Je mkristo anaweza akawa na mapepo?

Je mkristo anaweza akawa na mapepo?

JIBU: Swali la kwanza la kujiuliza, je! mkristo ni mtu gani?..Mkristo ni mtu aliyemwamini,Yesu Kristo, kisha akapokea msamaha wa dhambi,kwa toba ya kweli, ubatizo na kutiwa muhuri na Roho Mtakatifu.

Mtu wa namna hiyo anakuwa na Kristo ndani yake. Na mtu mwenye Kristo Hawezi kuwa na mapepo, kwasababu Yesu hana pepo.

Vifungu hivi vinatuthibitishia kuwa hilo jambo haliwezekani;

1 Yohana 4:4

[4]Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia.

2 Wakorintho 6:14

[14]Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?

Kuonyesha kuwa giza na nuru haviwezi kuwepo sehemu moja, wakati mmoja.

Lakini swali linakuja inakuwaje kuna baadhi ya watu waliokoka wanaonekana kuwa na mapepo ndani yao?

Kama tulivyoona mkristo hawezi kuwa na mapepo, lakini ni vema kufahamu kuwa kuna tofauti kati ya kukaliwa na mapepo, na kushambuliwa na kipepo. 

Mtu aliyeokoka hawezi kukaliwa na mapepo, lakini anaweza akashambuliwa au kusumbuliwa na  uwepo wa mapepo, hicho ndicho kinachoweza kumtokea, lakini sio kwamba ana mapepo ndani yake.

Sababu zinazoweza mpelekea asumbuliwe nayo, ni hizi kuu tatu;

  1. Kutoijua kweli vema
  2. Uchanga wa kiroho
  3. kutenda dhambi.

Tukianza na sababu ya kwanza.

  1. Kutoijua kweli.

Kukosa kujua nafasi na mamlaka uliyo nayo ndani ya Kristo, shetani anaweza kukusumbua kwelikweli. Na wakati mwingine kukutesa. mapepo yanaweza kuwasumbua watu kifikra na kwa kuwawekea mawazo machafu akilini mwao, kuwashitaki, kwa kuwatupia ndoto mbaya, au kuwakaba usiku, au kuwaletea majaribu mbalimbali, lakini huyu mtu akijua kuwa ameshakabidhiwa mamlaka yote ya kukanyaga nge na nyoka na nguvu zote za yule mwovu,(Luka 9:1), akaitumia vema, shetani atamwogopa kumsogelea kwasababu anajua nguvu ya kimamlaka iliyo ndani yake ni thabiti haitoki mdomoni bali inasukumwa na ufalme wa Mungu ulio nyuma yake.. Ni sawa na mtu anayetoa amri kwa kinywa chake mwenyewe na yule anayetoa kwa agizo la raisi watu watamwogopa yule anayetoa kwa mamlaka aliyopewa na raisi. Hivyo ni muhimu sana kuitafakari na kuiamini mamlaka uliyopewa na Kristo ndani yako ili hayo maroho  unapoona dalili ya kutaka kukusumbua unatamka jina la Yesu mara moja tu yanatetemeka na kukimbia. Mamlaka hiyo amepewa mkristo yoyote aliyeokoka, haijaishi ni mchanga au mkomavu.

2) Sababu ya pili ni uchanga wa kiroho.

Ukiokolewa, kwasababu ya kutoondoka mara moja kwa baadhi ya tabia, au msingi au mienendo ya kale, hivyo tabia hizo mara nyingine zinakuwa ni upenyo wa uwepo wa kipepo kuzunguka zunguka karibu yako. Vitu vichanga sikuzote hushambulika kirahisi, unyasi ukiwa mdogo hutikiswa sana na upepo, Ndio maana ni lazima uanze kuukulia wokovu, kwa kujifunza Neno, kujizoesha utakatifu, maombi, ibada, mambo ambayo adui hapendi kwasababu ni kama moto kwao.  Mtu asipokuwa mkristo wa vitendo, sikuzote atasumbuliwa na roho za kidunia, na hatimaye atajiona kama ni ana mapepo kabisa, na akiendelea kuishi hivyo, mpaka kurudi nyuma atakufa kiroho, na Roho Mtakatifu kuondoka ndani yake, na mapepo ndio yatapata nafasi ya kumtawala kabisa.  (2Petro 1:5-10)

3) Kutenda dhambi

Mtu aliyeokoka, akaanza kutenda dhambi za makusudi, anarudia yale yale kila siku, jambo hilo ni upenyo mwingine wa mapepo kumsumbua, kwasababu anakuwa ameyapa nafasi, na maandiko yanasema tumsimpe ibilisi nafasi. (Waefeso 4:27).

Kwamfano umeacha ulevi, baada ya kuokoka, na umekuwa hivyo kwa muda mrefu sasa, halafu ghafla unaanza tena kuwa mlevi, Mungu anakuonya uache hutaki, unaendelea kunywa pombe..kitendo hicho kinaweza kukupelekea kusumbuliwa sana na mapepo. Mfano tu wa Yule ambaye anatawaliwa nayo.

Mathayo 12:43 Pepo mchafu, amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika,asipate.

44 Halafu husema, Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka; hata akija, aiona tupu, imefagiwa, na

kupambwa.

45 Mara huenda, akachukua pamoja naye pepo wengine saba walio waovu kuliko yeye

mwenyewe, nao huingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kilicho kibaya.

Hivyo kwa hitimisho, ni kuwa mtu aliyeokoka, hawezi kukaliwa na mapepo, yaani kutawaliwa au  kupagawishwa, au kuendeshwa nayo.. Isipokuwa anaweza kushambuliwa, kusababishiwa madhara, lakini kuvamiwa na uwepo wao. Ndio maana tumeambiwa tuvae silaha zote za haki, ili tuweze kumpinga shetani (Waefeso 6:10). Kwa kulijua Neno, utakatifu, maombi, na ibada.

Bwana akubariki.                                                               

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Mbona ni maskini tu huwa ndio wanaolipuka mapepo, na sio matajiri?

DALILI TISA (9) ZA PEPO KUWEPO NDANI YA MTU.

Je mtu anaweza akawa hajaokoka akaombea mtu na Pepo likamtoka,

 

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Albertine usein
Albertine usein
13 hours ago

Mafunzo mazurisana