Jina la Mkuu wa Uzima na Mfalme wa haki na pekee, YESU KRISTO libarikiwe, karibu tujifunze Biblia, Neno la Mungu wetu, lililo taa na Mwanga wa Njia yetu (Zab.119:105).
Kama Mkristo ni lazima uzijue alama hizi kuu nne (04), zitakazothibitisha kuwa unaye KRISTO maishani mwako, na alama hizo ni HEKIMA, HAKI, UTAKATIFU na UKOMBOZI.
1Wakorintho 1:30 “Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi”
Maana yake kupitia Yesu Kristo tunapata Hekima, Haki, Utakatifu na Ukombozi.
1. HEKIMA YA MUNGU.
Kama Yesu ni hekima ya Mungu kwetu, je hii hekima ni nini na tunaipataje..
Ayubu 28:28 “Kisha akamwambia mwanadamu, Tazama, kumcha Bwana ndiyo hekima, Na kujitenga na uovu ndio ufahamu”.
Kumbe kumcha Bwana ndio hekima, maana yake kumpata Yesu ni kupata kumcha Bwana, na ndio hekima ya Mungu, na pasipo Yesu hakuna kumcha Mungu.
2. HAKI.
Na kama Yesu ni haki ya Mungu, je hii haki inapatikanaje..
Warumi 3:21 “Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii;
22 ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti;
23 kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;
24 wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu”
Tunapomwamini Yesu tunakuwa tumeipata haki ya Mungu, haki ya kupokea kila tuombacho, haki ya kuishi milele, haki ya kumkaribia Mungu, haki ya kuwa na afya, haki ya kuwa amani, haki ya kuwa na furaha n.k
3. UTAKATIFU.
Na kama pia Bwana Yesu ni Utakatifu wa Mungu.. Je huu utakatifu tunaupataje?
Hiki ni kipengele muhimu sana, ambacho kinakwepwa na wengi, kumbuka huwezi kumtenganisha Yesu na UTAKATIFU, Ikiwa umemwamini Yesu ni lazima uishi maisha ya Utakatifu, hiyo ni kanuni. Na utakatifu sio ule wa rohoni tu, bali pia wa mwilini..
2Wakorintho 7:1 “Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku TUKITIMIZA UTAKATIFU katika kumcha Mungu”.
Utakatifu unakuja kwa kujitenga na vichocheo vyote vya dhambi, ambavyo vyanzo vyake ni tamaa ya macho na mwili, mfano wa hizo ni maudhui yote machafu yanayopatikana kwenye luninga, Mitandao na Magazeti, vile vile mazungumzo mabaya na makundi mabaya..
4. UKOMBOZI.
Yesu Kristo amefanyika pia ukombozi kwetu, kupitia kifo chake.. Na hii ndio alama ya mwisho inayomtambulisha Yesu, ambayo kimsingi hii ndio inayojulikana sana na wengi!
Wakolosai 1:13 “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake.
14 ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi”
Ndugu ukimjua Yesu kama mkombozi tu! (yaani anayesamehe dhambi), pasipo kumjua kwamba yeye pia ni “Mtakatifu” na anataka tuwe watakatifu kuna shida katika kuaminini kwako, vile vile ukimjua tu kama ni mtakatifu pasipo kumjua kama ni Hekima ya Mungu na Haki ya Mungu, bado pia kuna kitu kitakuwa hakijakamilika.. Lakini tukimjua katika sifa hizo Nne na kuziishi basi tutakuwa tumemjua hasa, na kufikia ule utimilifu.
Waefeso 4:13 “hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo”
Bwana atusaidie tuweze kufikia cheo cha kimo cha utimilifu wake.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Maana ya Mithali 10:1 Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye;
HEKIMA NANE(8) ZA KIUINJILISTI, KATIKA KUWAVUA WATU KWA KRISTO.
Nini maana ya hekima ya maskini haisikilizwi? (Mhubiri 9:16)
Maana ya Mhubiri 9:18 Hekima ndiyo bora kupita silaha za vita;
About the author