JIBU: Tunapaswa tufahamu vizuri utumishi wa Mungu jinsi ulivyogawanyika ili tusikose maarifa tukidhani ya kuwa Mungu anatenda kazi sehemu moja tu kanisa, mahali pengine hayupo, wala hajihusishi na mambo hayo. Tukisoma biblia tunaona Mungu anao watumishi wa aina mbili: 1) Watumishi wa ufalme wa mbinguni: 2) Watumishi wa kidunia:
Watumishi wa ufalme wa mbinguni: Ni wale wote wanaofanya kazi zihusuzo ufalme wa mbinguni tu, kuhakikisha habari njema zinawafikia watu wengi kwa njia ya injili, kulichunga kundi la Mungu wakati wote, kulihudumia kwa kila namna kupitia karama za Roho ambazo Mungu aliziachia katika kanisa..Na mfano wa watumishi hawa tunawajua ni wachungaji, waalimu, mitume, manabii, na wainjilisti, mashemasi, karama za maombezi, lugha, uponyaji, Neno la Hekima, Maarifa n.k..
Lakini Mfano wa watumishi wa kidunia, ni wale ambao wameamuriwa na Mungu kutimiza kusudi lake maalumu hapa duniani. Na mfano wa hao ni Serikali na taasisi zake zote zilizo chini yake..
Na Wengine mfano, ni mashirika mengine yote yasiyo ya Umma, yanayohusika na kutoa huduma za kijamii kwa watu. Hawa wote wanatimiza kusudi maalumu la Mungu lakini sio kusudi kamilifu lile ambalo alilitaka kila mmoja alifikie. Hivyo Mungu huwa anatumia vyombo hivi vyote viwili kwa aidha kubariki, au kijilipizia kisasi, kwa walio waovu na walio wema. Sasa kama imetokea Mfano mtu anayo kiu ya kuijua haki, anapenda kutafuta kujua masuala ya Mungu kwa bidii hata kama yeye sio mkristo..Jambo Mungu analofanya ni kumsaidia kwa kumpelekea huyu mtu mtumishi wake wa ufalme wa mbinguni ili amfikishie huduma hiyo aliyokuwa anaihitaji mahali pale alipo.
Mfano tunamwona Kornelio katika biblia, yeye hakuwahi hata siku moja kumfahamu YESU, lakini kwa jinsi alivyokuwa anabidii katika kumtafuta Mungu na kutenda haki na kutoa sadaka nyingi, basi Petro alitumwa kwake kwenda kumshuhudia habari njema za YESU KRISTO (Matendo 10), Mfano wa mwingine kama huo tunaona kwa yule Mkushi aliyetoka Afrika kwenda kuhiji Yerusalemu, lakini alipokuwa njiana anarudi nchini kwake huku anasoma torati mahali palipoandikwa habari za YESU lakini katika fumbo. Mungu aliona kiu yake hivyo kutokana na bidii yake kwa Mungu ya kutaka kujua, basi Mungu akamtumia Mtumishi wake Filipo aende kumwelezea habari zile kwa ufasaha zaidi.
Vivyo hivyo mtoto wa Mungu anapomwomba Mungu ampe riziki za dunia, hawezi kwenda kumtafutia kazi kanisani kwasababu makanisa sio taasisi za kutengeneza fedha, au sio sehemu za biashara, Bwana Mungu atakachokifanya ni kuhakikisha anamtafutia nafasi nzuri katika taasisi Fulani husika, labda wizara Fulani ambapo pengine atamweka chini ya ma-manager Fulani wa serikali..ambao watamwajiri na kumpatia mshahara mzuri..sasa hao ma-manager ni watumishi wa Mungu kwa Yule mtoto wa Mungu anayetafuta riziki za kidunia.
Vivyo hivyo mtoto wa Mungu anapohitaji, maji safi au umeme mzuri, Bwana Mungu hawezi kumpelekea mchungaji au nabii kumpatia huduma hiyo, atampelekea watumishi wake wengine wanaohusika na mambo hayo kama tanesco na Idara ya Maji, watahakikisha wanamfikishia maji na umeme mpaka chumbani kwake anapolala.
Hali Kadhalika pale mtu anapokuwa mwovu, anapotenda mabaya, anapomfanyia Mungu makosa kwa makusudi wapo vile vile watumishi Mungu aliowaandaa kwa ajili ya shughuli kama hizo ili kujilipizia kisasi kwake, na mojawapo wa hao watumishi wa Mungu ndio hivyo vyombo vya dola, mtu anapoua, unapoiba, unapobaka, unapokula rushwa,. Asidhani kuwa Mungu atasema naye kwa upole kama asemavyo naye kanisani, Na ndio hapo anakamatwa na kutiwa gerezani na wakati mwingine kuhukumiwa kunyongwa kama atakuwa anastahili adhabu hiyo,. Sasa Kwa namna ya kawaida unaweza kusema ni hawa watu wamemtendea hivyo, lakini kiuhalisia sio wao bali ni Mungu ndiye aliyemlipiza kisasa kwa makosa yake mwenyewe. Na ndio maana biblia inasema:
Warumi 13:1 “Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu.
2 Hivyo amwasiye MWENYE MAMLAKA HUSHINDANA NA AGIZO LA MUNGU; NAO WASHINDANAO WATAJIPATIA HUKUMU.
3 Kwa maana watawalao hawatishi watu kwa sababu ya matendo mema, bali kwa sababu ya matendo mabaya. Basi, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Fanya mema, nawe utapata sifa kwake;
4 kwa kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu kwako kwa ajili ya mema. LAKINI UFANYAPO MABAYA, OGOPA; kwa maana hauchukui upanga bure; kwa kuwa ni mtumishi wa Mungu, amlipizaye kisasi mtenda mabaya kwa ajili ya ghadhabu.
5 Kwa hiyo ni lazima kutii, si kwa sababu ya ile ghadhabu tu, ila na kwa sababu ya dhamiri.
6 Kwa sababu hiyo tena mwalipa kodi; kwa kuwa wao ni wahudumu wa Mungu, wakidumu katika kazi iyo hiyo”.
Unaona hapo? Sasa tukirudi kwenye swali lililoulizwa linalosema: Mimi ni askari magereza, na nimeamuriwa kumnyonga mfungwa aliyekuwa mwalifu kwa kosa la uuaji. Je! kufanya hivyo ninatenda dhambi?. Jibu ni kuwa “hutendi dhambi” .
Kwani wewe umeamuriwa kutimiza wajibu wako, kwa kosa ambalo lilishaonekana limefanywa na mtu mwenyewe, mpaka kufikia hapo ni Mungu mwenyewe ameruhusu. kwasababu maagizo hayo hayajatoka kwako bali yametoka juu, lakini hutahesabiwa thawabu katika hilo mfano wa wale wanaomtumikia Mungu kwa habari ya kuokoa roho za watu na sio kuangamiza,..Na ndio maana ni vema pia kujua pale unapokuwa mkristo, ufahamu kazi unayotaka kuifanya ujue na majukumu yake yatakavyokuwa, Sio kila kazi itampa mkristo amani kuifanya, japo hata afanyapo hatahesabiwa makosa.
Uamuzi ni wako binafsi. Hivyo kabla hujaamua kujiingiza kwenye utumishi wowote piga kwanza faida zake na hasara zake. Je! Utumishi uufanyao ni ule utimizao mapenzi makamilifu ya Mungu au ni ule wa kisasi cha Mungu, kabla hujawa mwanajeshi jitafakari mara mbili mbili, kabla hujawa polisi jitafakari mara mbili mbili na daktari vivyo hivyo na kazi nyingine zote.
Ubarikiwe.
Mada Nyinginezo:
MAWE YALIYOKWISHA KUCHONGWA MACHIMBONI.
KUCHEZA KARATA NI SAHIHI KWA MTU ALIYE MKRITO?
WALIO NA HEKIMA NDIO WATAKAOELEWA.
About the author