Nini maana ya Kipaimara?..Na je! Ni jambo la kimaandiko?

Nini maana ya Kipaimara?..Na je! Ni jambo la kimaandiko?

Nini maana ya Kipaimara?..je watu wanaweza kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono na kwa kupitia mafunzo fulani ya kipaimara?

JIBU: Kipaimara ni Neno lenye maana ya “uthibitisho”…Neno hili linatumika katika madhehebu baadhi kama vile Katoliki, Orthodoksi na Anglikana kama kanuni muhimu ya ukristo..Kwamfano Kanisa Katoliki lina kanuni saba za kufuata wanazoziita Sakramenti. Kwahiyo kipaimara Ni moja wapo ya hizo kanuni saba (sakramenti 7), ni kanuni ya Imani ambapo mtu anapaswa aipitie ili awe AMETHIBIKA MBELE ZA MUNGU. Na kanuni hiyo si nyingine zaidi ya KUWEKEWA MIKONO NA MAASKOFU WA KANISA… Madhehebu yanayotumia kanuni hii yanasimamia mistari kutoka katika kitabu cha.. 

Matendo 8: 14 “Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohana;

15 ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu;

16 kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu.

17 NDIPO WAKAWEKA MIKONO YAO JUU YAO, NAO WAKAMPOKEA ROHO MTAKATIFU.”

Kwahiyo kinachotokea ni kwamba baada ya mtoto kubatizwa, atapaswa apitia mafunzo fulani yanayohusiana na kipaimara, na akishahitimu, ndipo atakusanyika kanisani na kuwekewa mikono na Askofu, na ndipo Roho Mtakatifu atashuka juu yake kama alivyoshuka juu ya hao wasamaria waliokuwa wamebatizwa tu lakini bado walikuwa hawajashukiwa na Roho Mtakatifu. Kwahiyo kwa lugha rahisi au nyepesi ni kwamba hao Wasamaria walipokea kipaimara kwanza kwa mikono ya akina Petro na Yohana, ndipo Roho Mtakatifu akashuka juu yao..ikiwa na maana kuwa kama wasingewekewa mikono na Mitume na Bwana Yesu Kristo kamwe wasingepokea kile kipawa cha Roho Mtakatifu. 

Kwahiyo Kanisa katoliki na mengine wakaichukulia hiyo kama ni kanuni ya MUHIMU SANA ya kufuata kwa kila mkristo, kwamba ili mtu athibitike kuwa mkristo kweli kweli na ili aweze kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu ni lazima abatizwe kwanza na kisha awekewe mikono na maaskofu wa kanisa, Na akishapitia hizo hatua kikamilifu ndipo anaweza kukubalika kama ni mshirika halali wa kanisa, na zaidi ya yote ni Mkristo..Kabla ya hapo anakuwa hajulikani kama ni mkristo.Sasa kwa namna ya kibinadamu, hiyo inaweza ikaonekana ni sawa, inaweza ikaonekana ni utaratibu mzuri, au ni kanuni ya kufuata siku zote,..Lakini je! Ni sahihi kulingana na maandiko?.

 Kwanza kabisa kabla ya kuelezea kipaimara, tuuzungumzie ubatizo kwa ufupi: ni muhimu kufahamu kuwa watoto wachanga hawabatizwi kulingana na Neno “Imani” lenyewe lilivyo, Ili iwe imani, ni lazima kwanza mtu aamini kitu fulani, sasa watoto wachanga hata kujielewa tu hawajajielewa, sasa wataaminije?..watamwamini vipi Yesu Kristo kuwa ni Bwana na mwokozi wa maisha yao, na kwamba amekufa kwa ajili yao, na kwamba wanapaswa watubu kwa ajili ya ondoleo la dhambi zao, wakati hata fahamu za kujitambua wao wenyewe hazipo ndani yao?Kwasababu biblia inasema..


Warumi 10: 13 “kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.

14 Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? TENA WAMWAMINIJE YEYE WASIYEMSIKIA? Tena wamsikieje PASIPO MHUBIRI?

15 Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema”

 Kwahiyo Ubatizo wa vichanga sio sahihi kulingana na uhalisia wa mambo yote, haihitaji ufahamu mwingi sana kuelewa jambo hilo. Kumbatiza mtoto mchanga ni sawa na kwenda mtaani na kumchukua mtu asiyemjua Mungu kabisa pasipo kumhubiria, wala kumfundisha chochote na kwenda kumzamisha kwenye maji na kumwambia tayari umebatizwa!…Hiyo ni kazi bure. Na pili, kuhusu kipaimara, Mitume hawakutoa kanuni Fulani kwamba mtu akitaka kupokea Kipawa cha Roho Mtakatifu ni lazima awekewe mikono na viongozi wao kwanza?..Hapana hawakutoa hiyo formula hata kidogo..Petro Na Yohana waliwawekea mikono wale wasamaria kwa wakati ule tu kwasababu ndio njia waliyoongozwa na Roho waitumie kwa wakati ule tu! Mahali pengine watu walishukiwa na Roho pasipo kuwekewa mikono na mtu yoyote.

Kama tu siku ya Pentekoste watu walishukiwa na Roho pasipo kuwekewa mikono na mtu yoyote. Na pia tunaona huyo huyo Petro alipokwenda nyumbani kwa Kornelio kumhubiria injili yeye na nyumba yake, Roho aliwashukia wale watu wote pasipo hata Mtume Petro kuwawekea mikono.. 

Matendo 10: 43 “Huyo manabii wote humshuhudia, ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi.

44 Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno.

45 Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu”.

Unaona hapo? Wakati Petro akiwa anazungumza tu! Roho aliwashukia juu yao, Na sehemu nyingine Petro alipowahubiria watu zaidi ya elfu 3, na walipoamini..aliwaambia namna ya kupokea Roho Mtakatifu pasipo kuwekewa mikono akawaambia..”

Matendo 2:36 “Basi nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulibisha kuwa Bwana na Kristo.

37 Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?

38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”. 

Unaona na hapo? Petro Hakuwaambia watu tubuni mkabatizwe na kisha njooni tuwawekee mikono ndipo mpokee kipawa cha Roho Mtakatifu badala yake maneno hayo yanaonyesha kuwa mtu anaweza kupokea Roho Mtakatifu pasipo hata kuwekewa mikono na mitume. Kwahiyo kuwekewa mikono sio kanuni ya kupokea Roho Mtakatifu, kanuni ya kupokea Roho ni kutubu na kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu.Mwingine anaweza akapokea Roho kwa kuwekewa mikono, mwingine anaweza apokee pasipo kuwekewa mikono…Na kwa jinsi Roho atakavyochagua njia ya kushuka juu ya huyo mtu, baada tu ya mtu kutubu na kubatizwa. 

Ni sawa na wakina Petro mahali pengine walikuwa wanatumia hata leso zao kuponya wagonjwa, na sehemu nyingine wanataja tu jina la Yesu pasipo kutumia chochote na watu wanafunguliwa..

kwahiyo ni njia tu ambayo Roho aliyokuwa anawaongoza kwa wakati husikia ndiyo waliyokuwa wanaitumia..lakini huwezi kuona Petro anatoa kanuni maalumu kuwa sehemu zote watu ili wafunguliwa lazima watumie leso, huwezi kuona jambo hilo.. Tofauti na ilivyo siku hizi za mwisho..Mafuta, chumvi, udongo ndio KANUNI ya kupokea uponyaji, kila tatizo linatatuliwa na maji ya maombezi, kila tatizo linatatuliwa na mafuta ya maombezi na chumvi…Inakuwa ni kanuni, jina la Yesu halitumiki tena…Ni roho hiyo hiyo iliyopo pia katika mifumo ya kipaimara na ubarikio. Kwahiyo kipaimara ni mfumo wa kimapokea ambao hausimami katika uhalisia wa kibiblia, ambao malengo yake ni kuwafanya watu waamini kuwa kuwekewa mikono na askofu, tayari wamekamilika na ndio tiketi ya kuthibitika mbele za Mungu..ni mfumo ambao unawafanya watu waridhike na kanuni za dini kuliko kanuni za biblia.

 Utamwuliza mtu unauhakika wa kwenda mbinguni, atakwambia ndio nimebatizwa na nimepokea kipaimara…lakini mwulize nini maana ya Roho Mtakatifu na matunda yake ni yapi?..atakwambia sijui?, muulize nini maana ya unyakuo atakuambia sijawahi kusikia hata hicho kitu, muulize umeokoka atakwambia dini yangu haifundishi hivyo, mwambie kuwa Tunaishi siku za mwisho atakuambia sijui?..lakini atajisifia kipaimara chake kwa sherehe kubwa aliyoifanya siku hiyo. Utakuta mtu analijua dhehebu lake kuliko anavyoijua biblia. Kwahiyo kanuni za kipaimara sio kanuni zilizokatibiwa na Mungu bali wanadamu, Mungu hajatoa kanuni maalumu kuwa mtu lazima apitie kipaimara au apakwe mafuta ya maombezi, au atumie chumvi ndipo afunguliwe au akubaliwe na yeye..yote hiyo ni mipango ya ibilisi kuwafanya watu wasitafakari maandiko kwa kina bali wapate njia za mkato za kutatua matatizo yao. Na kujiridhisha katika hizo kama ndio sababu ya kukubaliwa na Mungu, kumbe sio.

Ubarikiwe.

Mada Nyinginezo:

NI HALALI KUBATIZA WATOTO WADOGO?

JE! UMEBATIZWA UBATIZO SAHIHI?

SHETANI ANATOLEA WAPI FEDHA, ANGALI TUNAJUA FEDHA NA DHAHABU NI MALI YA BWANA?

UNAFANYA NINI HAPO?

MSTARI HUU UNA MAANA GANI? “YUKO MWENYE HAKI APOTEAYE KATIKA HAKI YAKE”?

WAPUNGA PEPO WANAOZUNGUMZIWA KWENYE BIBLIA NI WATU WA NAMNA GANI?

JE TATIZO LA KULA KUCHA NI ISHARA YA KUWA NA MAPEPO?


 

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

7 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Alphonce
Alphonce
9 months ago

Naomba kufahamu kubatizwa Maji Mengi au machache Kuna utofauti gani kibiblia

Fortunatus Mkuchu
Fortunatus Mkuchu
3 years ago

Nilikuwa nahitaji kitabu Cha mafundisho ya kipa imara

John Mathias Mturo
John Mathias Mturo
3 years ago

Nimefurahia somo,ni kweli.Mungu akubariki kwa fundisho hilo.Mungu atuokoe.

Gwamaka Mbwaga
Gwamaka Mbwaga
4 years ago

Asante Kwa Somo