea mapema kabla ya wakina Yeremia, Danieli, Ezekieli, Yona na wengine wengi..

Biblia haijaeleza kwa undani sana maisha ya Isaya, lakini maandiko yanasema alioa Nabii Mke na kuzaa nae watoto (Isaya 8:3), Na mwanamke huyo aliyemwoa, alimwoa kwa agizo la Bwana, kwasababu Mungu aliyafanya maisha yake kuwa ishara kwa Israeli, kama vile alivyoyafanya ya Hosea na Ezekieli.

Ni kawaida ya Mungu kuyafanya maisha ya watumishi wake kuwa Ishara kwa dunia, Kwamfano utaona Nabii Ezekieli kuna mahali aliagizwa na Mungu ale kinyesi, lengo ni kufikisha ujumbe fulani kwa watu fulani, kadhalika kuna mahali Nabii Hosea aliambiwa na Mungu akaoe mwanamke wa uzinzi, na kuzaa naye watoto ili kufikisha ujumbe fulani kwa watu fulani. Vile vile Nabii huyu  Isaya Mungu aliyachagua maisha yake kuyafanya ishara kama hawa wengine, ili kufikisha ujumbe fulani. Kwamfano utaona kuna mahali Nabii Isaya, aliambiwa na Mungu, atembee uchi..

Isaya 20:2 “wakati huo Bwana alinena kwa kinywa cha Isaya, mwana wa Amozi, akisema, Haya, uvue nguo ya magunia viunoni mwako, na viatu vyako miguuni mwako.

3 Naye akafanya hivyo akaenda uchi, miguu yake haina viatu. Bwana akasema, Kama vile mtumishi wangu Isaya anavyokwenda uchi, hana viatu, awe ishara na ajabu kwa muda wa miaka mitatu juu ya Misri na juu ya Kushi;

4 vivyo hivyo mfalme wa Ashuru atawachukua uchi, wafungwa wa Misri, na watu wa Kushi waliohamishwa, watoto kwa wazee, hawana viatu, matako yao wazi, Misri iaibishwe.

5 Nao watafadhaika, na kuona haya kwa ajili ya Kushi, matumaini yao, na Misri, utukufu wao”.

Kwa maelezo marefu kwanini Isaya aliagizwa atembee uchi unaweza kufungua hapa >>Kwanini Isaya aliagizwa atembee uchi?, (www.wingulamashahidi.org) Au ukatujuza kwa njia ya inbox, tukutumie somo kamili .

Kwahiyo Maisha ya Isaya, mbali na kutoa Unabii, Mungu aliyatumia maisha yake pia kama Ishara, kulingana na historia, Nabii Isaya alikufa kifo cha kukatwa na Msumeno sawasawa na Waebrania 11:37.

NABII ZA ISAYA.

Nabii za Isaya zimegawanyika katika vipengele vitano, 1) Unabii juu ya Yuda na Israeli kabla ya Uamisho wa Babeli, 2) Unabii juu ya Israeli baada ya Uamisho 3) Unabii wa kuja kwa Masihi, mara ya kwanza na mara ya pili  4) Unabii wa kuanguka kwa mataifa  5) Unabii wa hukumu ya Mungu na Utawala wa miaka Elfu .

Tutaziangalia Nabii hizi kwa uchache moja baada ya nyingine.

 1. Unabii wa Yuda na Israeli kabla ya Uamisho wa Babeli.

Nabii Isaya alitokea miaka miaka karibia 155 kabla ya Uamisho wa Babeli, Na Israeli pamoja na Yuda ilikuwa tayari imeshafanya machukizo makubwa mbele za Bwana, hivyo Nabii Isaya alianza kutabiri kuanguka kwa Yerusalemu miaka 155 kabla ya maangamizi hayo kutokea. (kuonyesha ni jinsi gani Mungu alivyo na huruma, jinsi anavyotoa kipindi kirefu cha watu kutubu, na kugeuka), lakini tunaona hawakutubu na siku ilipofikia uharibifu uliwajia ghafla na wote wakapelekwa utumwani.

Ufunuo 22: 4 “Kwa sababu hiyo nasema, Geuza uso wako usinitazame, nipate kulia kwa uchungu; usijishughulishe kunifariji, kwa ajili ya kuharibika kwake binti ya watu wangu.

5 Kwa maana siku ya kutaabika, siku ya kukanyagwa, siku ya fujo inakuja, itokayo kwa Bwana, Bwana wa majeshi, katika bonde la Maono; inabomoa kuta; na kuililia milima”.

Huo ni unabii wa kuharibiwa kwa Yuda, na Mfalme Nebukadreza.

 2. Unabii wa Israeli baada ya kuhamishwa.

Pamoja na Isaya kutabiri kuanguka kwa Yerusalemu, lakini pia alitabiri wayahudi kurejeshwa tena Yerusalemu kutoka Babeli, aliabiri atatokea mfalme anayeitwa Koreshi, atakayewaweka huru wayahudi, na kuwapa ruhusa warejee nchini mwao wakiwa huru..

Isaya 44:26 “nilithibitishaye neno la mtumishi wangu, na kuyafikiliza mashauri ya wajumbe wangu; niuambiaye Yerusalemu, Utakaliwa na watu, nayo miji ya Yuda, Itajengwa, nami nitapainua mahali pake palipobomoka;

27 niviambiaye vilindi, Kauka, nami nitaikausha mito yako;

28 nimwambiaye Koreshi, Mchungaji wangu, naye atayatenda mapenzi yangu; hata ataunena Yerusalemu, Utajengwa; na hilo hekalu, Msingi wako utawekwa”.

Unaweza kusoma tena juu ya Unabii huo wa Koreshi katika Isaya 45:1-2

 3. Unabii wa kuja kwa Masihi.

Baada ya Nabii Isaya kuonyeshwa kurejeshwa kwa Wayahudi kutoka utumwani, na kustarehe katika nchi yao, Mungu aliendelea kumwonyesha maono ya kuja kwa Masihi yaani Yesu, alimwonyesha tangu kuzaliwa kwake jinsi kutakavyokuwa kwamba, atazaliwa na Bikira(Isaya 7:14), Na jinsi atakavyopitia mateso na kufa, kwaajili ya dhambi zetu, kama vile mwanakondoo apelekwaye machinjoni.

Isaya 53:1 “Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta? Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani?

2 Maana alikua mbele zake kama mche mwororo, Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani.

3 Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.

4 Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa.

5 Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.

6 Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote.

7 Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake.

8 Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu”.

Hakuna mahali pengine popote katika biblia palipotabiri Bwana kuzaliwa na Bikira isipokuwa hapa katika Isaya tu,  wala hakuna kitabu kingine chochote kilichoelezea mateso ya Bwana Yesu kwa mapana namna hii kama hichi kitabu cha Isaya.

Nabii Isaya hakuishia tu kufunuliwa hayo juu ya Masihi, bali alifunuliwa mpaka utawala wake wa kifalme ambao utakuja baada ya hasira ya Bwana kupita, yaani utawala wa miaka elfu moja. (tutakuja kuuona  vizuri mbele kidogo), Lakini kwa habari za unabii wa ujio wa Masihi na tabia zake, unaweza pia kuzisoma katika mistari hii>>Isaya 11:1-2, Isaya 61, na Isaya 9:6.

 4. Unabii wa kuanguka kwa Mataifa.

Sehemu hii ya unabii ndio iliyochukua nafasi kubwa katika kitabu cha Isaya. Bwana Mungu alimwonyesha Isaya, Nabii juu ya Mataifa yote ambayo kwa namna moja au nyingine yalihusiana na taifa la Israeli, kuanzia Misri, Babeli, Ashuru, Moabu, Filisti, Tiro, Kushi, Edomu na mengine machache.

Mataifa hayo Bwana Mungu alitabiri kuanguka kwao, kwasababu na yenyewe yalifanya mabaya kama Israeli tu!, Kwamfano Taifa la Babeli liliwatesa Israeli watu wa Mungu, ijapokuwa aliliruhusu hilo kwa lengo la kuwaadhibu Israeli, lakini bado Babeli ilikuwa na hatia juu ya hilo, kadhalika Babeli ndio ilikuwa kitovu cha machukizo yote ya ulimwengu kipindi hicho. (Kumbuka katika siku hizi za mwisho pia kuna Babeli nyingine ya kiroho, ambayo inawachukua watu utumwani na vile vile Mungu kaitabiria hukumu, kama alivyoitabiria Babeli hii, kama utapenda kujua Babeli hiyo unaweza kufungua hapa  >>> Babeli ya rohoni au ukatutumia ujumbe inbox, tukutumie somo kamili). Hivyo Mungu aliyaadhibu na kutabiri kuanguka kwao.

Tutapitia mataifa machache, na mengine tutayasoma kwa nafasi zetu..

Taifa la Babeli.

Isaya 14: 4 “utatunga mithali hii juu ya mfalme wa Babeli, na kusema, Jinsi alivyokoma mwenye kuonea; Jinsi ulivyokoma mji ule wenye jeuri!

5 Bwana amelivunja gongo la wabaya, Fimbo ya enzi yao wenye kutawala.

6 Yeye aliyewapiga mataifa kwa ghadhabu, Kwa mapigo yasiyokoma; Aliyewatawala mataifa kwa hasira, Ameadhibiwa asizuie mtu”.

Soma tena..

Isaya 47:1 “Haya, shuka, keti mavumbini, Ewe bikira, binti Babeli; Keti chini pasipo kiti cha enzi, Ewe binti wa Wakaldayo; Maana hutaitwa tena mwororo, mpenda anasa.

2 Twaa mawe ya kusagia, usage unga; Vua utaji wako, ondoa mavazi yako, Funua mguu wako, pita katika mito ya maji.

3 Uchi wako utafunuliwa, Naam, aibu yako itaonekana. Nitalipa kisasi; simkubali mtu ye yote.

4 Mkombozi wetu, Bwana wa majeshi ndilo jina lake, Mtakatifu wa Israeli.

5 Kaa kimya, ingia gizani, Ee binti wa Wakaldayo; Maana hutaitwa tena Malkia wa falme.

6 Nalikuwa nimekasirika na watu wangu, naliutia unajisi urithi wangu, nikawatia mkononi mwako; wewe hukuwatendea rehema; uliwatia wazee nira yako, nayo nzito sana.

7 Ukasema, Mimi nitakuwa bibi milele; hata hukuyatia hayo moyoni mwako, wala hukukumbuka mwisho wa mambo hayo.

8 Sasa, basi, sikia haya, wewe upendaye anasa, ukaaye na kujiona salama, wewe usemaye moyoni mwako, Mimi ndiye, wala hapana mwingine zaidi yangu mimi; sitaketi mfano wa mjane, wala sitajua kufiwa na watoto”

Pia unaweza kusoma Isaya 13, inazungumzia unabii huo huo wa kuanguka kwa Babeli.

Misri.

Misri ni taifa lililowatesa Israeli, kipindi kabla hawajaingia nchi ya Ahadi, Taifa hili limekuwa adui kwa Israeli mara kadhaa, na pia limekuwa kitovu cha maasi mengi duniani, hata baada ya Israeli kuingia nchi ya kaanani. Bwana alilitabiria pia kuanguka kwake katika mistari hii >> Isaya 19:1-5

Ashuru.

Taifa Ashuru ni taifa lililowachukua pia Israeli utumwani, nalo pia Bwana alilitabiria kuanguka.. Hukumu ya taifa hilo unaweza kuisoma kupitia mistari hii >> Isaya 10:5, Isaya 14:25-27.

Ufilisti

Filisti ni mji uliokuwa unawatesa Israeli mara nyingi, na uliokuwa unaabudu miungu kwa kiwango kikubwa, Unabii kwa kuanguka kwake unaweza kuusoma kupitia mistari hii >> Isaya 142:8-38.

Moabu

Moabu ni Taifa lililokuwa adui wa Israeli kwa kipindi chote, ndilo taifa lililomwajiri Balaamu awalaani Israeli walipokuwa wanaiendea nchi yao ya Ahadi..Bwana alilitabiria kuanguka kwake kupitia nabii Isaya, katika mistari hii >> Isaya 15:1-5

Tiro

Tiro ni mji uliokuwa karibu na Sidoni, katika nchi ya Lebanoni, huku ndiko Yezebeli alipotokea na ndipo kulipokuwa kitovu cha ibada za mungu baali. Ulikuwa ni mji wa kibiashara, na wafanya biashara na ulikuwa umejaa udhalimu. Bwana aliutabiria kuanguka kwake katika mistari hii >> Isaya 23:1-6

Mataifa mengine madogo madogo kama Edomu, Kushi, Dameski na mengine yanayohusiana na miji hiyo, Bwana aliitabiria kuanguka kwao kupitia mistari hii>>(Isaya 63:1-6, Isaya 34:1-10, Isaya 17:1-6, na Isaya 18:1-3).

 5. Unabii wa hukumu ya Mungu na Utawala wa miaka Elfu .

Pamoja na Isaya kupewa unabii wa Kuanguka kwa Mataifa, alionyeshwa pia mwisho wa dunia, yaani hukumu ya ulimwengu mzima, wakati Ghadhabu ya Mungu itakapomwagwa duniani kutokana na maasi na maovu ya ulimwengu, na vile vile akaonyeshwa utawala wa amani wa Bwana Yesu wa miaka elfu moja duniani na mbingu mpya na nchi mpya.

Siku ya Ghadhabu ya Bwana na hasira yake.

Isaya 24:1 “Tazama, Bwana ameifanya dunia kuwa tupu, aifanya ukiwa, aipindua, na kuwatawanya wakaao ndani yake.

2 Na itakuwa kama ilivyo hali ya watu, ndivyo itakavyokuwa hali ya kuhani; kama ilivyo hali ya mtumwa, ndivyo itakavyokuwa hali ya bwana wake; kama ilivyo hali ya mjakazi, ndivyo itakavyokuwa hali ya bibi yake; kama ilivyo hali yake anunuaye, ndivyo itakavyokuwa hali yake auzaye; kama ilivyo hali yake akopeshaye, ndivyo itakavyokuwa hali yake akopaye; kama ilivyo hali yake atwaaye faida, ndivyo itakavyokuwa hali yake ampaye faida.

3 Dunia hii itafanywa tupu kabisa, na kuharibiwa kabisa; maana Bwana amenena neno hilo.

4 Dunia inaomboleza, inazimia; ulimwengu unadhoofika, unazimia; watu wakuu wa dunia wanadhoofika.

5 Tena dunia imetiwa unajisi kwa watu wanaoikaa; kwa maana wameziasi sheria, wameibadili amri, wamelivunja agano la milele.

6 Ndiyo sababu laana imeila dunia hii, na hao wanaoikaa wameonekana kuwa na hatia, ndiyo sababu watu wanaoikaa dunia wameteketea, watu waliosalia wakawa wachache tu”.

Utawala wa amani wa miaka elfu na wa mbingu mpya na nchi mpya.

Isaya 65:17 “Maana, tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya, na mambo ya kwanza hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni.

18 Lakini furahini, mkashangilie daima, kwa ajili ya hivi niviumbavyo; maana, tazama, naumba Yerusalemu uwe shangwe, na watu wake wawe furaha.

19 Nami nitaufurahia Yerusalemu, nitawaonea shangwe watu wangu; sauti ya kulia haitasikiwa ndani yake tena, wala sauti ya kuomboleza.

20 Hatakuwapo tena mtoto wa siku chache, wala mzee asiyetimia siku zake; kwa maana mtoto atakufa mwenye umri wa miaka mia; bali mtenda dhambi mwenye umri wa miaka mia atalaaniwa.

21 Nao watajenga nyumba, na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake.

22 Hawatajenga, akakaa mtu mwingine ndani yake; hawatapanda, akala mtu mwingine; maana kama siku za mti ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu, na wateule wangu wataifurahia kazi ya mikono yao muda wa siku nyingi.

23 Hawatajitaabisha kwa kazi bure, wala hawatazaa kwa taabu; kwa sababu wao ni wazao wa hao waliobarikiwa na Bwana, na watoto wao pamoja nao.

24 Na itakuwa ya kwamba, kabla hawajaomba, nitajibu; na wakiwa katika kunena, nitasikia.

25 Mbwa-mwitu na mwana-kondoo watalisha pamoja, na simba atakula majani kama ng’ombe; na mavumbi yatakuwa chakula cha nyoka. Hawatadhuru wala kuharibu katika mlima wangu mtakatifu wote, asema Bwana”.

Ni nini tunajifunza katika kitabu hichi cha Isaya?

Tunajifunza kuwa maneno ya Mungu hayapiti kamwe!. Alitabiri habari za kuanguka kwa Yerusalemu, zikatimia kama zilivyo, alitabiri habari za kuzaliwa Masihi kupitia bikira, na zikatimia kama zilivyo, na ametabiri kuanguka kwa mataifa pamoja na siku ya kisasi cha Bwana, vile vile zitatimia kama zilivyo.

Hizi ni siku za mwisho, siku ya hasira ya Bwana imekaribia, unyakuo wa kanisa utakapopita tu!, kitakachokuwa kimebaki ni dhiki kuu na hiyo siku ya hasira ya Bwana!, Jua litatiwa giza, maji yote yatakuwa damu, milima na visiwa vitahama, na Bwana atawahukumu wanadamu wote wanaotenda maasi, na mwisho wao utakuwa katika lile ziwa la moto. Lakini watakatifu, yaani wote waliooshwa kwa damu ya mwanakondoo, watairithi hiyo mbingu mpya na nchi mpya.

Je mimi na wewe tutakuwa wapi siku hiyo?

Bwana akubariki.

Usikose mwendelezo wa vitabu vinavyofuata.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

USITUPE LULU ZAKO MBELE YA NGURUWE.

MNARA WA BABELI

KUJIFUNUA KWA YESU KWA PILI.

KWA HIYO NDUGU, VUMILIENI, HATA KUJA KWAKE BWANA.

HEKIMA YA KIMUNGU, INAINGIAJE MIOYONI MWETU?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments